Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin L, Dkt Salome A, MD
Imeboreshwa:
4 Februari 2026, 06:29:11

Ugonjwa wa Rubella kwa Watoto: Dalili, Vipimo na Matibabu
Rubella ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na kirusi cha Rubella na huwapata zaidi watoto wasio na chanjo. Ingawa kwa watoto wengi ugonjwa huu huwa na dalili zisizo kali na hupona wenyewe, rubella ni hatari sana kwa mama mjamzito kwani huweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto aliye tumboni. Makala hii inalenga kutoa elimu kwa wazazi kuhusu rubella kwa watoto, dalili zake, madhara na umuhimu wa chanjo, na haitumiki kama mbadala wa uchunguzi wa daktari.
Rubella ni ugonjwa gani?
Rubella (pia hujulikana kama German measles) ni ugonjwa wa virusi unaoambukizwa kupitia hewa, hasa kwa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza karibu na mtu aliyeambukizwa. Ugonjwa huu hutokea sana katika maeneo yenye kiwango kidogo cha chanjo.
Kirusi cha Rubella huenea vipi mwilini?
Baada ya kirusi kuingia mwilini:
Huvamia koo na njia za hewa
Huzaliana kwenye mitoki ya limfu
Huingia kwenye damu (viremia)
Husambaa hadi kwenye ngozi, macho, maji ya mfumo wa fahamu na viungo vingine
Kwa mama mjamzito, kirusi huweza kupenya kupitia kondo la nyuma (plasenta) na kumwambukiza mtoto aliyeko tumboni.
Historia na hali ya Rubella duniani
Kabla ya chanjo kugunduliwa mwaka 1969, rubella ilikuwa ikisababisha milipuko mikubwa kila baada ya miaka 6–9 katika nchi nyingi. Nchini Marekani, maelfu ya watoto waliathirika kati ya miaka ya 1977–1981, lakini baada ya kuanzishwa kwa chanjo, idadi ya wagonjwa ilishuka kwa kiasi kikubwa. Katika nchi nyingi za Afrika, takwimu kamili hazipatikani kutokana na changamoto za mifumo ya taarifa za afya.
Rubella kwa mtoto aliyezaliwa na aliye tumboni
Mtoto aliyezaliwa: Mara nyingi hupata ugonjwa usio mkali, usioleta madhara ya kudumu.
Mtoto aliye tumboni (Rubela ya kuzaliwa): Hupata madhara makubwa hasa mama akiambukizwa katika miezi 2–3 ya mwanzoni mwa ujauzito(kipindi cha kwanza cha ujauzito).
Dalili za Rubella kwa Watoto
Dalili huanza baada ya siku 14–23 tangu kuambukizwa, na ni pamoja na:
Homa ya wastani
Uchovu wa mwili
Kukosa hamu ya kula
Maumivu ya kichwa
Macho kuwa mekundu au kuuma (Homa ya konjaktiva)
Mafua mepesi
Vipele vya Rubella
Huonekana siku 1–5 baada ya dalili za awali
Huanzia usoni na kusambaa kuelekea mwilini na miguu
Huwa na rangi ya pinki au nyekundu hafifu kwa watoto wenye rangi nyeupe au zambarau kwa watoto wenye rangi nyeusi
Hutoweka ndani ya siku 3 bila makovu
Dalili nyingine muhimu
Kuvimba kwa mitoki ya shingo, nyuma ya masikio na kichwani
Maumivu ya viungo (hasa kwa watoto wakubwa)
Madhara ya Rubella
Kwa watoto waliozaliwa
Ugonjwa hupona wenyewe
Madhara makubwa ni nadra sana
Kwa mtoto aliye tumboni (CRS)
Matatizo ya kuzaliwa ya moyo
Uharibifu wa macho (Mtoto wa jicho(katarakti), upofu)
Uharibifu wa mfumo wa fahamu
Ulemavu wa kusikia
Upungufu wa chembe za kugandisha damu (thrombosaitopenia)
Kuchelewa kukua na matatizo ya kinga mwilini
Hatari ni kubwa zaidi mama akiambukizwa:
Ndani ya miezi 2 ya mwanzo ya ujauzito
Hatari bado ipo hadi miezi 5 ya ujauzito
Uchunguzi wa Rubella
Uchunguzi hufanywa hospitalini na hujumuisha:
Historia ya dalili na chanjo
Kipimo cha damu (Rubella IgM na IgG)
Uchunguzi wa mama mjamzito endapo kuna hatari
Matibabu ya hospitali ya Rubella
Hakuna dawa maalum ya kuua kirusi cha rubella. Matibabu hulenga:
Kupunguza dalili (homa, maumivu)
Kupumzika
Kunywa maji ya kutosha
Antibiotiki hazitumiki isipokuwa kama kuna maambukizi ya bakteria yaliyojitokeza pembeni.
