top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Kutokwa majimaji meupe bila maumivu uumeni
shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.

14 Februari 2026, 08:16:19

Kutokwa majimaji meupe bila maumivu uumeni

Kutokwa na majimaji meupe au ute kutoka kwenye uume ni hali inayoweza kumtia hofu mwanaume, hata kama haileti maumivu yoyote. Ingawa mara nyingi hali hii huhusishwa na maambukizi ya magonjwa ya ngono, kuna wakati inaweza kutokea kutokana na sababu zisizohusiana na ngono. Uelewa sahihi kuhusu chanzo, dalili zinazoweza kuambatana, na lini kumwona daktari ni muhimu kwa ajili ya matibabu sahihi.


Maumbile ya kawaida ya majimaji kutoka kwenye uume

Kwa kawaida, mwanaume anaweza kuona ute mdogo wa kiasili kutoka kwenye uume, hasa wakati wa msisimko wa kimapenzi. Ute huu ni sehemu ya majimaji ya tezi zinazosaidia kulainisha njia ya mkojo na uume kabla ya kutoa shahawa. Hata hivyo, ikiwa ute unatoka bila msisimko, una rangi tofauti (nyeupe, kijivu au kijani), una harufu, au unatokea mara kwa mara, basi ni dalili ya tatizo linalohitaji uchunguzi wa kitaalamu.


Visababishi vya kutokwa na majimaji meupe kutoka kwenye uume bila maumivu


1. Maambukizi ya njia ya mkojo

Hii inaweza kusababisha kutokwa na ute mweupe au wa kijivu, japo maumivu huwa kawaida. Hata hivyo, baadhi ya maambukizi huweza kutokea bila maumivu mwanzoni.


2. Magonjwa ya zinaa

Klamidia: Husababisha ute usio na harufu mkali, mara nyingi mweupe au kijivu, na hali ya kutokwa na majimaji bila maumivu inaweza kutokea.


Kisonono(Gono): Ingawa huleta maumivu kwa kawaida, mwanzo wa maambukizi unaweza kuwa kimya.


Maikoplasma genitaliamu: Ni vimelea vya zinaa ambavyo huweza kusababisha ute usioambatana na maumivu.


Magonjwa ya zinaa

Hii ni kuvimba kwa mrija wa mkojo (urethra) bila kuwepo kwa vimelea vya gonorrhea. Inaweza kusababishwa na:

  • Klamidia

  • Mycoplasma genitalium

  • Ureaplasma urealyticum

  • Virusi kama herpes simplex


4. Uvimbe homa wa tezi dume (Prostataitis)

Ingawa huambatana zaidi na maumivu ya nyonga au mgongo wa chini, baadhi ya wanaume wanaweza kupata ute mweupe usio na maumivu kutoka kwenye uume.


5. Mzio au muingiliano na kemikali

Matumizi ya sabuni zenye kemikali kali, vilainishi au kondomu zenye kemikali maalum huweza kuathiri urethra na kusababisha ute.


Dalili za kuambatana zinazoweza kutokea

Hata kama hakuna maumivu, mgonjwa anaweza pia kuwa na:

  • Kujisikia haja ya kukojoa mara kwa mara

  • Kuwashwa kwenye uume au eneo la korodani

  • Harufu isiyo ya kawaida kutoka kwenye uume

  • Kuvimba kwa mrija wa mkojo

  • Kuhisi kama kuna kitu kinatoka kila wakati kwenye uume

  • Ute unaonekana asubuhi zaidi au baada ya kukojoa


Vipimo na uchunguzi

Mgonjwa anapofika kliniki au hospitali, daktari anaweza kupendekeza:

  1. Uchunguzi wa mkojo (Uchunguzi wa mkojo na uoteshaji wa vimelea kwenye mkojo – kutambua uwepo wa maambukizi ya kawaida au ya vimelea vya magonjwa ya zinaa.

  2. Uchunguzi wa sampuli ya ute kutoka kwenye uume – hupimwa kwa kutumia darubini au kufanyiwa kipimo cha PCR kutambua vimelea kama chlamydia, gonorrhea, na mengine.

  3. Kipimo cha damu – kama kuna mashaka ya maambukizi ya virusi kama Virusi vya UKIMWI au hepataitis.

  4. Ultrasound ya kibofu au tezi dume – iwapo dalili zimekuwa za muda mrefu au kuna mashaka ya matatizo ya ndani zaidi.


Matibabu

Matibabu hutegemea chanzo kilichogunduliwa. Kwa kawaida:

  • Klamidia: Hupatiwa dawa ya antibayotiki.

