Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Sospeter B, MD
20 Agosti 2026, 05:09:52

Maumivu ya kitovu
Maumivu ya kitovu ni nini?
Maumivu ya kitovu ni hali ya kupata maumivu, usumbufu au bugudha katika eneo la kitovu au sehemu inayokizunguka. Maumivu haya yanaweza kuwa ya ghafla au ya muda mrefu, ya kuja na kuondoka au kuendelea kwa muda bila kupungua. Wakati mwingine maumivu hutokana na tatizo lililopo kwenye kitovu chenyewe, lakini pia yanaweza kusababishwa na magonjwa ya viungo vya ndani ya tumbo kama utumbo, tumbo, kongosho, figo au mfumo wa uzazi.
Ingawa baadhi ya visababishi si hatari na hupona vyenyewe, vingine vinaweza kuwa dalili ya ugonjwa unaohitaji matibabu ya haraka ili kuzuia madhara makubwa. Kwa hiyo, maumivu ya kitovu yanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu hasa ikiwa ni makali, yanadumu kwa muda mrefu au yanaambatana na dalili nyingine zinazotia wasiwasi.
Katika makala hii, maneno maumivu ya kitovu, maumivu karibu na kitovu, maumivu ya katikati ya tumbo, na maumivu ya tumbo kuzunguka kitovu yanamaanisha hali inayofanana.
Dalili na Viashiria vya maumivu ya kitovu
Mbali na maumivu yenyewe, mtu anaweza kuwa na dalili nyingine kulingana na chanzo cha tatizo. Dalili hizo ni pamoja na:
Maumivu makali au yanayoendelea kwa muda mrefu.
Maumivu ya kuja na kuondoka.
Kuvimba, wekundu au maumivu unapogusa kitovu.
Homa.
Kichefuchefu na kutapika.
Kuharisha au kufunga choo.
Gesi nyingi tumboni na tumbo kujaa.
Maumivu yanayosambaa kuelekea mgongoni au sehemu za chini ya tumbo.
Kutokwa na usaha, damu au majimaji kwenye kitovu.
Kupungua hamu ya kula.
Maumivu yanayoongezeka wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuinua vitu vizito.
Visababishi vya maumivu ya kitovu
Maumivu ya kitovu yanaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali yanayohusisha mfumo wa chakula, njia ya mkojo, mfumo wa uzazi, misuli ya tumbo au mishipa ya damu.
1. Matatizo ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula
Haya ndiyo visababishi vinavyoonekana mara nyingi.
Vidonda vya tumbo.
Homa ya utumbo (gastroenteraitisi).
Gesi nyingi tumboni na umeng'enyaji hafifu.
Kuvimba kwa utumbo (Ugonjwa wa Crohn's na magonjwa mengine ya uchochezi wa utumbo).
Kuziba kwa utumbo mdogo.
Maumivu ya sehemu ya mwisho ya utumbo mwembamba au mwanzo wa utumbo mpana.
2. Dalili za awali za kidole tumbo (Maambukizi kwenye kidole tumbo)
Mwanzoni mwa ugonjwa wa kidole tumbo, maumivu huanza karibu na kitovu kabla ya kuhamia upande wa chini kulia wa tumbo ndani ya saa chache. Mara nyingi huambatana na homa, kichefuchefu na kukosa hamu ya kula.
3. Maambukizi
Maambukizi ya kitovu (Omphalaitisi).
Maambukizi ya njia ya mkojo.
Maambukizi ya figo.
Maambukizi yanaweza kusababisha homa, wekundu, usaha na maumivu kwenye kitovu.
4. Matatizo ya Figo na Njia ya Mkojo
Mawe kwenye figo.
Maambukizi ya figo.
Mawe kwenye ureta.
Maumivu yanaweza kuanzia karibu na kitovu na kusambaa mgongoni au kuelekea sehemu za siri.
5. Henia ya Kitovu
Henia ya kitovu au ngiri ya kitovu hutokea pale sehemu ya utumbo au mafuta ya ndani ya tumbo yanaposukuma kupitia sehemu dhaifu ya ukuta wa tumbo karibu na kitovu. Mara nyingi huonekana kama uvimbe unaoongezeka wakati wa kukohoa, kucheka au kuinua vitu vizito.
