Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dkt. Benjamin l, MD
Dkt. Peter A, MD
20 Agosti 2026, 05:09:52

Maumivu ya hedhi
Maumivu wakati wa hedhi kwa jina la tiba linalotumiwa na ulyclinic ni "dismenorea". Neno hili limetoholewa kutoka neno tiba "Dysmenorrhea" ambalo lina asili ya maneno ya Kigiriki na Kilatini
Dismenorea ni maumivu ya kubana au kuchoma yanayotokea kabla au wakati wa damu ya hedhi.
Maumivu yoyote yale ya hedhi huamshwa na kemikali zinazoitwa prostaglandin na leukotriene katika mfumo wa uzazi ambazo ni kawaida kuzalishwa wakati wa yai kutengenezwa na kutoka kwenye ovari.
Kiwango hiki huongezeka sana kwenye kipindi cha yai kutolewa kutoka katika ovari na wakati ukuta wa ndani ya mfuko wa kizazi unapoanza kuvunjika endapo uchavushwaji wa Yai haujatokea.
Kemikali hizi husababisha mfuko wa uzazi kubana na kuachia ili kutoa kuta zilizojengwa kwa muda wa siku 28 au 31 endapo tu yai lililotoka kwenye ovari halikuchavushwa. Ukuta huu unapovunjika hutoa dalili za damu ya kila mwezi, ukuta mwingine hujengwa tena baada ya damu ya mwezi kutatika.
Visababishi
Kuna aina mbili za maumivu ya hedhi Aina ya awali na aina ya sekondari.
Aina ya awali imezungumziwa hapa, kwa jina jingine hujulikana kama maumivu ya kawaida wakati wa hedhi na hutokea mwaka mmoja (1) au miwili baada ya mwanamke kuvunja ungo. Mwanamke hupata maumivu ya tumbo la chini ya kitovu au mgongoni.
Maumivu ya hedhi ya kawaida maranyingi huanza muda mfupi kabla mwanamke hajaanza kuona damu ya hedhi, hudumu muda wa siku tatu au pungufu. Maumivu hupungua siku zinavyoendelea na kuisha kabisa.
Dalili zake ni zipi?
Maumivu ya kubana chini ya kitovu na nyonga yanayoelekea kwenye;
Mapaja na
Mgongo
Endapo dalili zimekuwa mbaya zaidi mwanamke anaweza kupata;
Mvurugiko wa tumbo
Wakati mwingine kutapika
Kupata choo laini au
Kuharisha
Maumivu ya hedhi aina ya sekondari
Kwa wanawake wenye maumivu makali ya kupindukia asilimia 10 huwa na uvimbe usio saratani kwenye mfuko wa kizazi au kuwa na chembe hai za ndani ya mfuko wa kizazi nje ya mfuko wa ya kizazi huitwa kwa jina la tiba endometriosisi
Aina ya sekondari husababishwa na mabadiliko au magonjwa yaliyo katika kizazi kama vile tatizo la endometriosisi (kuwepo kwa ukuta wa ndani ya kizazi nje ya kizazi maeneo ya mirija ya uzazi, kibofu, nje ya ukuta wa kizazi, sehemu ya haja kubwa, kiwanda cha ovari)
Tatizo la endometriosis husababisha damu ya hedhi kuvilia kwenye ogani zilizo ndani ya nyonga, michomo na makovu nje ya mfumo wa kizazi na ogani zilizo ndani ya nyonga hutokea hivyo husababisha maumivu pengine yanayouma muda mrefu na yasiyo isha.
Visababishi
Maumivu ya hedhi mara chache husababishwa na;
Madhaifu/ugonjwa ndani ya nyonga (matatizo ya kuzaliwa ya mfuko wa uzazi).
Endometriosis
Ugonjwa wa michomo kwenye mfuko wa uzazi (Ugonjwa wa Pelvic inflammatori (PID)
Uvimbe kwenye mfuko wa kizazi (fibroids)
Nitafanya nini kutibu tatizo hili la maumivu makali ya hedhi?
Tiba zipo kuweza kutuliza maumivu yasiyo makali sana kwa kutumia dawa ya asprini au dawa zingine za kutuliza maumivu, itakupasa kunywa dawa mara utakapoanza kuona siku zako.
Kuoga maji ya moto au kujikanda kwa maji ya moto maeneo ya tumbo la chini na mgongoni kunaweza kusaidia kupunguza maumivu.