  • Gonorrhea: Mara nyingi hutibiwa kwa dawa mchanganyiko kutokana na usugu kwenye dawa moja

  • Maikoplasma genitalium: Huhitaji matibabu maalum kama Moxifloxacin iwapo antibayotiki nyingine hazifanyi kazi.

  • Urethraitis isiyo ya kisonono: Matibabu ya mchanganyiko wa dawa husaidia.

  • Uvimbe homa wa tezi dume(Prostataitis): Antibayotiki za muda mrefu kama husaidia endapo imethibitika.


Mambo ya kuzingatia:

  • Matibabu yanapaswa kuandikwa na mtaalamu wa afya.

  • Epuka kujitibu bila vipimo.

  • Watu wanaoshiriki ngono na mgonjwa wanapaswa pia kufanyiwa vipimo na kutibiwa.

  • Mgonjwa anapaswa kuepuka ngono hadi matibabu yakamilike.


Namna ya kujikinga

  • Tumia kondomu wakati wa ngono, hasa ikiwa na mwenza mpya au zaidi ya mmoja.

  • Pima afya mara kwa mara, hasa ikiwa unaishi mazingira yenye hatari kubwa ya magonjwa ya zinaa.

  • Jiepushe na matumizi holela ya sabuni zenye kemikali kali kwenye sehemu za siri.

  • Tumia maji safi na salama kujisafisha.


Lini kumwona daktari haraka

  • Ute unaongezeka au kubadilika rangi (kuwa kijani, njano au wenye harufu kali)

  • Unaendelea kutokwa na ute baada ya wiki kadhaa bila kubadilika

  • Kuwa na dalili za homa au maumivu ya korodani

  • Kutokwa na damu kwenye uume au mkojo

  • Mwenza wako amegundulika kuwa na ugonjwa wa zinaa


Hitimisho

Kutokwa na majimaji meupe kutoka kwenye uume bila maumivu ni dalili inayostahili kuchunguzwa kwa umakini. Ingawa inaweza kuonekana kama hali isiyo na madhara, mara nyingi huhusishwa na maambukizi ya ndani au ya zinaa ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa endapo hayatashughulikiwa mapema.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je, kutokwa na majimaji meupe kwenye uume bila maumivu ni hatari?

Si kila mara hali hii huwa hatari, lakini si jambo la kupuuzwa. Kutokwa na ute bila maumivu kunaweza kuashiria maambukizi ya awali ambayo bado hayajaanza kuleta dalili kali. Endapo hayatachunguzwa mapema, yanaweza kuendelea na kusababisha madhara kama kuathiri uwezo wa kupata watoto au kusambaa kwa mwenzi.

2. Je, ninaweza kuwa na ugonjwa wa zinaa kama natokwa na ute mweupe uumeni hata kama sina maumivu wala kuwashwa nikikojoa?

Ndiyo. Magonjwa kadhaa ya zinaa kama klamidia na Mykooplasma genitaliamu yanaweza kuwepo bila maumivu kabisa, hasa mwanzoni. Hii ndiyo sababu watu wengi huambukiza wenzao bila kujua, kwa kuwa hujiona wako salama ilhali maambukizi yapo.

3. Kwa nini ute mweupe uumeni unaonekana zaidi asubuhi?

Asubuhi, baada ya kulala kwa muda mrefu:

  • Mrija wa mkojo huwa umetulia

  • Majimaji hukusanyika bila kutoka

Hii husababisha ute kuonekana wazi zaidi wakati wa kukojoa kwa mara ya kwanza au hata kabla ya kukojoa. Hali hii huonekana sana kwa wanaume wenye homa ya mrija wa yurethra (yurethraitis).

4. Kwa mfano mtu wa kiume akiwa anatoa haja kubwa halafu ghafla majimaji meupe yakitoka kwenye uume, inamaanisha nini?

Hii hutokea mara nyingi kutokana na msukumo (pressure) unaotokea wakati wa kujikamua. Msukumo huu unaweza:

  • Kubana tezi dume (prostate)

  • Kusukuma ute wa tezi dume au majimaji ya mrija wa mkojo (urethra) yatoke

Mara nyingi hali hii si ya ngono wala si ugonjwa, hasa kama haina harufu, haina rangi isiyo ya kawaida, na haitokei mara kwa mara. Hata hivyo, ikijirudia sana, inaweza kuashiria prostatitis au tatizo la njia ya mkojo, hivyo uchunguzi unapendekezwa.