6. Magonjwa ya wanawake
Kwa wanawake, maumivu ya kitovu yanaweza kutokana na:
Mimba ya nje ya kizazi.
Endometriosisi.
Uvimbe kwenye ovari.
Maambukizi ya via ndani ya nyonga (PID).
7. Magonjwa ya kongosho
Kuvimba kwa kongosho (Pancreatitis) kunaweza kusababisha maumivu makali katikati ya tumbo karibu na kitovu ambayo huenea kuelekea mgongoni na mara nyingi huambatana na kutapika.
8. Kuumia kwa misuli ya tumbo
Mazoezi makali, kuinua vitu vizito au ajali vinaweza kusababisha misuli ya tumbo kuvutika na kuleta maumivu karibu na kitovu.
Visababishi vinavyoweza kutishia maisha
Baadhi ya magonjwa yanayosababisha maumivu ya kitovu ni dharura za kitabibu na yanahitaji matibabu ya haraka.
Hali hizo ni pamoja na:
Kuziba kwa utumbo.
Homa ya kidole tumbo.
Kutoboka kwa utumbo.
Kupasuka kwa ini, bandama au utumbo baada ya ajali.
Iskemia ya mezenteri (kukosa damu kwenye utumbo).
Homa kali ya kongosho.
Kupasuka kwa mshipa mkubwa wa aota.
Kupasuka kwa mimba ya nje ya kizazi.
Mshtuko wa moyo (kwa baadhi ya wagonjwa maumivu yanaweza kuonekana katikati ya tumbo).
Uchunguzi wa maumivu ya kitovu
Daktari anaweza kufanya uchunguzi ufuatao ili kubaini chanzo cha maumivu:
Kuchukua historia ya mgonjwa.
Uchunguzi wa mwili.
Vipimo vya damu.
Vipimo vya mkojo.
Kipimo cha ujauzito kwa wanawake wenye uwezo wa kushika mimba.
Ultrasound ya tumbo.
CT Scan au MRI pale inapohitajika.
X-ray ya tumbo.
Endoscopy ikiwa kuna shaka ya ugonjwa wa tumbo au utumbo.
Matibabu ya maumivu ya kitovu
Matibabu hutegemea chanzo cha maumivu.
Dawa
Daktari anaweza kuandika:
Antibiotiki kwa maambukizi ya bakteria.
Dawa za kupunguza asidi tumboni kama Omeprazole.
Dawa za kutibu maambukizi ya njia ya mkojo.
Dawa za maumivu ikiwa zinafaa baada ya uchunguzi.
Epuka kutumia dawa za maumivu bila ushauri wa daktari, hasa ikiwa maumivu ni makali, kwa sababu zinaweza kuficha dalili za magonjwa yanayohitaji upasuaji wa haraka.
Upasuaji
Upasuaji unaweza kuhitajika kwa:
Hernia ya kitovu.
Kidole tumbo.
Kuziba kwa utumbo.
Mimba ya nje ya kizazi.
Kutoboka kwa utumbo.
Mabadiliko ya mtindo wa maisha
Kula lishe yenye nyuzinyuzi nyingi.
Kunywa maji ya kutosha.
Epuka vyakula vinavyoongeza gesi ikiwa vinaongeza maumivu.
Fanya mazoezi ya kawaida.
Dumisha uzito unaofaa.
Matibabu ya nyumbani
Iwapo maumivu si makali na hakuna dalili za hatari:
Pumzika.
Tumia taulo la uvuguvugu juu ya tumbo.
Kunywa maji ya kutosha.
Kula chakula chepesi kinachosagika kwa urahisi.
Epuka kunyanyua vitu vizito.
Wakati gani wa kumwona daktari?
Muone daktari ikiwa maumivu:
Yanadumu zaidi ya saa 24–48 au yanaendelea kuongezeka.
Yanakuwa makali ghafla.
Yanaambatana na homa.
Yanakufanya ushindwe kutembea au kusimama.
Yanaambatana na kutapika kusikoisha.
Kuna damu kwenye kinyesi au matapishi.
Kitovu kinatoa usaha, damu au harufu mbaya.
Tumbo limevimba sana.
Kuna uvimbe kwenye kitovu unaouma na hauingii ndani.
Unapungua uzito bila sababu.
Una manjano.
