Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin L, MD
20 Agosti 2026, 05:09:52

Maumivu ya uke wakati wa tendo la ndoa(Kujamiiana)
Dispareunia (hutamkwa dis-pa-ROO-ni-a) ni neno la kitabibu linalomaanisha maumivu yanayotokea wakati wa tendo la kujamiiana. Neno hili linaweza kutumika kwa mwanamke au mwanaume, lakini katika makala hii linatumika kuelezea maumivu wakati wa kujamiiana kwa mwanamke, hasa maumivu ya uke au sehemu za ndani za nyonga.
Maumivu haya yanaweza kutokea wakati wa kuingiza uume ukeni, wakati wa tendo linapoendelea, au baada ya tendo. Yanaweza kusababishwa na mambo mbalimbali kama ukavu wa uke, maambukizi, mabadiliko ya homoni, majeraha, matatizo ya misuli ya sakafu ya nyonga au magonjwa ya mfumo wa uzazi. Makala hii inaeleza kwa kina sababu, dalili na namna ya kushughulikia maumivu ya uke wakati wa kujamiiana kwa mwanamke.
Dalili na viashiria
Dalili na viashiria vya maumivu ya uke makali wakati wa ngono huwa pamoja na
Kupata maumivu wakati uume unaingia
Kupata maumivu mara zote uume unapoingia au unapojisafisha
Kupata maumivu makali wakati uume unapoingia na kutoka wakati wa tendo
Kupata maumivu ya kuungua au kuchoma
Kupata maumivu ya kupwita pwita.
Visababishi vya maumivu ya uke wakati wa kujamiana kwa mwanamke
Visababishi vya maumivu makali ya uke wakati wa uume au kitu kigeni kinaingia ukeni ni pamoja na:
1. Kutokuwa na ute wa kutosha ukeni
Kwa kutoandaliwa vema wakati wa tendo la kujamiiana, kutokuwa na hisia za tendo au mabadiliko ya homoni kama yanayotokea kwa wanawake wanaoelekea kwenye umri wa komahedhi au walio kwenye komahedhi husababisha majimaji ya uke kuwa kidogo na kupelekea maumivu ya uke.
2. Matumizi ya dawa za aina fulani
Pia huweza kusababisha kupunguza hamu ya tendo na maji ya uke. Dawa hizi ni pamoja dawa za magonjwa ya akili (antidepressant), dawa za kushusha presha, dawa jamii ya sedativi, dawa za jamii ya antihistamini na dawa za kumeza za uzazi wa mpango.
3. Majeraha
Majeraha kwenye uke yanaweza kutokana na ajali, upasuaji wa nyonga, ukeketaji, au kuongezewa njia ya uke wakati wa kjifungua.
4. Michomo, maambukizi na matatizo ya Ngozi
Maambukizi kwenye uke au magonjwa ya Ngozi ya uke yanaweza kukusababishia maumivu wakati wat endo la kujamiana
Vajinizimu- hutokana na misuli ya uke kubana kwa muda mrefu pasipokuachia pasipo lazima, hali hii huleta maumivu makali sana wakati wa tendo.
5. Madhaifu ya kuzaliwa nayo
Matatizo ya kuzaliwa ambayo huonekana sana utotoni, kutokuwa na uke au kuwa na uke nusu au kuwa na ukuta wa bikra (haimen). (ukuta unaoziba kitu chochote kuingia kwenye uke) au kizazi kilichokaa vibaya huweza kusababisha maumivu ya uke.
6. Maumivu makali kwenye kilele cha uke
Maumivu ya ndani hutokea endapo uume umezama ndani kabisa. Maumivu haya huweza kuwa makali zaidi kutegemea pozi la wakati wa tendo. Visababishi vya maumivu haya huwa ni aina fulani ya magonjwa na hali kama vile uvimbe wa faibroidi, adenomayosisi, uvimbe maji kwenye ovari na bawasili, sindromu matumbo korofi na udhaifu kwenye sakafu ya nyonga. Sababu zingine ni ugonjwa wa Michomokinga kwenye nyonga, maambukizi kwenye vifuko maji ndani ya ovari na endometriosisi.
