Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin Lugonda, MD

26 Julai 2026, 07:21:27
Rangi ya ute ukeni na maana yake kiafya
Majimaji (ute) ya kawaida yanayotoka ukeni huzalishwa na tezi ndogo zinazopatikana kwenye tundu la uke na shingo ya kizazi.
Majimaji au ute huu hutoka kila siku ili kuondoa chembe zilizokufa na uchafu na kufanya uke uwe kwenye hali safi ya kiafya. Kiasi na rangi ya majimaji yatokayo ukeni hutofautiana kila siku na kwa kila mtu mmoja na mwingine. Kiasi na rangi ya majimaji yatokayo ukeni hutofautiana kila siku na kwa kila mtu mmoja na mwingine.
Makala hii imeelezea aina za ute na maana yake kiafya. Ute umetumika kumaanisha majimaji ya kawaida au uchafu unaoweza kutoka ukeni.
Je ni rangi gani za ute unaoweza kutoka ukeni?
Kuna rangi mbalimbali za ute unaoweza kutoka ukeni, rangi hizo ni;
Ute mweupe kama maziwa
Ute wa rangi ya maji
Ute wa rangi nyekundu
Ute wa rangi ya kijivu
Ute wa rangi ya kijani
Ute wa rangi ya njano
Ute wa rangi ya bluu
Kila rangi imeelezewa hapa chini ni nini kinaweza kuwa kisababishi
Ute mweupe wa maji ukeni
Ute wa kawaida wa uke mara nyingi huwa na rangi ya uwazi au nyeupe hafifu kama maji. Watu wengi huuita "ute mweupe", lakini si mweupe kama maziwa. Pia huwa na utelezi unaofanana na ute wa bamia au ute wa yai bichi.
Ute huu huongezeka na kuwa mtelezi zaidi wakati wa:
Kipindi cha rutuba (ovulesheni), ambapo yai hutolewa.
Kusisimka kingono.
Ujauzito.
Matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango.
Ikiwa ute huu hauna harufu mbaya, hauambatani na kuwashwa, maumivu au muwasho, mara nyingi ni ute wa kawaida na hauhitaji matibabu.
Ute mweupe kama maziwa ukeni
Kutokwa na ute mweupe mzito kama maziwa, krimu au mtindi kunaweza kuwa hali ya kawaida au dalili ya maambukizi, kutegemeana na dalili zinazoambatana nao.
Ikiwa ute huu hauna harufu mbaya na hauambatani na kuwashwa, maumivu au kuchoma, mara nyingi ni ute wa kawaida unaosaidia kulainisha na kulinda uke.
Hata hivyo, ikiwa ute huu unaambatana na kuwashwa sana, muwasho, wekundu wa uke au maumivu wakati wa kukojoa au kujamiiana, unaweza kuashiria maambukizi ya fangasi ukeni. Fangasi mara nyingi husababisha ute mzito unaofanana na maziwa yaliyoganda au mtindi, na kwa kawaida hauna harufu kali.
Ikiwa ute mweupe una harufu mbaya au kali, hasa harufu inayofanana na samaki, unaweza kuashiria maambukizi ya bakteria ukeni (vajinosisi ya bakteria au wakati mwingine trikomoniasisi, hasa ikiwa kuna dalili nyingine kama kuwashwa au maumivu. Uchunguzi wa mtaalamu wa afya unahitajika ili kubaini chanzo halisi.
Ute wa rangi ya njano ukeni
Kutokwa na ute wa njano hafifu usioambatana na dalili nyingine wakati mwingine kunaweza kuwa ute wa kawaida, hasa ikiwa umechanganyika na ute wa kawaida wa uke. Mabadiliko madogo ya rangi yanaweza pia kuhusishwa na lishe, matumizi ya virutubisho au kukaa kwa ute ndani ya uke kabla ya kutoka.
Hata hivyo, ikiwa ute una rangi ya njano iliyokolea, njano ya kijani au kijani, hasa ukiwa na harufu mbaya, kuwashwa, maumivu wakati wa kukojoa au kujamiiana, unaweza kuashiria maambukizi, yakiwemo magonjwa ya zinaa kama trichomoniasis, kisonono (gono) au klamidia .
