top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Kupoteza fahamu kwa muda mrefu: Mwongozo kamili
shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.

21 Februari 2026, 16:40:57

Kupoteza fahamu kwa muda mrefu: Mwongozo kamili

Kupoteza fahamu kwa muda mrefu ikifahamika pia kama Koma ni hali inayotia hofu kwa wagonjwa na ndugu, na mara nyingi hutokea ghafla bila kutarajiwa. Watu wengi huchanganya hali hii na usingizi wa kawaida au kuzimia kwa muda mfupi, ilhali kiuhalisia ni tatizo kubwa la kitabibu linalohitaji uchunguzi na matibabu ya haraka.


Makala hii inaeleza kwa lugha rahisi maana ya koma (kuzimia kwa muda mrefu), sababu zake, dalili zake, na hatua zinazopaswa kuchukuliwa mapema ili kulinda ubongo na maisha ya mgonjwa.


Kumbuka: Makala hii imetumia neno Koma na Kuzimia kwa muda mrefu ikimaanisha maneno yanayotumika kama mbadala.


Kuzimia kwa muda mrefu ni nini?

Kupoteza fahamu kwa muda mrefu ni hali ya kupoteza fahamu kwa kipindi kirefu ambapo mgonjwa huwa hai lakini hawezi kuamka, kuongea, au kuitikia vichocheo vya kawaida kama sauti, mguso au maumivu makali.


Neno koma hutumika kumaanisha hali hii na limetokana na neno coma ambalo asili yake ni Kigiriki “kōma” likimaanisha usingizi mzito usio wa kawaida.


Tofauti na usingizi wa kawaida, mtu aliye kwenye koma:

  • Hafumbui macho kwa hiari

  • Hawezi kuongea

  • Haitikii maelekezo

  • Hahitaji nguvu kuendelea kupumua au huweza kuhitaji mashine


Ni hali ya dharura inayohitaji matibabu ya haraka hospitalini.


Koma hutokea vipi?

Koma hutokea pale sehemu za ubongo zinazodhibiti fahamu (Koteksi ya serebramu na mfumo wa uamshaji wa retikula) zinaposhindwa kufanya kazi.

Hali hii hutokea kwa njia mbili kuu:

  1. Uharibifu wa moja kwa moja wa ubongomfano: kiharusi, ajali ya kichwa, uvimbe wa ubongo

  2. Mabadiliko ya kemikali mwilini (koma ya kimetaboli/Koma ya usumu)mfano: sukari kushuka sana au kupanda sana, sumu, upungufu wa oksijeni


Visababishi vya kupoteza fahamu kwa muda mrefu


i. Magonjwa ya ubongo

  • Kiharusi

  • Uvimbe kwenye ubongo

  • Jeraha la kichwa

  • Kifafa kikali

  • Maambukizi ya ubongo au uti wa mgongo (meninjaitisi na enkefalaitisi)


ii. Matatizo ya kimetaboliki

  • Sukari kushuka au kupanda sana

  • Upungufu wa oksijeni mwilini

  • Kuongezeka kwa sodium kwenye damu

  • Kuongezeka kwa calcium kwenye damu

  • Kushindwa kwa figo au ini

  • Mshtuko wa mwili


iii. Sumu na dawa

Koma inaweza kusababishwa na matumizi mabaya au sumu ya:

  • Pombe kupita kiasi

  • Dawa za kulevya

  • Dawa za usingizi (benzodiazepini, barbiturate)

  • Dawa za maumivu kali (opioidi)

  • Dawa za degedege

  • Antidepressants (tricyclics)

  • Antihistamines

  • Lithium

  • Digoxin

  • Insulin kupita kiasi

  • Sumu ya metali nzito

  • Organophosphates

  • Kemikali za petroli (haidrokaboni)


iv. Magonjwa ya moyo na mzunguko wa damu

  • Mapigo ya moyo kusimama

  • Kushindwa kwa moyo

  • Shinikizo la damu kali au la chini sana

  • Mshituko


Dalili za mtu aliye kwenye koma

  • Kutopata fahamu

  • Kutoitikia sauti au maumivu

  • Kupumua kwa shida au kwa mashine

  • Macho kutofunguka

  • Degedege wakati mwingine

  • Mwili kuwa baridi au moto kupita kawaida


Aina za kupoteza fahamu kwa muda mrefu

Kupoteza fahamu kwa muda mrefu hutofautiana kwa kina chake kulingana na kiwango cha uharibifu wa ubongo. Madaktari hutathmini hali hii kwa kuangalia mwitikio wa macho, sauti, maumivu na uwezo wa kupumua. Jedwali lifuatalo linaonyesha tofauti kuu za kitabibu kati ya viwango mbalimbali vya fahamu.


