Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Adolf S, MD
20 Agosti 2026, 05:09:52

Udhaifu wa umbile la kichwa cha mtoto- Kraniosinostosisi
Kraniosinostosisi: Sababu, Dalili, Aina, Utambuzi na Matibabu
Wazazi wengi huwa na wasiwasi wanapoona mtoto amezaliwa akiwa na umbo la kichwa lisilo la kawaida au kichwa chake hakikui kwa umbo linalotarajiwa. Mara nyingi mabadiliko madogo ya umbo la kichwa kwa mtoto mchanga yanaweza kuwa ya kawaida kutokana na hali ya kuzaliwa au mchakato wa kujifungua, lakini wakati mwingine yanaweza kuashiria tatizo la kitabibu.
Katika makala hii, udhaifu wa umbile la kichwa cha mtoto unatumika kumaanisha tatizo la kitabibu linalojulikana kama Kraniosinostosisi (Craniosynostosis).
Kraniosinostosisi ni hali inayotokea wakati sehemu zinazounganisha mifupa ya fuvu la mtoto zinapofunga mapema kuliko kawaida. Kufunga huku kabla ya wakati kunaweza kuathiri namna kichwa kinavyokua kwa sababu ubongo wa mtoto huendelea kukua kwa kasi hasa katika miaka miwili ya mwanzo ya maisha.
Ni nini maana ya Kraniosinostosisi?
Kraniosinostosisi ni tatizo la kuzaliwa linalosababishwa na kufunga mapema kwa mishono ya fuvu.
Kichwa cha mtoto hakijaundwa na mfupa mmoja mkubwa bali kina mifupa kadhaa iliyounganishwa na maeneo laini yanayoitwa mishono ya fuvu. Kati ya mifupa hiyo kuna tishu laini za aina ya faibrasi zinazosaidia mifupa kusogea na kuruhusu ubongo kukua.
Kwa mtoto asiye na tatizo hili, mishono ya fuvu hubaki wazi kwa kipindi fulani ili kuruhusu:
Ubongo kuongezeka ukubwa
Fuvu kupanuka kulingana na ukuaji wa ubongo
Kichwa kupata umbo lake la kawaida
Katika mtoto mwenye Kraniosinostosisi, mshono mmoja au zaidi wa fuvu hufunga mapema kabla ya ubongo kumaliza kukua.
Kwa kuwa sehemu hiyo haiwezi tena kupanuka, ubongo hulazimika kusukuma ukuaji kuelekea sehemu nyingine za fuvu ambazo bado ziko wazi. Hii husababisha kichwa kupata umbo lisilo la kawaida.
Kraniosinostosisi hutokea kwa watoto wangapi?
Kraniosinostosisi ni tatizo lisilo la kawaida lakini linaweza kutokea kwa mtoto yeyote.
Inakadiriwa kutokea kwa takribani mtoto mmoja kati ya watoto 2,500 wanaozaliwa duniani.
Baadhi ya watoto huwa na tatizo linalohusisha mshono mmoja tu wa fuvu, wakati wengine wanaweza kuwa na mishono kadhaa iliyofunga mapema.
Dalili za Kraniosinostosisi
Dalili zinaweza kuonekana tangu mtoto anapozaliwa au zinaweza kuonekana zaidi kadri mtoto anavyokua katika wiki na miezi ya mwanzo.
Dalili hutegemea:
Ni mshono gani wa fuvu umefungika
Ni mishono mingapi imeathirika
Kama tatizo linaambatana na ugonjwa mwingine wa vinasaba
Dalili zinaweza kujumuisha:
1. Umbo lisilo la kawaida la kichwa
Hii ndiyo dalili kuu.
Mtoto anaweza kuwa na:
Kichwa kirefu kuliko kawaida
Kichwa kipana au kifupi
Sehemu moja ya kichwa kuwa bapa au kuchomoza
Paji la uso kuwa mbele sana au upande mmoja kutokuwa sawa
Aina ya umbo hutegemea sehemu ya fuvu iliyofunga mapema.