Kwa kuwa rangi ya ute pekee haiwezi kuthibitisha chanzo cha tatizo, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi na vipimo ili kubaini sababu halisi na kupata matibabu sahihi. Kujitibu bila kujua chanzo kunaweza kufanya tatizo liendelee au kujirudia.
Ute wa rangi nyekundu ukeni
Ute wa rangi nyekundu huweza kuwa na wekundu mpauko au mkoleo ama rangi ya kutu. Mara nyingi ute wa rangi nyekundu husababisha na hedhi.
Endapo ute unatoka ndani ya siku za hedhi kila mwisho wa mwezi yaani kila baada ya siku 28 hadi 35 kutoka mzunguko mmoja hadi mwingine hii humaanisha ute wa kawaida baada au kabla ya hedhi.
Endao ute wa rangi hii unatoka katikati ya mzunguko wa hedhi, hii mara nyingi huashiria matatizo mbalimbali kama matatizo ya homoni, saratani ya shingo ya kizazi n.k
Endapo ute mwekundu unaambatana na harufu kali ukeni na katikati ya hedhi au kwenye hedhi, maranyingi ina maanisha dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi.
Endapo upo kwenye koma hedhi kipindi angalau mwaka mmoja mfululizo na unatokwa na majimaji ya rangi nyekundu ukeni, inaweza kumaanisha saratani ya mji wa uzazi, au saratani ya shingo ya kizazi.
Ute wa rangi ya pinki ukeni
Ute wa pinki unaweza kuwa pinki mpauko au ile iliyokolea, hii husababishwa mara nyingi na uwepo wa damu kidogo.
Kutokwa na ute wa rangi ya pinki humaanisha unakaribia kuingia hedhi na endapo umeshika ujauzito, humaanisha upo kipindi cha upandikizaji wa yai lililochochavushwa mwanzoni kabisa mwa ujauzito.
Baadhi ya wanawake wakiwa siku za hatari (yai linapotolewa), hupata matone ya damu kidogo yanayoweza kupelekea ute ukeni kuwa na rangi ya pinki ambayo ni kawaida.
Ute wa pinki pia unaweza kutokea baada ya kushiriki ngono na umepata majeraha kidogo kwenye uke yaliyosababisha damu kuvia na hivyo ikachanganyika na kusababisha majimaji kuwa na rangi hiyo ya pinki.
Ute wa rangi ya kijivu ukeni
Kutokwa na ute wa rangi ya kijivu si hali ya kawaida na mara nyingi huashiria kuwepo kwa maambukizi ukeni. Sababu inayopatikana mara nyingi ni vajinosisi ya bakteria (BV), ambayo hutokea pale uwiano wa bakteria wa kawaida wanaoishi ukeni unapobadilika.
Mbali na ute wa rangi ya kijivu, dalili nyingine zinazoweza kuambatana ni:
Harufu kali inayofanana na samaki, hasa baada ya kujamiiana.
Kuwashwa au muwasho ukeni.
Hisia za kuchoma wakati wa kukojoa kwa baadhi ya wanawake.
Wakati mwingine dalili zinaweza kuwa chache au kutokuwepo kabisa.
Ingawa ute wa kijivu mara nyingi huhusishwa na vajinosisi ya bakteria, si wanawake wote wenye dalili hizi huwa na ugonjwa huo. Uchunguzi wa mtaalamu wa afya unaweza kusaidia kubaini chanzo halisi na kutoa matibabu yanayofaa.
Ute wa rangi ya kijani ukeni
Kutokwa na ute wa rangi ya kijani au njano unaoelekea kijani si kawaida na mara nyingi huashiria kuwepo kwa maambukizi ya uke au magonjwa ya zinaa. Miongoni mwa visababishi vinavyopatikana mara nyingi ni trikomoniasisi, na wakati mwingine kisonono(gono) au maambukizi mengine ya njia ya uzazi. Dalili zinazoweza kuambatana na ute huu ni pamoja na:
Harufu mbaya au kali.
Kuwashwa au muwasho ukeni.
Maumivu au hisia za kuchoma wakati wa kukojoa.
Maumivu wakati wa kujamiiana.
Ute kuwa mzito, wenye povu au wakati mwingine wenye mabonge.
