top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dr.Sospeter Mangwella, MD

ULY CLINIC

22 Julai 2025, 13:22:05

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Haja kubwa kwa mtoto mchanga

Kisa halisi

Mama ULY, akiwa mama kwa mara ya kwanza, alihangaika baada ya kuona mtoto wake wa wiki mbili akipata haja kubwa mara sita kwa siku, kiasi kidogo, na wakati mwingine ikiwa majimaji. Alijiuliza: “Je, hii ni kawaida au dalili ya ugonjwa?” Hali kama hii ni ya kawaida kwa wazazi wapya, lakini ni muhimu kuelewa mabadiliko ya kawaida na yasiyo ya kawaida ya haja kubwa kwa watoto wachanga chini ya mwezi mmoja.


Majibu

Watoto wachanga, hasa wale wanaonyonya maziwa ya mama pekee, huwa wanapata haja kubwa mara nyingi zaidi kuliko watu wazima. Kwa kawaida:

  • Hupata haja kubwa mara 3 hadi 8 kwa siku

  • Haja kubwa huwa laini au majimaji, rangi ya manjano, kahawia nyepesi, au kijani hafifu

  • Wakati mwingine huambatana na gesi au sauti ya tumbo

Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya kopo (formula) hupata haja kubwa mara chache zaidi (mara 1–4 kwa siku) na kinyesi huwa kigumu zaidi na rangi ya kahawia iliyokolea.


Mabadiliko ya kawaida katika wiki za kwanza

Katika siku 1–3 za mwanzo:

Mtoto hutoa mekonium – kinyesi cheusi kama lami, kisicho na harufu


Baada ya hapo:

Haja kubwa hubadilika na kuwa majimaji na ya njano, hasa kama mtoto ananyonyeshwa maziwa ya mama


Kufikia wiki ya 3–4:

Baadhi ya watoto hupata haja kubwa mara chache, hata mara moja kwa siku 1–2, bila kuonyesha dalili za kuumwa


Dalili zinazoashiria shida

Haja kubwa kwa mtoto chini ya mwezi mmoja inaweza kuwa ishara ya tatizo ikiwa:

  • Inatoka kama maji maji kupita kiasi (kuharisha)

  • Ina damu au ute mwingi

  • Mtoto ana homa, anakataa kunyonya, au anazidi kudhoofika

  • Kinyesi ni cheupe, kijivu, au kama mkojo wa rangi ya maji ya mchele

  • Mtoto anatapika mara kwa mara au kwa nguvu

  • Ana kuvimbiwa sana (tumbo kujaa hewa au kuwa gumu)


Visababishi vya haja kubwa isiyo ya kawaida kwa watoto wachanga

  1. Maambukizi ya tumbo (gastroenteraitis)

    • Mara nyingi husababishwa na virusi au bakteria kama E. coli au Salmonella

    • Dalili hujumuisha kuharisha, homa, na kutapika

  2. Mzio wa maziwa ya ng’ombe (protini kwenye maziwa ya ng'ombe)

    • Mtoto anaweza kupata damu au ute kwenye haja kubwa

    • Inahitaji kubadilisha aina ya maziwa (kwa wanaotumia formula)

  3. Kutohimili Lactose kwa muda mfupi

    Baada ya maambukizi ya tumbo, baadhi ya watoto hupata kuharisha muda mfupi kwa sababu ya upungufu wa enzyme ya lactase

  4. Matatizo ya kimaumbile (mfano: Ugonjwa wa Hirschsprung )

    Haja kubwa inaweza kuchelewa sana, kuwa ngumu au kutotoka kabisa


Uchunguzi na vipimo

Daktari anaweza kupendekeza:

  • Kupima kinyesi ili kutambua vimelea vya maradhi au uwepo wa damu/sumu

  • Vipimo vya damu kama mtoto ana dalili za homa au kushuka uzito

  • Ultrasound ya tumbo kwa mashaka ya matatizo ya kimaumbile


Matibabu

Matibabu hutegemea chanzo cha tatizo:

  • Kama ni kawaida: Hakuna tiba inahitajika, elimu kwa mzazi tu

  • Kama ni maambukizi: Mtoto hulazwa hospitalini kwa uangalizi na tiba maalum kama antibayotiki au uongezaji maji

  • Aina maalum ya maziwa: Kwa watoto wenye allergy ya maziwa ya ng’ombe, formula hubadilishwa