Upasuaj na dawa unaweza kuchangia pamojakama upasuaji wa kuondolewa kizazi, na dawa za kemotherapi na mionzi.
7. Matatizo ya hali ya moyo
Maumivu wakati wa kujamiana huweza kusababishwa na magonjwa ya kisaikolojia kama ugonjwa wa Ang’zayati, dipresheni, hofu ya kuogopa mahusiano, msongo wa mawazo, magonjwa ya somataizesheni n.k.
Hata hvyo kufanyiwa ukatili wa kijinsia unaweza kuchangia maumivu wakati wa tendo, ikumbukwe tafiti zinaonyesha si kila mwanamke aliyepata ukatili wa kijinsia hupata tatizo la maumivu wakati wa tendo.
Jedwali 1: Baadhi ya visababishi vya maumivu wakati wa Tendo la ndoa kwa mwanamke
Sababu | Maelezo ya chanzo | Dalili kuu | Mapendekezo ya matibabu ya nyumbani |
Ukavu wa uke | Ukosefu wa ute ukeni kutokana na homoni, msongo wa mawazo, au hamasa hafifu. | Maumivu ya kuchoma, kukwaruza, maumivu mwanzoni mwa tendo. | Tumia vilainishi (water-based), ongeza muda wa hamasa, epuka sabuni zenye kemikali. |
Maambukizi ya ukeni (fangasi, vajinosisi ya bakteria, magonjwa ya zinaa) | Fangasi, bakteria au magonjwa ya zinaa yanayoshambulia uke au shingo ya kizazi. | Kuwashwa, harufu mbaya, uchafu wa rangi isiyo ya kawaida, maumivu wakati wa tendo. | Tumia dawa za fangasi (OTC), epuka “kujitakasa ukeni”, vaa nguo za pamba. |
Endometriosisi | Ukuaji wa tishu ya endometrium nje ya mji wa mimba; husababisha uvimbe na maumivu. | Maumivu ya kina wakati wa tendo, hedhi chungu, maumivu ya tumbo ya mara kwa mara. | Tumia dawa za kupunguza maumivu (NSAIDs), andika dalili zako, muone daktari kwa uchunguzi zaidi. |
Hofu au msongo wa mawazo (vajinizimu ya hofu) | Hali ya kisaikolojia inayosababisha misuli ya uke kukakamaa bila hiari. | Maumivu ya ghafla, uke kubana kupita kiasi, kushindwa kufurahia tendo. | Mazungumzo ya wazi na mwenzi, mazoezi ya kupumzika, ushauri wa kitaalamu). |
Jeraha la uke (baada ya kujifungua, upasuaji) | Mishono, kovu, au tishu kupona vibaya baada ya kujifungua au upasuaji. | Maumivu ya sehemu ya chini, hasa wakati uume unagusa sehemu yenye kovu. | Tumia vilainishi, subiri kupona kabisa, chagua mikao isiyo na msuguano mkubwa. |
Faibroidi au uvimbe kwenye misuli kizazi | Uvimbe wa kawaida wa misuli ya kizazi unaoweza kushinikiza njia ya uke au viungo vya karibu. | Maumivu ya kina wakati wa tendo, hedhi nzito au ndefu, shinikizo kwenye nyonga. | Punguza maumivu kwa NSAIDs, jadiliana na daktari kuhusu ultrasound. |
Maambukizi kwenye njia ya mkojo (UTI) | Maambukizi kwenye kibofu cha mkojo au yurethra, yanayosababisha uchochezi kinga na maumivu. | Maumivu wakati wa kukojoa, shinikizo kwenye tumbo la chini, maumivu wakati wa tendo. | Kunywa maji mengi, epuka kuchelewa kukojoa, tumia dawa ya kuua bakteria iwapo inawezekana. |
Mabadiliko ya homoni (komahedhi, kunyonyesha) | Kupungua kwa estrojeni hufanya uke kuwa mwembamba na mkavu (kusinyaa kuta za uke). | Ukavu, kuchoma, kupungua kwa ute wa ukeni, maumivu ya mara kwa mara. | Tumia vilainishi, ulizia daktari kuhusu krimu za estrojeni za kujipaka. |
Matibabu ya maumivu makali ya uke wakati wa ngono
Matibabu yataanza na vipimo kisha kupewa tiba kulingana na visababishi vilivyofahamika. Endapo unatatizo la kisaikolojia, daktari wa saikolojia atakuwa nawe kukushauri katika darasa maalumu ili urejee kwenye hali ya kawaida. Kuhusu matibabu zaidi soma kwenye jedwali namba 1 hapo juu.