2. Utosi kutokuwepo au kufunga mapema
Watoto wengi huzaliwa wakiwa na utosi ambao ni sehemu laini kwenye fuvu linaloruhusu ukuaji wa ubongo.
Kwa mtoto mwenye Kraniosinostosisi:
Utosi unaweza kuwa mdogo sana
Unaweza kutokuwepo kabisa
Unaweza kufunga mapema kuliko kawaida
Hata hivyo, kutokuwepo kwa utosi pekee hakuthibitishi tatizo hili kwa sababu baadhi ya watoto wanaweza kuwa na tofauti za kawaida.
3. Kichwa kutokua vizuri
Katika baadhi ya watoto, mzunguko wa kichwa unaweza kuongezeka taratibu sana au kutokua kulingana na umri.
Ndiyo maana kupima mzunguko wa kichwa wakati wa kliniki za mtoto ni muhimu.
4. Kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kichwa
Baadhi ya watoto wenye Kraniosinostosisi wanaweza kupata ongezeko la shinikizo ndani ya kichwa kutokana na nafasi ndogo ya fuvu.
Dalili zinazoweza kuonekana ni:
Mtoto kulia sana bila sababu inayoeleweka
Kutapika mara kwa mara
Kukasirika kupita kawaida
Kulala sana au kuwa dhaifu
Degedege
Lakini si kila mtoto mwenye Kraniosinostosisi hupata matatizo haya.
Aina za Kraniosinostosisi
Aina ya tatizo hutegemea mshono wa fuvu uliofungika mapema.
1. Kraniosinostosisi ya Sagito
Hii hutokea wakati mshono uliopo katikati ya kichwa kutoka mbele kwenda nyuma unafunga mapema.
Mtoto anaweza kuwa na:
Kichwa kirefu na chembamba
Paji la uso na sehemu ya nyuma ya kichwa kuchomoza
2. Kraniosinostosisi ya Korona
Hutokea wakati mshono unaopita kutoka upande mmoja wa kichwa kuelekea paji la uso unafunga mapema.
Inaweza kusababisha:
Paji la uso kutokuwa sawa
Jicho moja kuonekana tofauti na jingine
Upande mmoja wa kichwa kuwa bapa
3. Kraniosinostosisi ya Metopiki
Huhusisha mshono uliopo katikati ya paji la uso.
Mtoto anaweza kuwa na:
Paji la uso lenye umbo la pembetatu
Macho kuwa karibu kuliko kawaida
4. Kraniosinostosisi ya Lamboidi
Hii ni aina nadra inayohusisha sehemu ya nyuma ya kichwa.
Inaweza kusababisha:
Nyuma ya kichwa kuwa bapa
Umbo la kichwa kutokuwa sawa
Kraniosinostosisi na maendeleo ya ukuaji wa mtoto
Wazazi wengi huogopa kwamba mtoto mwenye Kraniosinostosisi atakuwa na tatizo la akili. Ukweli ni kwamba watoto wengi wenye Kraniosinostosisi rahisi (isiyoambatana na ugonjwa mwingine) wanaweza kukua na maendeleo ya kawaida.
Hata hivyo, baadhi ya watoto wenye:
Mishono mingi iliyofunga
Kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kichwa
Tatizo la vinasaba linaloambatana
wanaweza kuwa na changamoto za maendeleo zinazohitaji ufuatiliaji.
Visababishi vya Kraniosinostosisi
Mara nyingi chanzo halisi cha Kraniosinostosisi hakijulikani. Katika watoto wengi hutokea bila sababu inayoweza kutambuliwa, hali inayojulikana kama Kraniosinostosisi isiyo na sababu maalumu.
Hata hivyo, tafiti zimeonyesha kuwa baadhi ya mambo yanaweza kuongeza uwezekano wa mtoto kupata tatizo hili.
1. Mabadiliko katika vinasaba (jeni)
Baadhi ya watoto hupata Kraniosinostosisi kutokana na mabadiliko katika jeni zinazohusika na ukuaji na muunganiko wa mifupa ya fuvu. Mabadiliko haya yanaweza kutokea:
Bila kurithiwa kutoka kwa wazazi
Au yanaweza kurithiwa kutoka kwa mzazi mwenye mabadiliko hayo
Baadhi ya mabadiliko ya jeni yanayohusishwa na Kraniosinostosisi huathiri namna seli za mifupa zinavyokua na wakati gani mishono ya fuvu inapaswa kufungwa.