Tiba ya nyumbani na ushauri kwa wazazi

  • Hakikisha mtoto anaendelea kunyonya vizuri

  • Epuka kumpa dawa yoyote bila ushauri wa daktari

  • Angalia kwa makini idadi ya nepi zenye mkojo – angalau 6 kwa siku ni dalili nzuri

  • Weka kumbukumbu ya mabadiliko ya kinyesi – rangi, wingi, marudio


Lini umwone daktari haraka

  • Mtoto hapati haja kubwa kabisa kwa siku zaidi ya 2, hasa ikiwa anaonekana kutojisikia vizuri

  • Haja kubwa ina damu au ute mwingi

  • Mtoto ana homa, anakuwa mlegevu, hapumui vizuri, au hapati usingizi kabisa

  • Kinyesi ni cheupe, kijivu, au kama mkojo wa mchele


Hitimisho

Kwa watoto wachanga, haja kubwa ya mara kwa mara, yenye majimaji na rangi ya manjano ni hali ya kawaida, hasa kwa wanaonyonya maziwa ya mama. Hata hivyo, mabadiliko yasiyo ya kawaida yaweza kuwa ishara ya tatizo. Wazazi wanapaswa kuwa makini na dalili za hatari na kumpeleka mtoto hospitali haraka ikihitajika.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara

1: Je, ni kawaida kwa mtoto mchanga kupata haja kubwa mara kwa mara kwa kiasi kidogo kidogo?

Ndiyo, ni kawaida kabisa kwa mtoto mchanga kujisaidia haja kubwa mara kwa mara kwa kiasi kidogo, hasa katika wiki za mwanzo baada ya kuzaliwa. Hili ni jambo la kiafya linalosaidia kumaliza gesi tumboni na kupunguza maumivu ya tumbo (chango). Kadri mtoto anavyokua, mfumo wake wa chakula na utumbo huimarika, na hali hii hupungua taratibu.

2: Kinachonipa hofu ni pale ninapokuta mtoto amejisaidia majimaji tu yamechafua nepi sehemu ya haja kubwa, je, hii ni kawaida?

Ndiyo, mara nyingi majimaji haya yanayochafua sehemu ya haja kubwa huweza kuwa mkojo, hasa kama mtoto amevalishwa nepi au pampasi isiyofyonza maji vizuri. Watoto hulala kwa muda mrefu wakiwa chali, na mkojo huweza kupita kuelekea katikati ya mapaja na makalio. Hii ni hali ya kawaida kama hakuna harufu mbaya wala dalili za kuharisha.

3: Je, ni kawaida kichanga wa mwezi mmoja kwenda haja kubwa mara tisa kwa siku?

Ndiyo, ni jambo la kawaida kwa mtoto mchanga wa mwezi mmoja kujisaidia hadi mara 9 au zaidi kwa siku. Ilimradi kinyesi chake kiwe cha kawaida (kisicho na damu, harufu kali au ute mwingi) na mtoto awe na hali nzuri ya jumla — anaendelea kunyonya, analala vizuri, na hana homa — basi hakuna sababu ya kuwa na hofu.

 4: Habar Dr, mwanangu ana wiki 3 lakini hapat choo cha mara kwa mara, wala hajambi, tumbo lake kunguruma na anajikunja. Nimetumia beladona lakini bado hali inaendelea. Nifanyeje?

Dalili unazoeleza zinaweza kuashiria changamoto katika mfumo wa mmeng’enyo, hasa kama mtoto hajambo wala kupata haja kubwa. Ingawa ni kawaida kwa baadhi ya watoto kwenda haja kubwa kila baada ya siku kadhaa, hali ya kujikunja, tumbo kunguruma, na kutokujamba inaweza kuashiria gesi au matatizo ya choo. Beladona siyo dawa salama kwa watoto wachanga bila ushauri wa daktari. Tafadhali muone daktari haraka kwa uchunguzi zaidi.

5: Je, mtoto wa wiki mbili kutopata choo kwa siku mbili ni kawaida?

Ndiyo, kwa baadhi ya watoto, hasa wanaonyonya maziwa ya mama pekee, inaweza kuwa kawaida kutopata haja kubwa kwa siku 1 hadi 3. Maziwa ya mama hameg'anyika vizuri mwilini hivyo kinyesi hupungua. Ikiwa mtoto haonyeshi dalili za maumivu, anakula vizuri, na tumbo lake si ngumu sana, basi hali hiyo si ya kutia hofu. Lakini ikiwa hali itaendelea au mtoto awe na dalili za kukosa raha, tafuta ushauri wa kitaalamu.