Jedwali 1: Aina za kupoteza fahamu kwa muda mrefu(Koma)

Aina ya hali

Mwitikio wa mgonjwa

Hali ya macho

Kupumua

Uwezekano wa kupona

Koma nyepesi

Huitikia maumivu kwa kusogeza viungo

Hayafunguki kwa hiari

Karibu kawaida

Mzuri kama chanzo kinatibika mapema

Koma ya kati

Refleksi tu (kujikunja/kukaza misuli)

Hayafunguki

Huwa si thabiti

Wastani, huhitaji uangalizi wa karibu

Koma nzito

Hakuna mwitikio

Hayafunguki kabisa

Mara nyingi mashine husaidia

Mdogo zaidi

Hali ya uhai wa mwili bila utambuzi wa mazingira

Hakuna utambuzi wa mazingira

Hufumbuka na kufunga

Hupumua mwenyewe

Mdogo, huweza kudumu muda mrefu

Hali ya fahamu kidogo

Majibu madogo yasiyo thabiti

Hufuatilia kwa macho wakati mwingine

Hupumua mwenyewe

Bora kuliko vegetative state

Kifo cha ubongo

Hakuna kabisa

Hayaitikii mwanga

Hawezi kupumua bila mashine

Hakuna uwezekano wa kupona


Muhimu: Kadri mgonjwa anavyoanza kuonyesha mwitikio wa macho au mwili, ndivyo dalili nzuri ya kuanza kupona inavyoongezeka. Matibabu ya mapema huboresha matokeo.


Uchunguzi hospitalini

Madaktari hufanya vipimo kutafuta sababu:

  • Kipimo cha fahamu (Glasgow Coma Scale)

  • Sukari ya damu

  • CT scan au MRI ya ubongo

  • Vipimo vya sumu

  • Vipimo vya damu

  • EEG


Matibabu ya Koma

Matibabu hutegemea chanzo:

  • Kuweka mashini ya upumuaji

  • Kurekebisha sukari

  • Dawa za kifafa

  • Antibatotiki kwa maambukizi

  • Upasuaji wa ubongo

  • Kuondoa sumu mwilini

Lengo kuu ni kuokoa ubongo usiharibike.


Madhara ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu

Kupoteza fahamu kwa muda mrefu kunaweza kuathiri ubongo na viungo vingine vya mwili, hasa kama oksijeni au damu ilikosekana kwa muda. Madhara hutegemea chanzo cha tatizo, muda uliopita kabla ya matibabu, na umri wa mgonjwa.

i. Kupooza

Uharibifu wa sehemu za ubongo zinazodhibiti misuli unaweza kusababisha:

  • Kupooza upande mmoja wa mwili

  • Udhaifu wa mikono au miguu

  • Kushindwa kutembea au kushika vituBaadhi ya wagonjwa hupata nafuu kwa mazoezi ya viungo (physiotherapy), lakini wengine hubaki na udhaifu wa kudumu.


ii. Kupoteza kumbukumbu na matatizo ya akili

Ubongo unaweza kushindwa kuhifadhi au kukumbuka taarifa vizuri:

  • Kusahau watu au matukio

  • Kushindwa kuzingatia

  • Kuchanganyikiwa

  • Mabadiliko ya tabia au hasira harakaHali hii huitwa uharibifu wa utambuzi.


iii. Ulemavu wa kudumu

Baadhi ya wagonjwa hubaki na utegemezi wa msaada wa wengine katika maisha ya kila siku:

  • Kushindwa kuzungumza vizuri

  • Kushindwa kula bila kusaidiwa

  • Kutotembea

  • Kuhitaji huduma ya muda mrefu


4. Kifo

Ikiwa ubongo uliathirika sana au chanzo hakikutibiwa mapema, kuzimia kwa muda mrefu kunaweza kusababisha kifo.


Wakati wa kumkimbiza mgonjwa hospitali

Mtu akipoteza fahamu hata kwa dakika chache ni dharura.

Piga huduma ya dharura mara moja ikiwa:

  • Ameanguka na hajitambui

  • Haongei

  • Hawezi kuamka

  • Ana degedege

  • Ameumia kichwa


Maswali yanayoulizwa Mara kwa Mara

1. Je mtu aliyezimia kwa muda mrefu husikia watu wanaoongea?

Ndiyo, wakati mwingine ubongo bado hupokea sauti hata kama mgonjwa hawezi kufungua macho au kujibu. Hii hutokea kwa sababu sehemu za kusikia zinaweza kuwa zinafanya kazi lakini sehemu za kujibu zimeathirika. Ndiyo maana madaktari hupendekeza ndugu kuzungumza na mgonjwa hospitalini, kwani inaweza kusaidia kuchochea ubongo na kuharakisha kupona.

2. Kuzimia kwa muda mrefu hudumu kwa muda gani?

Muda hutofautiana sana kulingana na sababu na kiwango cha madhara ya ubongo.Inaweza kudumu:

  • Masaa machache (mfano sukari kushuka)

  • Siku kadhaa

  • Wiki au miezi (baada ya ajali ya kichwa au kiharusi kikubwa)

Kadri muda unavyoongezeka, ndivyo uwezekano wa madhara ya kudumu unavyoongezeka, hivyo matibabu ya mapema ni muhimu.