Kama maumivu ni makali zaidi
Pata muda wa kupumzika
Acha kunywa pombe
Acha vyakula vyenye caffeine au chumvi maana huongeza misuli kubana na kuachia na hivo kuleta maumivu
Kanda tumbo na mgongo
Pia fanya mazoezi kwa mujibu wa ratiba yako kwa maana tafiti zinaonesha kuwa mazoezi hupunguza maumivu ya hedhi na hufupisha siku za kuona damu. Hata hivyo kujamiiana wakati wa hedhi kunaweza kupunguza maumivu ya hedhi pia
Endapo maumivu yamezidi sana
Kunywa dawa zenye nguvu zaidi kama utavyoshauliwa na dakitari
Unaweza ukatumia dawa za uzazi wa mpango
Wakati gani upate msaada kutoka kwa daktari?
Kwa wanawake wengi baadhi ya maumivu wakati wa hedhi ni jambo la kawaida, hata hivyo unabidi kuwasiliana na daktari wako endapo;
Dawa jamii ya NSAIDS na matibabu yasiyo dawa hayajakusaidia kabisa
Maumivu ya hedhi yamekuwa makali Zaidi ghafla
Una Zaidi ya miaka 25 na umepata maumivu ya hedhi makali sana kwa mara ya kwanza
Maumivu ya hedhi yameambatana na homa
Unapata maumivu ya hedhi hata kama huoni damu ya hedhi(piriodi)
Utajuaje maumivu yako ni ya kawaida?
Kama unapata maumivu yanayozidi siku tatu na ni makali basi onana na dakitari maana matatizo haya hutibika hospitali endapo wataona kinachosababisha ni nini. Pia unaweza kusoma kuhusu tiba asilia namaumivu ya hedhi kwa kubonyeza hapa.
Maswali yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQ) kuhusu Maumivu ya Hedhi (Dismenorea)
1. Kwa nini maumivu ya hedhi yanakuwa makali zaidi kwa baadhi ya wanawake kuliko wengine?
Ukali wa maumivu ya hedhi hutofautiana kutoka kwa mwanamke mmoja hadi mwingine. Tofauti hii inaweza kusababishwa na kiwango cha kemikali zinazoitwa prostaglandini zinazozalishwa mwilini wakati wa hedhi. Wanawake wanaozalisha kiwango kikubwa cha prostaglandins huwa na mikazo mikali zaidi ya mfuko wa uzazi, jambo linaloongeza maumivu.
Sababu nyingine ni tofauti za kimaumbile, urithi wa kifamilia, umri, na uwepo wa magonjwa kama endometriosisi, adenomayosisi au uvimbe kwenye mfuko wa uzazi (faibroidi). Pia msongo wa mawazo, kukosa usingizi wa kutosha na baadhi ya magonjwa sugu yanaweza kufanya maumivu yaonekane makali zaidi.
Ikiwa maumivu yanakuzuia kwenda kazini, shuleni au kufanya shughuli zako za kawaida kila mwezi, si jambo la kupuuza. Ni muhimu kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kama kuna tatizo linalohitaji matibabu maalumu.
2. Je, maumivu ya hedhi yanaweza kuanza ghafla wakati hapo awali sikuwa nayo?
Ndiyo. Mwanamke anaweza kuanza kupata maumivu makali ya hedhi baada ya miaka mingi ya kutokuwa na maumivu. Hali hii inaweza kutokea kutokana na mabadiliko ya homoni yanayoambatana na umri au kutokana na kuanza kwa magonjwa ya mfumo wa uzazi.
Maumivu yanayoanza ghafla hasa baada ya umri wa miaka 25 yanaweza kuashiria tatizo kama endometriosisi, adenomyosisi, faibroidi au maambukizi ya nyonga. Tofauti na maumivu ya kawaida ya hedhi, maumivu haya yanaweza kuendelea hata baada ya hedhi kuisha au kuongezeka kadri miaka inavyopita.
Iwapo maumivu yameanza ghafla na ni makali kuliko kawaida, ni vyema kumuona daktari ili kubaini chanzo chake badala ya kuendelea kutumia dawa za maumivu kila mwezi bila uchunguzi.
3. Je, maumivu makali ya hedhi yanaweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito?
Maumivu ya kawaida ya hedhi (dismenorea ya awali) hayapunguzi uwezo wa mwanamke kupata ujauzito. Wanawake wengi wenye maumivu ya kawaida hupata ujauzito bila matatizo yoyote.
