Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
ULY CLINIC
20 Agosti 2026, 05:09:52

Jipu sehemu za siri: Mwanamke
Jipu sehemu za siri kwa wanawake ni hali ya kutokea kwa mkusanyiko wa usaha ndani ya tishu za eneo la siri kutokana na maambukizi. Kwa lugha ya kawaida, wanawake wengi huita hali hii jipu, na ikiwa yapo mengi huitwa majipu. Vijipu vidogo vidogo, hasa vile vyenye ukubwa mdogo chini ya takribani sentimita moja ya kipenyo, mara nyingi huitwa vijipu.
Majipu sehemu za siri yanaweza kutokea kwenye maeneo mbalimbali kama:
Ngozi ya mashavu ya uke (labia majora na labia minora)
Eneo lenye nywele karibu na uke
Sehemu ya kuingilia uke
Tezi za sehemu za siri kama tezi ya Batholini
au tishu za ndani zinazozunguka uke.
Tatizo hili linaweza kumpata mwanamke wa umri wowote, lakini huonekana zaidi kwa wanawake walio katika umri wa uzazi kutokana na sababu kama msuguano, kunyoa nywele za sehemu za siri, mabadiliko ya homoni, maambukizi ya ngozi, magonjwa ya zinaa au matatizo yanayoathiri kinga ya mwili.
Ingawa vijipu vidogo vinaweza kupona vyenyewe, majipu makubwa yanaweza kusababisha maumivu makali, kushindwa kukaa au kutembea vizuri, homa na wakati mwingine kuhitaji kufunguliwa na kutolewa usaha na mtaalamu wa afya.
Jipu ni nini?
Jipu ni mkusanyiko wa usaha unaotengenezwa ndani ya tishu kutokana na mwili kupambana na maambukizi.
Usaha ni mchanganyiko wa:
Bakteria
Seli nyeupe za damu zinazopambana na maambukizi
Seli zilizokufa
Mabaki ya tishu zilizoharibiwa
na majimaji mbalimbali ya uchochezi
Mwili unapogundua maambukizi, seli za kinga huenda eneo hilo ili kuua vijidudu. Katika baadhi ya hali, usaha hukusanyika ndani ya eneo lililofungwa na kutengeneza mfuko wenye shinikizo. Hapo ndipo jipu hutokea.
Tofauti na kidonda cha kawaida, jipu huwa na nafasi iliyojazwa usaha ndani ya tishu. Kwa sababu hiyo, mara nyingi antibiotiki pekee hazitoshi kwa majipu makubwa, kwa sababu dawa inaweza kushindwa kufika vizuri ndani ya mfuko wa usaha bila usaha huo kutolewa.
Aina za majipu sehemu za siri kwa wanawake
Majipu sehemu za siri yanaweza kutofautiana kulingana na sehemu yanapotokea na sababu yake.
1. Jipu la ngozi ya sehemu za siri
Hii ndiyo aina inayotokea mara nyingi.
Hutokea kwenye ngozi ya:
Mashavu makubwa ya uke (labia majora);
Sehemu yenye nywele karibu na uke;
Kinena;
au eneo la nje linalozunguka sehemu za siri.
Mara nyingi husababishwa na bakteria wanaoishi kawaida kwenye ngozi, hasa Staphylococcus aureus, ambao wanaweza kuingia ndani ya ngozi kupitia:
Mchubuko mdogo
Jeraha baada ya kunyoa
Kukwangua ngozi
au kuziba kwa vinyweleo
2. Vijipu vya sehemu za siri
Vijipu ni majipu madogo ambayo mara nyingi huanza kama:
Uvimbe mdogo
Sehemu yenye maumivu inapoguswa
Wekundu wa ngozi
au eneo lenye joto kuliko sehemu inayozunguka.
Baadhi ya vijipu huwa na ukubwa mdogo na hupona bila matibabu maalumu, hasa kama kinga ya mwili iko vizuri.
Hata hivyo, vijipu vinapokuwa vingi, vinaporudia mara kwa mara au vinaendelea kukua vinaweza kuhitaji uchunguzi zaidi ili kutafuta sababu inayochangia.
3. Jipu la tezi ya Batholini
Tezi ya Batholini ni tezi ndogo zilizopo pande zote mbili karibu na mlango wa uke. Kazi yake ni kutoa ute unaosaidia kulainisha eneo la uke.
Wakati mrija wa tezi hii unapoziba:
Ute huanza kukusanyika
Bakteria wanaweza kuongezeka
Usaha hutengenezwa
na jipu hutokea.
Jipu la Batholini mara nyingi huwa:
Upande mmoja wa mlango wa uke;
Kubwa kuliko vijipu vya kawaida;
Lenye maumivu makali hasa wakati wa kukaa, kutembea au kufanya tendo la ndoa.
Kwa baadhi ya wanawake, jipu hili linaweza kuambatana na homa na kuhitaji kufunguliwa ili kutoa usaha.
4. Majipu yanayoungana (Kabanko)
Hii ni hali ambapo majipu kadhaa yaliyo karibu yanaungana na kutengeneza eneo kubwa la maambukizi.
Kabanko huwa:
Kubwa;
Maumivu zaidi
Huweza kutoa usaha mwingi
na linaweza kuacha kovu baada ya kupona.
Hali hii huonekana zaidi kwa watu wenye:
Kisukari
Kinga dhaifu
au maambukizi ya ngozi yanayorudiarudia.
Sababu za jipu sehemu za siri kwa wanawake
1. Maambukizi ya bakteria kwenye ngozi
Hii ndiyo sababu inayopatikana mara nyingi. Ngozi ya binadamu ina bakteria wengi ambao kwa kawaida hawasababishi ugonjwa. Lakini bakteria hao wanapoingia ndani ya ngozi kupitia jeraha dogo wanaweza kusababisha maambukizi.
