Mwandishi:
Mhhariri
Imeboreshwa:
Dkt. Benjamin L, MD
Dkt. Salome A, MD
1 Novemba 2026, 17:14:22

Mpox (homa ya nyani)
Maelezo ya jumla
Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha mpox (monkeypox virus), cha familia moja na kirusi cha ndui iliyotokomezwa. Kina aina mbili kuu: clade I (Afrika ya Kati – mara nyingi kali zaidi, ikiwemo clade Ib iliyosambaa tangu 2023) na clade II (Afrika Magharibi – iliyosababisha mlipuko wa dunia mwaka 2022).
WHO ilitangaza mpox kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa mwaka 2022 na tena mwaka 2024 kutokana na kusambaa kwa clade Ib Afrika ya Kati na Mashariki. Tanzania imeripoti wagonjwa na imeweka tahadhari na ufuatiliaji.
Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yeyote. Unyanyapaa huwafanya watu kuficha dalili – jambo linalochochea kuenea.
Takwimu za ugonjwa
Tangu 2022, zaidi ya wagonjwa 100,000 wamethibitishwa katika zaidi ya nchi 120. Mwaka 2024–2025, Afrika iliripoti makumi ya maelfu ya wagonjwa, wengi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi jirani za Afrika Mashariki.
Vifo hutofautiana kwa clade na huduma: chini ya asilimia 1 kwa clade II, na zaidi kwa clade I, hasa kwa watoto, wenye VVU wasiotibiwa na wenye utapiamlo.
Visababishi na vihatarishi
Njia za maambukizi
Mguso wa moja kwa moja na vipele, vidonda, maganda au majimaji ya mwili ya mgonjwa – ikiwemo ngono.
Matone ya hewa wakati wa mazungumzo ya karibu kwa muda mrefu.
Vitu vilivyochafuliwa – mashuka, taulo, nguo.
Mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au kujifungua.
Wanyama – panya, kuke na nyani; kung'atwa, kukwaruzwa, kuwinda au kula nyama pori isiyopikwa vizuri.
Wanaoweza kuugua sana
Watoto wadogo.
Wajawazito.
Wenye VVU wasiotumia ARV na kinga dhaifu.
Wenye ukurutu na magonjwa ya ngozi.
Jinsi ugonjwa unavyotokea
Kirusi huingia kupitia michubuko ya ngozi, utando wa mdomo, macho, sehemu za siri au njia ya hewa, huzaliana kwenye tezi za limfu na kusambaa kwenye damu. Kipindi cha kupevuka ni siku 3–21 (mara nyingi 6–13).
Mgonjwa huambukiza kuanzia dalili zinapoanza mpaka maganda yote yamedondoka na ngozi mpya imeota.
Dalili na viashiria
Awamu ya kwanza (siku 0–5)
Homa, maumivu ya kichwa, misuli na mgongo.
Uchovu mkubwa.
Tezi kuvimba – shingo, kwapa, kinena (hutofautisha na tetekuwanga).
Vipele (siku 1–3 baada ya homa)
Huanza usoni, mikononi, miguuni (ikiwemo viganja na nyayo), mdomoni na sehemu za siri.
Hupita hatua: madoa → vipele vigumu → malengelenge ya maji → vidonda vya usaha vyenye kibonyeo katikati → maganda.
Vipele vinaweza kuwa vichache au maelfu; vinaweza kuuma sana.
Vidonda sehemu za siri na njia ya haja kubwa – maumivu wakati wa kujisaidia.
Vidonda machoni – maumivu na kuona ukungu.
Vipimo
PCR ya majimaji au ganda la kipele – kipimo cha uhakika; sampuli hupelekwa maabara ya taifa.
Kipimo cha VVU na magonjwa mengine ya zinaa.
Kutofautisha na tetekuwanga, kaswende, malengelenge ya herpes, upele na mzio wa dawa.
Mgonjwa anayeshukiwa huripotiwa mara moja kwa mamlaka za afya.
Matibabu
Kwa mujibu wa STG 2026:
Huduma saidizi: maji ya kutosha, lishe bora, paracetamol kwa homa na maumivu.
Utunzaji wa vipele: safisha kwa maji safi, usiyakune wala kuyatoboa, funika; maji ya chumvi au dawa za kupunguza mwasho.