3. Je mtu anaweza kupona kabisa baada ya kuzimia kwa muda mrefu?

Ndiyo inawezekana, hasa kama chanzo kilikuwa kinarekebishika mapema kama:

  • Sukari kushuka au kupanda sana

  • Sumu au dawa

  • Upungufu wa oksijeni uliorekebishwa haraka

Lakini kama ubongo uliathirika sana (mfano baada ya kukosa hewa muda mrefu), mgonjwa anaweza kupata ulemavu wa kudumu.

4. Kuzimia kwa muda mrefu ni sawa na kifo cha ubongo?

Hapana.

  • Kuzimia kwa muda mrefu: ubongo bado una shughuli fulani na mtu anaweza kupona.

  • Kifo cha ubongo: ubongo umeacha kufanya kazi kabisa na hakuna uwezekano wa kuamka.

Hizi ni hali mbili tofauti kitabibu.

5. Ni dalili gani huja kabla ya kuzimia kwa muda mrefu?

Mara nyingi mwili huonyesha dalili za tahadhari kabla ya kupoteza fahamu kabisa, kama:

  • Kizunguzungu kikali

  • Kuchanganyikiwa

  • Usingizi mwingi usio wa kawaida

  • Kuongea bila mpangilio

  • Maumivu makali ya kichwa

  • Degedege

  • Kupumua kwa shida

Dalili hizi zinahitaji kupelekwa hospitali mapema ili kuzuia hali kuwa mbaya.

6. Je pombe inaweza kusababisha kuzimia kwa muda mrefu?

Ndiyo. Kunywa pombe nyingi kupita kiasi kunaweza kushusha kiwango cha fahamu na hata kuzuia kupumua. Hali hii huitwa usumu wa pombe na ni dharura inayoweza kusababisha kifo bila matibabu ya haraka.

7. Mtu aliyezimia kwa muda mrefu hula au hunywa vipi?

Hawezi kula kwa kawaida. Hospitalini hupewa lishe kupitia:

  • Mirija ya puani kwenda tumboni

  • Mirija ya mishipani

  • Lishe maalum ya kitabibu

Hii husaidia mwili kuendelea kupata nguvu wakati ubongo unatibiwa.

8. Je familia inaruhusiwa kuzungumza na mgonjwa aliyepoteza fahamu kwa muda mrefu?

Ndiyo, na inashauriwa. Sauti za watu wanaowafahamu zinaweza kuchochea ubongo. Wagonjwa wengine huonyesha nafuu polepole wanaposikia sauti za ndugu.

9. Ni nani yuko hatarini kupata kuzimia kwa muda mrefu?

Watu wenye hatari kubwa ni:

  • Wagonjwa wa kisukari

  • Wenye shinikizo la damu

  • Wenye kifafa

  • Waliopata ajali ya kichwa

  • Waliotumia pombe au dawa za kulevya

  • Wazee wenye magonjwa ya moyo au ubongo

Kudhibiti magonjwa haya hupunguza hatari.

10. Nifanye nini nikiona mtu amepoteza fahamu?

Chukua hatua hizi haraka:

  1. Mlaze alalie ubavu

  2. Hakikisha anapumua

  3. Ondoa vitu vinavyoweza kumzuia hewa

  4. Usimpe chakula wala maji

  5. Mpeleke hospitali au piga huduma ya dharura mara moja

Kupoteza fahamu ni dharura ya kitabibu.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeandikwa:

21 Februari 2026, 16:40:57

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada

Posner JB, Saper CB, Schiff ND, Plum F. Plum and Posner's Diagnosis of Stupor and Coma. 5th ed. New York: Oxford University Press; 2019.

Adams RD, Victor M, Ropper AH, Samuels MA, Klein JP. Adams and Victor’s Principles of Neurology. 11th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2019.

Jameson JL, Fauci AS, Kasper DL, Hauser SL, Longo DL, Loscalzo J. Harrison’s Principles of Internal Medicine. 21st ed. New York: McGraw-Hill; 2022.

Simon RP, Greenberg DA, Aminoff MJ. Clinical Neurology. 11th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2021.

Daroff RB, Jankovic J, Mazziotta JC, Pomeroy SL. Bradley’s Neurology in Clinical Practice. 8th ed. Philadelphia: Elsevier; 2021.

Wijdicks EFM. The diagnosis of brain death. N Engl J Med. 2001;344(16):1215-21.

Teasdale G, Jennett B. Assessment of coma and impaired consciousness: A practical scale. Lancet. 1974;2(7872):81-4.

World Health Organization. Neurological disorders: public health challenges. Geneva: WHO Press; 2006.

American Diabetes Association. Hyperglycemic crises in diabetes. Diabetes Care. 2022;45(Suppl 1):S109-S118.

Greer DM, Shemie SD, Lewis A, Torrance S, Varelas P, Goldenberg FD, et al. Determination of brain death/death by neurologic criteria. Neurology. 2020;94(16):705-13.

bottom of page