Sababu zinazorahisisha kuingia kwa bakteria ni pamoja na:
Kunyoa nywele za sehemu za siri
Kutumia wembe wenye kuchafua au usafi hafifu
Mikwaruzo
Msuguano wa nguo
au kutokwa na jasho kwa muda mrefu
2. Nywele kuota ndani ya ngozi (Nywele kuotea ndani ya ngozi)
Baada ya kunyoa au kung'oa nywele za sehemu za siri, baadhi ya nywele zinaweza kushindwa kutoka nje na kuanza kukua ndani ya ngozi.
Mwili unaweza kuitambua nywele hiyo kama kitu kisicho cha kawaida na kusababisha:
Uvimbe
Maumivu
Wekundu au weusi
na wakati mwingine jipu lenye usaha.\
Tatizo hili mara nyingi huonekana katika maeneo yenye nywele nyingi kama mashavu makubwa ya uke na kinena.
3. Kuziba kwa vitundu vya vinyweleo
Vitundu vya vinyweleo vinaweza kuziba kutokana na:
Mafuta ya ngozi
Seli zilizokufa
Jasho
au msuguano
Kuziba huku kunaweza kutoa mazingira mazuri kwa bakteria kuzaliana na kusababisha kijipu au jipu.
4. Maambukizi ya tezi ya Batholini
Kuziba kwa njia ya kutoa ute kwenye tezi ya Baitolini kunaweza kusababisha uvimbe unaoitwa kifukomaji cha Batholini (sisti ya batholini). Ikiwa bakteria wataingia ndani ya kifuko hicho, kinaweza kugeuka kuwa jipu la Baitolini.
5. Magonjwa ya zinaa
Baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kuhusishwa na vidonda, uvimbe au maambukizi katika sehemu za siri.
Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha:
Si kila jipu la sehemu za siri ni ugonjwa wa zinaa
na si kila ugonjwa wa zinaa husababisha jipu
Magonjwa kama klamidia na kisonono kwa kawaida hayatoi jipu la ngozi moja kwa moja, lakini yanaweza kusababisha maambukizi ya mfumo wa uzazi yanayohitaji matibabu.
6. Kisukari
Wanawake wenye kisukari wanaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata majipu kwa sababu:
Sukari nyingi kwenye damu hupunguza uwezo wa kinga kufanya kazi vizuri
Bakteria hukua kwa urahisi zaidi
Uponaji wa vidonda huwa polepole
Majipu yanayorudia mara kwa mara yanaweza kuwa ishara ya kisukari ambacho hakijagunduliwa.
7. Upungufu wa kinga ya mwili
Hali zinazopunguza uwezo wa mwili kupambana na maambukizi zinaweza kuongeza hatari ya majipu.
Mfano:
Matumizi ya dawa zinazoshusha kinga
Baadhi ya magonjwa ya kinga
au hali nyingine zinazodhoofisha mfumo wa kinga
8. Ugonjwa wa hidradenaitisi supurativa
Hidradenaitis supurativa ni ugonjwa wa muda mrefu wa ngozi unaosababisha vijipu vinavyorudia mara kwa mara katika maeneo yenye tezi za jasho, ikiwemo:
Kinena
Makwapa
Chini ya matiti
na maeneo ya karibu na sehemu za siri
Tofauti na jipu la kawaida, hali hii hujirudia, inaweza kutengeneza njia chini ya ngozi (mfereji sainasi) na kuacha makovu.
Dalili za jipu sehemu za siri kwa wanawake
Dalili za jipu sehemu za siri hutegemea ukubwa wa jipu, eneo lilipo na kiwango cha maambukizi. Vijipu vidogo vinaweza kuanza taratibu na kusababisha usumbufu mdogo, wakati majipu makubwa yanaweza kusababisha maumivu makali na dalili za mwili mzima. Dalili zinazoweza kuonekana ni pamoja na:
1. Uvimbe wenye maumivu
Dalili ya kwanza mara nyingi huwa ni uvimbe mdogo unaouma unapoguswa.
Kadiri usaha unavyokusanyika:
Uvimbe huongezeka ukubwa
Eneo huwa gumu au lenye kukaza
Maumivu yanaweza kuongezeka hasa wakati wa kukaa, kutembea au kugusana na nguo.
Majipu mengi huwa na maumivu kwa sababu mkusanyiko wa usaha huongeza shinikizo ndani ya tishu.
2. Ngozi kuwa nyekundu/zambarau na yenye joto
Eneo linalozunguka jipu linaweza kuwa:
Jekundu/zambarau kwa watu weusi
Lenye joto kuliko ngozi inayozunguka
na wakati mwingine kuvimba zaidi
Hii hutokana na mwitikio wa mwili dhidi ya maambukizi ambapo damu nyingi na seli za kinga hupelekwa eneo hilo.
3. Kutokea kwa kichwa cha usaha
Kadiri jipu linavyokomaa, wakati mwingine sehemu ya juu ya uvimbe huwa laini na kuonekana kama ina rangi ya njano au nyeupe.
Hii hutokea kwa sababu usaha umekusanyika karibu na uso wa ngozi. Baadhi ya majipu hupasuka yenyewe na kutoa usaha, lakini si salama kila wakati kusubiri jipu lipasuke bila ushauri wa kitaalamu, hasa katika eneo la siri.
4. Kutoka usaha au majimaji
Jipu linapofunguka linaweza kutoa:
Usaha mzito wa njano au kijani;
Majimaji yenye harufu;
au damu kidogo iliyochanganyika na usaha.
Baada ya kutoa usaha, maumivu yanaweza kupungua kwa sababu shinikizo ndani ya jipu linapungua.
Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba maambukizi yameisha kila wakati. Wakati mwingine sehemu ya ndani bado huwa na maambukizi na inaweza kuhitaji matibabu.
5. Maumivu wakati wa kukaa, kutembea au tendo la ndoa
Kwa sababu sehemu za siri zina msuguano mkubwa wakati wa harakati, jipu linaweza kusababisha usumbufu mkubwa.