Wekundu au uvimbe kwenye uke na sehemu zinazouzunguka.
Kwa kuwa ute wa kijani mara nyingi huhusishwa na maambukizi yanayohitaji matibabu maalumu, ni muhimu kumwona mtaalamu wa afya kwa uchunguzi na vipimo. Ikiwa chanzo ni ugonjwa wa zinaa, mwenzi wa ndoa au ngono anaweza pia kuhitaji uchunguzi na matibabu ili kuzuia maambukizi kurudi tena. Epuka kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu, kwani matibabu hutegemea aina ya maambukizi yaliyopo.
Ute wa rangi ya bluu ukeni
Kutokwa na ute wa rangi ya bluu si hali ya kawaida na si rangi inayotarajiwa kwa ute wa uke. Mara nyingi, ute wa rangi hii hauhusiani na mabadiliko ya kawaida ya mwili, hivyo unahitaji uchunguzi wa mtaalamu wa afya ili kubaini chanzo chake.
Baadhi ya sababu zinazoweza kufanya ute uonekane wa bluu au wenye mchanganyiko wa rangi ya bluu ni pamoja na:
Maambukizi makali ya uke, ingawa si sababu ya kawaida.
Mchanganyiko wa ute na dawa za uke, krimu au jeli zinazoweza kubadilisha rangi ya uchafu.
Rangi kutoka kwenye bidhaa zinazowekwa ukeni, kama baadhi ya dawa, vilainishi au bidhaa za usafi wa uke.
Mara chache sana, inaweza kuwa kutokana na mwanga au namna rangi inavyoonekana kwenye nguo za ndani au taulo za kike, badala ya ute wenyewe kuwa wa bluu.
Wakati gani unapaswa kuwasiliana na daktari haraka?
Endapo unatokwa na uchafu(ute) ukeni unaoambatana na dalili zifuatazo tafuta msaada wa daktari.
Kujihisi hali isiyo kawaida ukeni
Kutokwa na damu wakati wa kushiriki ngono
Kutokwa na damu katikati ya vipindi vya hedhi
Kutokwa na damuu baada ya komahedhi
Kutokwa na harufu mbaya ukeni kama ya kitu kilichooza (samaki)
Kutokwa na ute wa rangi ya kijani, njano au kijivu
Kutokwa na ute wenye povu
Maumivu
Muwasho wa uke
Uchafu ukeni unaoambatana na hisia za kuungua wakati wa kukojo
Wapi utapata taarifa zingine zaidi?
Soma zaidikuhusu
Soma kuhusu harufu mbaya ukeni na visababishi vyake
Soma pia kuhusu uchafu wa rangi ya bluu kijani ukeni
Kusoma kuhsu vajinosis ya bakteria
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara
1 Je, ni kawaida kutoka na ute kila siku?
Ndiyo, ni kawaida kabisa kwa mwanamke kuwa na ute ukeni kila siku kwa kiwango kidogo. Uke hutengeneza ute muda wote ili kujisafisha, kulainisha na kulinda dhidi ya maambukizi. Kiasi na muonekano wake hubadilika kulingana na homoni, siku za mzunguko wa hedhi, msisimko wa kimapenzi au matumizi ya uzazi wa mpango.
Kwa kawaida ute huwa mweupe au wa uwazi na hauna harufu kali. Lakini ukianza kuwa na harufu mbaya, rangi ya njano/kijani, kuwasha au kuungua, hiyo si hali ya kawaida na ni vyema kufanyiwa uchunguzi kituo cha afya.
2 Ute hubadilika kulingana na siku za mzunguko wa hedhi?
Ndiyo. Ute wa ukeni hubadilika kulingana na hatua za mzunguko wa hedhi kutokana na mabadiliko ya homoni estrojeni na projesteroni. Baada ya hedhi ute huwa kidogo na mzito, kadri siku zinavyosogea kuelekea siku ya uovuleshaji ute huwa mwingi, laini na wa uwazi kama yai bichi (dalili ya siku za hatari). Baada ya uovuleshaji, ute hurudi kuwa mzito au mweupe, na kabla ya hedhi unaweza kupungua tena.