Hitimisho
Maumivu wakati wa tendo la ndoa kwa mwanamke si jambo la kawaida, wala si hali ya kuvumilia kimyakimya. Ni dalili muhimu inayoweza kuashiria matatizo ya kiafya, kihisia, au kisaikolojia. Kwa kutambua dalili mapema na kuchukua hatua sahihi- ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya wazi na mwenzi, matumizi ya tiba za nyumbani, na kufuata ushauri wa kitaalamu — matatizo haya yanaweza kutibiwa na maisha ya ndoa kurejea katika hali ya furaha na starehe.
Kumbuka:
Hakuna sababu ya aibu kutafuta msaada.
Mawasiliano baina ya wanandoa ni silaha ya kwanza ya uponyaji.
Na mwisho, mtaalamu wa afya yupo kusaidia, si kuhukumu — usisite kumwona unapohisi haja.
Majina mengine ya makala hii
Makala hii huwa na majina mengine yafuatayo yanayomaanisha maumivu ya uke wakati wa kujamiana
Maumivu ya uke wakati wa kujamiana
Maumivu ya uke wakati wa kuingiza uume
Maumivu ya uke wakati wa kufika kileleni
Maumivu ya uke wakati wa ngono
Maswali yanayoulizwa Mara kwa mara kuhusu Maumivu wakati wa Tendo la ndoa(kujamiiana au wakati wa ngono)
1. Je, chango (koliki) linaweza kuwa sababu ya maumivu wakati wa tendo kwa mwanamke?
Chango linaweza kuhusishwa na maumivu wakati wa tendo, lakini si kila maumivu wakati wa tendo husababishwa na chango. Chango ni maumivu yanayotokana na kujikaza kwa misuli ya viungo vya ndani, na kutegemea chanzo chake yanaweza kuhusisha tumbo, utumbo au viungo vya uzazi. Maumivu yanaweza kuongezeka wakati wa tendo kwa sababu ya msukumo na shinikizo kwenye maeneo hayo.
Kwa mfano, chango linalohusiana na hedhi au mikazo ya kizazi linaweza kufanya eneo la chini ya tumbo na nyonga kuwa na maumivu zaidi wakati wa tendo. Hata hivyo, maumivu wakati wa tendo yanaweza pia kutokana na hali nyingine kama maambukizi ya njia ya uzazi, ukavu wa uke, uvimbe kwenye kizazi au ovari, endometriosisi, au matatizo ya misuli ya nyonga.
Kwa hiyo, ikiwa maumivu wakati wa tendo yanajirudia, ni makali, yanaendelea baada ya tendo, au yanaambatana na uchafu usio wa kawaida ukeni, kutokwa damu, homa, maumivu makali ya chini ya tumbo au maumivu wakati wa kukojoa, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi na mhudumu wa afya ili kubaini chanzo. Chango pekee halipaswi kuchukuliwa kuwa sababu ya maumivu bila kutathmini sababu nyingine zinazowezekana.
2. Kwa nini mwanamke anaweza kupata maumivu baada ya tendo badala ya wakati wa tendo?
Maumivu yanaweza kuanza baada ya tendo kwa sababu misuli ya sakafu ya nyonga inaweza kuwa imekaza kwa muda mrefu wakati wa tendo. Kwa baadhi ya wanawake, kukaza huku kunaweza kuendelea kwa muda baada ya tendo na kusababisha maumivu ya chini ya tumbo, uke au nyonga.
Sababu nyingine ni msuguano uliosababisha michubuko midogo kwenye tishu za uke, hasa kama kulikuwa na ukavu au tendo lilikuwa la muda mrefu au lenye msuguano mkubwa. Maumivu yanaweza yasionekane mara moja lakini yakaanza baada ya tendo kutokana na muwasho wa tishu.
