top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Benjamin M, MD

17 Februari 2026, 04:17:18

Maziwa ya mchele: Faida za Kiafya
Maziwa ya mchele: Faida za Kiafya
Faida, Hasara na Matumizi Salama

Maziwa ya mchele ni aina ya maziwa ya asili ya mimea yanayotengenezwa kwa kuchanganya mchele uliochemshwa au kusagwa na maji, kisha kuchujwa ili kupata kimiminika chepesi chenye ladha laini. Yamekuwa maarufu kwa watu wenye mzio wa maziwa ya ng’ombe, wasiovumilia laktosi, au wanaofuata lishe ya mimea.


Kwa ujumla, maziwa ya mchele ni rahisi kumeng’enywa kuliko maziwa mengi ya mimea, na huwa na muundo mwepesi unaofaa kwa watu wenye matatizo ya tumbo au wanaoharisha. Hata hivyo, yana sifa na mapungufu muhimu yanayopaswa kufahamika kabla ya kuyatumia mara kwa mara.


Faida za maziwa ya mchele


1. Rahisi kumeng’enywa

Maziwa ya mchele hayana laktosi wala protini nzito kama casein inayopatikana kwenye maziwa ya ng’ombe. Hii huyafanya yafae kwa watu:

  • Wenye mzio wa maziwa ya ng’ombe

  • Wasiovumilia laktosi

  • Wenye tumbo nyeti


2. Hayana laktosi na gluteni

Kwa kuwa yanatokana na mchele, maziwa haya:

  • Hayana laktosi

  • Hayana gluteni (isipokuwa kama yameongezewa viambato vyenye gluteni wakati wa usindikaji)

Hivyo yanafaa kwa watu wenye tatizo la matumbo yasiyovumilia laktosi au ugonjwa wa seliaki.


3. Husaidia wagonjwa wa shinikizo la damu

Kwa asili yana:

  • Kiasi kidogo cha mafuta yaliyoshamiri

  • Hakuna lehemu mbaya

Hali hii hufanya yawe chaguo linaloweza kusaidia katika lishe ya watu wenye shinikizo la juu la damu au wanaotaka kulinda afya ya moyo.


4. Mafuta kidogo

Maziwa ya mchele yana kiwango kidogo cha mafuta na protini, jambo linalowafanya yawe mepesi kwa watu wanaotaka kupunguza ulaji wa mafuta.


Muundo wa lishe wa maziwa ya mchele

Kwa wastani (kwa kikombe kimoja):


Maziwa ya mchele yana:

  • Wanga nyingi zaidi kuliko maziwa ya mimea mengine

  • Kiasi kidogo cha protini

  • Mafuta yasiyoshamiri

  • Vitamin E

  • Madini ya chuma (mengi zaidi kuliko maziwa ya ng’ombe)

  • Kiasi kidogo cha kalsiamu (isipokuwa kama yameongezewa )


Baadhi ya maziwa ya mchele ya viwandani huongezewa:

  • Vitamin D

  • Vitamin B12

  • Kalsiamu


Maziwa ya mchele hupungukiwa na:

  • Laktosi

  • Gluteni

  • Lehemu

  • Protini ya kutosha

  • Vitamin B12 (isipokuwa kama yameongezewa)


Matumizi kwa Watoto wadogo

Hili ni eneo muhimu sana. Maziwa ya mchele hayana protini ya kutosha kwa ukuaji wa mtoto mdogo. Tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya muda mrefu bila lishe mbadala yenye protini ya kutosha yanaweza kuhusishwa na:

  • Utapiamlo

  • Udumavu

  • Upungufu wa uzito


Kwa watoto chini ya miaka 2, maziwa ya mchele hayapendekezwi kama mbadala wa maziwa ya mama au maziwa ya kopo. Ikiwa mzazi atachagua kuyatumia, ni muhimu kupata ushauri wa daktari au mtaalamu wa lishe ili kuhakikisha mtoto anapata protini na virutubisho vya kutosha.