Mabadiliko haya ni ya kawaida na husaidia kutambua siku za kupata mimba. Hata hivyo, ute ukiwa na harufu mbaya, rangi ya njano/kijani au kuwasha, si sehemu ya mzunguko wa kawaida na unahitaji uchunguzi.
3 Siku moja baada ya ngono nilitokwa na ute mweupe mwepesi na tumbo kuuma kama niko kwenye hedhi. Je, hii inamaanisha ujauzito au nina tatizo jingine?
1. Kuhusu ujauzito
Ujauzito hauwezi kugundulika mara moja baada ya tendo la ndoa. Yai linachukua siku 6–12 hivi kujipandikiza kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi, ndipo homoni za mimba zinaanza kutengenezwa na zinaweza kuonekana kwa vipimo.
Kwa hiyo, dalili ulizopata siku moja baada ya tendo (ute mweupe na maumivu ya tumbo) si dalili za mimba.
2. Sababu zinazowezekana za dalili zako
Ute mweupe mwepesi:Â Unaweza kuwa sehemu ya mzunguko wa kawaida wa hedhi (ute wa uovuleshaji) au ishara ya mabadiliko ya homoni.
Maumivu ya tumbo kama ya period:Â Hii inaweza kuwa dalili za kabla ya hedhi, uovuleshaji, au wakati mwingine ishara ya maambukizi madogo ya uke au kizazi.
Ikiwa ute ungekuwa na harufu mbaya, rangi ya kijani/kahawia, ukatoa muwasho au maumivu makali, basi ingeashiria zaidi maambukizi.
3. Nini cha kufanya
Subiri hadi kipindi chako cha hedhi kiishe au uchelewe ndipo unaweza kufanya kipimo cha ujauzito cha mkojo, mara nyingi kuanzia siku ya 7 baada ya hedhi kuchelewa.
Kama dalili zitaendelea (maumivu ya tumbo, ute usio wa kawaida, muwasho, au harufu mbaya), tafadhali muone daktari au nesi wa afya ya uzazi kwa uchunguzi wa maambukizi.
Hitimisho
Dalili ulizopata siku moja baada ya tendo la ndoa hazimaanishi mimba. Zinaweza kuwa mabadiliko ya kawaida ya homoni au dalili za tatizo jingine dogo.
4 Ute wa kawaida na ule wa maambukizi unatofautishwaje?
Tofauti kuu huonekana kwenye rangi, harufu na dalili zinazoambatana nao.
Ute wa kawaida:Â huwa mweupe au wa uwazi, laini, hauna harufu kali na hausababishi kuwasha au maumivu. Mara nyingi hubadilika kulingana na mzunguko wa hedhi, hasa kipindi cha rutuba au kabla ya hedhi.
Ute wa maambukizi:Â hubadilika kuwa wa njano, kijani au kijivu, huwa na harufu mbaya (wakati mwingine kama samaki), na huambatana na dalili kama kuwasha, kuungua wakati wa kukojoa au maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Ukiona mabadiliko yasiyo ya kawaida au dalili za muwasho, ni muhimu kufika kituo cha afya kwa uchunguzi na matibabu sahihi mapema.
5 Je, chakula ninachokula kinaweza kubadilisha ute wa ukeni?
Ndiyo, lishe inaweza kuathiri kiasi na harufu ya ute wa ukeni kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Vyakula vyenye sukari nyingi vinaweza kuongeza hatari ya fangasi kwa sababu huongeza ukuaji wa bakteria na kuvu mwilini, wakati maji ya kutosha, matunda na vyakula vyenye probiotic (kama mtindi) husaidia kudumisha uwiano mzuri wa bakteria wa uke.
Hata hivyo, chakula peke yake mara nyingi hubadilisha harufu au kiasi kidogo tu, si rangi kali au kuwasha. Ukiona ute wa njano/kijani, harufu mbaya au muwasho, huenda si chakula bali ni maambukizi — hivyo ni vyema kufanya uchunguzi kituo cha afya.
6 Kwanini wakati wa ujauzito ute huongezeka?
Wakati wa ujauzito mwili huzalisha homoni nyingi zaidi, hasa estrojeni na projesteroni, ambazo huongeza mtiririko wa damu kwenye uke na kuchochea tezi zake kutoa ute mwingi (leukorrhea). Ute huu husaidia kulinda mfuko wa uzazi dhidi ya bakteria na maambukizi, hivyo ni hali ya kawaida kwa wajawazito.