Kraniosinostosisi inayotokana na mabadiliko ya vinasaba mara nyingi inaweza kuambatana na matatizo mengine ya mwili kama sehemu ya magonjwa maalumu ya kurithi.
2. Magonjwa ya vinasaba yanayoambatana na Kraniosinostosisi
Baadhi ya watoto wenye Kraniosinostosisi huwa na tatizo kama sehemu ya ugonjwa mpana wa vinasaba.
Mifano ni:
Ugonjwa wa Apert
Ugonjwa wa Crouzon
Ugonjwa wa Pfeiffer
Katika hali hizi, mtoto anaweza kuwa na mabadiliko mengine kama:
Vidole vya mikono au miguu kuungana
Mabadiliko ya uso
Matatizo ya ukuaji wa mifupa
3. Sababu zisizojulikana
Kwa watoto wengi, hakuna sababu maalumu inayoweza kuonekana.
Mtoto anaweza kuzaliwa na Kraniosinostosisi hata kama:
Wazazi hawana historia ya tatizo hili
Ujauzito ulikuwa wa kawaida
Hakukuwa na tatizo linalojulikana wakati wa ujauzito
Hii ndiyo sababu wazazi hawapaswi kujilaumu wanapopata mtoto mwenye tatizo hili.
4. Mtoto kulalia upande mmoja kwa muda mrefu husababisha Kraniosinostosisi?
Hapana, kulalia upande mmoja kwa muda mrefu hakusababishi Kraniosinostosisi.
Hata hivyo, mtoto kulalia upande mmoja kwa muda mrefu kunaweza kusababisha tatizo jingine linaloitwa plagiosefali ya mkao, ambapo sehemu ya kichwa inaweza kuwa bapa kutokana na msukumo wa muda mrefu kwenye eneo moja la fuvu. Tofauti kubwa ni kwamba:
Kraniosinostosisi husababishwa na kufunga mapema kwa mishono ya fuvu
Plagiosefaali ya mkao husababishwa zaidi na shinikizo la nje kwenye fuvu ambalo bado ni laini
Madhara yanayoweza kutokea kutokana na Kraniosinostosisi
Madhara hutegemea aina ya tatizo, idadi ya mishono iliyofunga na kama kuna ongezeko la shinikizo ndani ya kichwa. Baadhi ya madhara yanaweza kuwa:
1. Mabadiliko ya kudumu ya umbo la kichwa
Bila matibabu yanayofaa, kichwa kinaweza kubaki na umbo lisilo la kawaida kwa sababu sehemu iliyofunga mapema haiwezi kupanuka kawaida.
2. Kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kichwa
Ubongo wa mtoto huendelea kukua kwa kasi, hasa miaka miwili ya kwanza ya maisha. Ikiwa fuvu halina nafasi ya kutosha, shinikizo linaweza kuongezeka ndani ya kichwa.
Hali hii inaweza kuathiri:
Ukuaji wa ubongo
Utendaji wa macho
Maendeleo ya mtoto
3. Matatizo ya kuona
Baadhi ya watoto wanaweza kupata matatizo ya macho kutokana na mabadiliko ya umbo la fuvu au kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kichwa. Matatizo yanaweza kujumuisha:
Misuli ya macho kutofanya kazi sawa
Macho kutokuwa katika mwelekeo mmoja
Kupungua kwa uwezo wa kuona katika baadhi ya hali
4. Degedege
Baadhi ya watoto wenye matatizo makubwa zaidi wanaweza kupata degedege, hasa ikiwa kuna athari kwenye ubongo au ongezeko kubwa la shinikizo ndani ya kichwa.
