top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Dkt. Adolf S, M.D

Dkt. Lugonda B, M.D

22 Agosti 2026, 17:08:26

Image-empty-state.png

Mimba ya miezi sita

Imeboreshwa:

Mimba ya miezi sita ni sawa na mimba ya wiki 21 hadi 24, katika kipindi hiki mabadiliko mbalimbali hutokea mwilini katika kila wiki. Makala hii imeelezea kuhusu mabadiliko yanayotokea katika lila wiki ya mimba ya miezi sita.


Mimba ya wiki sishirini na moja (21)

Humaanisha miezi mitano na siku moja ya ujauzito.


Nini hutokea kwa mtoto?


  • Huwa na urefu wa ndizi

  • Kichwa huwa na nywele zilizokuwa vema, na mwili wote hufunikwa na vinyweleo laini

  • Ngozi yake huwa na utando mweupe unaozuia isijikunje

  • Mifupa laini hubadilika kuwa migumu kiasi

  • Korodani ambazo zilikuwa pamoja na matumbo huanza kushuka kuelekea kwenye mifuko yake



Nini hutokea kwa mama?


  • Kuanza kuhisi mtoto akicheza tumboni hasa kwa wanawake ambao ni ujauzito wa kwanza

  • Kuvimba miguu kutokana na kuongezeka kwa maji katika damu

  • Kupata kiungulia na chakula kutomeng’enywa vema

  • Kushindwa kulala vema kutokana na mgandamizo wa mimba

  • Matiti hujaa na Sehemu ya chuchu huwa nyeusi Zaidi na kuwa na vitu kama vipele, na wakati mwingine kutoa maziwa

  • Katika kipindi hiki mimba huendelea kukua kwa kasi na kuwa usawa wa kitovu, na kuongezeka kwa takribani inchi moja na nusu kwa wiki zinazofuata

  • Mstari mweusi chini ya kitovu hutokea na ngozi ya tumbo huanza kuwa na michirizi




Mimba ya wiki ishirini na mbili (22)

Nini hutokea kwa mtoto

  • Mtoto huwa na uzito wa gramu 430 na uzito kati ya sentimeta 27.8

  • Urefu wake huwa sawa na ukubwa wa papai na urefu wa machenza matano

  • Vinyweleo vinavyofunika mwili wake huanza kupata rangi nyeusi

  • Mifupa yake hukomaa

  • Uwezo wake wa kusikia huongezeka zaidi na anaweza kutambua sauti ya mama

  • Pia huweza kuhisi sauti na mijongeo kutoka nje na kuonesha muitikio, mfano anaweza kuamka anaposikia kelele



Nini hutokea kwa mama

  • Mama huendelea kuona mabadiliko kama

  • Kuhisi vitu vinatembea kwenye mikono

  • Kupata maumivu ya miguu

  • Kuvimba miguu kiasi

  • Kubanwa pua na mafua ya mara kwa mara

  • Kutokwa damu kwenye fizi



Mimba ya wiki ishirini na tatu (23)


Nini hutokea kwa mtoto
  • Mtoto huwa na uzito wa gramu 450 na uzito kati ya sentimeta 28 hadi 36

  • Vinyweleo vinavyofunika mwili wake huanza kupata rangi nyeusi

  • Mifupa yake hukomaa

  • Uwezo wake wa kusikia huongezeka zaidi na anaweza kutambua sauti ya mama

  • Pia huweza kuhisi sauti na mijongeo kutoka nje na kuonesha muitikio, mfano anaweza kuamka anaposikia kelele



Nini hutokea kwa mama
  • Mama huendelea kuona mabadiliko kama

  • Kuhisi vitu vinatembea kwenye mikono

  • Kupata maumivu ya miguu

  • Kuvimba miguu kiasi

  • Kubanwa pua na mafua ya mara kwa mara

  • Kutokwa damu kwenye fizi


Mimba ya wiki ishirini na nne (24)


Nini hutokea kwa mtoto
  • Hadi kufikia mwisho wa wiki ya 24 mtoto huwa na uzito wa kati ya gramu 600 hadi 700

  • Ubongo na mfumo wa fahamu huendelea kukua na kuwa imara

  • Mapafu huwa yamekomaa kwa kiasi kikubwa na endapo akizaliwa katika kipindi hiki anaweza kujaribu kupumua mwenyewe