Kwa kawaida huwa mweupe au wa uwazi na hauna harufu kali. Lakini ukibadilika kuwa na harufu mbaya, rangi ya njano/kijani, kuwasha au maumivu, inaweza kuashiria maambukizi na ni muhimu kumuona mtaalamu wa afya mapema.
7 Je, matumizi ya dawa za homoni au uzazi wa mpango yanaweza kuathiri ute?
Ndiyo. Dawa za homoni na njia nyingi za uzazi wa mpango (kama vidonge, sindano, vipandikizi au kitanzi chenye homoni) hubadilisha kiwango cha estrojeni na projesteroni mwilini, hali inayoweza kuongeza au kupunguza ute ukeni. Baadhi ya wanawake hupata ute mwingi mweupe au wa uwazi bila harufu, wakati wengine hupata ukavu kidogo — yote ni athari za kawaida za homoni na si ugonjwa.
Hata hivyo, kama ute utabadilika kuwa na harufu mbaya, rangi ya njano/kijani, au kuambatana na kuwasha na maumivu, inaweza kuwa maambukizi yasiyohusiana na uzazi wa mpango, hivyo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi kituo cha afya.
8 Ute mweupe mzito kama maziwa bila harufu mbaya ni kawaida?
Ndiyo, mara nyingi ute mweupe mzito kama maziwa bila harufu mbaya huwa wa kawaida. Hutokea kutokana na mabadiliko ya homoni, hasa baada ya ovulation, kabla ya hedhi, au wakati wa ujauzito wa mapema. Ute huu husaidia kulinda uke na kudumisha mazingira salama dhidi ya bakteria.
Hata hivyo, kama utaanza kuambatana na kuwasha, kuungua, maumivu wakati wa kukojoa au kuwa kama mabonge ya jibini, inaweza kuashiria fangasi na ni vyema kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu sahihi.
9 Kwa nini ute unaweza kuongezeka baada ya kushiriki ngono?
Kuongezeka kwa ute ukeni baada ya tendo la ndoa mara nyingi ni hali ya kawaida. Wakati wa msisimko wa kimapenzi, tezi za uke hutengeneza majimaji mengi ili kulainisha uke na kupunguza msuguano. Pia, baada ya tendo mbegu za kiume na majimaji ya uke huchanganyika na kutoka taratibu baadaye, hali inayoweza kuonekana kama ute umeongezeka.
Hata hivyo, ute huo unapaswa kuwa hauna harufu kali wala kuwasha. Ukianza kuwa na harufu mbaya, rangi ya njano/kijani au kuambatana na muwasho, inaweza kuashiria maambukizi kama fangasi au bakteria na ni vyema kufanya uchunguzi kituo cha afya.
10. Ni wakati gani nitaweza kupima ujauzito ili kujua kwa uhakika?
Kawaida kipimo cha mkojo cha ujauzito hufanyika kuanzia siku ya 7 baada ya hedhi kuchelewa, na ndio kinatoa majibu sahihi zaidi.
11. Nimetokwa na maji ukeni lakini sisikii maumivu — je ni dalili ya ugonjwa?
Mara nyingi kutokwa na maji ukeni bila maumivu si ugonjwa bali ni hali ya kawaida ya mwili. Uke hutengeneza ute kusaidia kujisafisha, kulainisha na kurahisisha mbegu za kiume kufika kwenye yai. Hali hii huonekana zaidi wakati wa kipindi cha rutuba (uovuleshaji), mabadiliko ya homoni, msisimko wa kimapenzi, matumizi ya uzazi wa mpango, au ujauzito wa mapema. Ute wa kawaida huwa mweupe au wa uwazi, hauna harufu kali na hausababishi kuwasha.
Hata hivyo, inaweza kuashiria maambukizi kama fangasi, bacterial vaginosis au magonjwa ya zinaa endapo ute una harufu mbaya ya samaki, rangi ya njano/kijani/kijivu, unawasha, unaunguza au unatoka kwa muda mrefu bila kuisha. Ukiona mabadiliko hayo au hali inaendelea zaidi ya siku 5–7, ni vyema kufika kituo cha afya kwa uchunguzi ili kupata matibabu sahihi mapema.