Matibabu ya Nyumbani kwa Mtoto Mwenye Rubella
Rubella kwa watoto waliozaliwa mara nyingi ni ugonjwa mpole unaojiponya wenyewe, hivyo matibabu hulenga zaidi kupunguza dalili na kumfanya mtoto awe katika hali ya utulivu wakati mwili wake unapopambana na kirusi. Matibabu ya nyumbani yafanyike chini ya ushauri wa daktari na hayabadilishi umuhimu wa uchunguzi wa kitabibu.
1. Kudhibiti homa na maumivu
Ikiwa mtoto ana homa au anaonekana kuwa na maumivu:
Mpe paracetamol kwa kipimo sahihi kulingana na umri na uzito wa mtoto
Epuka kabisa kumpa aspirin, kwani inaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto
Hakikisha mtoto hapati baridi kali wala joto kupita kiasi
Muhimu:
Ikiwa homa ni kali, inaendelea zaidi ya siku 3, au mtoto ana degedege, mpeleke hospitali haraka.
2. Kumpumzisha mtoto vya kutosha
Mtoto anapaswa kupumzika nyumbani hadi dalili zipungue
Epuka kumpeleka shule au sehemu zenye watu wengi ili kuzuia maambukizi kwa watoto wengine, hasa wajawazito
Mazingira yawe tulivu, yenye hewa safi na bila vumbi au moshi
3. Kumpa maji na lishe ya kutosha
Mpe mtoto maji mara kwa mara ili kuzuia upungufu wa maji mwilini
Kwa watoto wachanga, maziwa ya mama yaendelee kutolewa mara kwa mara
Watoto wakubwa wape vyakula laini na vyepesi kama uji, supu na matunda
Usimlazimishe mtoto kula sana kama hana hamu; muhimu ni kunywa maji
4. Kutunza vipele na ngozi
Vipele vya rubella havihitaji kupakwa dawa maalum
Osha mtoto kwa maji ya kawaida (si ya moto sana)
Kama mtoto anajikuna:
Hakikisha kucha zimekatwa
Mvalishe nguo laini zisizobana
Epuka kupaka krimu au dawa za kienyeji bila ushauri wa daktari
5. Kupunguza mafua na usumbufu wa pua
Safisha pua kwa matone ya maji ya chumvi (saline- maji chumvi maalum) endapo mtoto ana mafua mengi
Kwa watoto wadogo, unaweza kutumia kifyonza mafua kwa uangalifu ili kupunguza kamasi
Epuka dawa za mafua za watu wazima au mchanganyiko wa dawa bila maelekezo ya daktari
6. Kumlinda mtoto na wengine dhidi ya maambukizi
Mtoto akae nyumbani angalau siku 7 baada ya vipele kuonekana
Epuka kabisa mawasiliano na:
Wanawake wajawazito
Watoto wachanga
Nawa mikono mara kwa mara baada ya kumhudumia mtoto
7. Mfuatilie mtoto kwa karibu
Wazazi wanapaswa kumuangalia mtoto kila siku na kumpeleka hospitali mara moja endapo ataonyesha:
Kupumua kwa shida
Homa kali isiyopungua
Kutokwa damu isiyo ya kawaida
Kulegea sana au kushindwa kula/kunywa
Dalili zozote zisizo za kawaida
Onyo muhimu kwa wazazi
Usimpe mtoto dawa yoyote (hasa antibiotiki) bila ushauri wa daktari.
Matibabu ya nyumbani ni ya kusaidia tu, si tiba kamili ya rubella.
Uchunguzi wa daktari kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ni muhimu ili kuthibitisha ugonjwa na kuondoa magonjwa mengine hatari yanayofanana na rubella.
Kinga ya Rubella
Chanjo ya MMR (Measles, Mumps, Rubella)
Chanjo hutolewa utotoni kulingana na ratiba ya taifa
Wanawake wanashauriwa kupima kinga kabla ya mimba
Hitimisho
Rubella ni ugonjwa unaoweza kuzuilika kwa chanjo. Kwa watoto waliozaliwa ugonjwa huwa na dalili za wastani, lakini kwa mama mjamzito ni hatari sana kiasi cha kusababisha madhaifu ya kuzaliwa nayo. Elimu, chanjo na uchunguzi wa mapema ni nguzo muhimu za kuzuia madhara yake.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Je, rubella ni sawa na surua?
Hapana. Ingawa magonjwa yote mawili husababisha vipele na homa, rubella na surua ni magonjwa tofauti kabisa yanayosababishwa na virusi tofauti. Surua huwa na dalili kali zaidi kama homa kali, kikohozi kikali na hatari kubwa ya vifo kwa watoto, ilhali rubella mara nyingi huwa mpole kwa mtoto aliyezaliwa lakini ni hatari sana kwa mama mjamzito kwa sababu ya madhara kwa mtoto aliye tumboni.