5. Changamoto za maendeleo
Watoto wengi hukua kawaida, lakini baadhi wanaweza kupata:
Kuchelewa kuanza kuzungumza
Kuchelewa kutembea
Changamoto za kujifunza
Hali hii hutokea zaidi kwa watoto wenye aina kali za Kraniosinostosisi au wanaokuwa na matatizo mengine yanayoambatana.
6. Changamoto za kihisia na kijamii
Kadri mtoto anavyokua, tofauti kubwa ya umbo la kichwa au uso inaweza kuathiri:
Kujiamini
Mahusiano na wengine
Hisia zake kuhusu mwonekano wake
Matibabu ya mapema yanaweza kusaidia kupunguza baadhi ya changamoto hizi.
Utambuzi wa Kraniosinostosisi
Utambuzi wa mapema ni muhimu ili mtoto apate msaada unaofaa wakati sahihi.
Daktari hutumia njia mbalimbali:
1. Uchunguzi wa kichwa cha mtoto
Daktari huangalia:
Umbo la kichwa
Ulinganifu wa pande zote za kichwa
Sehemu za mishono ya fuvu
Hali ya utosi
Mabadiliko fulani yanaweza kuonekana tangu mtoto anapozaliwa.
2. Kupima mzunguko wa kichwa
Mzunguko wa kichwa hupimwa kwa kutumia kipimo maalumu na kufuatiliwa kadri mtoto anavyokua. Kupima huku husaidia kuona kama kichwa kinakua kulingana na umri.
3. Picha za kichwa
Daktari anaweza kutumia vipimo vya picha kusaidia kuthibitisha hali hii. Vipimo vinaweza kujumuisha:
Kipimo cha mawimbi ya sauti kwenye baadhi ya hali
Picha ya kompyuta ya fuvu (CT scan) inapohitajika
Picha hizi husaidia kuona kama mishono ya fuvu imefunga mapema.
4. Uchunguzi wa vinasaba
Kama kuna dalili zinazoonyesha tatizo la kurithi, daktari anaweza kupendekeza vipimo vya vinasaba. Hii husaidia kujua kama Kraniosinostosisi ni sehemu ya ugonjwa mpana wa vinasaba.
Wakati gani mzazi anapaswa kumpeleka mtoto hospitali?
Ni muhimu mtoto kuchunguzwa ikiwa:
Kichwa kina umbo lisilo la kawaida sana tangu kuzaliwa
Utosi haupo au unaonekana kufunga mapema sana
Kichwa hakiongezeki ukubwa kadri mtoto anavyokua
Kuna uvimbe au mstari mgumu unaoonekana kwenye sehemu ya mshono wa fuvu
Mtoto anatapika mara kwa mara bila sababu
Mtoto ana degedege
Mtoto anaonekana kutokua au kutofikia hatua za ukuaji
Matibabu ya Kraniosinostosisi
Matibabu ya Kraniosinostosisi hutegemea mambo mbalimbali kama:
Umri wa mtoto
Aina ya mshono uliofungika
Idadi ya mishono iliyoathirika
Kama mtoto ana dalili za kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kichwa
Kama tatizo linaambatana na ugonjwa wa vinasaba
Lengo kuu la matibabu ni:
Kurekebisha au kuboresha umbo la kichwa
Kutoa nafasi ya kutosha kwa ubongo kukua
Kupunguza hatari ya kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kichwa
Kusaidia ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili
1. Ufuatiliaji wa karibu
Sio kila mtoto mwenye mabadiliko ya umbo la kichwa atahitaji upasuaji haraka. Katika baadhi ya watoto wenye mabadiliko madogo, daktari anaweza kupendekeza ufuatiliaji wa karibu kwa:
Kupima ukuaji wa kichwa mara kwa mara
Kufuatilia maendeleo ya mtoto
Kuangalia mabadiliko ya umbo la kichwa
Hata hivyo, mtoto mwenye Kraniosinostosisi iliyothibitishwa anahitaji kufuatiliwa na wataalamu kwa sababu mishono iliyofunga mapema haiwezi kufunguka yenyewe.
