Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Daktari wa ULY Clinic
Daktari wa ULY Clinic
28 Januari 2026, 09:40:40

Estriol
Estriol ni mojawapo ya homoni nne za estrogen ambazo ni estradiol, estrone, estriol, na estetrol. Estriol hujulikana pia kama Oestriol au E3. Kati ya homoni zote za estrogen, estriol ni homoni dhaifu zaidi, lakini ina umuhimu mkubwa sana hasa wakati wa ujauzito.
Estriol huzalishwa kwa kiwango kikubwa wakati wa ujauzito na hutumika kama kiashiria muhimu cha afya ya mama na mtoto aliyeko tumboni.
Estriol huzalishwa wapi?
Estriol huzalishwa kwa ushirikiano wa viungo vitatu muhimu:
Kondo la nyuma (plasenta)
Ini la mtoto
Figo za mtoto
Baada ya yai la kike kuchavushwa, ukuta maalum unaoitwa syncytiotrophoblast huanza kuundwa, na baadaye hutengeneza kondo la nyuma. Kondo la nyuma ndilo linalokamilisha uzalishaji wa homoni ya estriol.
Mabadiliko ya Estriol Wakati wa Ujauzito
Kiwango cha estriol kwenye damu ya mama huanza kuongezeka kuanzia wiki ya 8–9 ya ujauzito
Huendelea kuongezeka kadri ujauzito unavyokua
Hushuka kidogo mama anapokaribia kujifungua
Mabadiliko haya ni ya kawaida na husaidia madaktari kutathmini maendeleo ya ujauzito.
Kazi za Homoni ya Estriol
Estriol ina majukumu muhimu yafuatayo:
Huandaa mwili wa mama kwa ajili ya leba (uchungu wa kujifungua)
Huandaa matiti kwa ajili ya kunyonyesha
Huimarisha mfuko wa uzazi kwa ajili ya ukuaji salama wa mtoto
Huongeza ute ute ukeni na hivyo kuzuia uke kuwa mkavu
Hutumika kupima hali ya kiafya ya mtoto tumboni
Husaidia kutambua matatizo ya kimaumbile ya mtoto akiwa tumboni
Kuzidi kwa Homoni ya Estriol
Endapo kiwango cha estriol kitapanda zaidi ya kawaida, huweza kuashiria:
Mama anakaribia kuanza leba
Hatari ya kujifungua kabla ya wakati (mtoto njiti)
Hali hii huhitaji ufuatiliaji wa karibu wa kitaalamu.
Upungufu wa Homoni ya Estriol
Kiwango cha chini kisicho cha kawaida cha estriol kinaweza kuashiria:
Tatizo la kimaumbile ya mtoto, mfano Down syndrome
Matatizo katika kondo la nyuma (plasenta)
Hatari ya kuchelewa kujifungua, hali inayoweza kuhitaji njia za kuchochea leba
Matumizi ya Dawa za Estriol
Dawa za homoni mbadala ya estriol hutumika zaidi kwa:
Wanawake walioko kwenye kipindi cha komahedhi
Kupunguza dalili za komahedhi kama ukavu wa uke
Kuimarisha mifupa na kupunguza hatari ya mifupa kuvunjika kirahisi
Maudhi Madogo ya Dawa za Estriol
Baadhi ya madhara yanayoweza kujitokeza ni:
Tumbo kujaa gesi
Maumivu ya kichwa
Kichefuchefu
Vipele kwenye matiti
Kubana kwa misuli ya miguu
Kutokwa na damu ukeni
Matumizi ya dawa hizi yanapaswa kuwa chini ya ushauri wa mtaalamu wa afya.
Lishe na Estriol
Baadhi ya vyakula huweza kusaidia mwili katika usawa wa homoni, ikiwemo estriol:
Mboga za majani
Matunda
Mboga jamii ya kunde
Lishe bora husaidia afya ya jumla ya mama na homoni zake.
Hitimisho
Estriol ni homoni muhimu sana hasa wakati wa ujauzito. Ingawa ni dhaifu kuliko estrogen nyingine, ina mchango mkubwa katika maendeleo ya ujauzito, maandalizi ya leba, na tathmini ya afya ya mtoto tumboni. Kipimo chake hutumika kama nyenzo muhimu ya uchunguzi wa kitabibu.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliana na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii
Kwa ushauri zaidi na tiba unaweza kuwasialiana na daktari wa ULY CLINIC kupitia linki ya 'mawasialiano yetu' chini ya tovuti hii
Imeandikwa;
17 Aprili 2020, 06:41:18
Rejea za mada hii;
Konar H. DC Dutta’s Textbook of Obstetrics. 8th ed. New Delhi: Jaypee Brothers Medical Publishers; 2015. p. 61. ISBN: 9789351520672.
ScienceDirect. Estriol. Available from: ScienceDirect database. Accessed April 15, 2020.
Oatext. Estriol review: Clinical applications and potential biomedical importance. Available from: OAText database. Accessed April 15, 2020.
PubChem. Estriol. National Center for Biotechnology Information. Available from: PubChem database. Accessed April 15, 2020.