  • Ngozi yake huwa na mikunjo na mafuta huendelea kutengenezwa kwenye ngozi



Nini hutokea kwa mama
  • Mama anaweza kuona ongezeko la miguu yake kutokana na viatu alivyokuwa akivaa awali kutokumtosha

  • Ngozi ya tumbo kuwa kavu na kupata muwasho kutokana na michirizi

  • Kuota nywele kwenye maeneo ambayo sio rasmi kama vile kuzunguka kitovu na chuchu

  • Ngozi ya sehemu za siri na maeneo ya chuchu kuwa nyeusi zaidi

  • Kukoroma


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake ya kina kuhusu mimba ya miezi sita

1. Je, ni kawaida mtoto kucheza sana katika miezi sita ya ujauzito?

Katika miezi sita ya ujauzito, ni kawaida kabisa kuanza kuhisi mtoto akicheza mara kwa mara. Kufikia wiki ya 21 hadi 24, misuli, mifupa na mfumo wa neva wa mtoto huwa umeendelea kukomaa kiasi cha kumwezesha kufanya harakati mbalimbali kama kupiga mateke, kugeuka, kunyoosha mikono na miguu pamoja na kunyonya vidole vyake. Harakati hizi ni ishara nzuri kwamba mfumo wa neva na misuli vinaendelea kufanya kazi vizuri.


Kiwango cha kucheza kwa mtoto hutofautiana kati ya mtoto mmoja na mwingine. Wapo watoto wanaocheza mara nyingi mchana, wengine usiku, na wengine huwa na vipindi vya kulala vinavyoweza kudumu dakika 20 hadi 40. Mama anaweza kuhisi mtoto akicheza zaidi baada ya kula, kunywa kitu chenye sukari kidogo au anapolala ubavu wa kushoto.


Iwapo umeanza kuhisi harakati za mtoto halafu zikapungua sana au kutoweka kabisa kwa muda mrefu kuliko kawaida, usisubiri mpaka siku inayofuata. Ni muhimu kufika hospitali ili mtoto afanyiwe uchunguzi. Ingawa katika wiki 21–24 bado kuhesabu mateke hakujapendekezwa rasmi kama ilivyo baada ya wiki 28, mabadiliko makubwa ya harakati yanapaswa kuchunguzwa.

2. Kwa nini napata maumivu ya mbavu katika ujauzito wa miezi sita?

Maumivu ya mbavu ni malalamiko ya kawaida katika miezi sita ya ujauzito. Kadiri mfuko wa uzazi unavyoongezeka, huanza kusukuma viungo vya tumboni kuelekea juu. Hali hii husababisha misuli na mbavu kuvutika na wakati mwingine mama huhisi maumivu upande mmoja au pande zote mbili za kifua.


Mtoto anapoendelea kukua na kuanza kupiga mateke kwa nguvu zaidi, anaweza pia kugonga sehemu ya mbavu na kuongeza maumivu, hasa unapokaa muda mrefu au unapoinama mbele. Homoni ya relaxin pia hulegeza mishipa na viungio vya mwili ili kujiandaa kwa kujifungua, jambo ambalo linaweza kuongeza maumivu kwenye kifua na mgongo.


Hata hivyo, ikiwa maumivu ya mbavu yanaambatana na maumivu makali ya kichwa, kuona ukungu, kuvimba uso au shinikizo la damu, yanaweza kuwa dalili ya pre-eclampsia na yanahitaji uchunguzi wa haraka. Vivyo hivyo, maumivu makali ya kifua yanayoambatana na kupumua kwa shida yanapaswa kutathminiwa hospitalini mara moja.

3. Je, ni kawaida kupata maziwa kutoka kwenye matiti katika miezi sita ya ujauzito?

Baadhi ya wajawazito huanza kuona matone ya majimaji ya njano au yenye rangi ya dhahabu kutoka kwenye matiti katika miezi sita ya ujauzito. Majimaji haya huitwa kolostramu, ambayo ndiyo maziwa ya kwanza yenye kingamwili nyingi yanayomlinda mtoto dhidi ya maambukizi baada ya kuzaliwa.


Kolostramu huanza kutengenezwa mapema sana wakati wa ujauzito kutokana na athari za homoni za prolaktini, estrojeni na projesteroni. Si kila mama ataona maziwa haya yakitoka kabla ya kujifungua, na kutokuyapata hakumaanishi kuwa hutakuwa na maziwa baada ya kujifungua.