2. Upasuaji wa kurekebisha fuvu
Upasuaji ndiyo tiba kuu kwa watoto wengi wenye Kraniosinostosisi. Katika upasuaji, madaktari wa upasuaji wa watoto na wataalamu wa mifupa ya kichwa hufanya marekebisho kwenye mifupa ya fuvu ili:
Kufungua nafasi zaidi kwa ubongo kukua
Kuboresha umbo la kichwa
Kuzuia au kupunguza ongezeko la shinikizo ndani ya kichwa
Upasuaji hufanyika mapema zaidi kwa sababu fuvu la mtoto bado lina uwezo mkubwa wa kubadilika kadri anavyokua.
Umri gani mzuri wa kufanya upasuaji?
Muda wa upasuaji hutegemea hali ya mtoto, lakini mara nyingi hufanyika katika miezi ya mwanzo ya maisha.
Kwa watoto wengi:
Upasuaji unaweza kufanyika kati ya miezi 6 hadi 12 ya umri
Baadhi ya watoto wanaweza kufanyiwa mapema zaidi kulingana na aina na ukali wa tatizo
Kuchelewesha matibabu kwa muda mrefu kunaweza kufanya marekebisho kuwa magumu zaidi kwa sababu mifupa ya kichwa huwa migumu kadri mtoto anavyokua.
3. Upasuaji mdogo kupitia matundu madogo (upasuaji wa endoskopi)
Kwa baadhi ya watoto wadogo, kuna aina ya upasuaji unaotumia njia yenye majeraha madogo zaidi.
Njia hii:
Hufanyika kwa watoto waliochaguliwa kwa uangalifu
Huacha kovu dogo zaidi
Huwa na muda mfupi wa kupona
Baada ya upasuaji huu, mtoto anaweza kuhitaji kuvaa kofia maalumu ya kusaidia kuelekeza ukuaji wa fuvu.
4. Upasuaji mkubwa wa kurekebisha fuvu
Katika baadhi ya watoto, hasa wale wenye tatizo kubwa au wanaogundulika baadaye, huhitajika upasuaji mkubwa zaidi wa kurekebisha mifupa ya fuvu. Katika utaratibu huu:
Sehemu za mifupa ya fuvu huondolewa kwa muda
Hurekebishwa kuwa na umbo linalofaa
Hurudishwa ili kuruhusu ukuaji mzuri wa kichwa
Je, kila mtoto mwenye Kraniosinostosisi lazima afanyiwe upasuaji?
Sio kila mtoto atakuwa na mahitaji sawa. Uamuzi wa kufanya upasuaji hutegemea:
Aina ya Kraniosinostosisi
Ukali wa mabadiliko ya kichwa
Ukuaji wa mtoto
Dalili za shinikizo ndani ya kichwa
Baadhi ya watoto wenye aina nyepesi wanaweza kufuatiliwa kwa karibu, lakini watoto wengi wenye kufungwa mapema kwa mishono muhimu huhitaji matibabu ya upasuaji.
Je, mtoto atapona kabisa baada ya upasuaji?
Watoto wengi hupata matokeo mazuri baada ya matibabu, hasa pale tatizo linapogundulika na kutibiwa mapema. Baada ya matibabu, mtoto anaweza:
Kuwa na ukuaji wa kawaida wa ubongo
Kuwa na maendeleo ya kawaida
Kuendelea na maisha ya kawaida
Hata hivyo, baadhi ya watoto huhitaji ufuatiliaji wa muda mrefu ili kuangalia:
Ukuaji wa kichwa
Maendeleo ya kujifunza
Uwezo wa kuona
Matatizo mengine yanayoweza kujitokeza
Tofauti kati ya Kraniosinostosisi na plagiosefaali (kichwa kubonyea)
Wazazi wengi huchanganya Kraniosinostosisi na hali ya kichwa kuwa bapa kwa mtoto.
