top of page

Mwandishi:

Mhariri:

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

17 Juni 2021 20:22:35

Shambulio la Kizunguzungu pozi kipole
shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.

Shambulio la Kizunguzungu pozi kipole

Shambulio la kizunguzungu pozi kipole (SKPKP) ni moja ya kisababishi kikuu cha hisia ya ghafla ya kuzunguka au kuhisi vilivyomo ndani ya kichwa vinazunguka kwa kipindi kifupi nahuweza kutokea na dalili za wastani au kali.


SKPKP hutokea wakati wa kubadilisha pozi la kichwa, mfano wakati unainua kichwa ili kuangalia juu au kuangalia chini, wakati unalala au wakati unaamka kukaa kitandani.


Tatizo hili huweza kusumbua sana lakini huwa si kali isipokuwa linaongeza hatari ya kuanguka kirahisi.

SKPKP hutibiwa kwa kutumia manuva mbalimbali zilizoelezewa kwenye Makala hii na mtaalamu wa afya anayefahamu kuhusu tatizo hili.


Dalili


Dalili za shambulio la kizungunzugu pozi kipole huweza kutokea na ndani ya dakika moja na wakati mwingine kizunguzungu hiki hupotea kwa muda mrefu bila kutokea na kabla ya kutokea mara nyingi hutanguliwa na kucheza kwa macho pasipo udhibiti na kufuatiwa na;


 • Kizunguzungu

 • Hisia ya vinvitu avyokuzunguka kuwa vinazunguka

 • Kukosa uwiano wakati wa kutembea

 • Kichefuchefu

 • Kutapika


Shughuli gani zinaamsha dalili za SKPKP?


Shughuli zinazoamsha kizunguzungu cha SKPKP hazifanani kati ya mtu mmoja na mwingine lakini zote hutokana na kubadili pozi la kichwa na huweza kuwa;


 • Kusimama

 • Kuteembea

 • Unapotaka kuamka au kulala haswa endapo umekaa kwa muda mrefu

 • Kujigeuza kitandani

 • Kuangalia juu

 • Kupanda au kutoka kitandani

 • Kutikisa kichwa kwa haraka

 • Kuinama


Visababishi


Kisababishi halisi cha kizunguzungu cha SKPKP hakifahamiki mpaka sasa. Lakini inafahamika kuhusiana na;


 • Majeraha madogo au makubwa ya kubamiza kichwa

 • Majeraha ya upasuaji wa sikio la kati

 • Kipanda uso


Nini hutokea ndani ya sikio hadi kupata dalili za kizunguzungu cha SKPKP?


Ndani ya skio kuna ogani ndogo inayoitwa Vestibula labrinthi na mirija mitatu yenye vinyweleo ambavyo hufanya kazi kama kitambuzi cha pozi la kichwa kilipo(angalia kwenye picha ya sikio mfano kipo juu au chini kushoto au kulia.


Ndani ya mirija ya sikio la ndani pia kuna mawe ya kalisiamu ambayo yamekaa kwenye eneo linalotambua mvutano wa kichwa. Mawe haya huweza kuhama sehemu yalipo na hivyo kuhamisha sehemu halisi ya mvutano wa kichwa inayotambuliwa na ubongo wako kisha kupeleka kuwa na hisia zaidi zisizo kawaida za pozi la kichwa haswa wakati umelala na kukufanya uhisi kizunguzungu.


Hisia zisizo za kawaida pia hupelekea macho kucheza cheza bila sababu kutoka upande mmoja hadi mwingine, juu au chini na kusababisha uone kana kwamba vitu vinavyokuzunguka au vilivyo ndani ya kichwa chako vinazunguka.


Vihatarishi


Shambulio la kizunguzungu pozi kipole huweza kutokea kwenye umri wowote, licha ya hivyo, hutokea sana kwa watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea. Vihatarishi vingine nii;


 • Kuwa mwanamke (hutokea kwa wanawake kuliko wanaume)

 • Kuwa na madhaifu ya uwiano kwenye sikio la ndani

 • Kuwa na historia ya kufanyiwa upasuaji wa sikio

 • Kuwa na historia ya majeraha kichwani

 • Kuwa na kisukari

 • Kuugua kipanda uso


Utambuzi


Ili daktari atambue tatizo la SKPKP atakuuliza na atachunguza mwili wako kuhusu;


 • Dalili ya kizunguzungu inayoamshwa na mijongeo ya macho isiyo na mpangilio

 • Kizunguzungu kinachotokea wakati unalalia mgongo huku kichwa kimegeukia upande mmoja

 • Kujongea kwa macho bila mpangilio kutoa upande mmoja kwenda mwingine

 • Kushindwa kudhibiti mijongeo ya macho


Vipimo


Baaada ya kuangalia kizunguzungu chako, vipimo vifuatavyo vinaweza pendekezwa fanyika;


Kipimo cha ENG- kuangalia kama kizunguzungu chako kinatokana na ugonjwa ndani ya sikio au kwa sababu zingine za uwiano kutokana na kukosekana kwa uwiano wa hewa na maji ndani ya sikio.

Kipimo cha MRI- huangalia ogani mbalimbali ndani ya kichwa na kutambua magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababisha tatizo hili.