6: Mtoto wangu wa mwezi mmoja hujisaidia baada ya kila kunyonya. Hii ni dalili ya kuharisha?

Hapana. Kwa watoto wachanga, kujisaidia haja kubwa baada ya kila kunyonya ni jambo la kawaida. Mfumo wao wa mmeng’enyo huamshwa haraka na chakula. Kinyesi cha mtoto wa maziwa ya mama huwa laini na cha rangi ya njano, hivyo siyo dalili ya kuharisha isipokuwa kikiwa na harufu kali sana, damu, au mabadiliko makubwa ghafla.

 7: Je, kutumia supozitori au njia za kumsaidia mtoto kupata haja kubwa ni salama?

Hapana, kutumia supozitori au njia za kuchokonoa sehemu ya haja kubwa mara kwa mara siyo salama kwa watoto wachanga, kwani huweza kuwategemeza njia hizo na kuwadhuru. Kama mtoto anaonekana kuwa na tatizo sugu la kupata choo, ni bora kupata ushauri wa daktari badala ya kutumia njia hizo bila mwongozo.

8. Kinyesi cha mtoto wangu ni kijani na chenye povu. Je, kuna tatizo?

Kinyesi cha kijani chenye povu mara nyingi huonekana kwa watoto wanaonyonya maziwa ya mama pale wanapopata maziwa ya mwanzo zaidi (foremilk) ambayo huwa na sukari nyingi na mafuta kidogo. Hali hii si ya hatari ikiwa mtoto anakua vizuri, lakini inapodumu au kuambatana na dalili nyingine kama kukataa kunyonya au kuvimba tumbo, ni vyema kumwona daktari.

9: Mtoto wangu anahema kwa nguvu na anajikunja wakati wa kujisaidia, ni kawaida?

Ndiyo, watoto wachanga mara nyingi huhema kwa nguvu, kulia, na kujikunja wanapojaribu kujisaidia. Hii hutokana na kutokuwa na uzoefu wa kutumia misuli ya nyonga na tumbo kwa uratibu. Hali hii ni ya kawaida na hupungua kadri mtoto anavyokua. Ikiwa hakuna damu, maumivu makali, au tumbo kuwa ngumu, siyo dalili ya tatizo.

10: Ni lini nitambue kwamba mtoto ana choo kigumu au ukosefu wa haja kubwa unaohitaji matibabu?

Ukiona mtoto ana kinyesi kigumu kama cha mbuzi, tumbo limevimba, analia kila anapojaribu kujisaidia, hapati choo zaidi ya siku 3 hadi 5 (hasa mtoto wa chini ya miezi 3), au ana damu kwenye kinyesi, basi hayo ni dalili za kuvimbiwa au tatizo lingine linalohitaji uchunguzi wa daktari haraka.


Soma zaidi kuhusu mfumo wa haja kubwa kwa watoto wachanga chini ya miezi mitatu kwa kubofya sehemu husika katika tovuti hii ya ULY Clinic.
Linki za kujisomea zaidi:
Rejea za mada hii:
  1. World Health Organization. Infant and young child feeding: Model Chapter for textbooks for medical students and allied health professionals [Internet]. Geneva: WHO; 2009 [cited 2025 Jun 17]. Available from: https://www.who.int/publications/i/item/9789241597494

  2. American Academy of Pediatrics. Caring for Your Baby and Young Child: Birth to Age 5. 7th ed. Shelov SP, Altmann TR, editors. New York: Bantam Books; 2020.

  3. National Health Service (NHS) UK. Your baby's poo [Internet]. NHS; 2023 [cited 2025 Jun 17]. Available from: https://www.nhs.uk/conditions/baby/health/poo-nappies/

  4. Walker WA, Goulet O, Kleinman RE, Sherman PM, Shneider BL, Sanderson IR. Pediatric gastrointestinal disease: Pathophysiology, diagnosis, management. 6th ed. Hamilton, Ontario: BC Decker; 2018.

  5. Mayo Clinic. Newborn poop: What to expect [Internet]. Rochester, MN: Mayo Foundation for Medical Education and Research; 2023 [cited 2025 Jun 17]. Available from: https://www.mayoclinic.org/healthy-lifestyle/infant-and-toddler-health/expert-answers/newborn-poop/faq-20058016


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page