top of page

Mwandishi:

Mhariri:

ULY CLINIC

Dkt. Benjamin S, MD, Dkt. Adolf S, MD.

16 Aprili 2025, 13:45:26

Image-empty-state.png

Dalili za mimba ya miezi tisa

Imeboreshwa:

Utangulizi

Mimba ya miezi tisa ni sawa na ujauzito wa wiki 33 hadi 36. Kwa wakati huu, mtoto huwa karibu kufikia ukamilifu, na mwili wa mama hujiandaa kwa uchungu wa uzazi na kujifungua. Ingawa furaha ya kukutana na mtoto huwa kubwa, pia kuna changamoto nyingi za kimwili na kihisia. Kufahamu mabadiliko yanayotokea mwilini, dalili zinazoweza kujitokeza, na wakati wa kumuona daktari ni muhimu kwa usalama wa mama na mtoto.


Je, ni zipi dalili za mimba ya miezi tisa?

Katika wiki za mwisho za ujauzito, dalili huweza kuwa kali zaidi. Baadhi ya dalili za kawaida ni:

  • Uchungu wa uongo: Hii ni mikazo ya kizazi inayoandaa kizazi kwa ajili ya leba, haina maumivu na hudumu kwa muda mfupi sana bila muendelezo.

  • Kukojoa mara kwa mara: Mtoto anaposhuka kwenye nyonga, shinikizo kwenye kibofu huongezeka hivyo mkojo hushindwa kutoka wote na kufanya kukojoa mara kwa mara.

  • Maumivu ya nyonga na tumbo la chini: Mtoto anapokaa chini zaidi, huleta maumivu au usumbufu sehemu ya chini ya tumbo na mgongo.

  • Kuchoka sana: Uzito wa mimba hukulemea, na usingizi hukatizwa mara kwa mara.

  • Mwili kuvimba: Mikono, miguu na vifundo vya miguu vinaweza kuvimba kutokana na kuongezeka kwa maji mwilini.

  • Hamasa ya kufanya maandalizi: Mama hupata nguvu ghafla na hamu ya kuandaa mazingira kwa ajili ya mtoto.

  • Kupoteza ute mzito kutoka ukeni: Hii ni ishara kwamba uchungu wa uzazi unaweza kuwa karibu, lakini haimaanishi utaanza mara moja.


Mambo ya kuzingatia

Mwezi huu unahusu maandalizi ya kimwili na kiakili. Mambo muhimu ya kuzingatia ni:

  • Hakikisha umemalizia mpango wa kujifungua

  • Andaa mzigo wako wa kwenda hospitalini ukiwa na vitu muhimu kama nguo zako, mavazi ya mtoto, vifaa vya usafi, nyaraka muhimu nk.

  • Endelea kula vyakula vya afya, kunywa maji ya kutosha, na kupata mapumziko kadri inavyowezekana

  • Fanya mazoezi mepesi kama kutembea na yoga


Je, ni wakati gani unapaswa kumuona daktari?

Ingawa dalili nyingi ni za kawaida, baadhi ya ishara zinahitaji msaada wa haraka wa kitabibu. Muone daktari mara moja iwapo:

  • Una mikazo ya uchungu wa uzazi inayokuja kwa mfululizo

  • Maji yanamwagika kutoka ukeni

  • Kutokwa na damu ukeni

  • Maumivu makali ya kichwa, kuona ukungu, au kuvimba sana

  • Kupungua kwa mjongeo wa mtoto tumboni

  • Homa kali au baridi kali na kutetemeka


Wapi utapata maelezo zaidi kuhusu mimba ya miezi tisa?

Ili  kupata maelezo zaidi kuhusu mimba ya miezi tisa bofya hapa.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

16 Aprili 2025, 13:43:48

Rejea za dawa

  1. Mayo Clinic. (2025). Pregnancy week by week. Mayo Foundation for Medical Education and Research. https://www.mayoclinic.org/healthy-lifestyle/pregnancy-week-by-week/basics/healthy-pregnancy/hlv-20049471. Imechukuliwa 16.04.2025

  2. WebMD. (2024, October 30). 7 to 9 Months Pregnant - 3rd Trimester Baby Growth & Development. https://www.webmd.com/baby/pregnancy-your-babys-growth-development-months-7-to-9. Imechukuliwa 16.04.2025

  3. American College of Obstetricians and Gynecologists. (2019). Your pregnancy and childbirth: Month to month. American College of Obstetricians and Gynecologists.

  4. Adamo, C., van de Paal, E., & Stewart, L. (2017). 9 months: A month-by-month guide to pregnancy for the family to share. Frances Lincoln Children's Books.

  5. Angelo White, D., & Lang, J. (2016). The whole 9 months: A week-by-week pregnancy nutrition guide with recipes for a healthy start. Sourcebooks Inc. ​

  6. Brin, L. (2011). How to exercise when you're expecting: For the 9 months of pregnancy and the 5 months it takes to get your best body back. Plume.

bottom of page