Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin Lugonda, MD
5 Juni 2021 11:28:15
Kutounga na kuunga vibaya kwa mifupa
Mara mfupa unapovunjika, mwili hutambua hilo na kutuma kemikali kwenye fomu ya umeme haswa kwenye chembe za mifupa ili kuamsha uzalishaji wa chembe na kemikali mbalimbali zinazohusika na uponyaji wa mfupa. Chembe na kemikali hizo husafiri kwenye damu na kufika eneo la mfupa uliovunjika na kuanzisha hatua za uponyaji kutokea.
Endapo mfupa uliovunjika una mishipa ya damu ya kutosha na umekutanishwa vema, mfupa huo hupona haraka zaidi ukilinganisha na mfupa ambao hauna mishipa ya damu au kutokutanishwa vema.
Kutokutanishwa vema kwa miishio ya mfupa uliovunjika hupelekea kupona vibaya au kuunga vibaya kwa mifupa, na kutokutanishwa kabisa au kutengana kwa vipande vya mifupa hupeleka mfupa huo kutounga kabisa.
Kutounga kwa mifupa ina maanisha nini?
Kutounga kwa mifupa ni kufeli kwa vipande vya mifupa vilivofanyika baada ya kuvunjika kuungana licha ya kukutanishwa pamoja katika mpangilio wa awali au kwa maana nyingine ni kufeli kupona kwa mfupa uliovunjika. Kwa kawaida mfupa wa binadamu uliovunjika endapo itakutanishwa vema huunga ndani ya miezi 3 hadi 6, na endapo mfupa haujaunga kabisa baada ya miezi 9 hii huitwa mfupa kutounga.
Kuunga vibaya kwa mfupa ina maanisha nini?
Mwili una uwezo wa kujiponya wenyewe, hivyo hivyo mfupa uliovunjika huanza mara moja kujiponya baada ya kuvunjika. Ili mfupa uweze kuunga ni lazima miishio ya vipande vya mifupa ikutanishwe vema na kwa mpangilio asili, endapo miishio ya mifupa haijakutana katika mpangilio mzuri, hupelekea mfupa kupona kwenye umbile lisilo la kawaida na hivyo kuleta nje mwonekano wa kupinda au uvimbepamoja na dalili zingine kama maumivu n.k.
Sehemu gani ya mwili mifupa yake huunga vibaya au kutounga kabisa?
Mara nyingi mifupa kuunga vibaya au kutounga hutokea sana kwenye
Mifupa ya alna na radias ( iliyo kwenye mkono wa mbele)
Shingo ya fupa fima (inayounganisha fupa paja na fupa nyonga)
Mfupa wa kifundo cha mguu
Mifupa ya vidole vya miguu
Mifupa kutounga hutokea sana kwenye maeneo gani?
Kutounga kabisa kwa mifupa hutokea kewnye mifupa ifuatayo;
Mifupa ya bega
Kiwiko cha mkono
Alna
Radias
Mifupa ya vidole vya mkono
Fupa patella ( mfupa wa kwenye goti)
Vihatarishi vya mifupa kuunga vibaya
Matumizi ya tumbaku au sigara
Uzito mkubwa kupita kiasi (ugonjwa wa obeziti)
Kuugua kisukari
Vihatarishi vya mfupa kutokuunga kabisa
Mfupa husemekana 'umeunga ndani ya muda' endapo umeunga ndani ya muda wa miezi 3 hadi 6, na 'umechelewa kuunga' endapo imeunga kai ya muda wa miezi 6 hadi 9 . Baada ya kipindi cha miezi tisa kupita, endapo mfupa haujaunga huitwa ' kutounga kwa mfupa' . Visababishai vya kutounga kwa mfupa ni pamoja na;
Uvutaji wa tumbaku au sigara
Madhaifu ya homoni kama vile kuwa na ugonjwa wa kisukari, madhaifu ya homoni thyroid na parathyroid, upungufu wa uzalishaji wa homoni testosterone na estrogen, upungufu wa vitamin D, upungufu wa madini ya kalisiamu na phosphorus mwilini
Utapiamlo (kutokula mlo kamili)
Matumizi ya dawa jamii ya steroid, dawa za saratani virusi, dawa za kifafa na za kushusha kinga ya mwili
Mifupa dhaifu na kutokuwepo kwa mishipa inayopeleka damu maeneo ya mfupa uliovunjika
Kutozingatia kwa mashariti ya kutotumia mguu au kuupa mguu uliovunjika uzito mkubwa kupita kiasi haswa kwa wenye magonjwa ya akili na ugonjwa wa kusahau kwa wazee (dementia)
Visababishi vya kuunga vibaya
Zinaweza zikawa sababu zilizosababishwa na mgonjwa, maumbile ya mgonjwa au kusababishwa na mtoa tiba (daktari)
Kutokutanishwa kwenye mpangilio wa awali vipande vya mfupa uliovunjika
Kushindwa kushikiriwa vema kwa vipande vya mifupa iliyokutanishwa vema na hivyo kupelekea kuhama. Mara nyingi vipande vya mifupa iliyokutanishwa hushikiriwa na uzito, vyuma vinavyowekwa ndani au nje ya mfupa na kufungwa na nati au mhogo (POP) unaofungwa nje ya mfupa uliovunjika ili kuzuia usicheze. Endapo vishikio hivi vimeruhusu kucheza kwa mifupa iliyokutanishwa, hupelekea kuhama na kuunga vibaya au kutounga kabisa
Kuhangaishwa kwa mfupa uliokutanishwa vema au kushikiriwa vema- mfano mtu aliyevunjika mguu kutumia mguu uliovunjika badala ya kutumia gongo ili kuzuia mguu uliovunjika kufanya kazi kabla ya kuunga
Kubomoka kwa mifupa iliyodhaifu
Majeraha kwenye sahani ya epiphyseal
Maambukizi kwenye mfupa
