Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin L, MD, Dkt. Adolf S, MD
29 Agosti 2021 08:12:36
Kukojoa mara kwa mara usiku
Tatizo la kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku huongezeka kwa jinsi umri wa mtu unavyoongezeka kufikia mtu 1 kati ya 3 baada ya kutimiza miaka 30. Visababishi vikuu ni mwili kutengeneza mkojo mwingi wakati wote au usiku tu na uwezo mdogo wa kibofu kutunza au kutoa mkojo. Ongea na mtaalamu wa afya kupata tiba inayoendana na tatizo lako.
Mfumo wa mkojo unafanyaje kazi?
Mfumo wa mkojo huwa na ogani zinazofanya kazi ya kutengeneza, kuhifadhi na kutoa mkojo nje ya mwili. Mkojo hutengenezwa pale figo inapochuja damu ili kutoa uchafu nje ya mwili. Kwa kawaida figo hutengeneza lita moja na nusu hadi mbili za mkojo kwa siku na kiwango kwa mtoto huwa pungufu ya hiki.
Mkojo unapotengenezwa kwenye figo husafirishwa kwenda kwenye kibofu kupitia mrija wa yureta ili kuhifadhiwa kabla ya kutoka nje ya mwili kupitia mrija wa yurethra
Ubongo na kibofu cha mkojo vimeunganishwa kwa mishipa ya fahamu inayotuma taarifa kuhusu hali ya mkojo kwenye kibofu. Ubongo hutambua kibofu kina mkojo kiasi gani na wakati gani wa kutoa mkojo huo baada ya kujaa kwa kupokea taarifa kupitia mishipa ya fahamu.
Misuli ya sakafu ya nyonga hushikiria kibofu katikaa sehemu yake. Misuli iliyo karibu na shingo ya kibofu hufungwa ili kushikiria mkojo ndani ya kibofu.mirija inayotoa mkojo nje ya kibofu pia imetengenezwa kwa misuli yenye uwezo wa kuruhusu au kuzuia mkojo kutoka mpaka pale ubongo wako utakaporuhusu
Mara unapokuwa tayari kukojoa, ubongo hutuma taarifa kwenye kibofu cha mkojo ili misuli ya kiwiliwili cha kibofu isinyae kusukuma mkojo, na misuli ya shingo ya kibofu ilegee ili kufungua njia ya mkojo. Tendo hili husababisha mkojo kutoka nje ya mwili kwa nguvu.
Dalili
Kama unaamka ili kukojoa mara mbili au zaidi wakati wa usiku, hii ni dalili ya kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku na si kawaida kwa binadamu kwa kuwa unapaswa kulala angalau masaa 6 hadi 8 bila kupata haja ya kwenda kojoa wakati wa usiku.
Kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku huathiri usingizi na ubora wa maisha yako. Watu wengi hawawezi fanya kazi vema kama hawatapata muda mzuri wa kulala wakati wa usiku.
Visababishi
Kumbuka kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku ni dalili tu ya jambo fulani linaloendelea ndani ya mwili. Vitu vinavyoweza kupelekea kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku ni;
Tabia ya kutumia vinywaji vyenye kafeini na kileo au maji mengi kabla ya kulala
Matumizi ya dawa aina fulani zinazoongeza uzalishaji wa mkojo
Magonjwa yanayoathiri uwezo wa kubofu kutunza au kutoa mkojo
Madhaifu ya kulala kama vile kukosa usingizi na kusimama kwa upumuaji wakati umelala
Tabia
Tabia zinazoweza kusababisha kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku ni;
Kunywa vinywaji vingi kabla ya kulala haswa vinywaji vyenye kilevi na kafeini
Tabia yako ya kukojoa usiku( kama umeufunza mwili wako kuamka na kukojoa usiku hata kama huna mkojo, utajikuta unaamka muda ule kwenda kukojoa)
Kunywa dawa muda mbaya haswa zile zinazoongeza uzalishaji wa mkojo mfano
Dawa zinazoongeza uzalishaji wamkojo wakati wa usiku
Dawa za kupunguza maji
Chlorthalidone (Hygroton)
Chlorothiazide (Diuril)
Hydrochlorothiazide or HCTZ (Esidrix, Hydrodiuril, Microzide)
Indapamide (Lozol)
Metolazone (Mykrox, Zaroxolyn)
Amiloride (Midamor)
Bumetanide (Bumex)
Furosemide (Lasix)
Spironolactone (Aldactone)
Torsemide (Demadex)
Triamterene (Dyrenium)
Dawa jamii ya cardiac glycoside
Digoxin (Lanoxicaps, Lanoxin, Digibind)
Digitoxin (Crystodigin)
Dawa zingine
Demeclocycline
Lithium
Methoxyflurane
Phenytoin
Propoxyphene
Vitamin D kwa wingi
Magonjwa
Magonjwa yanayopelekea kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku ni;
Kisukari
Shinikizo la juu la damu
Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu
Mawe kwenye kibofu cha mkojo
Kibofu kinachofanya kazi sana
Kuziba njia ya mkojo kutokana na tezi kuwa kubwa
Kudondoka kwa uke
Komahedhi
Kujifungua
Kudondoka kwa
Kudondoka kwa via vya ndani ya nyonga
Kukua kwa tezi duma
Sindromu ya kutotulia kwa miguu
Kuvimba kwa miguu
Ugonjwa wa Interstitial cystitis
Kupungua kwa uwezo wa kibofu kutunza mkojo