Maumivu yanayojirudia baada ya kila tendo yanafaa kuchunguzwa. Ikiwa yanaambatana na kutokwa damu, uchafu usio wa kawaida, harufu mbaya, homa, maumivu ya kukojoa au maumivu makali ya chini ya tumbo, kuna uwezekano wa tatizo linalohitaji matibabu badala ya kuhusisha maumivu hayo na tendo pekee.
3. Kwa nini maumivu wakati wa tendo yanaweza kuwa makali katika mikao fulani?
Mikao mbalimbali hubadilisha kina cha uume kuingia na namna viungo vya nyonga vinavyobanwa. Ikiwa maumivu hutokea hasa wakati wa kuingia kwa kina, mkao unaoruhusu uume kufika karibu na shingo ya kizazi au sehemu za ndani za nyonga unaweza kuongeza maumivu kwa baadhi ya wanawake.
Maumivu ya aina hii yanaweza kuonekana katika hali zinazohusisha viungo vya ndani vya nyonga, kama endometriosis, uvimbe kwenye ovari, baadhi ya uvimbe wa kizazi au matatizo ya sakafu ya nyonga. Hata hivyo, ukweli kwamba maumivu yanatokea katika mkao fulani pekee hauwezi kutambua ugonjwa fulani.
Ni muhimu kumwambia mhudumu wa afya ni sehemu gani inauma, kama maumivu hutokea wakati wa kuingia au wakati wa kusukumwa kwa kina, na kama yanaendelea baada ya tendo. Taarifa hii inaweza kusaidia kutofautisha maumivu ya sehemu ya nje ya uke na maumivu yanayotoka kwenye viungo vya ndani vya nyonga.
4. Je, maumivu wakati wa tendo yanaweza kusababishwa na tatizo la misuli ya sakafu ya nyonga?
Misuli ya sakafu ya nyonga inaweza kuwa sehemu ya chanzo cha maumivu wakati wa tendo. Misuli hii husaidia kushikilia kibofu cha mkojo, utumbo na viungo vya uzazi, na inapaswa kukaza na kulegea kwa mpangilio unaofaa. Ikiwa inakuwa imekaza kupita kiasi au inashindwa kulegea, kuingizwa kwa uume kunaweza kusababisha maumivu.
Baadhi ya wanawake huhisi maumivu kama kubana, kuchoma, kuvuta au shinikizo kwenye uke na nyonga. Maumivu yanaweza pia kuendelea baada ya tendo au kutokea wakati wa kuingiza tamponi au kitu kingine ukeni. Wakati mwingine mtu anaweza kuwa amepata maumivu kwa muda mrefu na kuanza kukaza misuli bila kujua kwa sababu ya kutarajia maumivu.
Matibabu hutegemea chanzo na yanaweza kuhusisha tiba ya misuli ya sakafu ya nyonga, mazoezi maalumu ya kulegeza misuli na ushauri wa kitaalamu. Si kila tatizo la sakafu ya nyonga linahitaji kuimarisha misuli; kwa mtu ambaye misuli imekaza kupita kiasi, kulenga kulegeza misuli kunaweza kuwa muhimu zaidi.
5. Kwa nini maumivu wakati wa tendo yanaweza kuambatana na kutokwa damu?
Kutokwa damu wakati au baada ya tendo kunaweza kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo msuguano unaosababisha jeraha dogo kwenye uke, ukavu, au mabadiliko kwenye shingo ya kizazi. Kwa baadhi ya wanawake, shingo ya kizazi inaweza kuwa nyeti na kuguswa wakati wa tendo na kusababisha damu kidogo.
Hata hivyo, kutokwa damu baada ya tendo kunaweza pia kuhusishwa na maambukizi ya njia ya uzazi, magonjwa ya zinaa, polyps kwenye shingo ya kizazi au mabadiliko mengine ya shingo ya kizazi. Kwa hiyo, damu inayotokea mara kwa mara haipaswi kupuuzwa hata ikiwa kiasi chake ni kidogo.