Mwanamke anaweza kupata:
Maumivu wakati wa kukaa muda mrefu;
Maumivu wakati wa kutembea;
Maumivu wakati wa kuvaa nguo zinazobana;
Maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Hii huonekana sana kwa majipu yaliyo kwenye mashavu ya uke au karibu na mlango wa uke.
6. Homa na dalili za mwili mzima
Majipu madogo ya ngozi mara nyingi hayasababishi homa.
Lakini maambukizi yanapokuwa makubwa yanaweza kusababisha:
homa;
kutetemeka;
uchovu;
maumivu ya mwili;
kuhisi mgonjwa kwa ujumla.
Dalili hizi zinaweza kuonyesha kuwa maambukizi yameanza kuathiri mwili mzima na yanahitaji tathmini ya haraka.
Tofauti kati ya jipu, uvimbe, kifuko cha maji na vidonda vya sehemu za siri
Wanawake wengi huchanganya jipu na matatizo mengine ya sehemu za siri kwa sababu yanaweza kuonekana kama uvimbe au kidonda. Kutofautisha hali hizi ni muhimu kwa sababu matibabu yake hutofautiana.
1. Jipu dhidi ya kifuko cha maji (sisti)
Kifuko cha maji (sisti) ni mfuko uliojaa majimaji au ute ambao unaweza kutokea kwenye sehemu mbalimbali za mwili.
Mfano unaojulikana ni:
Kifuko cha tezi ya batholini (Sisti ya batholini).
Tofauti kubwa ni kwamba:
Sisti isiyoambukizwa mara nyingi haina maumivu
Huwa laini au yenye kuhama kidogo
Haina usaha
Mara nyingi haina homa
Lakini cyst inapopata maambukizi inaweza kubadilika na kuwa:
Jipu la tezi Batholini.
Hapo huwa:
na Maumivu
Kubwa
Lenye joto
na linaweza kuwa na Usaha.
2. Jipu dhidi ya chunusi ya sehemu za siri
Chunusi inaweza kutokea sehemu za siri kutokana na kuziba kwa vinyweleo.
Mara nyingi:
Huwa ndogo
Hupungua yenyewe
Huwa juu juu kwenye ngozi
Jipu huwa tofauti kwa sababu:
Huingia ndani zaidi ya ngozi
Huwa na maumivu zaidi
Huwa kubwa zaidi
na mara nyingi huwa na mkusanyiko wa usaha
3. Jipu dhidi ya vidonda vya magonjwa ya zinaa
Baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kusababisha vidonda au uvimbe sehemu za siri.
Kwa mfano:
Malengelenge ya sehemu za siri (Herpes ya sehemu za siri yanaweza kusababisha malengelenge madogo yenye maumivu;
Kaswende inaweza kusababisha kidonda kisichouma.
Tofauti ni kwamba jipu kwa kawaida huwa:
Uvimbe uliojaa usaha;
Lina maumivu;
Linaweza kuwa na joto na wekundu.
Kwa sababu baadhi ya dalili zinaweza kufanana, uchunguzi wa daktari ni muhimu hasa kama kuna uwezekano wa maambukizi ya zinaa.
4. Jipu dhidi ya saratani ya sehemu za siri
Ingawa si kila uvimbe ni saratani, uvimbe unaodumu muda mrefu unapaswa kuchunguzwa.
Dalili zinazoweza kuhitaji uchunguzi zaidi ni:
uvimbe usioisha baada ya matibabu;
kidonda kisichopona;
kutokwa damu bila sababu;
mabadiliko ya ngozi yanayoendelea.
Majipu kwa kawaida huanza ghafla na huwa na dalili za maambukizi kama maumivu, joto na usaha.
Vipimo vya kutambua jipu sehemu za siri
Mara nyingi daktari anaweza kutambua jipu kwa kulichunguza eneo husika. Uchunguzi unaweza kujumuisha:
1. Uchunguzi wa mwili
Daktari ataangalia:
Ukubwa wa uvimbe
Eneo lilipo
Kama lina usaha
Kiwango cha maumivu
Kama maambukizi yameenea kwenye ngozi inayozunguka
2. Kuchukua sampuli ya usaha (Kuotesha usaha)
Kwa baadhi ya majipu, hasa:
Makubwa
Yanayojirudia
Yasiyopona
au yanayoambatana na kushindwa kwa tiba
Daktari anaweza kuchukua sampuli ya usaha kwa ajili ya uchunguzi wa maabara. Kipimo hiki husaidia kujua aina ya bakteria wanaosababisha maambukizi na antibayotiki inayoweza kufanya kazi vizuri zaidi.
3. Vipimo vya magonjwa mengine yanayochangia
Ikiwa majipu yanarudia mara kwa mara, daktari anaweza kupendekeza vipimo kama:
Kipimo cha sukari kwenye damu kutafuta kisukari
Vipimo vya maambukizi ya zinaa kulingana na historia
Tathmini ya kinga ya mwili ikiwa kuna sababu ya kushuku
Je, jipu sehemu za siri ni hatari?
Mara nyingi vijipu vidogo vya ngozi si hatari na vinaweza kupona bila madhara makubwa.
Hata hivyo, eneo la siri lina umuhimu maalumu kwa sababu:
Lina mishipa mingi ya damu;
Lina unyevunyevu unaoweza kusaidia bakteria kukua;
Maambukizi yanaweza kuenea kwenye tishu zinazozunguka.
Majipu makubwa au yasiyotibiwa yanaweza kusababisha:
Kuenea kwa maambukizi kwenye ngozi (selulaitisi)
Kutokea kwa majipu yanayorudia
Makovu
Maambukizi makubwa mwilini (Sepsisi) katika hali nadra lakini hatari
Matibabu ya jipu sehemu za siri kwa wanawake
Matibabu ya jipu sehemu za siri hutegemea mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na:
Ukubwa wa jipu
Eneo lilipo
Kama ni kijipu kidogo au jipu kubwa
Kiwango cha maambukizi
Uwepo wa homa au dalili za mwili mzima
Kama jipu limerudia mara kwa mara
na hali ya afya ya mwanamke, kama vile uwepo wa kisukari au matatizo ya kinga
Ni muhimu kuelewa kuwa matibabu ya jipu si sawa kwa kila mwanamke. Kijipu kidogo cha ngozi kinaweza kupona kwa hatua rahisi za nyumbani, lakini jipu kubwa lenye mfuko wa usaha mara nyingi huhitaji kutolewa usaha na mtaalamu wa afya.