Matibabu


Kizunguzungu cha SKPKP kinaweza potea chenyewe bila matibabu ndani ya wiki chache au miezi kadhaa endapo ubongo utapata taarifa nzuri kutoka kwenye sikio lako. Endapo hakijapotea kwa haraka daktari wa mazoezi atakufanyia tiba zifuatazo ili kuleta uwiano wa ogani za ndani ya sikiona kupata nafuu au kupona haraka;


Kurejesha kwenye makazi yake sahihi mawe ya kalisiamu ndani ya sikio

Ikiwa daktari ameshatambua sehemu mawe ya kalisiamu yaliohamia, anaweza kukufanyia tiba ifuatayo ili kurejesha mawe ya kalisiamu kwenye makazi yake;


Maneva ya Epley

Maneva ya epiley ni njia ya kurejesha mawe yaliyohama ndani ya sikio kwenye makazi yake asilia. Hufanywa na mtaalamu aliyebokea kwa;


 • Kukuomba kwenye kitanda ukiwa umefumbua macho kisha kugeuza kichwa kwenye nyuzi 45 upande wa kulia

 • Baada ya hatua ya kwanza, wakati umeshika pembeni ya kitanda, utaambiwa kulalia mgongo ghafla na kupumzikia kwenye pozi ambalo kichwa chako kitaning’inia nyuzi 20 kutoka kwenye kitanda kisha

 • Kichwa chako kitageuzwa nyuzi 90 upande wa kushoto na

 • Utasubiria kwa sekunde 30 kisha

 • Utaambiwa usimame wima au kukaa upande wa kushoto wa meza


Endapo hutapata unafuu kwenye manuva hii, daktari atarudi hatua hizo mpaka upate. Angalia picha kwa uelewa zaidi.


Manuva ya Liberatori

Mawe yaliyohama sehemu yake kwenye sikio yanaweza kurudishwa pia kwa kufanya manuva ya liberatori. Njia hii huhusisha kujongesha kichwa kwa haraka kwenye mwelekeo wa sikio lenye shida ili kujaribu kutikisha mawe sehemu yalipo fanya makazi yasiyo sahihi. Mawe yanapokuwa huru kwa kutumia manuva hii, manuva nyingine hufanyika ili kuyaelekeza yaende kukaa sehemu yake asilia.


Tiba ya upasuaji

Endapo njia zote zimefeli, matibabu ya upasuaji yatafanyika.


Matibabu ya nyumbani ya shambulio la kizunguzungu pozi kipole (SKPKP)


 • Zuia mijongeo inayokuletea kizunguzungu kama kuangalia juu n.k

 • Kaa chini haraka unapohisi kizunguzungu

 • Kuwa makini wakati wote kwamba unaweza kupoteza uwiano na ukaanguka

 • Tumia tochi endapo unaamka usiku kuepuka kuanguka

 • Tumia miguu ya ziada wakati unatembea kuepuka kuanguka

 • Shirikiana na daktari wako kushibiti dalili kama anavyokuelekeza


Matibabu haya yana mafanikio yoyote?


Mara nyingi, asilimia 90 ya wagonjwa hupo mara wakatapofanyiwa vipindi vitatu vya matibabu. Endapo mawe yamehama kwenye kila sikio, itachukua muda mrefu kwa sababu kila sikio litatibiwa kwa muda wake binafsi.


Wakati gani uonane na daktari ukiwa na kizunguzungu cha pozi?


 • Endapo dalili zinajirudia rudia

 • Maumivu endelevu ya kichwa

 • Dalili zinazotokea ghafla

 • Kudumu kwa kizunguzungu muda mrefu mara kinapotokea

 • Kupata maumivu mapya ya kichwa au yaliyopo kuzidi

 • Unapatwa na homa

 • Unaona makengeza

 • Umepoteza usikivu

 • Umepoteza uwezo wa kuongea

 • Kufa ganzi kwa viungo vya mwili

 • Kupoteza fahamu

 • Kukosa uwiano wakati wa kutembea

 • Ganzi au hisia za kuchomachoma mwilini


Madhara


Kwa sababu kizunguzungu cha SKPKP hutokea na dalili ya kizunguzungu, hupelekea hatari kuyumbayumba na kuanguka.


Majina mengine ya ugonjwa wa SKPKP


Kizunguzungu cha SKPKP hufahamika kwa jina la lugha ya kizungu kama 'Benign paroxysmal positional vertigo na kwa kifupi cha BPPV.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeboreshwa, 

8 Oktoba 2021 04:53:34

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada

1. Barton JJS, et al. Benign paroxysmal positional vertigo. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 16.06.2021

2. Elsevier Point of Care. Clinical Overview: Benign paroxysmal positional vertigo. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 16.06.2021

3. Ferri FF. Benign paroxysmal positional vertigo. In: Ferri's Clinical Advisor 2021. Elsevier; 2021. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 16.06.2021

4. Furman JM. Causes of vertigo. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 16.06.2021

5. Lalwani AK. Benign paroxysmal positional vertigo In: Current Diagnosis & Treatment Otolaryngology — Head & Neck Surgery. 4th ed. McGraw-Hill Education; 2020. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 16.06.2021

bottom of page