Kraniosinostosisi
Husababishwa na:
Kufunga mapema kwa mshono wa fuvu
Sifa zake:
Mara nyingi mtoto huzaliwa akiwa na mabadiliko hayo
Kunaweza kuwa na mstari mgumu kwenye eneo la mshono
Umbo la kichwa hubadilika kutokana na ukuaji wa fuvu
Plagiosefaali ya mkao
Husababishwa na:
Mtoto kulalia sehemu moja ya kichwa kwa muda mrefu
Sifa zake:
Sehemu ya nyuma au upande mmoja wa kichwa kuwa bapa
Mishono ya fuvu huwa bado wazi
Mara nyingi huboreka kwa kubadilisha mkao na mazoea ya mtoto
Je, utosi wa mtoto unaweza kufunga mapema bila kuwa Kraniosinostosisi?
Ndiyo, kuna watoto ambao utosi unaweza kuwa mdogo au kufunga mapema lakini bado wakawa na ukuaji wa kawaida. Utosi pekee hauwezi kutumika kuthibitisha Kraniosinostosisi. Daktari huangalia mambo mengine kama:
Umbo la kichwa
Ukuaji wa mzunguko wa kichwa
Hali ya mishono ya fuvu
Maendeleo ya mtoto
Ushauri kwa wazazi wenye mtoto mwenye umbo la kichwa lisilo la kawaida
Wazazi wanapaswa:
Kuepuka kujilaumu kwa sababu mara nyingi chanzo hakijulikani
Kumpeleka mtoto kliniki kwa ufuatiliaji wa ukuaji
Kuepuka kutumia vifaa au njia za kubadilisha umbo la kichwa bila ushauri wa mtaalamu
Kufuatilia dalili kama kutapika mara kwa mara, degedege au kuchelewa kwa maendeleo
Ni muhimu kukumbuka kuwa watoto wengi wenye Kraniosinostosisi wanaweza kukua vizuri wakipata uangalizi na matibabu yanayofaa kwa wakati.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu Kraniosinostosisi na majibu yake ya kina
1. Mtoto wangu amezaliwa na kichwa chenye umbo lisilo la kawaida, je ni lazima awe na Kraniosinostosisi?
Kichwa cha mtoto mchanga kinaweza kuwa na umbo lisilo la kawaida kwa sababu mbalimbali na si kila mtoto mwenye kichwa chenye umbo tofauti huwa na Kraniosinostosisi.
Wakati wa kujifungua, hasa kwa njia ya kawaida, mifupa ya kichwa cha mtoto huwa na uwezo wa kusogea ili kurahisisha mtoto kupita kwenye njia ya uzazi. Hali hii inaweza kufanya kichwa kuonekana kimebanwa, kirefu au kisicho sawa katika siku za mwanzo baada ya kuzaliwa.
Kwa watoto wengi, umbo la kichwa hubadilika taratibu kadri siku na wiki zinavyopita. Hata hivyo, kama umbo lisilo la kawaida linaendelea, linaongezeka au linaambatana na kutokuwepo kwa utosi, mstari mgumu kwenye fuvu au kichwa kutokua vizuri, mtoto anapaswa kuchunguzwa.
Daktari huangalia hali nzima ya mtoto, si umbo la kichwa pekee, ili kutofautisha mabadiliko ya kawaida na Kraniosinostosisi.
2. Mtoto wangu utosi hauchezi na kichwa chake hakijakaa katika shape nzuri, nifanye nini?
Utosi wa mtoto kwa kawaida unaweza kuonekana kama sehemu laini inayocheza au kupiga mdundo unaofanana na mapigo ya moyo. Hii hutokea kwa sababu kuna mishipa ya damu chini ya utosi na ni hali ya kawaida kwa watoto wengi.
Hata hivyo, kutocheza kwa utosi pekee hakumaanishi moja kwa moja kuwa mtoto ana tatizo. Baadhi ya watoto wana utosi mdogo, uliofichika au mabadiliko yake hayaonekani wazi.
Kama mtoto ana umbo la kichwa lisilo la kawaida, hatua muhimu ni kumpeleka kwa mtaalamu wa afya kwa uchunguzi wa kichwa. Daktari ataangalia kama mishono ya fuvu imefungwa mapema, kama kichwa kinakua kulingana na umri na kama kuna sababu nyingine inayoweza kueleza hali hiyo.