1. Matibabu ya nyumbani kwa vijipu vidogo
Vijipu vidogo ambavyo havina dalili kali vinaweza kuanza kutibiwa kwa njia rahisi za kusaidia mwili kupona.
Hatua zinazoweza kusaidia ni pamoja na:
Kukanda na kitambaa kilichochovywa kwenye maji ya uvuguvugu
Kuweka kitambaa safi chenye maji ya uvuguvugu kwenye eneo lenye jipu dogo kwa dakika 10–15 mara kadhaa kwa siku kunaweza kusaidia:
Kuongeza mzunguko wa damu kwenye eneo hilo
Kupunguza maumivu
Kusaidia mwili kuleta seli za kinga kwenye eneo la maambukizi
na wakati mwingine kusaidia jipu kukomaa na kujifungua lenyewe
Maji yanapaswa kuwa ya uvuguvugu, si ya moto sana, kwa sababu joto kali linaweza kuchoma ngozi nyeti ya sehemu za siri.
Kulinda eneo lisipate msuguano
Ni muhimu:
kuvaa chupi safi za pamba;
kuepuka nguo zinazobana sana;
kubadilisha nguo zenye jasho;
kuweka eneo la siri katika hali safi na kavu.
Msuguano unaweza kuongeza maumivu na kufanya ngozi iliyowaka kuumia zaidi.
Kutunza usafi bila kuharibu ngozi
Sehemu za siri hazihitaji kusafishwa kwa sabuni kali au dawa za kuua vijidudu kila mara.
Kutumia kemikali kali kunaweza:
kuharibu kinga ya kawaida ya ngozi;
kusababisha muwasho;
kuongeza uwezekano wa michubuko.
Mara nyingi kusafisha kwa maji safi na sabuni laini upande wa nje wa sehemu za siri kunatosha.
2. Kutoboa au kufungua jipu na kutoa usaha (Kukamua jipu)
Hii ndiyo tiba muhimu zaidi kwa majipu mengi makubwa. Jipu linapotengeneza mfuko mkubwa wa usaha, mara nyingi dawa pekee haitoshi kwa sababu:
Damu haiwezi kufikisha antibiotiki kwa kiwango kizuri ndani ya mfuko wa usaha
Bakteria wanaweza kuwa wamejificha ndani ya usaha
Shinikizo ndani ya jipu huendelea kusababisha maumivu
Katika utaratibu huu:
Eneo husafishwa
Dawa ya ganzi ya eneo lenye shida hutolewa ili kupunguza maumivu
Daktari hufungua sehemu ndogo ya jipu
Usaha hutolewa
Eneo husafishwa na kupewa maelekezo ya uangalizi
Baada ya usaha kutoka, wagonjwa wengi hupata nafuu kubwa ya maumivu kwa sababu shinikizo linapungua.
3. Je, kila jipu linahitaji kutobolewa?
Hapana, sio kila jipu linapaswa kufunguliwa.
Uamuzi hutegemea:
Ukubwa
Hatua ya ukuaji
Eneo
Kiwango cha maumivu
na kama tayari linaonyesha dalili za kuwa na usaha uliokusanyika
Kwa mfano:
kijipu kidogo juu ya ngozi kinaweza kupona bila kufunguliwa
jipu kubwa lenye maumivu makali na usaha mwingi mara nyingi linahitaji kutolewa
Kwa majipu yaliyo karibu na mlango wa uke, hasa jipu la tezi ya Baitolini, ni muhimu zaidi kufanyiwa tathmini na mtaalamu kwa sababu eneo hilo lina umuhimu mkubwa katika matibabu.
4. Matibabu ya jipu la tezi batholini
Jipu la Baitolini lina matibabu maalumu kwa sababu linatokea ndani ya tezi yenye njia iliyoziba.
Njia zinazotumika ni pamoja na:
Kufungua na kuweka mrija mdogo(katheta)
Katika utaratibu huu, daktari:
hufungua sehemu ndogo ya jipu
hutoa usaha
huweka mrija mdogo
Mrija huu huwekwa kwa muda ili:
Kuruhusu usaha uliobaki kutoka
Kusaidia kutengeneza njia mpya ya kudumu ya kutoa ute
Kupunguza uwezekano wa kurudia
Kutengeneza njia mpya ya kudumu (Masupialaizesheni)
Kwa wanawake wenye majipu ya Baitolini yanayorudia, daktari anaweza kufanya upasuaji mdogo unaoitwa masupialaizesheni
Katika upasuaji huu:
Kifuko hufunguliwa
Kingo zake hushonwa ili kuacha njia wazi
Hivyo ute usizuiliwe tena kwa urahisi
Kuondoa tezi batholini
Hii hufanyika mara chache, hasa:
Kama tatizo linarudia sana
Kama kuna mashaka ya ugonjwa mwingine
au kama matibabu mengine yameshindwa
Kwa wanawake wenye umri mkubwa zaidi, hasa baada ya kukoma hedhi, uvimbe wa eneo la Baitolini unaohitaji uchunguzi maalumu kwa sababu kuna uwezekano mdogo wa magonjwa mengine yanayofanana na jipu.
5. Matumizi ya antibayotiki
Antibayotiki hazitumiki kwa kila jipu. Kwa jipu ambalo limefunguliwa na usaha umetolewa vizuri, mara nyingi mwili unaweza kupona bila antibiotiki isipokuwa kuna sababu maalumu.
