Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
ULY CLINIC
27 Novemba 2026, 07:29:04
Kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua: Dalili, Visababishi, Vipimo na Matibabu
Imeboreshwa:
Kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua ni kupoteza damu mililita 500 au zaidi baada ya kujifungua kwa njia ya kawaida, au mililita 1,000 baada ya upasuaji, au damu yoyote inayoleta dalili za mshtuko. Chanzo kikuu ni mji wa mimba kushindwa kusinyaa. Ni dharura: pedi kujaa ndani ya muda wa saa moja, mabonge makubwa au kizunguzungu kunahitaji hospitali mara moja.
Habari daktari, ninatokwa na damu baada ya kujifungua. Naomba kufahamu kisababishi ni nini, na je ni hatari? Swali hili huulizwa na akina mama wengi. Damu kiasi fulani baada ya kujifungua ni ya kawaida, lakini damu nyingi ni moja ya visababishi vikuu vya vifo vya akina mama Tanzania na duniani. Makala hii inaeleza aina za tatizo hili, dalili za hatari, visababishi, vipimo, matibabu ya hospitali, msaada wa nyumbani wakati wa kupona, na tofauti kati ya lokia ya kawaida na damu inayohitaji daktari.
Aina za kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua
Ya mapema
Hutokea ndani ya masaa 24 ya kwanza baada ya kujifungua, na mara nyingi ndani ya saa ya kwanza. Hii ndiyo aina ya kawaida zaidi na hatari zaidi, kwa sababu damu nyingi huweza kupotea ndani ya dakika chache.
Ya kuchelewa
Hutokea baada ya masaa 24 hadi wiki 12 baada ya kujifungua. Mara nyingi husababishwa na mabaki ya kondo la nyuma yaliyobaki ndani ya mji wa mimba, au maambukizi ya mji wa mimba. Mama huweza kuwa amerudi nyumbani, akaona damu nyingi ghafla, mabonge, au uchafu wenye harufu mbaya pamoja na homa.
Dalili na ishara za hatari
Damu nyingi au mabonge makubwa kwenye pedi.
Pedi moja kujaa damu ndani ya dakika 15 hadi 30, au zaidi ya pedi moja kwa saa.
Mapigo ya moyo kwenda kasi, zaidi ya 100 kwa dakika.
Presha kushuka, baridi kali na jasho jingi.
Ngozi kuwa baridi na nyeupe, na midomo au vidole kuwa na rangi ya bluu.
Kizunguzungu, kuchanganyikiwa, udhaifu mkubwa au kupoteza fahamu.
Damu au uchafu wenye harufu mbaya, homa na maumivu ya tumbo, kwa aina ya kuchelewa.
Tahadhari: dalili za mwanzo huweza kuwa ndogo. Mama huweza kuonekana yuko sawa wakati damu bado inaendelea kutoka, au inakusanyika ndani ya mji wa mimba bila kutoka nje. Mwili wa mama mjamzito hustahimili upotevu wa damu kwa muda, kisha presha hushuka ghafla. Kwa sababu hiyo, damu hupimwa na mama huangaliwa mara kwa mara katika masaa ya kwanza baada ya kujifungua.
Visababishi vikuu
Wataalamu hukumbuka visababishi vinne vikuu:
Mji wa mimba kushindwa kusinyaa
Baada ya mtoto na kondo la nyuma kutoka, mji wa mimba hujikaza na kubana mishipa ya damu iliyokuwa ikilisha kondo. Mji wa mimba usipojikaza vizuri, mishipa hiyo huendelea kutoa damu. Hiki ndicho chanzo kikuu, na husababisha visa vingi vya tatizo hili.
Mabaki ya kondo la nyuma au utando
Kipande cha kondo au utando kikibaki ndani, mji wa mimba hushindwa kujikaza kikamilifu, na damu huendelea kutoka. Mabaki pia huweza kuleta maambukizi na damu ya kuchelewa.
Majeraha ya njia ya uzazi
Michaniko ya uke, shingo ya kizazi, msamba au mji wa mimba wenyewe huweza kutoa damu nyingi hata kama mji wa mimba umesinyaa vizuri. Mji wa mimba kupasuka ni hatari sana na huhitaji upasuaji wa haraka.