Mwanamke anayepata kutokwa damu kunakorudia baada ya tendo anapaswa kufanyiwa tathmini ya kitabibu kulingana na umri, historia yake ya afya na kama anafanya uchunguzi wa kawaida wa shingo ya kizazi. Kutokwa damu nyingi, maumivu makali au uwezekano wa ujauzito kunahitaji tathmini ya haraka zaidi.
6. Je, maumivu wakati wa tendo yanaweza kuathiri hamu ya kufanya tendo?
Maumivu yanaporudiwa mara kwa mara yanaweza kuathiri hamu ya tendo kwa sababu mtu anaweza kuanza kulihusisha tendo na maumivu badala ya starehe. Hii inaweza kusababisha hofu au wasiwasi kabla ya tendo, na wasiwasi huo unaweza kufanya mwili ushindwe kupumzika vizuri.
Kwa mwanamke, hofu ya kupata maumivu inaweza pia kusababisha misuli ya uke na sakafu ya nyonga kukaza bila hiari. Hali hii inaweza kufanya kuingiza uume kuwa kugumu au kuuma zaidi, na hivyo kuunda mzunguko ambapo maumivu husababisha hofu, hofu husababisha kukaza kwa misuli, na kukaza kwa misuli huongeza maumivu.
Kutibu tatizo la msingi ni muhimu kuliko kumlazimisha mtu kuvumilia maumivu. Mawasiliano na mwenzi, kuacha tendo linapokuwa linauma na kutafuta tathmini ya kitaalamu vinaweza kusaidia kuvunja mzunguko huu na kurejesha usalama na faraja wakati wa tendo.
7. Kwa nini maumivu wakati wa tendo yanaweza kutokea baada ya kujifungua?
Baada ya kujifungua, tishu za uke na eneo linalozunguka uke zinaweza kuchukua muda kupona, hasa ikiwa kulikuwa na kuchanika, kushonwa au kufanyiwa utaratibu wa kusaidia mtoto kuzaliwa. Kovu linapopona linaweza kuwa na unyeti au kubana na kusababisha maumivu wakati wa msuguano au kuingizwa kwa uume.
Mabadiliko ya homoni baada ya kujifungua, hasa wakati wa kunyonyesha, yanaweza pia kupunguza unyevunyevu wa uke kwa baadhi ya wanawake. Hii inaweza kufanya tendo kuwa na msuguano mkubwa na kusababisha maumivu au hisia ya kuchoma.
Maumivu yasipopungua kadiri mwili unavyopona, au ikiwa yanaendelea kwa muda mrefu baada ya kujifungua, si lazima mwanamke ayavumilie. Uchunguzi unaweza kusaidia kutambua kama tatizo linahusiana na kovu, ukavu, misuli ya sakafu ya nyonga au sababu nyingine inayoweza kutibiwa.
8. Je, maambukizi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kusababisha maumivu wakati wa tendo bila kuwa na dalili nyingine?
Baadhi ya maambukizi ya zinaa yanaweza kuwepo bila dalili zilizo wazi, lakini mtu bado anaweza kupata maumivu wakati wa tendo. Maambukizi yanapoathiri uke, shingo ya kizazi au viungo vya ndani vya uzazi, yanaweza kusababisha uchochezi ambao hufanya eneo hilo kuwa na maumivu wakati wa tendo.
Kutokuwepo kwa uchafu usio wa kawaida, kuwashwa au maumivu wakati wa kukojoa hakumaanishi moja kwa moja kwamba hakuna maambukizi. Baadhi ya maambukizi yanaweza kuwa na dalili chache au kutokuwa na dalili kabisa, ndiyo maana historia ya ngono na hatari ya maambukizi ni muhimu wakati wa tathmini.
Ikiwa kuna uwezekano wa maambukizi ya zinaa, ni muhimu kupimwa badala ya kutumia dawa bila kujua chanzo. Matibabu hutegemea aina ya maambukizi, na wakati mwingine mwenzi pia huhitaji kupimwa na kutibiwa ili kuzuia maambukizi kurudi.