Daktari anaweza kuagiza antibiotiki ikiwa kuna:
Homa
Maambukizi yanayoenea kwenye ngozi (selulaitisi)
Kinga dhaifu
Kisukari kisichodhibitiwa
Jipu kubwa sana
Maambukizi yanayorudia
au uwezekano wa bakteria maalumu kama Staphylococcus aureus walio na ukinzani kwenye Methicillin (MRSA)
Ni muhimu kutotumia antibiotiki bila ushauri kwa sababu:
Si kila jipu husababishwa na bakteria wanaohitaji dawa hizo
Matumizi yasiyo sahihi huongeza usugu wa bakteria dhidi ya dawa (Ukinzani wa bakteria kwenye dawa)
6. Je, jipu linaweza kupasuliwa nyumbani?
Jipu kubwa lenye mkusanyiko wa usaha mara nyingi huhitaji kufunguliwa ili kutoa usaha (kukamuliwa), kwa sababu kutoa usaha hupunguza shinikizo ndani ya jipu na kusaidia kupona. Katika jamii nyingi, watu wamekuwa wakifungua majipu madogo au ya kawaida kwa muda mrefu, na baadhi hupata nafuu bila matatizo.
Hata hivyo, si kila uvimbe unaofanana na jipu unapaswa kufunguliwa bila uchunguzi. Tatizo kubwa ni kwamba mtu anaweza kudhani ana jipu wakati kumbe ni tatizo lingine kama kifuko cha maji (sisti), uvimbe mwingine au kidonda kinachohitaji matibabu tofauti. Pia, sehemu za siri zina tishu laini na nyeti ambazo zinaweza kuumia zaidi ikiwa utaratibu utafanywa bila uangalifu.
Ikiwa mtu anafungua jipu mwenyewe, hatari kubwa zaidi huhusiana na usafi duni wa vifaa, kutokutoa usaha wote, au kuchelewesha kupata huduma wakati maambukizi ni makubwa. Kwa hiyo, jipu linaloongezeka, lenye maumivu makali, linalorudia, linaloambatana na homa au lililo karibu na mlango wa uke linapaswa kutathminiwa na mtaalamu wa afya.
7. Matibabu ya majipu yanayorudia mara kwa mara
Ikiwa mwanamke anapata majipu sehemu za siri mara kwa mara, si vizuri kutibu kila jipu pekee bila kutafuta sababu. Daktari anaweza kuchunguza sababu kama:
i. Kisukari
Vipimo vya sukari vinaweza kupendekezwa kwa sababu kisukari huongeza uwezekano wa kupata maambukizi ya ngozi.
ii. Hidradenaitisi supurativa
Ikiwa kuna:
Vijipu vinavyorudia sehemu zilezile
Makovu
Mashimo madogo kwenye ngozi
au usaha unaotoka mara kwa mara
daktari anaweza kufikiria ugonjwa huu wa ngozi
iii. Kubeba bakteria kwenye ngozi
Baadhi ya watu hubeba bakteria kama Staphylococcus aureus kwenye ngozi au puani bila kuwa wagonjwa, lakini wanaweza kupata majipu mara kwa mara. Katika hali maalumu, daktari anaweza kupendekeza hatua za kupunguza uwepo wa bakteria hao.
8. Mambo ya kuepuka unapokuwa na jipu sehemu za siri
Epuka:
Kulikamua jipu kwa nguvu
Kutumia dawa za kienyeji zisizojulikana usalama wake
Kupaka kemikali kali
Kutumia antibayotiki bila kuandikiwa
Kunyoa eneo lenye jipu
Kufanya tendo la ndoa ikiwa linaongeza maumivu au msuguano
Wakati gani mwanamke mwenye jipu anatakiwa kwenda hospitali haraka?
Tafuta huduma ya afya mapema ikiwa:
Jipu ni kubwa au linaongezeka haraka
Maumivu ni makali sana
Una homa
Unaishiwa nguvu au unatetemeka
Wekundu/ rangi ya zambarau unaenea kuzunguka jipu
Jipu lipo karibu na mlango wa uke na linazuia kukaa au kutembea
Usaha una harufu kali
Una kisukari
Una kinga dhaifu
Majipu yanarudia mara kwa mara
au haliponi baada ya siku kadhaa
Kinga ya kupata majipu sehemu za siri
Si kila jipu linaweza kuzuilika, lakini hatua hizi zinaweza kupunguza hatari:
Epuka kunyoa kwa njia inayosababisha michubuko
Tumia vifaa safi vya kunyoa na usishirikiane wembe
Vaa nguo za ndani safi na zinazopitisha hewa
Epuka nguo zinazobana kwa muda mrefu
Tibu maambukizi ya ngozi mapema
Fanya uchunguzi wa kisukari ikiwa majipu yanarudia
Tumia kinga wakati wa ngono ikiwa uko katika hatari ya magonjwa ya zinaa
Usitumie dawa za kuingiza ukeni bila sababu ya kitabibu
Hitimisho
Jipu sehemu za siri kwa wanawake ni tatizo linaloweza kutokea kutokana na maambukizi ya ngozi, kuziba kwa tezi, nywele kuota ndani ya ngozi au hali zinazopunguza kinga ya mwili. Vijipu vidogo vinaweza kupona kwa uangalizi rahisi, lakini majipu makubwa mara nyingi huhitaji kutolewa usaha na wakati mwingine matibabu mengine.
Kutambua tofauti kati ya jipu, kifuko cha maji, vidonda vya magonjwa ya zinaa na matatizo mengine ya sehemu za siri ni muhimu ili kupata tiba sahihi. Mwanamke mwenye jipu linalorudia, lenye maumivu makali, homa au linaloongezeka anapaswa kupata tathmini ya mtaalamu wa afya badala ya kujitibu mwenyewe.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu jipu sehemu za siri kwa wanawake
1. Je, jipu sehemu za siri linaweza kupona lenyewe bila matibabu?
Baadhi ya vijipu vidogo vinaweza kupona vyenyewe hasa ikiwa mwili una kinga nzuri na maambukizi hayajaendelea sana. Kwa mfano, kijipu kidogo kinachotokana na nywele kuota ndani ya ngozi baada ya kunyoa kinaweza kupungua ndani ya siku kadhaa kwa kuweka eneo safi, kuepuka msuguano na kutumia kitambaa chenye maji ya uvuguvugu. Hata hivyo, si kila jipu linaweza kupona bila msaada wa kitabibu.
