top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Jumanne, 6 Aprili 2021

Mafua ya kirusi Influenza

Mafua ya kirusi Influenza

Mafua ni tatizo linalofahamika sana duniani kote na hutokea mara kwa mara kwa binadamu. Makala hii imeangalia mafua yanayosababishwa na kirusi maarufu cha jina la kirusi cha influenza.


Je mafua ya kirusi cha influenza hufahamika kwa jina gani jingine?


Mafua ya kirusi cha influenza kwa jina jingine hufahamika kama homa ya mafua, hii ni kwa sababu kirusi huyu huleta mafua ambayo yanaambatana na homa.


Aina za virusi vya influenza


Virusi vya influenza vinavyosababisha sana mafua kwa binadamu ni kirusi aina


 • Influenza A

 • Influenza B


Kirusi huyu hukaa kwenye majimaji ya mfumo wa hewa kwa mgonjwa aliyeambukizwa na mara baada ya mambukizi huchukua takribani siku 1 hadi 4 kuanza kupata dalili za mafua na chafya.


Hata hivyo kuna aina ya tatu ya kirusi cha influenza ambaye husababisha mafua yasiyo makali sana, kirusi huyo ni Influenza C


Usambazaji wa kirusi cha mafua ya influenza


Mafua yanayosababishwa na kirusi huyu huwa yanaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya;


 • Matone ya maji wakati wa kupiga chafya, kukohoa

 • Kugusa maeneo ambayo yameguswa na mgonjwa wa mafua

 • Kutumia vifaa na vyombo pamoja na mtu mwenye mafua

 • Kukaa karibu na mtu mwenye mafua


Hata hivyo ni vema kufahamu kuwa mtu anaweza kusambaza kirusi huyu siku 5 hadi 10 kabla ya kuanza kuonyesha dalili, kwa watoto na watu wenye kinga za mwili za chini kirusi huweza kusambazwa kwa watu wengine takribani siku 10 hadi miezi kadhaa baada ya kupata dalili za mafua.


Mafua ya kirusi Influenza hutokea wakati gani katika mwaka?


Mafua ya virusi hutokea kipindi cha miezi yenye baridi, hii ni kwa sababu watu katika wakati huu huwa wanapenda kukaa karibu karibu kwa sababu ya baridi. Wakati huu kirusi cha influenza husambazwa kutoka kwa mtu mmoja na kwenda kwa mwingine


Dalili za mafua ya kirusi cha Influenza


Dalili huambatana na kuanza ghafla kwa


 • Homa

 • Maumivu ya kichwa

 • Maumivu ya misuli

 • Na uchovu wa mwili


Dalili zingine za mafua ya Kirusi cha Influenza


Dalili pia zinaweza kuambatana na dalili zingine za maambukizi mfumo wa hewa kama


 • Kikohozi kikavu

 • Koo kavu

 • Kutokwa na makamasi


Dalili za mafua ya kirusi cha Influenza hupotea baada ya muda gani?


Dalili za mafua ya virusi hupotea baada ya siku 2 hadi 5, hata hivyo ugonjwa unaweza kudumu kwa wiki moja au zaidi


Kinga na matibabu ya mafuaa ya kirusi cha Influenza


 • Ingawa ugonjwa huu huambukizwa, unaweza kujikinga kwa kupata chanjo ya kirusi cha influenza. Chanjo mara nyingi ni muhimu kwa watu ambao wapo kwenye hatari ya kupata madhara makubwa kutokana na maambukizi ya kirusi huyu.

 • Dawa za antivirus hutumika kupunguza makali ya dalili za kirusi huyu lakini huwa haziondoi ugonjwa kabisa. Matumizi ya dawa hushauriwa kutumika ndani ya masaa 48 toka dalili za maambukizi kuanza kuonekana

 • Matibabu ya mafua haya hufanya mtu ajihisi vema, hata hivyo tiba huwa haifupishi muda wa ugonjwa kukaa ndani ya mwili


Matibabu pia yasiyo dawa ya mafua ya kirusi cha Influenza


 • Kupumzika mpaka dalili kali zitakapoisha- kwa wale wenye dalili kali za mafua

 • Kunywa maji ya kutosha ili kujikinga na kuishiwa maji mwilini

 • Matumizi ya panado kupunguza homa na maumivu ya kichwa

 • Kujifukiza kwa mvuke wa maji ya moto yenye mchanganyiko wa majani au dawa asilia zinazosemekana kuzibua pua kama vile tangawizi n.k chukua tahadhar kuepuka kuungua mfumo wa hewa, wasiliana na daktari wako kabla ya kufanya hivi


Kumbuka


Dawa za kuzuia kukohoa huwa hazisaidii kwa sababu kikohozi huisha chenyewe pasipo matibabu

Madhara ya mafua ya kirusi cha Influenza.


Madhara mara nyingi huwa hayatokei, hata hivyo huweza kutokea kwa baadhi ya watu wenye kinga za mwili za chini kama vile


 • Nimoni ya virusi

 • Nimonia ya bakteria

 • Mayolisisi

 • Perikadaitis

 • Rabdomayolisisi

 • Sindromu ya toksik shoku


Wakati gani wa kwenda hospitali endapo una mafua ya kirusi cha Influenza?


Endapo mgonjwa anapata dalili zifuatazo hakikisha anafika hospitali kupata matibabu ya haraka


Kwa mtoto

 • Kuhema kwa haraka haraka au kupata shida ya kuhema

 • Kubadilika rangi na kuwa na rangi ya bluu

 • Kuishiwa maji

 • Homa pamoja na harara kwenye ngozi

 • Kushindwa kula vema


Kwa mtu mzima

 • Kupumua kwa shida, au kuishiwa pumzi

 • Maumivu au kuhisi mgandamizo wa kifua

 • Kizunguzungu cha ghafla

 • Kuchanganyikiwa

 • Kutapika sana au kutapika kunakoendelea

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

26 Oktoba 2021 21:05:22

Rejea za mada hii:

1. Viral vs allergic rhinitis.https://journals.co.za/content/journal/mp_sapj. Imechukuliwa 12.11.2020

2.Post nasal drip. https://www.webmd.com/allergies/postnasal-drip. Imechukuliwa 12.11.2020

3.Diagnosing Rhinitis: Viral and Allergic Characteristics.https://journals.lww.com/tnpj/Citation/2008/09000/Diagnosing_Rhinitis__Viral_and_Allergic.5.aspx#. Imechukuliwa 12.11.2020

bottom of page