Antibiotiki – kama vipele vimepata maambukizi ya bakteria.
Utunzaji wa macho na mdomo – suuza kwa maji ya chumvi.
Dawa za kuua virusi (mf. tecovirimat) – kwa wagonjwa mahututi au makundi hatarishi, pale zinapopatikana kupitia mpango maalum.
Kujitenga – kukaa peke yako, kufunika vipele, kuvaa barakoa mpaka maganda yote yadondoke.
ARV kwa wenye VVU.
Kulazwa kwa wenye ugonjwa mkali.
Matatizo yanayoweza kutokea
Maambukizi ya bakteria kwenye vipele.
Nimonia.
Upungufu wa maji kwa kushindwa kula au kunywa.
Vidonda machoni na upofu.
Uvimbe wa ubongo – nadra.
Makovu.
Kwa wajawazito: mimba kuharibika au mtoto kuzaliwa na maambukizi.
Kifo – hasa watoto, wenye VVU wasiotibiwa, clade I.
Kinga
Epuka mguso wa karibu, ikiwemo ngono, na mtu mwenye vipele vya mpox.
Nawa mikono kwa sabuni mara kwa mara.
Usishiriki mashuka, taulo wala nguo za mgonjwa.
Vaa barakoa na glovu unapomhudumia mgonjwa.
Epuka kushika au kula wanyama pori wagonjwa au waliokufa; pika nyama vizuri.
Chanjo ya mpox – hutolewa kwa makundi hatarishi kama inavyoelekezwa na Wizara ya Afya.
Tumia kondomu – hupunguza lakini haiondoi hatari.
Lini umwone daktari
Vipele vipya vya malengelenge au vidonda pamoja na homa na tezi kuvimba.
Umekuwa karibu na mgonjwa wa mpox – fuatilia dalili kwa siku 21.
Haraka: vidonda machoni, kushindwa kula au kunywa, kupumua kwa shida, kuchanganyikiwa, au vipele vingi sana.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Mpox na tetekuwanga zinatofautianaje?
Mpox huleta tezi kuvimba, vipele vilivyo katika hatua moja kwa wakati mmoja na mara nyingi kwenye viganja na nyayo. Tetekuwanga huwa na vipele vya hatua tofauti kwa wakati mmoja. Kipimo huthibitisha.
2. Mpox ni ugonjwa wa zinaa?
Si ugonjwa wa zinaa pekee, lakini huambukizwa kwa urahisi kwa mguso wa karibu wakati wa ngono.
3. Mpox inaua?
Wengi hupona ndani ya wiki 2–4. Hatari ya kifo ni kubwa zaidi kwa watoto, wenye VVU wasiotibiwa na kwa clade I.
4. Nijitenge kwa muda gani?
Mpaka maganda yote yadondoke na ngozi mpya iote – mara nyingi wiki 2–4.
5. Kuna chanjo?
Ipo, hutolewa kwa makundi hatarishi na wakati wa milipuko kama inavyoelekezwa na Wizara ya Afya.
6. Mpox inatoka kwa nyani tu?
Hapana. Jina lilitokana na kugunduliwa kwa nyani wa maabara, lakini chanzo kikuu cha wanyama ni panya na kuke. Sasa huambukizwa zaidi kati ya binadamu.
7. Je, wenye VVU wako hatarini?
Wenye VVU wasiotumia ARV au wenye CD4 chini huugua sana. ARV hupunguza hatari.
8. Ninaweza kunyonyesha nikiwa na mpox?
Kunaweza kumwambukiza mtoto kwa mguso wa karibu. Mama apate ushauri wa mtaalamu kuhusu namna salama.
9. Vipele vinaacha makovu?
Vinaweza, hasa vikikunwa au kupata maambukizi. Usivikune.
10. Nifanye nini kama nimekaa karibu na mgonjwa?
Fuatilia dalili kwa siku 21, epuka mguso wa karibu na wengine, na nenda kituoni ukipata homa au vipele.
Imeandikwa:
29 Oktoba 2026, 18:08:41
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba, au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii
Rejea za mada hii:
Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026. Section: Mpox (monkeypox).
World Health Organization. Clinical management and infection prevention and control for mpox: living guideline. Geneva: WHO; 2025.
World Health Organization. Mpox fact sheet. Geneva: WHO; 2025.