Tatizo ni kwamba jipu linapotengeneza mfuko mkubwa wa usaha ndani ya tishu, mwili wakati mwingine hushindwa kuondoa usaha huo wote. Katika hali hiyo, jipu linaweza kuendelea kukua, kuuma zaidi au kupasuka lenyewe bila kutoa usaha wote uliomo ndani. Mabaki ya usaha yanaweza kusababisha maambukizi kuendelea au kurudi tena baada ya muda.
Kwa hiyo, ukubwa wa jipu, eneo lilipo na dalili zinazoambatana nalo ni muhimu zaidi kuliko kusubiri muda tu. Kijipu kidogo kisicho na homa kinaweza kufuatiliwa kwa uangalifu, lakini jipu kubwa, lenye maumivu makali, linaloongezeka au linalosababisha kushindwa kukaa linahitaji tathmini ya mtaalamu wa afya.
2. Je, jipu sehemu za siri linaweza kusababishwa na uchafu au kutokuwa msafi?
Si sahihi kusema kuwa kila jipu linasababishwa na uchafu. Wanawake wengi hupata majipu licha ya kuwa na usafi mzuri wa mwili. Jipu hutokea hasa pale bakteria wanapoingia ndani ya ngozi au kuziba kwa tezi kunapotengeneza mazingira ya maambukizi.
Ngozi ya binadamu kwa kawaida ina bakteria wengi wanaoishi bila kusababisha madhara. Tatizo hutokea bakteria hao wanapoingia ndani ya ngozi kupitia michubuko midogo, mikwaruzo, jeraha baada ya kunyoa au maeneo yaliyopata msuguano mkubwa. Hivyo, hata mtu anayezingatia usafi anaweza kupata jipu.
Hata hivyo, mazingira yenye unyevunyevu mwingi, kutobadilisha nguo zenye jasho, kuvaa nguo zinazobana kwa muda mrefu au kutotibu maambukizi ya ngozi yanaweza kuongeza uwezekano wa bakteria kuzaliana. Lengo si kusafisha sehemu za siri kupita kiasi, bali kudumisha usafi wa kawaida bila kuharibu kinga ya asili ya ngozi.
3. Je, kunyoa nywele za sehemu za siri kunaweza kusababisha jipu?
Kunyoa nywele za sehemu za siri kunaweza kuongeza uwezekano wa kupata vijipu kwa baadhi ya wanawake, lakini si kwa kila mtu. Wakati wa kunyoa, wembe unaweza kusababisha michubuko midogo isiyoonekana kwenye ngozi. Michubuko hiyo inaweza kuwa njia ya bakteria kuingia ndani na kusababisha maambukizi.
Pia, baada ya kunyoa baadhi ya nywele zinaweza kukua kuelekea ndani ya ngozi badala ya kutoka nje. Hali hii huitwa nywele kuota ndani ya ngozi. Mwili unapoitambua nywele hiyo kama kitu kisicho kawaida, unaweza kusababisha uchochezi unaoweza kuishia kuwa kijipu au jipu.
Ili kupunguza hatari, mwanamke anayenyoa anashauriwa kutumia vifaa safi, kuepuka kunyoa kwa nguvu sana, kutotumia wembe wa mtu mwingine na kuepuka kunyoa eneo ambalo tayari lina muwasho au vidonda. Pia ni muhimu kufahamu kuwa kuacha nywele za sehemu za siri au kuzipunguza si tatizo la kiafya, na uchaguzi huo hutegemea mtu binafsi.
4. Je, jipu la sehemu za siri linaweza kuwa dalili ya ugonjwa wa zinaa?
Si lazima. Majipu mengi ya sehemu za siri husababishwa na bakteria wa kawaida wa ngozi, si magonjwa ya zinaa. Kwa mfano, bakteria aina ya Staphylococcus aureus wanaweza kusababisha majipu baada ya kuingia ndani ya ngozi kupitia jeraha dogo.
Hata hivyo, baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kusababisha vidonda au uvimbe unaoweza kuchanganywa na jipu. Kwa mfano, malengelenge ya sehemu za siri (herpes ya sehemu za siri) yanaweza kusababisha malengelenge yenye maumivu, wakati kaswende inaweza kusababisha kidonda ambacho mara nyingi hakiumi.
Kwa hiyo, mwanamke mwenye uvimbe au kidonda sehemu za siri hasa baada ya kufanya ngono bila kinga, kuwa na mwenzi mpya au kupata uchafu usio wa kawaida ukeni anapaswa kufanyiwa uchunguzi badala ya kudhani moja kwa moja kuwa ni jipu la kawaida. Kutambua chanzo sahihi husaidia kupata matibabu sahihi.
5. Je, jipu la tezi ya Batholini linaweza kurudi baada ya kutibiwa?
Ndiyo, jipu la tezi ya batholini linaweza kurudi kwa baadhi ya wanawake. Hii hutokea kwa sababu tatizo la msingi mara nyingi huwa ni kuziba kwa njia inayotoa ute kutoka kwenye tezi hiyo. Ikiwa njia hiyo itaziba tena baada ya matibabu, usaha unaweza kujikusanya upya.
Hatari ya kurudia huwa kubwa zaidi kwa wanawake ambao wamewahi kupata jipu la Baitolini hapo awali. Ndiyo maana kwa baadhi ya wagonjwa, daktari hufanya utaratibu maalumu kama kuweka katheta au upasuaji wa masupialaizesheni ili kutengeneza njia inayosaidia ute kutoka vizuri na kupunguza uwezekano wa kurudia.