Mwanamke mjamzito au anayeshuku ujauzito anapata maumivu makali ya kitovu au tumbo.
Hitimisho
Maumivu ya kitovu ni dalili inayoweza kusababishwa na magonjwa mengi, kuanzia matatizo madogo kama gesi tumboni hadi hali zinazohatarisha maisha kama kidole tumbo, kuziba kwa utumbo au mimba ya nje ya kizazi. Kwa kuwa chanzo hakiwezi kubainishwa kwa dalili pekee, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ili kupata utambuzi sahihi na matibabu yanayofaa. Kutafuta huduma za afya mapema husaidia kuzuia madhara makubwa na kuongeza uwezekano wa kupona haraka.
Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara kuhusu maumivu ya kitovu
1. Kwa nini kitovu kinauma nikibonyeza kwa kidole?
Watu wengi hugundua kuwa hawana maumivu wakati wa kawaida, lakini wanapobonyeza kitovu ndipo maumivu hujitokeza. Hali hii inaweza kusababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo maambukizi madogo kwenye kitovu, mkusanyiko wa uchafu ndani ya kitovu, kuumia kwa misuli ya tumbo, hernia ya kitovu, au uvimbe wa tishu zinazozunguka kitovu. Ikiwa kitovu ni cha ndani, uchafu na unyevunyevu vinaweza kujikusanya na kusababisha muwasho au maambukizi ambayo huleta maumivu unapokigusa.
Maumivu yanayojitokeza unapobonyeza yanaweza pia kuwa yanatokana na viungo vya ndani ya tumbo badala ya kitovu chenyewe. Kwa mfano, mwanzoni mwa ugonjwa wa appendicitis maumivu huanza karibu na kitovu kabla hayajahamia upande wa chini kulia wa tumbo. Vivyo hivyo, matatizo ya utumbo mdogo, tezi za limfu zilizovimba au majeraha ya misuli yanaweza kufanya eneo la kitovu kuwa laini na lenye maumivu unapoligusa.
Iwapo maumivu yanaendelea kwa zaidi ya siku chache, yanaongezeka, yanaambatana na uvimbe, usaha, harufu mbaya, homa au kutokwa na damu, ni muhimu kufika hospitalini kwa uchunguzi. Epuka kubonyeza kitovu mara kwa mara au kuingiza vitu vyenye ncha kali ndani yake kwani vinaweza kuongeza maambukizi au kuharibu ngozi ya eneo hilo.
2. Je, maumivu ya kitovu yanaweza kuwa dalili ya ujauzito?
Maumivu ya kitovu pekee si dalili ya kuthibitisha ujauzito. Katika wiki za mwanzo za ujauzito wanawake wengi hupata mabadiliko mbalimbali mwilini kama maumivu madogo ya tumbo, kujaa gesi, kuvimbiwa au hisia za kuvutwa tumboni ambazo wakati mwingine zinaweza kuhisiwa karibu na kitovu. Hata hivyo, dalili hizi zinaweza pia kusababishwa na magonjwa mengine yasiyohusiana na ujauzito.
Kadiri ujauzito unavyokua, uterasi huongezeka ukubwa na kunyoosha misuli na mishipa ya ukuta wa tumbo. Hali hii inaweza kusababisha maumivu au hisia za kuvutika karibu na kitovu hasa wakati wa kusimama, kukohoa, kucheka au kubadilisha mkao. Kwa baadhi ya wanawake, kitovu kinaweza pia kujitokeza nje na kuwa nyeti zaidi kuliko kawaida.
Ikiwa mwanamke anashuku ujauzito, njia sahihi ni kufanya kipimo cha ujauzito baada ya kuchelewa hedhi au kufanyiwa kipimo hospitalini. Endapo maumivu ya kitovu yanaambatana na kutokwa na damu ukeni, maumivu makali upande mmoja wa tumbo, kizunguzungu au kuzimia, anapaswa kuwahi hospitali kwani yanaweza kuashiria mimba ya nje ya mfuko wa uzazi ambayo ni hali ya dharura.