Mwili kuzalisha mkojo mwingi wakati wa usiku
Utambuzi
Mtaalamu wa afya atataka kufahamu kuhusu tatizo lako kwa kukuuliza maswali pamoja na kufanya vipimo vya awali ili kuchunguza mwili. Utaombwa pia kurekodi tabia yako ya kukojoa na kiasi cha na nini unatumia usiku ili kusaidia tambua kisababishi. Kama mtaalamu wa afya ameamua kuchunguza kwa kutumia vipimo
Vipimo
Vipimo ambavyo unaweza fanyiwa miongoni mwake ni;
Kipimo cha kuotesha mkojo ili kuangalia kama una maambukizi kwenye mkojo na maambukizi ya bakteria gani
Kipimo cha urinalysis ili kuangalia kama una maambukizi kwenye mkojo
Vipimo vya damu kuangalia utendaji kazi wa tezi thyroid, kiwango cha kolestro, upungufu wa damu, kisukari na matatizo mengine yanayoweza sababisha kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku
Kipimo cha kupima uwezo wa kibofu kutunza mkojo baada ya kukojoa
Kipimo cha Cystoscopy ili kuangalia kama kuna uvimbe au visababishi vingine kwenye njia ya mkojo inavyopelekea ukojoe mara kwa mara
Matibabu
Kubadili mtindo wa maisha
Matibabu ya tatizo la kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku huhusisha dawa na kubadili mtindo wa maisha;
Ili kubadili mtindo wa maisha;
Dhibiti kiasi cha vinywaji unavyotumia usiku. Pendelea kunywa maji mchana na uzuia kunywa maji masaa 2 hadi 4 kabla ya kulala. Usitumie vyakula vyenye kafein au pombe kabla ya kulala mfano soda, kahawa na chai
Kama unatumia dawa za kupunguza maji mwilini, kunywa dawa hizo angalau masaa 6 kabla ya kulala, hii itapunguza kukojoa mara kwa mara usiku
Nyanyua miguu yako juu wakati umelala au tumia soksi mgandamizo kama miguu yako imejaa maji. Hii itasaidia kuondoa maji yaliyovia kwenye miguu na kupunguza kojoa sana wakati wa usiku.
Lala muda mfupi wakati wa mchana. Kama hupati usingizi wa kutosha wakati wa usiku kutokana na kukojoa mara kwa mara, pata vipindi vifupi vya kulala wakati wa mchana kwa afya ya mwili wako lakini usilale muda mrefu kiasi cha kukosa usingizi wakati wa usiku.
Matibabu ya dawa
Kubadili mfumo wa maisha pekee hakusaidii kukabiliana na tatizo la kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku hivyo unapaswa kutumia baadhi ya dawa kama utakavyoshauriwa na daktari wako. Hata hivyo si kila mtu pia atafaidika kwa sawa na si kila dawa inaweza mfaa mtu yoyote lakini ni vema kuzifahamu.
Dawa zinazopunguza uzalishaji wa mkojo kama Desmopressin
Dawa za kutibu matizo ya misuli ya kibofu kama Darifenacin, Oxybutynin, Tolterodine, Trospium Chloride au Solifenacin
Dawa za kupunguza shinikizo la juu la damu( kwa wagonjwa wenye tatizo hilo) mfano Bumetanide na Furosemide
Tiba inayolenga kisababishi
Kama kisababishi kitatibiwa, tatizo la kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku litaisha mfano kupata matibabu ya;
Kisukari
Shinikizo la juu la damu
Kuferi kwa moyo
Tezi dume iliyokuwa
Kusimama kwa upumuaji wakati wa usiku
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
8 Oktoba 2021 04:52:54
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Diuretics (Water Pills) for High Blood Pressure. https://www.webmd.com/hypertension-high-blood-pressure/guide/diuretic-treatment-high-blood-pressure. Imechukuliwa 29.08.2021
2. NHS. Organ prolapse. https://www.nhs.uk/conditions/pelvic-organ-prolapse/#. Imechukuliwa 29.08.2021
3. Urinary frequency. Merck Manual Professional Version. http://www.merckmanuals.com/professional/genitourinary-disorders/symptoms-of-genitourinary-disorders/urinary-frequency. Imechukuliwa 29.08.2021
4. Rakel RE, et al. Urinary tract disorders. In: Textbook of Family Medicine. 9th ed. Philadelphia, Pa.: Elsevier Saunders; 2016. http://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 29.08.2021
5. Nocturia. https://my.clevelandclinic.org/health/diseases/14510-nocturia. Imechukuliwa 29.08.2021
6. National Association for Continence. Nocturia. https://www.nafc.org/nocturia. Imechukuliwa 29.08.2021
7. Marinkovic SP, et al.Managing Noctura. BMJ 2004;328:1063.
8. SleepFoundation.org. Nocturia or Frequent Urination at Night. https://www.sleepfoundation.org/articles/nocturia-or-frequent-urination-night.Imechukuliwa 29.08.2021
9. American Urological Association,Urology Care Foundation. Nocturia. https://www.urologyhealth.org/urologic-conditions/nocturia. Imechukuliwa 29.08.2021