Usijaribu kukamua matiti mara kwa mara ili kutoa maziwa isipokuwa umeelekezwa na daktari kwa sababu kuchochea chuchu kupita kiasi kunaweza kuongeza utolewaji wa homoni ya oxytocin. Ikiwa maji yanayotoka yana damu nyingi, yana harufu mbaya au yanaambatana na uvimbe mkali wa matiti, unapaswa kumuona daktari.

4. Kwa nini napata ganzi au kufa ganzi mikononi wakati wa ujauzito wa miezi sita?

Kupata ganzi, kuwashwa au hisia za sindano kwenye mikono ni hali inayowapata baadhi ya wanawake wakati wa ujauzito, hasa kuanzia miezi ya kati na kuendelea. Mara nyingi hali hii husababishwa na sindromu ya shimo kapa, ambayo hutokea pale maji yanapoongezeka mwilini na kusababisha uvimbe unaobana mshipa wa median nerve unaopita kwenye kifundo cha mkono. Matokeo yake ni ganzi, maumivu au udhaifu wa vidole, hasa kidole gumba, cha shahada na cha kati. Dalili hizi zinaweza kuwa mbaya zaidi usiku au unapoamka asubuhi.


Kuongezeka kwa homoni za ujauzito pamoja na ongezeko la damu na maji mwilini huchangia uvimbe huu. Wanawake wenye ujauzito wa mapacha, kisukari au uzito mkubwa wanaweza kuwa katika hatari zaidi ya kupata tatizo hili. Ingawa hali hii inaweza kusumbua, mara nyingi si hatari kwa mtoto na huanza kupungua baada ya kujifungua kadri kiwango cha maji mwilini kinavyorejea kawaida.


Unaweza kupunguza dalili kwa kupumzisha mikono mara kwa mara, kuepuka kukunja vifundo vya mikono unapolala na kutumia sprinti ya maungio ya mkono hasa usiku ikiwa daktari atashauri. Ikiwa ganzi ni kali sana, mkono unakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kushika vitu au maumivu yanaendelea kuongezeka, ni muhimu kumuona daktari ili kuhakikisha hakuna sababu nyingine kama ugonjwa wa kisukari, matatizo ya shingo au upungufu wa vitamini.

5. Kwa nini fizi zangu zinatoa damu ninapopiga mswaki nikiwa na ujauzito wa miezi sita?

Kutokwa na damu kwenye fizi wakati wa ujauzito ni jambo linalotokea kwa wanawake wengi kutokana na mabadiliko ya homoni, hasa estrojni na projesteroni. Homoni hizi huongeza mtiririko wa damu kwenye fizi na kuzifanya ziwe nyepesi kuvimba na kuvuja damu hata wakati wa kupiga mswaki au kutumia uzi wa meno. Hali hii hujulikana kama gingivaitisi ya ujauzitoni na huanza kuonekana kuanzia trimester ya pili kwa wanawake wengi.


Ingawa kutokwa na damu kidogo kunaweza kuwa jambo la kawaida, kutotunza afya ya kinywa kunaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi. Plaque na bakteria wanaokusanyika kwenye meno huongeza uvimbe wa fizi na wakati mwingine husababisha ugonjwa wa fizi (periodontaitisi). Tafiti zimeonyesha kuwa ugonjwa mkali wa fizi unaweza kuhusishwa na ongezeko la hatari ya kujifungua kabla ya wakati au mtoto kuzaliwa na uzito mdogo, ingawa uhusiano huu bado unaendelea kufanyiwa tafiti.


Ili kulinda afya ya fizi, piga mswaki angalau mara mbili kwa siku kwa kutumia mswaki laini na dawa ya meno yenye fluoride, tumia uzi wa meno kila siku na hudhuria kliniki ya meno ikiwa una maumivu au kutokwa na damu nyingi. Usiogope kwenda kwa daktari wa meno ukiwa mjamzito, kwani matibabu mengi ya msingi ya meno ni salama wakati wa ujauzito na yanaweza kusaidia kuzuia matatizo makubwa zaidi.