3. Maumivu ya kitovu yanamaanisha nina apendeksi(maambukizi ya kidole tumbo)?
Sio kila maumivu ya kitovu yanamaanisha mtu ana appendicitis, lakini ni kweli kwamba ugonjwa huu mara nyingi huanza kwa maumivu karibu na kitovu. Katika hatua za mwanzo, maumivu huwa hafifu na yanaweza kuzunguka eneo la kitovu kabla ya kuhamia upande wa chini kulia wa tumbo ndani ya saa kadhaa. Hii ndiyo sababu appendicitis mara nyingi huchanganywa na matatizo mengine ya tumbo mwanzoni.
Kadiri ugonjwa unavyoendelea, maumivu huwa makali zaidi na huambatana na dalili kama homa, kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika na maumivu makali wakati wa kutembea, kukohoa au kuruka. Wagonjwa wengi pia huhisi tumbo kuwa gumu na kugusa eneo husika kunakuwa na maumivu makali.
Kwa kuwa appendicitis inaweza kusababisha kupasuka kwa appendix na maambukizi makubwa ndani ya tumbo, ni muhimu kutafuta matibabu mapema ikiwa maumivu yanaendelea kuongezeka au kuhamia upande wa chini kulia. Usitumie dawa nyingi za kutuliza maumivu kabla ya kufanyiwa uchunguzi kwa sababu zinaweza kuficha dalili muhimu zinazomsaidia daktari kufanya utambuzi.
4. Kwa nini maumivu ya kitovu huongezeka nikikohoa, kupiga chafya au kuinua vitu vizito?
Kuongezeka kwa maumivu wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuinua mizigo mara nyingi kunahusiana na ongezeko la shinikizo ndani ya tumbo. Ikiwa kuna udhaifu kwenye misuli ya ukuta wa tumbo, hernia ya kitovu, au misuli iliyochanika, shinikizo hili husababisha eneo hilo kuvutika zaidi na hivyo kuongeza maumivu. Hii ndiyo sababu baadhi ya watu huhisi maumivu tu wanapofanya shughuli zinazotumia nguvu.
Katika hernia ya kitovu, sehemu ya utumbo au mafuta ya ndani ya tumbo inaweza kusukuma kupitia sehemu dhaifu ya ukuta wa tumbo. Mtu anaweza kuona uvimbe unaojitokeza karibu na kitovu hasa anapokohoa au kusimama. Hernia ndogo inaweza isiwe na maumivu makubwa mwanzoni, lakini inaweza kuanza kuuma kadiri muda unavyopita.
Ikiwa uvimbe unakuwa mgumu, hauingii ndani unapolala, unaambatana na maumivu makali, kutapika au kushindwa kutoa choo au gesi, hiyo inaweza kuwa dalili ya hernia iliyokwama na inahitaji matibabu ya haraka. Kwa hali zisizo za dharura, daktari anaweza kupendekeza kufuatiliwa au kufanyiwa upasuaji kulingana na ukubwa wa tatizo.
5. Je, maumivu ya kitovu yanaweza kusababishwa na gesi tumboni?
Ndiyo. Gesi nyingi ndani ya utumbo ni moja ya sababu zinazoweza kusababisha maumivu karibu na kitovu. Gesi zinapojikusanya kwenye utumbo mdogo au mpana, husababisha utumbo kutanuka na hivyo kuleta hisia za maumivu, kubanwa au kujaa tumboni. Mara nyingi maumivu haya hubadilika sehemu na yanaweza kupungua baada ya mtu kujamba au kupata choo.
Baadhi ya vyakula kama maharage, kabichi, broccoli, soda, vyakula vyenye sukari nyingi na kula haraka vinaweza kuongeza uzalishaji wa gesi. Watu wenye matatizo ya kutovumilia maziwa au baadhi ya vyakula pia wanaweza kupata maumivu ya kitovu yanayosababishwa na gesi mara kwa mara.
Iwapo maumivu yanapungua baada ya kutoa gesi au kubadilisha mlo, mara nyingi si tatizo kubwa. Hata hivyo, ikiwa gesi zinaambatana na kupungua uzito bila sababu, damu kwenye kinyesi, homa, kutapika mara kwa mara au maumivu makali yasiyopungua, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi ili kuondoa uwezekano wa magonjwa mengine ya utumbo.