5. Je, ute mweupe uumeni unaweza kusababishwa na kukosa kufanya ngono kwa muda mrefu?

Ndiyo, kwa baadhi ya wanaume, kukaa muda mrefu bila kutoa shahawa kunaweza kusababisha:

  • Kujikusanya kwa majimaji ya tezi

  • Kutoka taratibu bila msisimko

Hata hivyo, hii hutokea kwa nadra na haipaswi kuendelea kwa muda mrefu. Ikiwa inaendelea, chanzo kingine kinapaswa kuchunguzwa.

6. Je, ute mweupe uumeni bila harufu bado unaweza kuwa dalili ya maambukizi?

Ndiyo. Kutokuwa na harufu hakumaanishi hakuna maambukizi. Klamidia na baadhi ya vimelea vingine hutokeza ute usio na harufu wala maumivu, lakini bado ni maambukizi halisi yanayohitaji matibabu.

7. Je, matumizi ya dawa au virutubisho yanaweza kusababisha ute kutoka kwenye uume?

Baadhi ya dawa:

  • Dawa za homoni

  • Dawa za kuongeza misuli au nguvu za kiume

  • Dawa za matatizo ya tezi dume

zinaweza kubadilisha namna tezi zinavyofanya kazi na kusababisha ute kutoka. Ndiyo maana ni muhimu kumweleza daktari dawa zote unazotumia, hata za mitishamba.

8. Je, ninaweza kuacha hali hii ya ute mweupe uumeni ipotee yenyewe bila matibabu?

Si busara. Ingawa wakati mwingine ute unaweza kupungua:

  • Maambukizi mengi hayaponi bila dawa sahihi

  • Kuacha bila matibabu kunaweza kusababisha maambukizi sugu

  • Pia kuna hatari ya kuwaambukiza wengine

Uchunguzi wa kitaalamu ndio njia salama zaidi.

9. Je, kipimo cha mkojo pekee kinatosha kugundua chanzo cha kutokwa na ute mweupe uumeni?

Si kila mara. Kipimo cha mkojo kinaweza kusaidia, lakini:

  • Baadhi ya vimelea vya zinaa hutambulika vizuri zaidi kwa kipimo cha PCR

  • Sampuli ya ute hutoa taarifa sahihi zaidi

Ndiyo maana daktari anaweza kupendekeza vipimo zaidi ya kimoja.

10. Nifanye nini kabla ya kufika hospitali kama ninatoa ute kwenye uume?

Hatua bora ni:

  • Epuka ngono hadi uchunguzi ufanyike

  • Usitumie dawa bila ushauri wa daktari

  • Usisafishe uume kwa kemikali kali kabla ya kipimo

  • Nenda hospitali mapema ili kupata vipimo sahihi

Hatua hizi husaidia kupata majibu sahihi na matibabu yanayofaa.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeandikwa:

16 Mei 2025, 15:45:46

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada

1. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.

2. Holmes KK, Sparling PF, Stamm WE, Piot P, Wasserheit JN, Corey L, et al., editors. Sexually Transmitted Diseases. 4th ed. New York: McGraw-Hill Medical; 2008.

3. Taylor-Robinson D, Jensen JS. Mycoplasma genitalium: from Chrysalis to Multicolored Butterfly. Clin Microbiol Rev. 2011;24(3):498–514.

4. Centers for Disease Control and Prevention. Chlamydia – CDC Fact Sheet (Detailed). [Internet]. 2022 [cited 2025 May 16]. Available from: https://www.cdc.gov/std/chlamydia/stdfact-chlamydia-detailed.htm

5. Barbee LA. Preparing for an era of untreatable gonorrhea. Curr Opin Infect Dis. 2014;27(3):282–7.

6. Stamm WE. Chlamydia trachomatis infections of the adult. In: Mandell, Douglas, and Bennett’s Principles and Practice of Infectious Diseases. 8th ed. Philadelphia: Elsevier; 2015. p. 2133–46.

7. Horner PJ, Taylor-Robinson D. Association of Mycoplasma genitalium with urethritis and other sexually transmitted infections. Int J STD AIDS. 2011;22(3):158–64.

8. Njeuhmeli E, Forsythe S, Reed J, et al. Voluntary medical male circumcision: modeling the impact and cost of expanding male circumcision for HIV prevention in eastern and southern Africa. PLoS Med. 2011;8(11):e1001132.

bottom of page