6. Je, mtoto anaweza kusikia sauti yangu akiwa na ujauzito wa miezi sita?

Kufikia miezi sita ya ujauzito, mfumo wa kusikia wa mtoto huwa umeendelea kukomaa kiasi cha kuweza kutambua sauti mbalimbali kutoka ndani na nje ya mwili wa mama. Tafiti zinaonyesha kuwa mtoto anaweza kusikia mapigo ya moyo wa mama, mtiririko wa damu, sauti ya tumbo pamoja na sauti ya mama anapozungumza. Kadiri ujauzito unavyoendelea, uwezo huu huimarika zaidi.


Sauti ya mama ndiyo mtoto huisikia vizuri zaidi kwa sababu husafiri kupitia mwili wa mama pamoja na maji ya uzazi. Pia mtoto anaweza kuanza kuonyesha mwitikio kwa sauti kubwa kwa kubadilisha harakati zake au mapigo ya moyo. Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa watoto wachanga wanaweza kutambua sauti ya mama wao mara tu baada ya kuzaliwa kutokana na kuisikia mara kwa mara wakiwa tumboni.


Kwa sababu hiyo, wataalamu wengi wanawahimiza wazazi kuzungumza na mtoto, kuimba au kusoma kwa sauti wakati wa ujauzito. Ingawa hakuna ushahidi kuwa kufanya hivyo huongeza akili ya mtoto, kuna ushahidi unaoonyesha kuwa kunaweza kusaidia kujenga uhusiano wa kihisia kati ya wazazi na mtoto kabla hata hajazaliwa. Pia inaweza kumsaidia mama kupunguza msongo wa mawazo na kufurahia ujauzito wake.

7. Je, ni salama kulala chali nikiwa na ujauzito wa miezi sita?

Katika miezi sita ya ujauzito, wataalamu wengi wanashauri kulala ubavu wa kushoto au kulia badala ya kulala chali kwa muda mrefu. Kadiri mfuko wa uzazi unavyokuwa mkubwa, unaweza kubana mshipa mkubwa unaoitwa Vena kava ya shini, ambao hurudisha damu kutoka miguuni kwenda moyoni. Kubanwa kwa mshipa huu kunaweza kupunguza mtiririko wa damu kwa mama na mtoto na kusababisha kizunguzungu au kushuka kwa shinikizo la damu kwa baadhi ya wanawake.


Kulala ubavu wa kushoto mara nyingi hupendekezwa kwa sababu kunaweza kuboresha mtiririko wa damu kwenda kwenye kondo la nyuma na figo za mama. Hata hivyo, tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kulala ubavu wa kulia pia ni salama kwa wanawake wengi. Jambo muhimu zaidi ni kuepuka kukaa chali kwa muda mrefu ikiwa hali hiyo inakusababishia kizunguzungu, kupumua kwa shida au usumbufu.


Usiwe na wasiwasi ukijikuta umegeuka na kulala chali wakati wa usingizi. Hilo hutokea kwa wanawake wengi na si sababu ya kuogopa. Unapoamka, geuka tu na ulale ubavuni tena. Unaweza kutumia mto kati ya magoti au nyuma ya mgongo ili kusaidia kudumisha mkao unaokufanya ujisikie vizuri wakati wa kulala.

8. Kwa nini miguu na vifundo vya miguu vinavimba katika miezi sita ya ujauzito?

Kuvimba miguu na vifundo vya miguu ni hali ya kawaida kwa wanawake wengi kuanzia trimester ya pili. Hali hii hutokea kwa sababu mwili huzalisha damu na maji mengi zaidi ili kumsaidia mtoto kukua. Wakati huo huo, mfuko wa uzazi unaokua huanza kubana mishipa ya damu inayorudisha damu kutoka miguuni kwenda moyoni, hivyo maji hukusanyika kwenye tishu za miguu na vifundo vya miguu.


Uvimbe huu mara nyingi huongezeka mwisho wa siku, baada ya kusimama muda mrefu au wakati wa hali ya hewa ya joto. Kwa kawaida hupungua baada ya kupumzika ukiwa umeinua miguu juu kidogo au unapolala. Wanawake wengi hupata uvimbe kwenye miguu yote miwili kwa kiwango kinachofanana, na hali hii huwa ya kawaida ikiwa haijaambatana na dalili nyingine.