Matatizo ya kuganda kwa damu
Upungufu wa chembe sahani, magonjwa ya kurithi ya kuganda kwa damu, kifafa cha mimba kikali, kondo kujitenga mapema, au damu kuganda ovyo mwilini kisha kushindwa kuganda kunaweza kufanya damu isisimame.
Nani yuko kwenye hatari zaidi?
Aliyewahi kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua awali.
Mimba ya mapacha au mtoto mkubwa sana.
Maji mengi ya mimba.
Uchungu wa muda mrefu, au uliohitaji dawa ya kuongeza uchungu.
Kujifungua mara nyingi awali.
Kondo la nyuma la chini au lililojishika vibaya.
Upasuaji wa kujifungua awali.
Upungufu wa damu kabla ya kujifungua.
Kifafa cha mimba au presha ya mimba.
Homa wakati wa uchungu.
Hata hivyo, wanawake wengi wanaopata tatizo hili hawana kihatarishi chochote. Kwa sababu hiyo, kila mama anapaswa kujifungulia kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma ya dharura.
Vipimo na uchunguzi
Kupima kiasi cha damu kwa kutumia kitambaa maalumu chenye vipimo chini ya makalio, au kwa kupima uzito wa pedi na nguo.
Presha, mapigo ya moyo, kupumua na joto, kila baada ya dakika chache.
Kugusa tumbo kuona kama mji wa mimba umesinyaa.
Kuchunguza kondo la nyuma kama limetoka kamili.
Kuchunguza uke na shingo ya kizazi kutafuta michaniko.
Vipimo vya wingi wa damu, chembe sahani, kundi la damu na kuganda kwa damu.
Picha ya mawimbi ya sauti ya tumbo kutafuta mabaki ya kondo, hasa kwa damu ya kuchelewa.
Matibabu hospitalini
Matibabu huanza mara moja, na hatua kadhaa hufanyika kwa pamoja ndani ya dakika chache:
Kuita msaada, kumlaza mama na kuangalia njia ya hewa, kupumua na mzunguko wa damu.
Kukanda mji wa mimba juu ya tumbo ili ujikaze.
Dawa za kusinyaa mji wa mimba, kuanzia oksitosini, na nyingine kama misoprostoli au ergometrini kulingana na hali ya mama.
Dawa ya kusaidia damu kuganda, asidi traneksamiki, ndani ya masaa 3 tangu damu ianze.
Kuweka mirija ya maji ya mshipa na kuongeza maji.
Kuchunguza na kushona michaniko.
Kuondoa mabaki ya kondo kwa mikono au kwa kifaa, chini ya dawa ya maumivu.
Kuongezewa damu kama damu nyingi imepotea au kuna dalili za mshtuko.
Damu isiposimama, hatua zaidi hufuata: puto maalumu ndani ya mji wa mimba, kubana mji wa mimba kwa mikono, upasuaji wa kufunga mishipa au kushona mji wa mimba, na mwisho, ikibidi kuokoa maisha, kuondoa mji wa mimba.
Dozi za dawa hizi hutolewa na mtoa huduma kwa mwongozo wa taifa. Mama haruhusiwi kunywa dawa za kienyeji kuzuia damu.
Kuzuia wakati wa kujifungua
Kuhudhuria kliniki ya mama mjamzito na kutibu upungufu wa damu mapema.
Kujifungulia kituo cha afya.
Kupewa dawa ya kusinyaa mji wa mimba mara tu baada ya mtoto kuzaliwa.
Mtoa huduma kuhakikisha kondo limetoka kamili na mji wa mimba umesinyaa.
Kuangaliwa kwa karibu masaa 2 ya kwanza na siku ya kwanza baada ya kujifungua.
Kunyonyesha mapema, jambo linalosaidia mji wa mimba kujikaza.
Msaada wa nyumbani wakati wa kupona
Muhimu: hatua hizi ni za kumsaidia mama aliyekwisha kutibiwa na kuthibitishwa yuko salama. Haziwezi kuchukua nafasi ya matibabu ya dharura.