Hasara na Tahadhari


1. Protini kidogo sana

Ikilinganishwa na maziwa ya ng’ombe au hata maziwa ya soya, maziwa ya mchele yana protini kidogo sana. Hivyo hayafai kuwa chanzo kikuu cha protini.


2. Wanga mwingi

Kwa sababu yana wanga mwingi, watu wenye kisukari wanapaswa kuyatumia kwa kiasi na kufuatilia kiwango cha sukari.


3. Arseniki (Kwa tahadhari)

Mchele kwa asili unaweza kufyonza kiasi kidogo cha arseniki, kemikali inayopatikana kwenye udongo na maji. Arseniki katika viwango vya juu au matumizi ya muda mrefu inaweza kuwa na madhara kiafya, hasa kwa watoto wadogo.

Ingawa bidhaa nyingi za maziwa ya mchele zinazozalishwa viwandani huchunguzwa na kuwekwa ndani ya viwango vinavyokubalika kiafya, si busara kuyatumia kama chanzo pekee cha maziwa kila siku kwa muda mrefu. Inashauriwa kubadilisha na aina nyingine za maziwa ya mimea (kama ya soya, lozi au nazi) ili kupunguza uwezekano wa kukusanya kiwango kikubwa cha arseniki mwilini na kuhakikisha mwili unapata virutubisho vya aina mbalimbali.


Kwa watoto wadogo na wajawazito, tahadhari inahitajika zaidi, hivyo ni vyema kushauriana na mtaalamu wa afya kabla ya kuyatumia mara kwa mara.


Nani wanaofaa kutumia maziwa ya mchele?

Maziwa ya mchele yanafaa kwa:

  • Watu wasiovumilia laktosi

  • Wenye mzio wa maziwa ya ng’ombe

  • Wenye mzio wa soya au karanga

  • Wanaofuata lishe ya mimea

  • Wenye tumbo nyeti


Hitimisho

Maziwa ya mchele ni chaguo jepesi, rahisi kumeng’enywa na lisilo na laktosi wala lehemu. Hata hivyo, yana protini kidogo na hayafai kuwa chanzo kikuu cha lishe kwa watoto wadogo bila ushauri wa kitaalamu.

Kwa watu wazima wenye mzio wa maziwa au wanaotafuta mbadala wa mimea, maziwa ya mchele yanaweza kuwa sehemu salama ya lishe — hasa yakichaguliwa yale yaliyoongezewa vitamini na madini muhimu.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Maziwa ya mchele ni nini na hutengenezwa vipi?

Maziwa ya mchele ni kinywaji kinachotengenezwa kutokana na mchele uliopikwa au kusagwa na kuchanganywa na maji, kisha kuchujwa kupata kinywaji laini. Mara nyingi hutengenezwa kwa mchele mweupe au kahawia, na baadhi ya bidhaa huongezewa vitamini na madini ili kuboresha thamani ya lishe.

2. Je, maziwa ya mchele ni salama kwa watoto wadogo?

Maziwa ya mchele yanahitaji tahadhari kwa watoto wadogo kwa sababu hayana protini ya kutosha na yanaweza kuchangia utapiamlo. Kwa mtoto chini ya miaka 5, ni muhimu kupata ushauri wa daktari au mtaalamu wa lishe kabla ya kuyatumia kama sehemu ya lishe ya kila siku.

3. Kwa nini maziwa ya mchele yanapendekezwa kwa watu wenye matatizo ya tumbo?

Maziwa ya mchele ni rahisi kumeng’enywa kuliko aina nyingi za maziwa ya mimea. Hayana mafuta mengi, hayana laktosi wala gluteni, hivyo huwa laini kwa tumbo hasa wakati wa:

  • Kuharisha

  • Kichefuchefu

  • Maumivu ya tumbo

  • Urejeshaji baada ya sumu ya chakula

4. Je, maziwa ya mchele yanafaa kwa wagonjwa wa shinikizo la damu?

Ndiyo. Maziwa ya mchele yana kiasi kidogo cha mafuta kuliko maziwa ya wanyama. Hivyo yanaweza kusaidia watu wenye shinikizo la juu la damu kama sehemu ya lishe yenye mafuta kidogo.