Hata hivyo, uvimbe unaotokea ghafla, hasa ukiwa mkubwa kwenye uso, mikono au mguu mmoja pekee, unaweza kuwa dalili ya tatizo kama shinikizo la damu la kifafa cha mimba au kuganda kwa damu kwenye mshipa ya ndani. Ikiwa uvimbe unaambatana na maumivu makali ya kichwa, kuona ukungu, maumivu ya juu ya tumbo au kupumua kwa shida, unapaswa kwenda hospitali mara moja kwa uchunguzi.

9. Je, ni kawaida kupata mikazo ya tumbo (uchungu wa uongo) katika miezi sita ya ujauzito?

Kuanzia miezi sita ya ujauzito, wanawake wengi huanza kupata mikazo ya tumbo inayojulikana kama uchungu wa uongo au mikazo ya Braxton Hicks. Hii ni mikazo ya kawaida ya misuli ya mfuko wa uzazi ambayo huandaa uterasi kwa ajili ya kujifungua baadaye. Mikazo hii si uchungu wa kujifungua na mara nyingi huwa ya muda mfupi, haitokei kwa mpangilio maalumu na haiongezeki nguvu kadri muda unavyopita.


Mikazo hii inaweza kuchochewa na kutembea sana, kujamiiana, upungufu wa maji mwilini au kibofu cha mkojo kujaa. Mara nyingi mikazo hupungua unapopumzika, kubadilisha mkao au kunywa maji. Wanawake wengine huhisi tumbo linakuwa gumu kwa sekunde 30 hadi 60 kisha hurudi kawaida bila maumivu makali.


Ni muhimu kutofautisha uchungu wa uongo na uchungu wa kujifungua kabla ya wakati. Ikiwa mikazo inatokea kwa vipindi vya kawaida, inaongezeka nguvu, inaambatana na maumivu ya mgongo, kutokwa na damu au kuvuja maji ukeni kabla ya wiki 37, unapaswa kufika hospitali mara moja kwa uchunguzi. Matibabu ya mapema yanaweza kusaidia kuchelewesha uchungu ikiwa ni kujifungua kabla ya wakati.

10. Nina ujauzito wa miezi sita lakini uzito wangu haujaongezeka sana. Je, mtoto anakua vizuri?

Kutokuongezeka sana kwa uzito wa mama hakumaanishi moja kwa moja kuwa mtoto hakui vizuri. Ongezeko la uzito wakati wa ujauzito hutegemea uzito wa mama kabla ya kushika mimba, lishe anayokula, kiwango cha shughuli anazofanya na kama anapata kichefuchefu au kutapika. Wanawake waliokuwa na uzito mkubwa kabla ya ujauzito wanaweza kuongezeka uzito kwa kiwango kidogo kuliko waliokuwa na uzito wa kawaida au pungufu.


Njia sahihi ya kutathmini ukuaji wa mtoto si kuangalia uzito wa mama pekee. Daktari hufuatilia ukuaji wa mtoto kwa kupima urefu wa mfuko wa uzazi, kufanya uchunguzi wa ultrasound inapohitajika na kufuatilia maendeleo ya ujauzito katika kila kliniki. Ikiwa vipimo hivi vinaonyesha mtoto anakua vizuri, kutokuongezeka sana kwa uzito kunaweza kuwa si tatizo.


Hata hivyo, ikiwa uzito wako unapungua, hushindi kula kutokana na kutapika, una dalili za utapiamlo au daktari anaona mtoto hakui kwa kiwango kinachotarajiwa (Ukinzani kwenye ukuaji wa mtoto tumboni), utahitaji uchunguzi zaidi na ushauri wa lishe. Hakikisha unakula mlo kamili wenye protini, nafaka zisizokobolewa, mboga, matunda na kutumia virutubisho ulivyoandikiwa ili kusaidia ukuaji mzuri wa mtoto.

11. Mimi ni mjamzito wa miezi 6, nina maumivu makali kwenye uke kiasi kwamba nashindwa hata kutembea au kunyanyua mguu. Pia napata maumivu kwenye nyonga. Tatizo linaweza kuwa nini?