Njia ya msaada | Maelezo |
Kunyonyesha mara kwa mara | Huchochea homoni ya oksitosini, inayosaidia mji wa mimba kujikaza na kupunguza damu. |
Lishe bora | Chakula chenye madini chuma kama maini, nyama nyekundu, dagaa, maharage na mboga za majani, pamoja na vitamini C kama machungwa, na protini, kusaidia kurejesha damu. |
Vidonge vya madini chuma | Endelea kumeza kama ulivyoandikiwa, kwa miezi kadhaa, hadi damu irudi kawaida. |
Kunywa maji ya kutosha | Angalau lita 2 hadi 3 kwa siku, hasa kwa mama anayenyonyesha. |
Kupumzika | Epuka kazi nzito na kubeba vitu vizito kwa wiki kadhaa, lakini tembea kidogo kidogo kila siku. |
Kuangalia damu kwenye pedi | Angalia rangi, wingi na harufu, na mweleze mtoa huduma mabadiliko yoyote. |
Kuepuka mitishamba | Baadhi ya dawa za asili huongeza damu au kuathiri kuganda kwa damu. |
Lokia ya kawaida na damu isiyo ya kawaida
Baada ya kujifungua, damu na uchafu unaoitwa lokia hutoka kwa wiki 4 hadi 6. Mwanzoni ni nyekundu, kisha hupungua na kuwa ya pinki au kahawia, na mwisho ya njano au nyeupe. Mabonge madogo siku za mwanzo huweza kutokea.
Si kawaida kama damu inarudi kuwa nyekundu nyingi baada ya kupungua, ina harufu mbaya, inaambatana na homa au maumivu makali ya tumbo, au ina mabonge makubwa kuliko yai. Soma lokia baada ya kujifungua kawaida na lokia baada ya kujifungua kwa upasuaji.
Wakati wa kwenda hospitali haraka
Damu inaendelea kutoka kwa kasi au ina mabonge makubwa.
Pedi zaidi ya moja kujaa ndani ya muda wa saa moja.
Kizunguzungu, ngozi baridi, kuzimia au mapigo ya moyo kwenda kasi.
Homa au damu yenye harufu mbaya.
Damu kurudi baada ya kuisha, hasa pamoja na homa au maumivu makali ya tumbo.
Mtu wa familia ampeleke mama hospitali mara moja, au apige 112. Usisubiri kuona kama damu itasimama yenyewe. Soma dalili za upungufu wa damu.
Hitimisho
Kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua ni dharura inayoweza kuua ndani ya muda mfupi, lakini hutibika vizuri ikigunduliwa mapema. Chanzo kikuu ni mji wa mimba kushindwa kusinyaa, na vingine ni mabaki ya kondo, michaniko na matatizo ya kuganda kwa damu. Jifungulie kituo cha afya, tibu upungufu wa damu wakati wa mimba, na nenda hospitali mara moja ukiona pedi kujaa ndani ya muda wa saa moja, mabonge makubwa, kizunguzungu au damu yenye harufu mbaya na homa.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Kwa nini baadhi ya wanawake hupata tatizo hili na wengine hawapati?
Hatari huongezeka kwa aliyewahi kupata tatizo hili, mimba ya mapacha, mtoto mkubwa, uchungu wa muda mrefu, upasuaji wa awali, kondo la chini na upungufu wa damu. Hata hivyo, wanawake wengi wanaopata tatizo hili hawana kihatarishi chochote, ndiyo maana kila mama ajifungulie kituo cha afya.
2. Mama aliyewahi kutokwa damu nyingi anaweza kupata mimba tena?
Anaweza, na wengi hujifungua salama mimba inayofuata. Anapaswa kumweleza mtoa huduma historia yake mapema, kutibu upungufu wa damu, kufuatiliwa kwa karibu zaidi, na kujifungulia hospitali yenye uwezo wa kuongeza damu na kufanya upasuaji.
3. Kuna uhusiano kati ya upungufu wa damu wakati wa mimba na tatizo hili?
Upo. Mama mwenye upungufu wa damu hustahimili upotevu mdogo wa damu kwa shida zaidi, na hupata mshtuko haraka. Upungufu wa damu pia huongeza hatari ya mji wa mimba kushindwa kusinyaa. Kumeza vidonge vya madini chuma na asidi ya foliki wakati wa mimba husaidia.