2. Mtoto anaweza kuambukiza rubella kwa muda gani?
Mtoto aliye na rubella huweza kuambukiza wengine kuanzia takribani siku 7 kabla ya vipele kuonekana hadi siku 7 baada ya vipele kuanza. Hii ina maana kuwa mtoto anaweza kueneza ugonjwa hata kabla mzazi hajagundua kuwa ana rubella, jambo linaloifanya kuwa rahisi kuenea kwenye shule na jamii.
3. Je, mtoto aliyechanjwa anaweza kupata rubella?
Ni nadra sana. Chanjo ya rubella hutoa kinga ya muda mrefu na yenye ufanisi wa zaidi ya asilimia 95. Hata kama mtoto aliyechanjwa ataambukizwa kwa nadra sana, dalili huwa nyepesi mno na hatari ya kueneza ugonjwa huwa ndogo sana ukilinganisha na mtoto asiyechanjwa.
4. Rubella inaweza kurudi mara ya pili?
Kwa kawaida hapana. Mara tu mtu anapopata rubella au kuchanjwa, mwili hutengeneza kinga ya kudumu dhidi ya kirusi hicho. Ndiyo maana visa vya rubella kwa mtu mmoja mara mbili ni nadra sana na hutokea zaidi kwa watu wenye matatizo makubwa ya kinga ya mwili.
5. Rubella huathiri watoto wachanga zaidi?
Kwa watoto wachanga waliozaliwa, rubella mara nyingi husababisha dalili chache au zisizo kali. Hata hivyo, hatari kubwa zaidi ipo kwa mtoto aliye tumboni, kwani maambukizi yanaweza kuathiri ukuaji wa viungo muhimu kama moyo, macho, masikio na ubongo kabla ya kuzaliwa.
6. Je, rubella huua?
Kwa watoto waliozaliwa na wana afya njema, rubella mara chache sana husababisha kifo. Hatari kubwa ya vifo na ulemavu ipo kwa watoto walioambukizwa wakiwa tumboni (Rubella ya kuzaliwa), hasa endapo mama aliambukizwa katika miezi ya mwanzo ya ujauzito.
7. Je, mtoto mwenye rubella anahitaji kulazwa hospitalini?
Mara nyingi hapana. Watoto wengi wenye rubella hutibiwa nyumbani kwa uangalizi wa daktari, kwa kuwa ugonjwa hupona wenyewe. Kulazwa hospitalini kunahitajika tu endapo mtoto ana dalili kali, madhara, au matatizo mengine yanayohitaji uangalizi wa karibu.
8. Je, mama anaweza kunyonyesha mtoto mwenye rubella?
Ndiyo. Kwa kawaida kunyonyesha ni salama na kunapendekezwa, kwani maziwa ya mama husaidia kuongeza kinga ya mtoto. Hata hivyo, mama anapaswa kufuata ushauri wa daktari hasa kama mtoto ana matatizo mengine ya kiafya au kama mama ana dalili za maambukizi.
9. Rubella huenea kwa kugusa?
Maambukizi makuu ya rubella hutokea kupitia hewa (matone ya mate wakati wa kukohoa au kupiga chafya). Hata hivyo, kugusa majimaji ya pua au mate ya mtu aliyeambukizwa na kisha kugusa mdomo, pua au macho kunaweza pia kusababisha maambukizi, hasa kwa watoto wadogo.
10. Njia bora ya kuzuia rubella ni ipi?
Njia bora na yenye ufanisi mkubwa zaidi ni chanjo ya rubella, inayotolewa kwa watoto kulingana na ratiba ya chanjo ya taifa. Kwa wanawake, ni muhimu kuhakikisha wana kinga kabla ya kupata ujauzito, kwani chanjo huzuia kabisa hatari ya rubella kwa mtoto aliye tumboni.
Rejea za mada hii:
World Health Organization. Rubella vaccines: WHO position paper. Wkly Epidemiol Rec. 2011;86:301–316.
Centers for Disease Control and Prevention. Rubella (German measles). CDC; 2023.
Plotkin SA, Orenstein WA, Offit PA. Vaccines. 7th ed. Elsevier; 2018.
Cherry JD, Harrison GJ, Kaplan SL, et al. Feigin and Cherry’s Textbook of Pediatric Infectious Diseases. 8th ed. Elsevier; 2019.
American Academy of Pediatrics. Rubella. In: Red Book. 2021.
Reef SE, Plotkin S. Rubella vaccine. In: Plotkin’s Vaccines. Elsevier; 2018.
Cutts FT, Robertson SE. Control of rubella and congenital rubella syndrome (CRS) in developing countries. Bull World Health Organ. 1997;75(1):55–68.
