top of page

Mwandishi:

Dkt. Sospeter M, MD

Mhariri:

Dkt. Lugonda B, MD

4 Mei 2020 23:33:25

Pantoprazole

Pantoprazole

Ni dawa iliyo kundi la Protoni pumpu inhibita inayofanya kazi ya kuzuia uzalishaji wa tindikali tumboni.


Majina ya kibiashara


Pantoprazole hupatikana kwa jina jingine kama;


 • Protonix

 • Protium

 • Pantozol

 • Pantor

 • Pantoloc


Fomula ya kikemikali


Fomula ya kikemia ya Pantoprazole ni C16H15F2N3O4S


Jina la kisayansi (IUPAC)


Pantoprazole hufahamika kwa jina la kisayansi kama 6-(difluoromethoxy)-2-[(3,4-dimethoxypyridin-2-yl)methylsulfinyl]-1H-benzimidazole


Fomu na uzito wa Pantoprazole


Hupatikana kama vidonge vya

Miligramu 20

Miligramu 40


Dozi ya dawa ya kimiminika

Pakiti yenye miligramu 40


Dozi ya kuchoma kwa sindano;

Kila kichupa ina miligramu 40.


Pantoprazole hutibu nini?


 • Pantoprazole hutumika yenyewe au pamoja na dawa zingine katika matibabu ya;

 • Vidonda vya tumbo.

 • Vidonda vya tumbo vinavyo sababishwa na dawa zilizopo kwenye kundi la NSAID.

 • Sindromu ya Zollinger-Ellison.

 • Kupunguza uzalishaji wa tindikali tumboni baada ya upasuaji

 • Kutibu kucheua tindikali- Gastroesofajio rifluksi

 • Kutibu michubuko kwenye koo la chakula kutokana na tindikali.


Namna Pantoprazole inavyofanya kazi


Huzuia seli za gastrini katika tumbo kuzalisha tindikali


Ufyonzwaji wa Pantoprazole


 • Hufyonzwa hadi kwa asilimila 77 kama ukinywa

 • Huanza kuafanya kazi baada ya saa 24 baada ya kumezwa na kama imetolewa kupitia mshipa wa damu huanza kufanya kazi mara baada ya kutolewa.

 • Huweza kufanya kazi hadi kwa siku 7


Nusu maisha ya Pantoprazole


Nusu ya dawa hutumika mwilini baada ya saa 1.


Utoaji Pantoprazole mwilini


Pantoprazole na mabaki yake hutolewa mwilini kwa njia ya mkojo (asilimia 71) na kwenye kinyesi (asilimia 18).


Maudhi ya Pantoprazole


Maudhi madogo ya Pantoprazole


 • Kichwa kuuma

 • Kuaharisha

 • Kichefuchefu

 • Maumivu ya tumbo

 • Kutapika

 • Kujamba

 • Kizunguzungu

 • Maumivu ya viungo

 • Homa kwa watoto.

 • Maambukizi kwenye mfumo wa upumuaji kwa watoto


Wagonjwa wasiopaswa kutumia Pantoprazole


Marufuku kwa wagonjwa wafuatao;


 • Wagonjwa wenye aleji na dawa hii

 • Mgonjwa anaetumia dawa zenye rilpivirine


Angalizo la Pantoprazole


 • Kuhara wakati wakutumia dawa ya pantoprazole kunaweza kusababishwa na bakteria clostridium difficile.

 • Kutumia dawa hii kila siku zaidi ya mara moja kwa muda mrefu kunaongeza uwezekano wa mifupa kuvunjika kwa urahisi.

 • Matumizi ya kila siku kwa muda mrefu kama zaidi ya miaka mitatu yaweza kusbabisha upungufu wa vitamini B-12 kwa kupunguza ufyonzwaji wa vitamini hizo.

 • Matumizi ya muda mrefu yanaweza kusababisha kiwango cha magnesium kwenye damu kushuka chini ya kiwango cha kawaida.

 • Matumizi ya zaidi ya mwaka yanaongeza atari ya polipsi kwenye tezi zilizo kwenye fandazi.

 • Inaweza leta ugonjwa wa kusambaa wa lupazi erithromatosasi


Muingiliano wa Pantoprazole na dawa zingine


Ufyonzwaji wake hupungua ikitumika pamoja na sucralfate.


Pantoprazole hupunguza utendaji kazi wa dawa zifuatazo:-

 • Ketoconazole

 • Itraconazole

 • Digoxin

 • Dawa za chumvi zenye madini ya chuma

 • Erlotinib

 • Dasatinib


Kutumia kwa pamoja na dawa ya warfarin inaweza kusababisha kuvuja damu nyingi na kuhatarisha maisha. Inabidi kufuatilia muda wa prothrombini.


Huongeza kasi ya dawa ya theophylline kutolewa mwilini, hivyo ni muhimu kuongeza dozi ya theophylline ikiwa zitatolewa kwa pamoja.


Pantoprazole kwa mjamzito


Dawa itumike kwa tahadhari kama faida ya kutumia ni kubwa kuliko madhara; Majaribio kwa wanyama yanaonesha madhara na majaribio kwa binadamu hayajafanyika. Au majaribio kwa wanyama na kwa binadamu hayajafanyika.


Pantoprazole wakati wa kunyonyesha


Ni vyema kujitahidi kuepuka matumizi ya dawa hii wakati wa kunyonyesha kwani hufika kwenye maziwa ya mama na inaweza kumdhuru mtoto anaye nyonya. Uamuzi wa kuitumia wakati wakati wa kunyonyesha utategemea faida na hasara za kuitumia.

ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha  vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

23 Julai 2023 16:55:55

Rejea za mada hii:-

1.Goodman & Gilman’s The Pharmacological Basis of THERAPEUTICS twelfth edition ISBN: 978-0-07-176939-6 ukurasa wa 1311.

2.A Textbook of Clinical Pharmacology and TherapeuticS Fifth ISBN 978-0-340-90046-8 ukurasa wa 251.

3.U.S. Food and Drug Administration:
https://www.accessdata.fda.gov/drugsatfda_docs/label/2018/020987s054,022020s016,020988s060lbl.pdf. Imechukuliwa 30/04/2020.

4.Medscape: https://reference.medscape.com/drug/protonix-pantoprazole-342001#6.Imechukuliwa 30/04/2020 .
bottom of page