Mwanamke anayepata uvimbe unaorudia upande mmoja wa mlango wa uke anapaswa kupata tathmini ya daktari badala ya kila mara kusubiri jipu likue. Hii husaidia kutofautisha kati ya sisti, jipu linalorudia na matatizo mengine yanayoweza kufanana.
6. Je, kutumia dawa za kienyeji kunaweza kutibu jipu sehemu za siri?
Hakuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi unaothibitisha kuwa dawa za kienyeji zinaweza kuondoa mfuko wa usaha uliokwisha kutengenezwa ndani ya tishu. Baadhi ya vitu vinavyopakwa kwenye ngozi vinaweza kupunguza muwasho au kutoa hisia ya nafuu kwa muda, lakini haviwezi kuondoa bakteria au usaha uliopo ndani ya jipu.
Tatizo la kutumia vitu visivyojulikana kwenye sehemu za siri ni kwamba ngozi ya eneo hilo ni nyeti sana. Baadhi ya dawa au mimea inaweza kusababisha muwasho, kuchoma ngozi au kuongeza uharibifu wa eneo lililoambukizwa.
Njia salama zaidi ni kutathmini ukubwa na aina ya jipu. Kijipu kidogo kinaweza kusaidiwa kwa hatua rahisi kama joto la uvuguvugu na usafi, lakini jipu kubwa linahitaji matibabu yanayolenga chanzo cha tatizo, hasa kutoa usaha pale unapohitajika.
7. Je, jipu sehemu za siri linaweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito?
Kwa kawaida, jipu la ngozi kwenye sehemu za nje za siri halisababishi ugumba kwa sababu halihusishi moja kwa moja mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi au ovari. Kwa mfano, kijipu kwenye labia au eneo lenye nywele hakizuii yai kutungwa au kijusi kukua.
Hata hivyo, baadhi ya maambukizi makubwa au yanayoachwa bila kutibiwa yanaweza kuenea kwenye maeneo ya ndani na kusababisha matatizo. Pia, baadhi ya hali zinazosababisha majipu yanayorudia, kama magonjwa fulani ya ngozi au maambukizi ya muda mrefu, yanaweza kuhitaji uchunguzi maalumu.
Kwa hiyo, si sahihi kuogopa kwamba kila jipu sehemu za siri litasababisha ugumba. Muhimu ni kutambua aina ya jipu, kulitibu ipasavyo na kutafuta huduma ikiwa kuna dalili zinazoonyesha maambukizi makubwa.
8. Kwa nini napata majipu sehemu za siri mara kwa mara?
Majipu yanayorudia yanaweza kuwa na sababu mbalimbali. Baadhi ya watu huwa na tabia ya kubeba bakteria kwenye ngozi au puani bila dalili, na bakteria hao wanaweza kusababisha majipu mara kwa mara wanapoingia kwenye ngozi iliyojeruhiwa.
Sababu nyingine zinazoweza kuchangia ni pamoja na kisukari, unene uliopitiliza, msuguano wa ngozi, kunyoa mara kwa mara, kuvurugika kwa kinga ya mwili au ugonjwa wa ngozi kama hidradenaitisi supurativa. Katika hali hii, vijipu hurudia kwenye maeneo yenye msuguano na vinaweza kuacha makovu.
Mwanamke anayepata majipu mara nyingi hapaswi kupewa antibiotiki kila mara bila kutafuta chanzo.
Uchunguzi wa sababu inayosababisha kurudia ni muhimu ili kupata suluhisho la muda mrefu na kupunguza madhara kama makovu au maambukizi makubwa.
9. Je, ninaweza kufanya tendo la ndoa nikiwa na jipu sehemu za siri?
Inashauriwa kusubiri hadi jipu lipone, hasa kama lina maumivu, lina usaha au lipo karibu na mlango wa uke. Msuguano wakati wa tendo la ndoa unaweza kuongeza maumivu, kuchelewesha uponaji na wakati mwingine kusababisha eneo lililoathirika kuumia zaidi.
Pia, ikiwa jipu linasababishwa na maambukizi ambayo hayajajulikana, kufanya tendo la ndoa bila uchunguzi kunaweza kufanya iwe vigumu kutambua chanzo halisi cha tatizo, hasa kama kuna uwezekano wa maambukizi yanayohusiana na ngono.
Baada ya jipu kupona na ngozi kurudi katika hali ya kawaida, mwanamke anaweza kurudia tendo la ndoa. Ikiwa jipu lilikuwa la Baitolini au linarudia mara kwa mara, ni vizuri kupata ushauri wa mtaalamu kabla ya kuendelea ikiwa bado kuna uvimbe au maumivu.
10. Je, jipu kubwa sehemu za siri linaweza kuwa hatari kwa maisha?
Mara nyingi majipu ya sehemu za siri hutibiwa bila matatizo makubwa, lakini jipu kubwa linaweza kuwa hatari ikiwa maambukizi yataenea. Hatari huwa kubwa zaidi kwa wanawake wenye kisukari, kinga dhaifu au wale wanaochelewa kupata matibabu.
Maambukizi yanaweza kusambaa kwenye ngozi inayozunguka jipu na kusababisha selulaitisi, au katika hali nadra sana yanaweza kuingia kwenye damu na kusababisha sepsisi, ambayo ni hali hatari inayohitaji matibabu ya haraka.
Dalili zinazohitaji kwenda hospitali haraka ni pamoja na homa kali, kutetemeka, udhaifu mkubwa, maumivu yanayoongezeka haraka, wekundu unaosambaa, harufu mbaya ya usaha au kuhisi mgonjwa sana kwa ujumla.
Kwa hiyo, jipu sehemu za siri halipaswi kupuuzwa ikiwa linaongezeka, linauma sana au linaambatana na dalili za mwili mzima. Kupata huduma mapema husaidia kuzuia matatizo na kuharakisha kupona.
