top of page
kuchomo za kizazi ukeni-ulyclinic

Imeandikwa na daktari wa ULY CLINIC

​

Kuchomoza kwa kizazi ukeni

 

Kuchomoza kwa kizazi ukeni katika makala hii imemaanisha kuhisi au kuonekana shingo ya kizazi pamoja au bila mfuko wa uzazi maeneo ya uke (angalia kwa kubonyeza kwenye picha ya juu). Katika tiba hali hii huitwa yuterini prolapsi, hutokea pale misuli na ligament zinazoshikiria mfuko wa kizazi zinapokuwa zimelegea kiasi cha kushindwa kukishika vema katika sehemu yake ya asilia.

​

Kwa baadhi ya wanawake huwa hawaonyeshi dalili kabisa au kuwa na dalili kiasi au dalili kali za mfuko wa kizazi huweza kuchomoza chote na  kuonekana nje ya uke, wanawake walio katika hatua hii huweza kupata maambukizi kwenye kizazi.

​

Uchaguzi wa matibbu hutegemea hatua ya tatizo, hata hivyo watu wengi waliofikia umri ambao hawahitaji watoto, au wenye watoto wa kutosha hufanyiwa upasuaji wa kuondoa mfuko wa kizazi.

​

Ikitegemea hatua ya kuchomoza kwa uzazi, matibabu yanaweza kuwa mazoezi au kufanyiwa upasuaji wa kuimarisha mfuko wa uzazi ili usichomoze nje.

 

Dalili

​

Dalili za awali za tatizo hili huwa hazionekani kabisa, hata hivyo jinsi hatua zinavyoongezeka dalili huwa kati ya hizi zifuatazo;

​

  • Kuhisi nyonga imekuwa nzito au kuvuta

  • Kutokwa na damu au majimaji mengi ukeni

  • Kupata shida/maumivu wakati wa tendo la ndoa

  • Mkojo kutoka wenyewe, kuhisi mkojo umebaki kwenye kibofu wakati umemaliza kukojoa na kupata maambukizi ya UTI mara kwa mara

  • Kupata ugumu wakati wa kutoa haja kubwa- konstipesheni

  • Maumivu chini ya mgongo

  • Kuonekana kwa kizazi ukeni au kuhisi kitu kinachomoza kwenye uke

  • Kuhisi unashika kitu ndani ya uke wakati wa kujifafisha

  • Kuhisi umekalia mpira au kitu kinaanguka kupitia uke

  • Kulegea kwa misuli ya uke

​

Visababishi

​

  • Historia ya kuwa mjamzito  (waliokuwa na mimba nyingi zaidi wapo kwenye hatari zaidi)

  • Kupata shida wakati wa kujifungua ikiwa pamoja na kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa kupita kiasi au kujifungua kwa njia ya uke

  • Kunyanyua vitu vizito mara kwa mara

  • Kuzeeka, haswa kipindi baada ya komahedhi ambapo homoni za mwanamke zimeshuka sana kama estrogen

  • Kukenya sana wakati wa kutoa haja kubwa(kutumia nguvu nyingi kutoa haja kubwa)

  • Kukohoa kwa muda mrefu

  • Kufanyiwa upasuaji kwenye via vya nyonga

  • Tatizo la kurithi la udhaifu wa misuli

​

Je tatizo hutambuliwaje

​

Tatizo hili hutambuliwa kwa kuulizwa maswali na daktari wako, kisha baada ya hapo utafanyiwa vipimo vya kuangalia mwili. Daktari anaweza kushauri ufanye vipimo vingine kutokana na alichoona pamoja na hali yako ya kiafya. VIpimo vya  ultrasound na MRI hufanyika sana.

 

Namna ya kujitibu tatizo hili

​

Kama ilivyosemwa hapo awali, matibabu hutegemea hatua ya ugonjwa, baadhi ya mambo unaweza kufanya ili kupunguza ukali au kuendelea kwa ugonjwa ni;

​

  • Kufanya mazoezi ya kegeli ili kuimarisha misuli ya sakafu ya nyonga

  • Kutibu na kuzuia kupata haja ngumu(zuia kukenya wakati wa kujisaidia haja kubwa)

  • Acha kunyanyua vitu vizito

  • Tumia mapozi sahihi yanayoshauriwa wakati unanyanyua vitu(chuchumaa badala ya kukunja mgongo wakati wa kunyanyua kitu kizito) Bonyeza hapa kusoma zaidi

  • Tibu tatizo sugu la kukohoa

  • Kuw ana uzito w akiafya kwa kuzingatia mlo na mazoezi

  • Tumia dawa za kurejesha homoni endapo umeingia kipindi cha  komahedhi

​

Matibabu mengine ya hospitali yapo?

​

Ndio kuna matibabu mengine yapo kwa  wale wenye hatua za ugonjwa zilizo songa mbele zaidi, matibau hayo ni;

​

  • Utumiaji wa vishika kizazi vinavyowekwa kupitia uke ili kuzuia kizazi kisijitokeze nje ya uke

  • Upasuaji- huweza kufanyika kupitia uke au tumboni, hufanyika kwa kuweka tishu kutoka kwako au mtu mwingine ili kushika kizazi. Upasuaji wa kuondoa kizazi pia unaweza kufanyika na hufanyika kwa watu wengi haswa wale ambao hawahitaji kupata watoto wengine.

​

Aina ya mazoezi

 

Kusoma zaidi kuhusu mazoezi ,soma kwenye makala ya mazoezi ya kufanya wakati wa ujauzito katika tovuti hii. bonyeza hapa.

​

Mazoezi ya kuimarisha sakafu ya nyonga huwa muhimu sana, hufanyika endapo tatizo halijafikia hatua kali. Mazoezi haya huitwa kegeli, hufanyika pamoja na kuzingatia matibabu ya nyumbani ambayo yamezungumziwa hapo awali katika makala hii.

 

Namna gani ya kufanya mazoezi ya kegeli?

 

Bana misuli ya sakafu ya nyonga(soma zaidi kuhusu misuli ya nyonga kwa kubonyeza hapa) kama vile  katika kukojoa ghafla kisha shika hapo hapo kwa sekunde tano kisha achia, fanya hivi kabla ya kupumzika sekunde 5, unaweza kurudia zoezi hili mara 10 kwa siku.

​

Madhumuni ni kubana misuli inayozuia kukojoa kwa muda wa sekunde 10 kila wakati unapofanya mazoezi haya. Ongea na mtaalamu wako wa afya kukushauri zaidi kulingana na afya yako.

 

ULY clinic inakushauri siku zote ufuate ushauri wa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile inayodhuru afya yako.

​

Wasiliana na daktari wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba kwa kupiga simu au kubonyeza neno 'Pata Tiba' chini ya tovuti hii

​

Imeboreshwa mara ya mwisho, 08.08.2020

 

Rejea za mada hii;

​

  1. Uterine and vaginal prolapse. Merck Manuals: Professional Version. http://www.merckmanuals.com/professional/gynecology-and-obstetrics/pelvic-relaxation-syndromes/uterine-and-vaginal-prolapse. Imechukuliwa 08.08.2020

  2. Uterine prolapse. https://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/uterine-prolapse/symptoms-causes/syc-20353458. Imechukuliwa 08.08.2020

  3. Women's Health Stats and Facts. (n.d.). https://www.acog.org/-/media/NewsRoom/MediaKit.pdf. Imechukuliwa 08.08.2020

bottom of page