Hata hivyo, ikiwa maumivu yanasababishwa na magonjwa kama endometriosisi, ugonjwa wa uchochezikinga kwenye nyonga kutokana na maambukizi (PID) au baadhi ya matatizo ya mirija ya uzazi, magonjwa hayo yanaweza kuathiri uwezo wa kushika mimba ikiwa hayatatibiwa mapema.
Kwa hiyo, ikiwa una maumivu makali ya hedhi pamoja na kushindwa kupata ujauzito baada ya miezi 12 ya kufanya ngono bila kutumia uzazi wa mpango (au miezi 6 ikiwa una miaka 35 au zaidi), ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa uzazi.
4. Je, ni kawaida kupata maumivu ya hedhi lakini damu kutoka kidogo sana?
Ndiyo, inaweza kuwa kawaida kwa baadhi ya wanawake. Kiasi cha damu kinachotoka wakati wa hedhi hakina uhusiano wa moja kwa moja na ukali wa maumivu. Mwanamke anaweza kupata maumivu makali lakini damu ikawa kidogo, au damu nyingi bila maumivu makali.
Hata hivyo, ikiwa mabadiliko haya yametokea ghafla au yanaambatana na kuchelewa kwa hedhi, uwezekano wa ujauzito, matumizi ya dawa za homoni au matatizo ya homoni unaweza kuhitaji kuchunguzwa.
Ikiwa una maumivu makali kila mwezi na hedhi yako imebadilika sana kuliko ulivyozoea, muone mtoa huduma za afya kwa uchunguzi zaidi.
5. Je, mazoezi yanaweza kuongeza maumivu ya hedhi?
Kinyume na imani za watu wengi, mazoezi mepesi hadi ya wastani mara nyingi husaidia kupunguza maumivu ya hedhi. Wakati wa mazoezi, mwili huzalisha kemikali zinazoitwa endorphins ambazo husaidia kupunguza maumivu na kuboresha hali ya hisia.
Mazoezi kama kutembea kwa kasi, kuendesha baiskeli, kuogelea au yoga yanaweza kusaidia kupunguza mikazo ya misuli na kuboresha mzunguko wa damu kwenye nyonga.
Hata hivyo, ikiwa maumivu ni makali sana au una ugonjwa unaosababisha maumivu ya hedhi, huenda ukahitaji kupunguza kiwango cha mazoezi hadi utakapopata matibabu sahihi.
6. Je, maumivu ya hedhi yanaweza kusababisha kizunguzungu au kuzimia?
Ndiyo, baadhi ya wanawake hupata kizunguzungu wakati wa hedhi kutokana na maumivu makali, kushuka kwa shinikizo la damu kwa muda mfupi, kutokula vizuri au kupoteza damu nyingi wakati wa hedhi.
Ikiwa unavuja damu nyingi kwa muda mrefu, unaweza kupata upungufu wa damu (anemia), hali ambayo inaweza kusababisha uchovu, mapigo ya moyo kwenda kasi na kizunguzungu.
Iwapo umewahi kuzimia, kupata maumivu makali yasiyo ya kawaida au kutokwa damu nyingi sana, ni muhimu kwenda hospitali kwa uchunguzi haraka.
7. Je, chakula kinaweza kusaidia kupunguza maumivu ya hedhi?
Hakuna chakula kinachoweza kuondoa maumivu ya hedhi moja kwa moja, lakini lishe bora inaweza kusaidia kupunguza ukali wa dalili kwa baadhi ya wanawake. Vyakula vyenye matunda, mboga za majani, nafaka zisizokobolewa na samaki wenye mafuta vinaweza kusaidia kupunguza uchochezi mwilini.
Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa ulaji wa kutosha wa madini ya magnesium, calcium na vitamini B1 unaweza kusaidia kupunguza maumivu kwa baadhi ya wanawake, ingawa ushahidi bado unaendelea kuchunguzwa.
Ni vyema pia kunywa maji ya kutosha na kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta mengi au pombe ikiwa unaona vinaongeza dalili zako.
8. Je, maumivu ya hedhi yanaisha baada ya kujifungua?
Kwa wanawake wengi, maumivu ya hedhi hupungua baada ya kupata mtoto, hasa ikiwa walikuwa na dismenorea ya awali. Inaaminika kuwa baadhi ya mabadiliko yanayotokea kwenye mlango wa kizazi na mfuko wa uzazi baada ya kujifungua yanaweza kupunguza maumivu.
Hata hivyo, si wanawake wote hupata mabadiliko haya. Wengine huendelea kupata maumivu yale yale, na ikiwa chanzo ni ugonjwa kama endometriosis au adenomyosis, maumivu yanaweza kuendelea hata baada ya kujifungua.