12. Je, kutokwa na uchafu mweupe ukeni kunaweza kusababisha ushindwe kuona siku zako?
Hapana — uchafu mweupe haucheleweshi wala kufanya ushindwe kuona hedhi, iwe ni uchafu wa kawaida au ule wa fangasi.
1. Uchafu mweupe wa kawaida
Huu hutokea kutokana na mabadiliko ya homoni wakati wa mzunguko wa hedhi. Huweza kuongezeka kabla ya hedhi au wakati wa ovulation. Hauna uwezo wa kuzuia hedhi kutoka.
2. Uchafu mweupe wa fangasi
Mara nyingi huwa una kuwasha na mnato zaidi na kwa kawaida hauchangii kukosa hedhi, lakini huleta tu usumbufu ukeni.
Kwa nini basi hedhi inaweza kuchelewa?
Kuchelewa hedhi kunahusishwa zaidi na:
Mabadiliko ya homoni
Msongo wa mawazo
Usingizi hafifu
Mabadiliko ya uzito
Mzunguko kutokuwa thabiti (haswa kwa wasichana walio kwenye ujana)
Kwa ujumla, uchafu mweupe uwe wa kawaida au wa fangasi si kisababishi cha kukosa hedhi. Ni mabadiliko ya homoni ndiyo yanaweza kuathiri uchafu na muda wa hedhi kwa wakati mmoja.
13. Je, uchafu mweupe ambao upo kama tishu ni ishara gani ukeni?
Uchafu mweupe unaofanana na rangi ya tishu unaweza kutokea kama sehemu ya mabadiliko ya kawaida ya mwili, hasa kabla au baada ya hedhi. Kama hauna harufu mbaya, muwasho, au maumivu, mara nyingi huu ni uchafu wa kawaida wa uke.
Hata hivyo, ikiwa uchafu huo ni:
Mweupe na mzito kama maziwa mgando,
Unaambatana na muwasho,
Una harufu kali, au
Unaambatana na hisia za kuungua ukeni,
hii inaweza kuashiria maambukizi ya fangasi au hali nyingine ya kiafya inayohitaji tathmini ya kitaalamu. Ni muhimu kumwona mtoa huduma wa afya ili kupata ushauri sahihi na uchunguzi unaofaa.
14. Nimejiona nina tofauti ukeni, nimeanza kutokwa na uchafu mweupe wenye harufu. Ni dalili za nini?
Kutokwa na uchafu mweupe wenye harufu ukeni kunaweza kuwa dalili ya hali mbalimbali, na si mara zote huwa ni jambo la kawaida. Kwa kawaida, uke hutoa uchafu mweupe au wa uwazi usio na harufu kali, ambao husaidia kuusafisha na kuulinda dhidi ya maambukizi. Hata hivyo, uchafu unapobadilika rangi, kuwa na harufu mbaya au kali, au kuambatana na kuwashwa, muwasho, maumivu au kuchoma wakati wa kukojoa, inaweza kuashiria kuwepo kwa maambukizi au tatizo jingine la kiafya.
Moja ya sababu zinazopatikana mara nyingi ni vajinosisi yabakteria (BV), ambayo hutokea pale uwiano wa bakteria wa kawaida ukeni unapobadilika. Hali hii mara nyingi husababisha uchafu mweupe au wa kijivu wenye harufu kali inayofanana na samaki, hasa baada ya kujamiiana. Sababu nyingine ni fangasi wa ukeni, ambao mara nyingi husababisha uchafu mweupe mzito unaofanana na maziwa yaliyoganda na huambatana na kuwashwa sana, ingawa kwa kawaida hauna harufu kali. Baadhi ya magonjwa ya zinaa, kama trikomoniasisi, yanaweza pia kusababisha uchafu wenye harufu mbaya, pamoja na kuwashwa au maumivu.
