Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. Benjamin l, MD
Dkt. Salome A, MD
Jumanne, 31 Mei 2022

Gonorea
Gonorea ni moja ya ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria anayeitwa Neisseria gonorrhoeae. Kimelea huyu mara nyingi huathiri mrija wa mkojo wenye jina la urethra pamoja na shingo ya kizazi kwa wanawake.
Dalili mara nyingi huwa hazionekani na endapo zitaonekana kwa kawaida huwa pamoja na maumivu wakati wa kukojoa na kutokwa uchafu kwenye mrija wa mkojo.
Ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa jamii ya antibayotiki. Matibabu huhusisha pande mbili yaani wewe na mpenzi wako.
Kama mgonjwa akipata matibabu mapema, huzuia kupata madhara ya muda mrefu kama makovu kwenye njia ya mkojo na utasa.
Dalili za Gonorea
Mara nyingi Gonorea hakisababishi dalili yoyote ile na endapo zitaonekana huwa pamoja na:
Maumivu kama ya kuungua wakati wa kukojoa
Kutokwa na uchafu au usaha sehemu za siri
Maumivu wakati wa kumwaga manii
Kuvimba korodani
Kutokwa damu ukeni baada ya kujamiiana
Kutokwa na damu katikati ya vipindi vya hedhi
Maumivu chini y kitovu
Dalili zingine za Gonorea
Kama maambukizi yamesambaa sehemu nyingine ya mwili mbali na mfumo wa uzazi, dalili zinaweza kujumuisha:
Maumivu ya koo
Maumivu wakati wa kutoa haja kubwa
Kutokwa na uchafu kwenye haja kubwa
Maumivu ya jicho
Maumivu ya koo
Unaweza kusoma zaidi kuhusu dalili za Gonorea kwa wanaume na wanawake katika makala zingine ndani ya tovuti ya ULY CLINIC
Vihatarishi vya kupata Gonorea
Gonorea mara nyingi huambukizwa kwa njia ya kujamiiana na mtu mwenye maambukizi pasipo kutumia kinga, ngono inaweza kuwa ya uke kwa kinywa, uume kwa kinywa, uume kwa njia ya haja kubwa au uume kwa uke au uke kwa uke.
Watoto wachanga wanaweza kupata maambukizi kutoka kwa wazazi wao wakati wa kuzaliwa.
Tafiti zinaonyesha kuwa watu wenye umri kati ya miaka 15 na 35 wanapata maambukizi sana kutokana na kushiriki ngono
Vipimo
Mara nyingi vipimo huwa havihitajiki kugundua ugonjwa huu, na ugonjwa hutibiwa kwa kutumia dalili pamoja na uchunguzi wa mwili unaofanywa na daktari.
Kama vipimo vitahitajika huhusisha kipimo cha bacteria culture and sensitivity ambacho huangalia uwepo wa bakteria kwenye majimaji ya sehemu iliyoathirika
Matibabu ya Gonorea
Gonorea hutibiwa kwa dawa jamii ya antibayotiki. Matibabu huhusisha pia kutibu mpenzi au wapenzi unaoshiriki ngono ili kuzuia mwendelezo wa maambukizi. Endapo unaoshiriki nao ngono hawajapata tiba, unaweza kupata maambukizi mara moja baada ya kushiriki nao.
Kinga maambukizi ya Gonorea
Gonorea huepukwa mara nyingi kwa kutumia kondomu kwa kila tendo moja. Ni muhimu pia kupima kabla ya kushiriki ngono na endapo mmoja wenu ana maambukizi, mnapaswa kutibiwa wote ili kuvinja mwendelezo wa maambukizi.
Madhara ya Gonorea
Kama Gonorea isipotibiwa kwa wakati mara nyingi huweza kusababisha madhara yafuatayo;
Makovu kwenye mrija urethra na falopia
Kusinyaa kwa mrija wa urethra na falopia
Maumivu sugu ya mrija wa urethra au uume
Utasa
Maambukizi kwenye via vya uzazi (PID)