6. Kwa nini kitovu kinatoa harufu mbaya na kuuma kwa wakati mmoja?
Kitovu kina mikunjo inayoweza kuhifadhi jasho, mafuta ya ngozi, seli zilizokufa na uchafu. Endapo usafi hautazingatiwa au unyevunyevu utabaki kwa muda mrefu, bakteria na fangasi wanaweza kuongezeka na kusababisha maambukizi. Maambukizi haya huweza kuleta harufu mbaya, maumivu, wekundu, kuwasha na wakati mwingine kutokwa na usaha.
Watu wenye kisukari, uzito mkubwa au wanaotoboa kitovu kwa ajili ya hereni wanaweza kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya kitovu. Vilevile, ikiwa kuna uvimbe mdogo au mfuko wenye uchafu ndani ya kitovu, dalili zinaweza kujirudia mara kwa mara hata baada ya kusafisha eneo hilo.
Usitumie dawa za kupaka bila ushauri wa mtaalamu wa afya. Safisha kitovu kwa upole kwa maji safi na sabuni laini, kisha kikaushe vizuri. Ikiwa kuna usaha, harufu kali, homa, uvimbe unaoongezeka au maumivu makali, unapaswa kufika hospitalini kwa uchunguzi na matibabu sahihi.
7. Je, watoto wanaopata maumivu ya kitovu huwa na ugonjwa mkubwa?
Watoto wengi hupata maumivu ya kitovu kutokana na sababu zisizo hatari kama gesi tumboni, kuvimbiwa, maambukizi ya virusi au maumivu ya kawaida ya tumbo. Kwa baadhi ya watoto wa umri wa shule, msongo wa mawazo au hofu pia unaweza kujionyesha kama maumivu yanayozunguka kitovu bila kuwepo ugonjwa mkubwa wa mwili.
Hata hivyo, maumivu ya kitovu kwa mtoto yanahitaji kuchukuliwa kwa uzito ikiwa yanaendelea kwa muda mrefu, yanazidi kuwa makali au yanaambatana na homa, kutapika mara kwa mara, kushindwa kula, kuharisha damu au tumbo kuvimba. Katika baadhi ya watoto, appendicitis huanza kwa maumivu karibu na kitovu kabla ya kuhamia upande wa kulia wa tumbo.
Mzazi hapaswi kumpa mtoto dawa za maumivu mara kwa mara bila kujua chanzo cha tatizo. Ikiwa mtoto anaonekana mchovu sana, analia kutokana na maumivu, anakataa kula au kunywa, au ana dalili nyingine zinazotia wasiwasi, apelekwe hospitalini mapema kwa uchunguzi wa kina.
8. Maumivu ya kitovu baada ya kufanya mazoezi ni ya kawaida?
Ndiyo, kwa baadhi ya watu maumivu ya kitovu yanaweza kutokea baada ya mazoezi makali, hasa yanayohusisha misuli ya tumbo kama kukimbia, kunyanyua vyuma, kufanya sit-ups au mazoezi ya nguvu. Misuli inapovutika kupita kiasi inaweza kusababisha maumivu yanayohisiwa karibu na kitovu kwa saa kadhaa au siku chache.
Wakati mwingine mazoezi yanaweza kufichua hernia ya kitovu ambayo hapo awali haikuwa na dalili. Ikiwa maumivu yanaambatana na uvimbe unaojitokeza karibu na kitovu wakati wa kusimama au kufanya mazoezi, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kama kuna udhaifu wa ukuta wa tumbo.
Ili kupunguza hatari ya maumivu, fanya mazoezi ya kujinyoosha kabla na baada ya mazoezi, ongeza uzito wa mazoezi taratibu na tumia mbinu sahihi. Ikiwa maumivu ni makali, yanadumu kwa muda mrefu au yanarudi kila unapofanya mazoezi, wasiliana na daktari badala ya kuendelea kufanya mazoezi huku ukiwa na maumivu.
9. Je, maumivu ya kitovu yanaweza kuwa yanatokana na minyoo?
Minyoo wa utumbo wanaweza kusababisha maumivu ya tumbo yanayohisiwa karibu na kitovu, hasa kwa watoto lakini pia kwa watu wazima. Mbali na maumivu, mtu anaweza kuwa na kujaa gesi, kukosa hamu ya kula, kupungua uzito, kuwashwa sehemu ya haja kubwa hasa usiku au kuona minyoo kwenye kinyesi kulingana na aina ya maambukizi.