5. Maziwa ya mchele yana kiasi gani cha protini ukilinganisha na maziwa ya ng’ombe?

Maziwa ya mchele huwa na kiasi kidogo sana cha protini. Hiki ndicho chanzo kikuu cha changamoto kwa watoto wadogo na watu wanaohitaji protini nyingi. Kwa watu wazima, yanafaa zaidi kama kinywaji kuliko chanzo cha protini.

6. Je, maziwa ya mchele yana virutubisho gani muhimu?

Kwa kawaida, maziwa ya mchele yana:

  • Omega-3 na mafuta yasiyo na kolesteroli

  • Vitamin E kwa kinga ya mwili na afya ya ngozi

  • Madini kama chuma, ingawa bado huwa chini kuliko mahitaji ya kila siku

  • Wanga unaotoa nguvu haraka

Bidhaa nyingi huongezewa Vitamini D na B12, hivyo soma lebo kabla ya kununua.

7. Ni nani anayeweza kufaidika zaidi kutokana na maziwa ya mchele?

Maziwa ya mchele yanafaa kwa:

  • Watu wenye mzio wa maziwa ya ng’ombe

  • Watu wasiotumia bidhaa za wanyama (wanaotumia mimea tu)

  • Wenye matatizo ya kumeng’enya laktosi (wasiohimili laktosi)

  • Wenye kuvimbiwa kwa sababu hayana mafuta mengi

  • Wagonjwa wanaopona kutoka kuharisha

8. Je, maziwa ya mchele yana sukari nyingi?

Ndiyo. Kiasili, mchele una wanga ambao hubadilika kuwa sukari wakati wa utengenezaji. Baadhi ya bidhaa huwongezewa sukari zaidi.Kwa hivyo, watu wenye kisukari au wanaodhibiti sukari wanapaswa kuangalia kiwango cha sukari kwenye lebo.

9. Naweza kutumia maziwa ya mchele kupikia?

Ndiyo. Maziwa ya mchele yana ladha tamu na mwili mwepesi, hivyo yanafaa kwa:

  • Uji (shayiri)

  • Sharubati

  • Mayai ya kupikia (bila kuhitaji protini nyingi)

  • Keki na vitafunwa

  • Kwenye chai au kahawa

Lakini si mazuri sana kwenye mapishi yanayohitaji protini kama custard au maziwa ya kuganda.

10. Ni tofauti gani kati ya maziwa ya mchele na maziwa mengine ya mimea kama ya soya au mlozi?

Tofauti kuu ni:

Kipengele

Maziwa ya mchele

Maziwa ya soya

Maziwa ya mlozi

Protini

Kidogo sana

Nyingi

Kiasi kidogo

Mzio

Mara chache

Baadhi ya watu wana mzio

Watu wenye mzio wa karanga hawafai

Mafuta

Kiaci cha chini

Kati

Chini

Uwezo wa kupandisha kiwango cha sukari kwenye famu

Juu (sukari)

Kati

Chini

Muundo

Mwembamba

Mnene

Mwembamba

Kwa watoto, maziwa ya soya mara nyingi hupendekezwa zaidi kuliko mchele isipokuwa mtaalamu wa afya aseme vingine.


Imeandikwa;
16 Desemba 2021, 15:43:26
Bofya hapa kusoma zaidi kuhusu namna ya kuandaa vyakula mbalimbali vinavyoweza kukukinga dhidi ya magonjwa ya shinikizo la damu la juu na Kisukari, pia kuupa mwili wako uwezo wa kudhibiti magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu(presha).

 

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
 

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Rejea za mada hii

  1. Keller MD, et al. Severe malnutrition resulting from use of rice milk in food elimination diets for atopic dermatitis. Isr Med Assoc J. 2012 Jan;14(1):40-2. PMID: 22624441.

  2. Sethi, Swati et al. “Plant-based milk alternatives an emerging segment of functional beverages: a review.” Journal of food science and technology vol. 53,9 (2016): 3408-3423. doi:10.1007/s13197-016-2328-3

bottom of page