4. Mazoezi mepesi kama kutembea yanafaa baada ya kutokwa damu nyingi?
Yanafaa baada ya mtoa huduma kuthibitisha uko salama. Kutembea kidogo kila siku husaidia mzunguko wa damu na kuzuia damu kuganda kwenye mishipa ya miguu. Ongeza muda polepole, na pumzika ukihisi kizunguzungu au uchovu mkubwa.
5. Mama aliyepata tatizo hili asubiri muda gani kabla ya mimba nyingine?
Inashauriwa kusubiri angalau miaka 2 baada ya kujifungua kabla ya kushika mimba nyingine. Muda huu humsaidia mwili kurudisha damu na nguvu, na hupunguza hatari kwa mimba inayofuata. Tumia njia ya uzazi wa mpango inayokufaa.
6. Tatizo hili linaweza kutokea bila damu kuonekana nje?
Linaweza. Damu huweza kukusanyika ndani ya mji wa mimba au ndani ya tumbo, kama mji wa mimba umepasuka, bila kutoka nje kwa wingi. Dalili huwa kizunguzungu, mapigo ya moyo kwenda kasi, ngozi baridi na tumbo kuvimba, na ni dharura.
7. Kuna nafasi gani ya kupona baada ya kutokwa damu nyingi?
Nafasi ya kupona ni kubwa sana kama matibabu yanaanza haraka na damu inaongezwa pale inapohitajika. Wanawake wengi hupona kikamilifu. Baada ya kurudi nyumbani, endelea na vidonge vya madini chuma, lishe bora na kliniki ya baada ya kujifungua.
8. Chai ya limao au tangawizi inaweza kupunguza damu?
Haiwezi. Hakuna ushahidi kwamba vinywaji hivi hupunguza damu baada ya kujifungua. Kuvitegemea huchelewesha matibabu ya hospitali ambayo ndiyo huokoa maisha. Damu nyingi inahitaji dawa za kusinyaa mji wa mimba na huduma ya dharura.
9. Mama hukaa hospitalini kwa muda gani baada ya tatizo hili?
Kwa kawaida hukaa siku 2 hadi 7, kutegemea kiasi cha damu kilichopotea, matibabu aliyopata na hali yake. Huruhusiwa kurudi nyumbani damu ikiwa imesimama, presha iko sawa na wingi wa damu unaridhisha, kisha hufuatiliwa kliniki.
10. Tatizo hili huzuiwaje wakati wa kujifungua?
Kwa kumpa mama dawa ya kusinyaa mji wa mimba mara tu mtoto anapozaliwa, kuhakikisha kondo la nyuma limetoka kamili, kuangalia mji wa mimba umesinyaa, na kumfuatilia mama kwa karibu masaa ya kwanza. Kutibu upungufu wa damu wakati wa mimba pia husaidia.
11. Kutoka damu kidogo kidogo kwa wiki kadhaa baada ya kujifungua ni kawaida?
Ni kawaida. Lokia hutoka kwa wiki 4 hadi 6, ikipungua taratibu na kubadilika rangi kuwa pinki, kahawia na mwisho njano au nyeupe. Damu ikirudi kuwa nyekundu nyingi, ikiwa na harufu mbaya, homa au maumivu makali, mwone daktari.
12. Damu ikitoka kidogo kidogo kwa zaidi ya wiki 6 nifanye nini?
Damu kidogo inayoendelea zaidi ya wiki 6 hadi 8 inahitaji kuchunguzwa, kwa sababu huweza kutokana na mabaki ya kondo, maambukizi, au hedhi kurudi mapema. Nenda kliniki upimwe, hasa kama damu inaongezeka, ina harufu mbaya, au una homa.
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeandikwa:
27 Novemba 2026, 07:25:51
Rejea za dawa
World Health Organization. WHO recommendations on the assessment of postpartum blood loss and use of a treatment bundle for postpartum haemorrhage. Geneva: WHO; 2023.
Gallos I, et al. Randomized trial of early detection and treatment of postpartum hemorrhage (E-MOTIVE). N Engl J Med. 2023;389(1):11–21.
WOMAN Trial Collaborators. Effect of early tranexamic acid administration on mortality, hysterectomy, and other morbidities in women with post-partum haemorrhage (WOMAN). Lancet. 2017;389(10084):2105–16.
Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026.