Ikiwa maumivu yanaendelea kuwa makali baada ya kujifungua, unapaswa kufanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo chake.
9. Je, ninaweza kutumia dawa za maumivu kila mwezi bila madhara?
Dawa za kupunguza maumivu kama NSAIDs zinaweza kuwa salama kwa watu wengi zinapotumiwa kwa kufuata ushauri wa daktari au maelekezo ya dawa. Hata hivyo, matumizi ya muda mrefu au ya mara kwa mara yanaweza kuongeza hatari ya vidonda vya tumbo, kutokwa damu tumboni, matatizo ya figo au kuongeza shinikizo la damu kwa baadhi ya watu.
Ikiwa unalazimika kutumia dawa hizi kila mwezi kwa muda mrefu, ni muhimu kumuona daktari ili kuhakikisha kuwa hakuna tatizo linalosababisha maumivu hayo na kujadili njia nyingine za matibabu.
Usiongeze dozi au kuchanganya dawa mbalimbali za maumivu bila ushauri wa mtaalamu wa afya.
10. Nitajuaje kama maumivu yangu ya hedhi si ya kawaida tena?
Maumivu ya hedhi yanapaswa kuchunguzwa ikiwa yanabadilika ghafla, yanakuwa makali zaidi kuliko ulivyozoea, yanadumu zaidi ya hedhi, au hayapungui hata baada ya kutumia dawa za maumivu na njia nyingine za kujitunza.
Pia unapaswa kumuona daktari ikiwa maumivu yanaambatana na kutokwa damu nyingi sana, homa, kutokwa na uchafu wenye harufu mbaya, maumivu wakati wa kujamiiana, maumivu wakati wa kukojoa au kupata choo, au ikiwa yanakuzuia kufanya shughuli zako za kila siku.
Kumbuka kwamba maumivu makali si jambo la kuvumilia kila mwezi bila kujua chanzo chake. Uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kugundua na kutibu magonjwa yanayosababisha maumivu kabla hayajaleta madhara makubwa zaidi.
11. Je, kupata maumivu ya hedhi bila kuona hedhi ni tatizo?
Maumivu yanayofanana na ya hedhi bila hedhi kuanza si lazima yawe dalili ya tatizo. Wakati mwingine hutokea kwa sababu hedhi inakaribia kuanza, mabadiliko ya homoni, msongo wa mawazo, matumizi ya dawa za homoni kama uzazi wa mpango wa dharura (P2), au wakati wa ovulesheni. Kwa wanawake wengi, maumivu haya huisha yenyewe au hedhi huanza ndani ya siku chache.
Hata hivyo, maumivu ya hedhi bila hedhi yanaweza pia kuwa dalili ya ujauzito wa mapema, hasa kama umewahi kufanya ngono bila kinga. Pia yanaweza kusababishwa na matatizo mengine kama uvimbe kwenye nyonga, maambukizi ya viungo vya uzazi, uvimbe wa kizazi (faibroidi), endometriosis, uvimbe kwenye ovari au matatizo ya mfumo wa mkojo na utumbo. Kwa hiyo, sababu hutegemea historia ya afya na dalili nyingine unazopata.
Unapaswa kufanya kipimo cha ujauzito ikiwa hedhi imechelewa na umewahi kufanya ngono bila kinga, hata kama ulitumia P2 au njia nyingine ya uzazi wa mpango wa dharura. Muone mtoa huduma za afya ikiwa maumivu ni makali sana, yanaendelea kwa siku nyingi bila kupata hedhi, yanaambatana na homa, kutokwa damu nyingi isiyo ya kawaida, kutokwa na uchafu wenye harufu mbaya, maumivu wakati wa kukojoa au kujamiiana, au kama unapata kizunguzungu au kuzimia. Uchunguzi wa kitabibu unaweza kusaidia kubaini chanzo halisi na kutoa matibabu yanayofaa.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
24 Desemba 2021, 12:44:59
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada hii:
1. Hassan Nagy, et al. Dysmenorrhea. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK560834/.Imechukuliwa 24.12.2021
2. Bernardi, et al. “Dysmenorrhea and related disorders.” F1000Research vol. 6 1645. 5 Sep. 2017, doi:10.12688/f1000research.11682.1
3.Period pain.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK279324/. Imechukuliwa 24.12.2021.
4. Proctor, et al. “Diagnosis and management of dysmenorrhoea.” BMJ (Clinical research ed.) vol. 332,7550 (2006): 1134-8. doi:10.1136/bmj.332.7550.1134
