top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

ULY CLINIC

18 Septemba 2026, 14:24:24

Cantharanthus roseus

Catharanthus roseus ni mmea unaotajwa kuwa na uwezo wa kutumika katika tiba ya kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani. Asili yake ni Madagaska, ambako hapo awali ulikuwa ukitumika kwa kiasi kidogo na wataalamu wa tiba asilia. Kwa sasa hupatikana katika maeneo mengi barani Afrika na sehemu mbalimbali duniani, kwa kuwa hulimwa kama mmea wa urembo na hutumika kupendezesha mazingira ya ndani na nje.


Sifa za mmea Catharanthus roseus

Mmea huu hukua mwaka mzima katika vipindi mbalimbali na unaweza kufikia urefu wa takribani sentimita 50. Maua yake huwa na rangi ya pinki, huku baadhi yakiwa meupe. Kila ua huwa na petali tano zilizoshikamana na kuunda umbo la mviringo. Mmea huu hulimwa kama ua la urembo na hukua vizuri katika udongo wa kichanga.


Uwezo wa kitiba wa Catharanthus roseus

Mmea huu huwa na kampaundi aina ya alkaloidi zinazohusishwa na uwezo wa kutumika katika matibabu ya kisukari. Baadhi ya alkaloidi zinazopatikana katika mmea huu hutumika katika matibabu ya saratani ya damu, yaani lukemia.


Mizizi ya mmea huu huwa na kampaundi za alkaloidi za aina ya indole, ikiwemo ajmalicine, ambayo hutajwa kuwa na uwezo wa kutumika katika matibabu ya shinikizo la juu la damu.


Matumizi ya Catharanthus roseus kama tiba


Msongo

Tumia dikoksheni iliyotengenezwa kwa gramu tano za unga wa mizizi yake katika mililita 150 za maji, kisha unywe wakati tumbo halina kitu.


Kisukari

Kunywa dikoksheni iliyotengenezwa kwa kutumia miligramu 30 za majani ya mmea katika lita moja ya maji.

Namna ya kuandaa aina mbalimbali za dawa kutoka kwenye mmea


Namna ya kuandaa infusheni ya dawa asilia

Infusheni huandaliwa kwa kuzamisha sehemu ya mmea unayotaka kutumia kama dawa kwenye kiasi cha maji yaliyochemka. Baada ya kuzamisha kwenye maji yaliyochemka, maji hayo huchujwa baada ya dakika 15. Dozi ya dawa inayotakiwa kuandaliwa kwa wastani huwa ni gramu 1 kwa kila mililita 10 za maji.


Kuna dawa nyingi asilia ambazo tayari zimetengenezwa na kufungwa kwenye vifungashio vya karatasi, ambapo unaweza kuzitumia kwa urahisi kama majani ya chai ya kuchovywa. Dawa zilizo katika fomu hiyo hupunguza muda wa kuandaa.


Namna ya kuandaa dikokshen ya dawa asilia

Dikokshen hutumika kuvuna kiini cha dawa ambacho hakiathiriwi na joto.

Ili kuandaa dikokshen ya dawa, chemsha magome au mizizi ya mmea kwa muda wa dakika 15 hadi 60, kutegemea aina ya mmea au kiini cha dawa. Kisha ipooze na ongeza maji ya baridi ili kutengeneza kiasi cha dawa na wingi wa kiini unaohitaji.


Endapo dawa inatakiwa kuchemshwa kwa muda mrefu, unatakiwa kuongeza kiasi cha maji yaliyopotea ili dawa isiungue.


Dozi ya dikokshen ni sawa na infusheni, yaani gramu 1 ya mmea kwa kila mililita 10 za maji, isipokuwa endapo dawa ina uteute mwingi. Katika hali hiyo, gramu 1 inatakiwa kuchanganywa na mililita 20 za maji.


Namna ya kuandaa mmeng’enyo wa dawa

Kuandaa mmeng’enyo wa dawa kwa njia hii, unatakiwa kuweka dawa yako kwenye chombo kisha kuongeza maji yenye joto linalotakiwa. Mara nyingi joto linatakiwa kuwa kati ya nyuzi 35 hadi 40 za sentigredi, kutegemea aina ya dawa.

Lengo kuu la kuzingatia joto ni kutoharibu kiini cha dawa ambacho kinategemea joto.


Namna ya kuandaa masalesheni ya dawa

Ili kuandaa masalesheni ya dawa, saga au katakata dawa katika vipande vidogo sana, kisha viweke kwenye chombo cha kioo chenye kimiminika cha kufyonza dawa.

Funika mchanganyiko huo na uache kwa muda wa siku tatu au zaidi kwenye joto la ndani ya nyumba. Baada ya kutimia kwa siku tatu, tikisa kwa nguvu mara nyingi ili dawa iingie kwenye kimiminika.