9. Je, maumivu wakati wa tendo yanaweza kuendelea hata baada ya kuacha tendo kwa muda?
Maumivu yanaweza kuendelea kwa muda baada ya tendo ikiwa tishu za uke zimepata msuguano, misuli ya nyonga imekaza sana au kuna tatizo katika viungo vya ndani vya nyonga. Muda ambao maumivu hudumu unaweza kutofautiana kulingana na chanzo na ukubwa wa tatizo.
Ikiwa maumivu ni madogo na yanatokea mara chache, yanaweza kupungua baada ya mwili kupumzika. Lakini maumivu yanayodumu kwa saa nyingi, kurudia baada ya kila tendo au kuongezeka kadiri muda unavyopita yanahitaji kuangaliwa zaidi.
Ni muhimu pia kuzingatia dalili zinazoambatana nayo. Maumivu makali yanayoendelea pamoja na homa, kutapika, kutokwa damu nyingi, kuzimia au maumivu makali ya upande mmoja wa chini ya tumbo yanaweza kuhitaji huduma ya haraka.
10. Mwanamke mwenye maumivu wakati wa tendo anapaswa kumweleza daktari mambo gani?
Wakati wa uchunguzi, ni muhimu kueleza kwa uwazi sehemu ambayo inauma, kwa mfano kwenye mdomo wa uke, ndani ya uke, chini ya tumbo au sehemu ya ndani kabisa ya nyonga. Pia ni muhimu kueleza kama maumivu hutokea wakati wa kuingiza uume, wakati wa tendo kuendelea, wakati wa kuingia kwa kina, au baada ya tendo.
Muda wa kuanza kwa tatizo na uhusiano wake na hedhi, kujifungua, upasuaji, matumizi ya dawa, uzazi wa mpango au maambukizi ya awali pia vinaweza kuwa taarifa muhimu. Mabadiliko kama ukavu wa uke, kutokwa damu, uchafu usio wa kawaida, kuwashwa, maumivu wakati wa kukojoa au maumivu ya hedhi yanapaswa kutajwa pia.
Kutoa taarifa hizi kwa uwazi hakupaswi kuwa jambo la aibu. Maumivu wakati wa tendo yanaweza kuwa na sababu nyingi, na maelezo sahihi humsaidia mhudumu wa afya kuamua kama kuna haja ya uchunguzi wa uke na nyonga, vipimo vya maambukizi, kipimo cha ujauzito, picha ya ultrasound au uchunguzi mwingine kulingana na dalili.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
6 Novemba 2024, 15:19:44
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada hii:
Kingsberg S, et al. Approach to the woman with sexual pain [Internet]. UpToDate; [cited 2020 Apr 17]. Available from: https://www.uptodate.com/contents/search
American College of Obstetricians and Gynecologists. When sex is painful: Frequently asked questions. Gynecologic Problems FAQ020 [Internet]. [cited 2020 Apr 17]. Available from: https://www.acog.org/Patients/FAQs/When-Sex-Is-Painful
Merck Manual Professional Edition. Dyspareunia [Internet]. [cited 2020 Apr 17]. Available from: https://www.merckmanuals.com/professional/gynecology-and-obstetrics/sexual-dysfunction-in-women/dyspareunia
Barbieri R. Differential diagnosis of sexual pain in women [Internet]. UpToDate; [cited 2020 Apr 17]. Available from: https://www.uptodate.com/contents/search
Kellerman RD, et al. Female sexual dysfunction. In: Conn's Current Therapy 2019. Philadelphia: Elsevier; 2019. Available from: https://www.clinicalkey.com. [cited 2020 Apr 17].
Faubion SS, et al. Genitourinary syndrome of menopause: Management strategies for the clinician. Mayo Clinic.
Facts & Comparisons eAnswers. Ospemifene oral [Internet]. [cited 2020 Apr 17]. Available from: http://fco.factsandcomparisons.com/lco/action/search?q=Ospemifene%20oral&t=name&va=Ospemifene%20oral
Sauer U, et al. Efficacy of intravaginal dehydroepiandrosterone (DHEA) for symptomatic women in the peri- or postmenopausal phase. Maturitas. 2018. doi:10.1016/j.maturitas.2018.07.016.
