Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
5 Mei 2020, 17:00:36

Maumivu ya tumbo kwa mwanamke (Mitoshimaz)
Mitoshimaz ni neno tiba linalotumiwa na ULY clinic kumaanisha “mittelschmerz”. Mittelschmerz ni neno lililotokana na neno la Kijerumani linalomaanisha “maumivu ya katikati” na kitiba linatumika kumaanisha maumivu ya tumbo upande mmoja wakati wa ovulesheni- yai linalotolewa kutoka kwenye ovari. Maumivu haya hutokea takribani kipindi cha siku 14 kabla ya kuona damu ya hedhi kwa mwanamke mwenye mzunguko wa hedhi wa siku 28. Hii inamaanisha maumivu katikati ya mzunguko wa hedhi kwa kuwa maumivu haya hutokea siku ya 14 kati ya siku 28.
Maumivu haya ya tumbo upande mmoja hutokana na kuvilia kwa dam una majimaji kiasi yanayotoka kipindi foliko inapasuka kutoa yai.
Je unahitaji kufanyiwa matibabu?
Mara nyingi jibu ni hapana. Hata hivyo licha ya kuwa maumivu haya mara nyingi hayahitaji matibabu, maumivu ya wastani yanaweza kutibiwa kwa dawa za kuondoa maumivu, lakini endapo maumivu ni makali zaidi unapaswa kutafuta msaada kutoka kwa daktari wako.
Utajuaje una maumivu ya mitoshimaz?
Maumivu ya mitoshimaz hutokea wiki mbili kabla ya kuona damu ya mwezi, ukipata maumivu haya kipindi hiki kama una mzunguko wa siku 28 ni dhahiri kuwa utakuwa na maumivu ya mitoshimaz.
Kuna magonjwa mengine yanaweza kusababisha maumivu ya tumbo la chini upande?
Ndio, magonjwa yafuatayo yanaweza kupelekea maumivu ya upande mmoja wat umbo ila si lazima yawe siku ya 14 kabla ya kuona damu ya hedhi;
Ovariani sisti
Apendisaitizi
Vidonda vya tumbo
PID
Faibroidi upande mmoja wa kizazi
Maumivu ya hedhi
Mimba kutungwa nje ya mfuko wa kizazi (mimba ya ekitopiki)
Payeronefraitizi
Maumivu ya misuli(kubana kwa misuli ya uzazi na tumbo)
Dalili
haya hudumu kwa muda wa dakika au masaa machache, wakati mwingine maumivu yanaweza kudumu kwa siku moja au mbili. Dalili mara nyingi huwa ni;
Maumivu ya upande mmoja wa tumbo
Maumivu butu na ya kubana
Maumivu yanaweza kuwa makali na ya ghafla
Huweza kuambatana na kutokwa damu au majimaji kiasi ukeni
Kwa mara chache sana maumivu yanaweza kuwa makali sana
Kisababishi ni nini?
Kisababishi halisi cha Mitoshimaz hakifahamiki, hata hivyo inafahamika kuwa, foliko inapopasuka kutoa yai, huambatana na kutokwa damu na majimaji. Damu na majimaji haya humwagikia kwenye ukuta wa peritoniamu na kusababisha inflamesheni inayoambatana na dalili ya maumivu upande mmoja wa tumbo la chini. Maumivu haya huhama kila mwezi kutoka upande mmoja kwenda mwingine kutokana na kupokezana utoaji wa yai(ovari) upande wa kushoto au kulia.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
8 Oktoba 2021, 04:53:20
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1.Offord medical dictionary
2.Dictionary.com. mittelschmerz. https://www.dictionary.com/browse/mittelschmerz. Imechukuliwa 4.5.2020
3.Blechman AN, et al. Evaluation and management of ruptured ovarian cyst. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 4.5.2020
4.Lower abdominal pain in women. https://www.netdoctor.co.uk/conditions/digestive-health/a11617/lower-abdominal-pain-in-women/