Mfupa kuvunjika kama vipande vipande
Mifupa dhaifu
Visababishi vya kutounga kabisa
Visababishi vya mifupa Kutokuunga kabisa ni pamoja na;
Mifupa iliyovunjika kutokuwa na mishipa ya damu inayopeleka damu ya kutosha
Miishio ya mifupa iliyovunjika kutokutana (kuto gusana)
Mfupa uliovunjika kucheza kabla ya kupona vema kutokana na kutotulia kwa eneo lililovunjika
Madhara
Matokeo ya kutounga au kuunga vibaya kwa mfupa hutokea na ishala hizi;
Kupinda kwa mfupa uliovunjika
Kuvimba kwa eneo lililovunjika
Maumimvu yasiyoisha
Kuzunguka kwa mfupa uliovunjika
Mikono au mguu mmoja wenye mfupa uliovunjika kuwa mfupi kuliko mwingine
Tatizo la arthraitis(linaloambatana na maumivu ya maungioa) endapo mifupa ya maungio ya mwili imehusika
Kushindwa kufanya kazi kwa kiungo cha mwili ambacho mfupa wake umevunjika
Kinga
Kuna mambo mgonjwa anaweza fanya ili kujikinga na hatari ya mifupa kutounga au kuunga vibaya, hata hivyo baadhi ya hatua zinatakiwa kuchukuliwa na mtaalamu wa afya anayetibu mgonjwa na kumpa mgonjwa elimu sahihi na ufuatiliaji kwenye kliniki. Hatua zilizotajwa hapa ni kwa ajili ya kuchukuliwa na mgonjwa.
Kupunguza uzito endapo una uzito mkubwa kupita kiasi haswa endapo umevunjika mifupa ya miguu au mikono
Kuacha kuvuta tumbaku au sigara
Ongea na daktari endapo unataka kutumia dawa hizi zinazochelewesha kupona au kuunga vibaya kwa mifupa, dawa za steroid, dawa za kutibu saratani, virusi, kifafa na za kushusha kinga ya mwili
Kula mlo kamili wenye mchanganyiko wa makundi matano ya chakula ili upate vitamin na madini muhimu kwa ajili ya uponyaji wa mifupa iliyovunjika(soma katika makala za uly clinic makundi matano ya chakula)
Kutoweka mzigo mkubwa zaidi ya ule ulioshauriwa kiungo chenye mfupa uliovunjika
Kujizuia kufanya kazi nzito, kubeba mizigo mizito au kufanya kazi zinazotikisa kwa kiasi kikubwa mfupa uliovunjika mpaka pale utakaporuhusiwa na daktari au utakapopona. Hata hivyo daktari atakushauri kutumia mguu uliovunjika kidogokidogo ili kuharakisha uponyaji, ni vema kumuuliza aina ya matumizi unayotakiwa fanya ili kuzuia kuchelewa unga, kutounga au kuunga vibaya kwa mifupa
Kufuata maelekezo ya daktari kuhusu kutumia au kutotumia kwa kiungo chenye mfupa uliovunjika
Kuhudhuria kliniki ya mifupa ili kufuatilia maendeleo yako kama ulivyoshauriwa na daktari
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
8 Oktoba 2021 04:53:09
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Malunion and Nonunion. https://www.upmc.com/services/orthopaedics/conditions-treatments/malunion-nonunion. Imechukuliwa 05.06.2021
2. What Are The Common Causes Of Malunion Fracture?. https://drvasuortho.com/what-are-the-common-causes-of-malunion-fracture/. Imechukuliwa 05.06.2021
3. Malunion Fractures. https://www.uofmhealth.org/conditions-treatments/cmc/fracture/malunion. Imechukuliwa 05.06.2021
4. Malunion of the distal radius. Karl-Josef Prommersberger, et al. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/22294090/. Imechukuliwa 05.06.2021
5. Brady T. Evans, et al. Best Approaches in Distal Radius Fracture Malunions. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6542911/. Imechukuliwa 05.06.2021
6. Hong Seop Lee, et al. Mid-term follow-up results of calcaneal reconstruction for calcaneal malunion. https://bmcmusculoskeletdisord.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12891-019-2419-1. Imechukuliwa 05.06.2021
7. Alexej Barg MD, et al. Can a fibular malunion be corrected by a Z-shaped fibular osteotomy?. https://link.springer.com/article/10.1007/s00132-019-03850-2. Imechukuliwa 05.06.20218.
8. K D Johnson, et al. Management of malunion and nonunion of the tibia. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/3540774/. Imechukuliwa 05.06.2021
9. J C Flynn, et al Prevention and treatment of non-union of slightly displaced fractures of the lateral humeral condyle in children. An end-result study. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/1201992/. Imechukuliwa 05.06.2021
10. Fracture Nonunion. https://www.ortho.wustl.edu/content/Patient-Care/6815/Services/TraumaFracture-Care/Overview/Nonunions.aspx#. Imechukuliwa 05.06.2021
11. General Principles in the Assessment and Treatment of Nonunions. https://ota.org/sites/files/2018-06/G17-The%20Principles%20and%20the%20Management%20of%20Nonunions.pdf. Imechukuliwa 05.06.2021