Hata hivyo, si kila maumivu ya kitovu husababishwa na minyoo. Kuna magonjwa mengi ya utumbo yanayoweza kutoa dalili zinazofanana, hivyo si sahihi kutumia dawa za minyoo kila unapopata maumivu ya kitovu bila kufanyiwa uchunguzi. Wakati mwingine tatizo linaweza kuwa maambukizi ya kidole tumbo, maambukizi ya utumbo, vidonda vya tumbo au ugonjwa mwingine unaohitaji matibabu tofauti.
Ikiwa unashuku maambukizi ya minyoo, ni vyema kufika kituo cha afya kwa uchunguzi wa kinyesi au vipimo vingine vinavyofaa. Pia zingatia usafi wa mikono, matumizi ya maji salama, kunawa matunda na mboga vizuri na kupika chakula kikamilifu ili kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya minyoo.
10. Nifanye nini ikiwa maumivu ya kitovu hayapungui kwa siku kadhaa?
Maumivu ya kitovu yanayoendelea kwa zaidi ya siku chache bila kupungua yanahitaji tathmini ya kitabibu. Ingawa baadhi ya sababu kama gesi au kuvimbiwa huweza kuisha zenyewe, maumivu yanayoendelea yanaweza kuwa ishara ya ugonjwa unaohitaji matibabu kama maambukizi ya kidole tumbo(homa ya kidole tumbo) henia(ngiri), maambukizi, magonjwa ya utumbo au matatizo ya mfumo wa mkojo.
Unaposubiri kufika hospitalini, unaweza kuendelea kunywa maji ya kutosha, kula chakula chepesi kinachosagika kwa urahisi na kuepuka kuinua vitu vizito ikiwa maumivu yanaongezeka wakati wa kufanya kazi. Pia ni muhimu kufuatilia dalili nyingine kama homa, kutapika, kuharisha, kutokwa na usaha kwenye kitovu au maumivu yanayohamia sehemu nyingine za tumbo kwa kuwa taarifa hizi zitamsaidia daktari katika utambuzi.
Usichelewe kutafuta huduma za afya ikiwa maumivu yanakuwa makali ghafla, tumbo linaanza kuvimba, unashindwa kutoa choo au gesi, unatapika mfululizo, unazimia au unaona damu kwenye matapishi au kinyesi. Uchunguzi wa mapema husaidia kugundua chanzo halisi cha maumivu na kuanza matibabu kabla ya tatizo kuwa kubwa zaidi.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
7 Machi 2025, 09:25:16
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada hii:
Mayo Clinic. Umbilical hernia: symptoms & causes [Internet]. Rochester (MN): Mayo Foundation for Medical Education and Research; [date unknown] [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.mayoclinic.org
Verywell Health. Belly button pain: common causes and when to seek care [Internet]. [place unknown]: Verywell Health; 2023 [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.verywellhealth.com
Cincinnati Children's Hospital. Umbilical hernia: causes, symptoms, diagnosis & treatment [Internet]. Cincinnati (OH): Cincinnati Children's Hospital Medical Center; [date unknown] [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.cincinnatichildrens.org
WebMD. Caring for your belly button: how to prevent problems [Internet]. [place unknown]: WebMD; 2023 [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.webmd.com
Johns Hopkins Medicine. Umbilical hernia [Internet]. Baltimore (MD): Johns Hopkins Medicine; [date unknown] [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.hopkinsmedicine.org
Health.com. Belly button pain: causes, seriousness, relief [Internet]. [place unknown]: Health.com; 2023 [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.health.com
Medical News Today. 13 reasons for belly button pain [Internet]. [place unknown]: Medical News Today; 2023 [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.medicalnewstoday.com
MedicineNet. Belly button problems: infection symptoms, treatments, pain [Internet]. [place unknown]: MedicineNet; 2023 [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.medicinenet.com
Healthline. Periumbilical pain: causes of pain around the belly button [Internet]. [place unknown]: Healthline; 2023 [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://www.healthline.com
Cleveland Clinic. Belly button yeast infection: symptoms, causes & treatment [Internet]. Cleveland (OH): Cleveland Clinic; [date unknown] [cited 2026 Aug 8]. Available from: https://my.clevelandclinic.org