Usijaribu kubonyeza utosi, kuufanyia masaji au kutumia vifaa vya kubadilisha umbo la kichwa bila ushauri wa mtaalamu kwa sababu unaweza kumuumiza mtoto.
3. Kraniosinostosisi huonekana mtoto anapozaliwa au inaweza kuanza baadaye?
Mara nyingi Kraniosinostosisi huanza kuwepo tangu mtoto anapozaliwa kwa sababu tatizo linahusiana na kufunga mapema kwa mishono ya fuvu.
Kwa baadhi ya watoto, mabadiliko yanaweza yasionekane sana wakati wa kuzaliwa lakini hujitokeza zaidi katika wiki au miezi ya mwanzo kwa sababu ubongo unaendelea kukua na kusukuma sehemu za fuvu ambazo bado zina nafasi.
Ndiyo maana uchunguzi wa ukuaji wa mtoto wakati wa kliniki ni muhimu. Kupima mzunguko wa kichwa mara kwa mara husaidia kugundua kama ukuaji wa kichwa unaendelea vizuri.
4. Je, kulaza mtoto upande mmoja kunaweza kusababisha Kraniosinostosisi?
Kulaza mtoto upande mmoja kwa muda mrefu hakusababishi Kraniosinostosisi. Kraniosinostosisi hutokea kwa sababu mishono ya fuvu hufunga mapema kutokana na mabadiliko ya ukuaji wa mifupa au sababu za vinasaba.
Hata hivyo, mtoto kukaa au kulala upande mmoja kwa muda mrefu kunaweza kusababisha hali nyingine inayoitwa plagiosefaali ya mkao. Hii hutokea kwa sababu fuvu la mtoto mchanga bado ni laini na linaweza kubadilika kutokana na shinikizo la muda mrefu kwenye eneo moja.
Tofauti kubwa ni kwamba plagiosefaali ya mkao mara nyingi huhusiana na mazingira au mkao wa mtoto, wakati Kraniosinostosisi huhusiana na mishono ya fuvu kufunga mapema.
5. Je, Kraniosinostosisi inaweza kuathiri akili ya mtoto?
Kraniosinostosisi haimaanishi moja kwa moja kwamba mtoto atakuwa na tatizo la akili.
Watoto wengi wenye aina rahisi ya Kraniosinostosisi hukua vizuri na wanaweza kuwa na maendeleo ya kawaida ya kujifunza, kuzungumza na kufanya shughuli za kila siku.
Changamoto za maendeleo zinaweza kutokea zaidi kwa watoto ambao wana:
Aina kali ya Kraniosinostosisi
Mishono mingi ya fuvu iliyofunga mapema
Kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kichwa
Ugonjwa wa vinasaba unaoambatana
Ufuatiliaji wa karibu husaidia kugundua mapema kama mtoto anahitaji msaada wa ziada katika ukuaji au kujifunza.
6. Je, mtoto mwenye Kraniosinostosisi anaweza kuishi maisha ya kawaida?
Watoto wengi wenye Kraniosinostosisi wanaweza kuishi maisha ya kawaida hasa ikiwa tatizo litagunduliwa na kutibiwa mapema.
Baada ya matibabu, watoto wengi hupata maboresho ya umbo la kichwa na hupata nafasi nzuri ya ukuaji wa kawaida wa ubongo.
Hata hivyo, baadhi ya watoto wanaweza kuhitaji ufuatiliaji wa muda mrefu kutokana na uwezekano wa matatizo kama:
Matatizo ya kuona
Changamoto za kujifunza
Mabadiliko ya ukuaji wa kichwa
Matokeo hutegemea aina ya tatizo na hali ya mtoto binafsi.
7. Ni dalili zipi zinaonyesha kuwa mtoto mwenye kichwa kisicho kawaida anahitaji kuonekana na daktari haraka?
Mzazi anapaswa kutafuta ushauri wa kitabibu ikiwa mtoto ana:
Kichwa chenye umbo lisilo la kawaida linalozidi kuwa baya kadri anavyokua
Utosi kutokuwepo au kufunga mapema sana
Kichwa kutokua kwa kasi inayotarajiwa
Kutapika mara kwa mara bila sababu inayoeleweka
Degedege
Mtoto kuwa mchovu sana au kushindwa kula vizuri
Kuchelewa kufikia hatua za ukuaji
Dalili hizi hazimaanishi lazima mtoto ana Kraniosinostosisi, lakini zinahitaji uchunguzi ili kujua chanzo.