Ni muhimu kufahamu kuwa dalili hizi pekee haziwezi kuthibitisha chanzo cha tatizo. Uchunguzi wa mtaalamu wa afya na, inapohitajika, vipimo vya uchafu wa uke husaidia kubaini sababu halisi na kuchagua matibabu sahihi. Epuka kujinunulia dawa bila ushauri wa kitaalamu, kwani kutumia dawa isiyo sahihi kunaweza kufanya tatizo liendelee au kujirudia.
Muone mtaalamu wa afya mapema ikiwa:
Harufu ni kali au inazidi kuongezeka.
Unapata kuwashwa, maumivu au vidonda ukeni.
Uchafu umebadilika na kuwa wa kijani, njano au wenye damu bila sababu ya hedhi.
Una maumivu ya tumbo la chini au homa.
Wewe ni mjamzito na umeanza kupata uchafu wenye harufu au dalili nyingine zisizo za kawaida.
Kwa uchunguzi na matibabu sahihi, sababu nyingi za kutokwa na uchafu wenye harufu zinaweza kutibiwa kwa mafanikio. Kupata huduma mapema husaidia kuzuia madhara na kupunguza uwezekano wa tatizo kujirudia.
15. Kutoka na majimaji ukeni yenye harufu na rangi ya krimu ni ugonjwa gani?
Kutokwa na majimaji ukeni yenye harufu isiyo ya kawaida na rangi ya krimu hakumaanishi moja kwa moja kuwa una ugonjwa mmoja maalumu. Dalili hizi zinaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali, na chanzo chake kinaweza kujulikana baada ya kufanyiwa uchunguzi na vipimo.
Baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha hali hii ni vajinosisi ya bakteria (BV), ambayo mara nyingi husababisha uchafu wenye rangi ya kijivu au nyeupe na harufu inayofanana na samaki; fangasi ukeni, ambao unaweza kusababisha uchafu mzito wa rangi nyeupe au ya krimu unaofanana na maziwa yaliyoganda na mara nyingi huambatana na kuwashwa; pamoja na maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama trichomoniasis, kisonono (gono) au klamidia, ambayo yanaweza pia kusababisha uchafu usio wa kawaida wenye harufu, hasa kama kuna maumivu wakati wa kukojoa au kufanya tendo la ndoa.
Kwa kuwa dalili zinazofanana zinaweza kusababishwa na magonjwa tofauti, haiwezekani kujua ugonjwa husika kwa kuangalia rangi au harufu ya majimaji pekee. Unashauriwa kufika kituo cha afya kwa uchunguzi ili kubaini chanzo na kupata matibabu sahihi. Tafuta huduma ya haraka ikiwa majimaji yanaambatana na maumivu makali ya tumbo la chini, homa, kutokwa na damu isiyo ya kawaida, au ikiwa una ujauzito. Kuepuka kujinunulia dawa bila uchunguzi ni muhimu, kwani matibabu hutegemea chanzo halisi cha tatizo.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
17 Juni 2021, 11:47:37
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. 5 Types of vaginal discharge & what they mean.
https://www.unitypoint.org/livewell/article.aspx?id=06f8f035-9f6e-4a79-bb58-9045b9d7d0d8. Imechukuliwa 16.06.2021
2. Merck manual. Vaginal discharge. https://www.merckmanuals.com/home/women-s-health-issues/symptoms-of-gynecologic-disorders/vaginal-discharge. Imechukuliwa 16.06.2021
3. Vaginal discharge. http://www.pamf.org/teen/health/femalehealth/discharge.html. Imechukuliwa 16.06.2021
4. Vaginal discharge. https://familydoctor.org/condition/vaginal-discharge/. Imechukuliwa 16.06.2021. Imechukuliwa 16.06.2021
5. Vaginal discharge. https://www.hhs.gov/opa/reproductive-health/fact-sheets/vaginal-discharge/index.html. Imechukuliwa 16.06.2021
6. Vaginal discharge. https://www.sutterhealth.org/health/teens/female/vaginal-discharge. Imechukuliwa 16.06.2021
7. Vaginal discharge.https://www.drugs.com/health-guide/vaginal-discharge.html. Imechukuliwa 16.06.2021
8. What's the cervical mucus method of FAMs?. https://www.plannedparenthood.org/learn/birth-control/fertility-awareness/whats-cervical-mucus-method-fams. Imechukuliwa 16.06.2021