Baada ya hapo, chuja dawa na kamua unga au vipande ili dawa yote itoke. Kisha unaweza kuchuja dawa kwa ajili ya matumizi au kuifanyia dekatensheni ili kupata kiini safi cha dawa.


Namna ya kuandaa pakolesheni ya dawa

Hii ni njia maarufu ya kuandaa tinkcha ya dawa au kufyonza dawa kutoka kwenye kimiminika. Njia hii inahitaji chombo maalumu chenye jina la pakoleta na unatakiwa kuwa mtaalamu zaidi ili kuandaa dawa kwa njia hii.


Soma zaidi kuhusu njia hii kupitia kiungo kilichowekwa chini ya tovuti hii.


Namna ya kuandaa dawa ya kufyonza kwa kimiminika

Njia hii huandaa dawa kutoka kwenye kimiminika chenye dawa au tishu za mnyama kwa kufyonza dawa hiyo kwa kutumia kimiminika kingine, hasa pombe aina ya ethanol au maji.

Kiasi cha pombe na maji kinachowekwa hutegemea aina ya dawa. Njia hii inahitaji uwe mtaalamu wa kuandaa dawa. Unaweza kujifunza zaidi namna ya kuandaa dawa kwa njia hii kupitia kiungo kilichowekwa chini ya tovuti hii au kutumia dawa ambazo tayari zimeandaliwa.


Namna ya kuandaa tinkcha ya dawa

Tinkcha ya dawa huandaliwa kwa kufanya masalesheni au pakolesheni ya dawa kwa kutumia kimiminika cha pombe pekee. Njia hii ni nzuri ya kuvuna kiwango cha kiini unachotaka kutoka kwenye mimea au mnyama.


Soma zaidi kuhusu njia hii kupitia rejea zilizo chini ya makala hii.


KUMBUKA

Kama kuna haja ya kuchemsha dawa, hakikisha unatumia chombo kilichotengenezwa kwa udongo au sufuria za chuma cha pua (stainless steel), na usifunike wakati wa kuchemsha ili kutoa sumu na kutobadili kiini cha dawa.


Usitumie zaidi ya dawa moja kutibu tatizo moja au mawili tofauti ili kuepuka madhara na mwingiliano wa dawa.


Endapo unatumia dawa za hospitali, wasiliana na daktari wako akushauri ili kuepuka mwingiliano wa dawa na madhara yanayoweza kutokea.

Imeandikwa:

8 Julai 2021, 21:16:18

ULY CLINIC inakushauri siku zote utafute msaada kutoka kwa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba kupitia kitufe cha 'Pata tiba' au 'Mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii.

Rejea za mada hii;

  1. KY LOH. Know the Medicinal Herb: Catharanthus roseus (Vinca rosea). https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4170313/. Imechukuliwa 08.07.2021

  2. Catharanthus Wikipedia Online Free Encyclopedia. http://en.wikipedia.org/wiki/Vinca_alkaloids#vinca_alkaloids. Imechukuliwa 08.07.2021

  3. Periwinkle: About MAKNA. http://www.makna.org.my/periwinkle.asp. Imechukuliwa 08.07.2021

  4. Catharantus Flora of China. http://www.efloras.org/florataxon.aspx?flora_id=12&taxon_id=105876.

  5. Catharantus Roseus – periwinkle. Tropiclab Inc. www.tropilab.com/periwinkle.html. Imechukuliwa 08.07.2021

  6. Johnson IS, Armstrong JG, Gorman M, Burnett JP. The vinca alkaloids: a new class of oncolytic agents. Cancer Res. 1963;23:1390–427

  7. Infusion methods. https://www.medicinalplants-pharmacognosy.com/pharmacognosy-s-topics/extraction-methods/infusion/#. Imechukuliwa 27.06.2021

  8. Decoction extraction. https://www.medicinalplants-pharmacognosy.com/pharmacognosy-s-topics/extraction-methods/decoction/. Imechukuliwa 27.06.2021

  9. Extraction methods digestion. https://www.medicinalplants-pharmacognosy.com/pharmacognosy-s-topics/extraction-methods/digestion/. Imechukuliwa 27.06.2021

  10. Fluid extract. https://www.medicinalplants-pharmacognosy.com/pharmacognosy-s-topics/extracts/fluid-extract/. Imechukuliwa 27.06.2021

  11. Tincture. https://www.medicinalplants-pharmacognosy.com/pharmacognosy-s-topics/extracts/tincture/. Imechukuliwa 27.06.2021

  12. Perolation. https://www.medicinalplants-pharmacognosy.com/pharmacognosy-s-topics/extraction-methods/percolation/. Imechukuliwa 27.06.2021

  13. Maceration. https://www.medicinalplants-pharmacognosy.com/pharmacognosy-s-topics/extraction-methods/maceration/. Imechukuliwa 27.06.2021

bottom of page