8. Je, upasuaji wa Kraniosinostosisi ni hatari kwa mtoto?
Upasuaji wa fuvu kwa mtoto ni upasuaji mkubwa unaohitaji timu yenye uzoefu, lakini hufanyika kwa usalama mkubwa katika vituo vyenye wataalamu wanaohusika na matibabu ya watoto.
Kabla ya upasuaji, mtoto hufanyiwa tathmini ili kuhakikisha muda unaofaa na aina ya upasuaji inayofaa.
Baada ya upasuaji, mtoto hufuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha:
Jeraha linapona vizuri
Hakuna maambukizi
Ukuaji wa kichwa unaendelea vizuri
Faida ya matibabu mara nyingi huwa kubwa kuliko hatari kwa watoto wanaohitaji upasuaji.
9. Je, Kraniosinostosisi inaweza kujirudia baada ya upasuaji?
Kwa watoto wengi, upasuaji mmoja hutoa matokeo mazuri na tatizo halirudi tena kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, baadhi ya watoto wanaweza kuhitaji ufuatiliaji au upasuaji mwingine kulingana na:
Aina ya Kraniosinostosisi
Idadi ya mishono iliyohusika
Kama kuna ugonjwa wa vinasaba
Ndiyo maana mtoto huendelea kufuatiliwa kwa miaka kadhaa baada ya matibabu.
10. Ninawezaje kujua kama umbo la kichwa cha mtoto wangu ni la kawaida?
Hakuna umbo moja linalofanana kwa watoto wote. Kichwa cha mtoto kinaweza kutofautiana kidogo kulingana na:
Njia ya kujifungua
Mkao wa mtoto
Vinasaba vya familia
Kasi ya ukuaji
Njia bora ya kujua kama ukuaji wa kichwa ni wa kawaida ni kupitia:
Kupima mzunguko wa kichwa kliniki
Kufuatilia ukuaji wa mtoto
Uchunguzi wa daktari
Mzazi anapaswa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea badala ya kuangalia umbo la kichwa siku moja pekee. Kichwa kinachobadilika haraka, kutokua vizuri au kuambatana na dalili nyingine kinahitaji tathmini ya kitaalamu.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
9 Desemba 2020, 23:12:11
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada hii:
Centers for Disease Control and Prevention. Craniosynostosis. Available from: https://www.cdc.gov/ncbddd/birthdefects/craniosynostosis.html. Accessed November 8, 2020.
Genetic and Rare Diseases Information Center. Craniosynostosis. Available from: https://rarediseases.info.nih.gov/diseases/6209/craniosynostosis. Accessed November 8, 2020.
National Institute of Neurological Disorders and Stroke. Craniosynostosis Information Page. Available from: https://www.ninds.nih.gov/Disorders/All-Disorders/Craniosynostosis-Information-Page. Accessed November 8, 2020.
Sharma VP, Fenwick AL, Brockop MS, McGowan SJ, Goos JAC, Hoogeboom AJM, et al. Mutations of TCF12, encoding a basic-helix-loop-helix partner of TWIST1, are a frequent cause of coronal craniosynostosis. Nat Genet. 2013;45(3):304-307. doi:10.1038/ng.2531.
TCF12 mutations and craniosynostosis. Nature Genetics. Available from: https://www.nature.com/articles/ng1013-1261a.epdf. Accessed November 8, 2020.
Centers for Disease Control and Prevention. Facts about Craniosynostosis. Available from: https://www.cdc.gov/ncbddd/birthdefects/craniosynostosis.html. Accessed November 8, 2020.
Dunaway DJ. Plagiocephaly in Adults. Available from: https://www.daviddunaway.co.uk/treatments/plagiocephaly-in-adults/. Accessed November 8, 2020.