11. Je, kutokwa na vijipu sehemu za siri vinaweza kupelekea kutoshika ujauzito?
Kwa kawaida, vijipu sehemu za siri (jipu/majipu) havisababishi mwanamke kushindwa kupata ujauzito (ugumba). Vijipu vingi hutokea kwenye ngozi ya nje ya sehemu za siri kama shavu la uke (labia majora), sehemu yenye nywele au maeneo yanayopata msuguano. Hali hii mara nyingi huhusisha ngozi na tishu zilizo juu ya mfumo wa uzazi, hivyo haiathiri moja kwa moja ovulation (kutolewa kwa yai), mirija ya uzazi (Mirija ya Falopia au mfuko wa uzazi.
Pia ni muhimu kutofautisha vijipu vya ngozi na maambukizi ya ndani ya mfumo wa uzazi. Baadhi ya maambukizi yanayoweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito, kama ugonjwa wa uchochezi wa nyonga (PID), mara nyingi husababishwa na maambukizi yanayoanzia kwenye mlango wa kizazi au uke na kupanda kwenda kwenye mfuko wa uzazi na mirija ya uzazi. PID inaweza kusababisha kuziba kwa mirija ya Falopia, lakini si sawa na kijipu cha ngozi kwenye sehemu za nje za siri.
Kwa hiyo, mwanamke mwenye vijipu sehemu za siri asiogope kwamba atakuwa tasa. Lakini anapaswa kutafuta ushauri wa mtaalamu ikiwa vijipu:
Vinatokea mara kwa mara
Vinakuwa vikubwa au vinauma sana
Vinaacha makovu
Vinaambatana na homa
Vinatoa usaha mwingi
Vinatokea pamoja na maumivu ya ndani ya nyonga au uchafu usio wa kawaida ukeni
Utambuzi sahihi husaidia kutofautisha kati ya tatizo la kawaida la ngozi na matatizo mengine ambayo yanaweza kuhitaji matibabu maalumu.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
29 Julai 2026, 11:41:00
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada hii:
Stevens DL, Bisno AL, Chambers HF, Dellinger EP, Goldstein EJC, Gorbach SL, et al. Practice guidelines for the diagnosis and management of skin and soft tissue infections: 2014 update by the Infectious Diseases Society of America. Clin Infect Dis. 2014;59(2):e10-e52. doi:10.1093/cid/ciu296.
Raff AB, Kroshinsky D. Cellulitis: a review. JAMA. 2016;316(3):325-337. doi:10.1001/jama.2016.8825.
May AK. Skin and soft tissue infections. Surg Clin North Am. 2009;89(2):403-420. doi:10.1016/j.suc.2008.09.010.
Sartelli M, Guirao X, Hardcastle TC, Kluger Y, Boermeester MA, Raşa K, et al. 2018 WSES/SIS-E consensus conference: recommendations for the management of skin and soft-tissue infections. World J Emerg Surg. 2018;13:58. doi:10.1186/s13017-018-0219-9.
Talan DA, Krishnadasan A, Gorwitz RJ, Fosheim GE, Limbago B, Albrecht V, et al. Comparison of Staphylococcus aureus from skin and soft-tissue infections and nasal colonization in the emergency department setting. Clin Infect Dis. 2011;53(2):144-149. doi:10.1093/cid/cir308.
Lee LK, Dinneen MD. Management of Bartholin's cyst and abscess. BMJ. 2019;364:l168. doi:10.1136/bmj.l168.
Wechter ME, Wu JM, Marzano D, Haefner H, Geller EJ, Myers ER. Management of Bartholin duct cysts and abscesses: a systematic review. Obstet Gynecol Surv. 2009;64(6):395-404. doi:10.1097/OGX.0b013e3181a3a4f2.
American College of Obstetricians and Gynecologists. ACOG Practice Bulletin No. 215: Vaginitis in nonpregnant patients. Obstet Gynecol. 2020;135(1):e1-e17.
Centers for Disease Control and Prevention. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1-187. doi:10.15585/mmwr.rr7004a1.
Alikhan A, Lynch PJ, Eisen DB. Hidradenitis suppurativa: a comprehensive review. J Am Acad Dermatol. 2009;60(4):539-561. doi:10.1016/j.jaad.2008.11.911.
Zouboulis CC, Desai N, Emtestam L, Hunger RE, Ioannides D, Juhász I, et al. European S1 guideline for the treatment of hidradenitis suppurativa/acne inversa. J Eur Acad Dermatol Venereol. 2015;29(4):619-644. doi:10.1111/jdv.12966.
World Health Organization. WHO guidelines for the treatment of Treponema pallidum (syphilis). Geneva: World Health Organization; 2016.
World Health Organization. WHO guidelines for the treatment of sexually transmitted infections. Geneva: World Health Organization; 2021.
Lipsky BA, Dryden M, Gottrup F, Nathwani D, Seaton RA, Stryja J. Antibiotic therapy for diabetic foot infections. Diabetes Metab Res Rev. 2016;32(Suppl 1):45-51. doi:10.1002/dmrr.2739.
Pappas PG, Kauffman CA, Andes DR, Clancy CJ, Marr KA, Ostrosky-Zeichner L, et al. Clinical practice guideline for the management of candidiasis: 2016 update by the Infectious Diseases Society of America. Clin Infect Dis. 2016;62(4):e1-e50. doi:10.1093/cid/civ933.
Kessous R, Sheiner E. Clinical significance of Bartholin gland cysts and abscesses in women of reproductive age. Eur J Obstet Gynecol Reprod Biol. 2013;170(2):347-350. doi:10.1016/j.ejogrb.2013.07.013.
Omole F, Simmons BJ, Hacker Y. Management of Bartholin's duct cyst and gland abscess. Am Fam Physician. 2003;68(1):135-140.
Raff AB, Kroshinsky D. Cellulitis: a review. JAMA. 2016;316(3):325-337.
Stevens DL, Bryant AE. Necrotizing soft-tissue infections. N Engl J Med. 2017;377(23):2253-2265. doi:10.1056/NEJMra1600673.
Centers for Disease Control and Prevention. Methicillin-resistant Staphylococcus aureus (MRSA): General Information. Atlanta: CDC; updated resources.