Maumivu makali kwenye uke yanayoambatana na kushindwa kunyanyua mguu au kutembea wakati wa ujauzito wa miezi sita si jambo linalopaswa kupuuzwa. Moja ya sababu zinazojulikana zaidi ni Maumivu ya ukanda wa nyonga, ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama ukosefu wa utendaji wa mfupa simfisisi. Hali hii hutokea pale viungio vya nyonga vinapolegea kupita kiasi tokana na homoni ya relaksini, pamoja na kuongezeka kwa uzito wa mtoto na mfuko wa uzazi. Maumivu huweza kuhisiwa katikati ya mfupa wa kinena, ndani ya uke, sehemu za mapaja, makalio au mgongoni, na mara nyingi huongezeka unaponyanyua mguu mmoja, kupanda ngazi, kuingia au kutoka kwenye gari, kuvaa nguo ukiwa umesimama kwa mguu mmoja au kugeuka kitandani.


Ingawa Maumivu ya ukanda wa nyonga ndiyo sababu inayopatikana mara nyingi, maumivu makali yanaweza pia kusababishwa na matatizo mengine kama maambukizi ya njia ya mkojo, maambukizi ya uke, mawe kwenye figo, matatizo ya nyonga au hata uchungu wa kujifungua kabla ya wakati endapo maumivu yanaambatana na mikazo ya tumbo inayojirudia, kutokwa na damu au kuvuja maji. Kwa sababu hizo, ni muhimu usifanye hitimisho kuwa ni maumivu ya kawaida bila kufanyiwa uchunguzi. Daktari anaweza kufanya uchunguzi wa mwili, kupima mkojo na, inapohitajika, kufanya vipimo vingine ili kubaini chanzo halisi cha maumivu.


Matibabu hutegemea chanzo cha tatizo. Ikiwa ni maumivu ya ukanda wa nyonga, daktari anaweza kupendekeza mazoezi maalumu yanayoongozwa na mtaalamu wa tiba ya viungo, matumizi ya mkanda wa kushikilia nyonga, kubadilisha namna ya kutembea na kulala, pamoja na kutumia paracetamol ikiwa inahitajika kwa ushauri wa daktari. Unapaswa kwenda hospitali haraka ikiwa maumivu ni makali sana kiasi cha kushindwa kutembea, yanaambatana na homa, kutokwa na damu ukeni, kuvuja maji, kupungua kwa harakati za mtoto au mikazo ya tumbo inayotokea kwa vipindi vya kawaida, kwa kuwa dalili hizi zinaweza kuashiria tatizo linalohitaji matibabu ya haraka. Tafiti zinaonyesha kuwa utambuzi na matibabu ya mapema ya maumivu ya ukanda wa nyonga husaidia kupunguza maumivu, kuboresha uwezo wa kutembea na kuendelea na shughuli za kila siku, pamoja na kuboresha ubora wa maisha ya mjamzito.









ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

3 Aprili 2026, 06:13:41

Rejea za dawa

  1. American Society for Reproductive Medicine; American College of Obstetricians and Gynecologists' Committee on Gynecologic Practice. Prepregnancy counseling: Committee Opinion No. 762. Fertil Steril. 2019 Jan;111(1):32-42. [PubMed]

  2. Berglund A, et al. Preconception health and care (PHC)-a strategy for improved maternal and child health. Ups J Med Sci. 2016 Nov;121(4):216-221. [PMC free article] [PubMed]

  3. Annadurai K, et al. Preconception care: A pragmatic approach for planned pregnancy. J Res Med Sci. 2017;22:26. [PMC free article] [PubMed]

  4. McClatchey T, et al. Missed opportunities: unidentified genetic risk factors in prenatal care. Prenat Diagn. 2018 Jan;38(1):75-79. [PubMed]

  5. Ko SC, et al. Estimated Annual Perinatal Hepatitis B Virus Infections in the United States, 2000-2009. J Pediatric Infect Dis Soc. 2016 Jun;5(2):114-21. [PubMed]

  6. Tohme RA, et al. Hepatitis B virus infection among pregnant women in Haiti: A cross-sectional serosurvey. J Clin Virol. 2016 Mar;76:66-71. [PMC free article] [PubMed]

  7. Bhavadharini B, et al. Screening and diagnosis of gestational diabetes mellitus - relevance to low and middle income countries. Clin Diabetes Endocrinol. 2016;2:13. [PMC free article] [PubMed]

  8. ACOG Practice Bulletin No. 190 Summary: Gestational Diabetes Mellitus. Obstet Gynecol. 2018 Feb;131(2):406-408. [PubMed]

  9. Rule T, et al. Introducing a new collaborative prenatal clinic model. Int J Gynaecol Obstet. 2019 Mar;144(3):248-251. [PubMed]

bottom of page