Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Benjamin M, MD
Imeboreshwa:
29 Januari 2026, 11:07:26

Damu nyingi kwenye hedhi: Sababu, Dalili, Vipimo na Matibabu
Hedhi (piriod) ni kutokwa na damu kutoka kwenye mfuko wa uzazi kama sehemu ya mzunguko wa kawaida wa uzazi wa mwanamke. Kwa wanawake wengi, hedhi huwa ya kawaida na hudhibitika, lakini kwa baadhi, hutokea ikiwa nyingi kupita kiasi, hali inayoweza kuathiri afya, kazi za kila siku na ubora wa maisha.
Kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi kitaalamu huitwa menoragia.
Mzunguko wa Hedhi kwa Ufupi
Kwa kawaida:
Mzunguko wa hedhi huchukua siku 21–35
Wastani wa wanawake wengi: siku 28
Hedhi hutokea mara 10–17 kwa mwaka
Mwanamke:
Mwenye mzunguko wa siku 21 → hadi vipindi 17 kwa mwaka
Mwenye mzunguko wa siku 35 → karibu vipindi 10 kwa mwaka
Mabadiliko Yasiyo ya Kawaida ya Mzunguko
Mizunguko mingi ya hedhi (hedhi nyingi au polimenorea): Hedhi chini ya siku 21 au zaidi ya vipindi 17 kwa mwaka.
Mizunguko michache ya hedhi (hedhi chache au oligomenorea): Hedhi chini ya vipindi 10 kwa mwaka au mzunguko zaidi ya siku 35.
Hedhi nyingi mara nyingi huambatana na kutokwa na damu nyingi.
Damu Nyingi ya Hedhi Ni Kiasi Gani?
Kwa kawaida:
Mwanamke hupoteza mililita 30–80 za damu kwa hedhi yote
Hii ni sawa na takribani pedi 3–6 zilizojaa kabisa damu
Huashiria damu nyingi isiyo ya kawaida endapo:
Pedi 1 hujaa kabisa ndani ya saa 1–2
Unabadilisha pedi 2 zilizojaa ndani ya masaa 2
Hedhi hudumu zaidi ya siku 7
Damu inaambatana na kizunguzungu, uchovu au kuzimia
Visababishi vya Kutokwa na Damu Nyingi Wakati wa Hedhi
1. Mabadiliko ya Homoni
Kutokuwepo kwa uwiano wa homoni (hormonal imbalance) kunaweza kusababishwa na:
Msongo wa mawazo
Mabadiliko ya usingizi
Lishe duni
Mabadiliko ya mfumo wa maisha
Hali hii inaweza kuambatana na kuongezeka uzito, mabadiliko ya hisia na hedhi isiyo ya kawaida.
2. Endometriosis
Ni hali ambapo chembe za ukuta wa ndani wa uzazi huota nje ya mfuko wa uzazi (kwenye ovari, mirija ya uzazi n.k).
Dalili zake ni:
Maumivu makali ya hedhi
Kutokwa na damu nyingi
Vipindi vingi vya hedhi kwa mwaka
3. Faibroidi za Mfuko wa Uzazi
Faibroidi ni uvimbe usio wa saratani unaoota kwenye kuta za uzazi.
Huonekana zaidi kwa wanawake > miaka 35, na husababisha:
Damu nyingi ya hedhi
Maumivu makali
Mizunguko isiyo ya kawaida
4. Kipindi cha kuelekea Koma Hedhi
Kwa wanawake wa miaka 45 na kuendelea, mabadiliko ya homoni yanaweza kusababisha:
Vipindi vingi au visivyo na mpangilio
Damu nyingi
Jasho la usiku na mabadiliko ya hisia
5. Magonjwa ya zinaa
Maambukizi kama:
Klamidia
Kisonono
Huambatana na:
Uchafu ukeni
Maumivu ya tumbo la chini
Kubadilika kwa hedhi
Visababishi vingine
Adenomaosis
Saratani ya mfuko wa uzazi
Haipaplazia ya ukuta wa uzazi (kunenepa kwa ukuta wa kizazi)
Matatizo ya damu kuganda
Madhara ya dawa fulani
Sababu zisizojulikana
Vipimo na Uchunguzi
Daktari anaweza kuagiza:
Ultrasound ya via vya uzazi
Vipimo vya homoni (FSH, LH, TSH)
CT scan au MRI
Kipimo cha kamera ya uzazi
Vipimo vya magonjwa ya zinaa
Vipimo vya damu kuganda
Matibabu
Hutegemea kisababishi, na yanaweza kuwa:
Dawa za kugandisha damu
Dawa za kurekebisha homoni
Dawa za uzazi wa mpango
Upasuaji (kwa baadhi ya wagonjwa)
Ushauri wa kitabibu
Nini cha kufanya ukiwa na damu nyingi ya Hedhi?
Tumia virutubisho vya kuongeza damu (kwa ushauri wa daktari)
Kula vyakula vyenye chuma, mboga za majani na matunda
Wasiliana na mtaalamu wa afya mapema
Wakati wa kumuona Daktari haraka
Unabadilisha pedi 2 zilizojaa ndani ya masaa 2
Unapata kizunguzungu au kuzimia
Unahisi mapigo ya moyo kwenda kasi
Damu inanuka au inaambatana na maumivu makali
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Aina za damu ya hedhi na maana zake ni zipi?
Damu ya hedhi inaweza kuwa nyekundu ang’avu, nyekundu iliyokolea au kahawia; mabadiliko haya mara nyingi ni ya kawaida kulingana na siku za hedhi.
2. Damu ya hedhi yenye vinyama (vipande) ina maana gani?
Damu ya hedhi yenye vinyama hutokea pale damu inapokaa muda mfupi kwenye mfuko wa uzazi; ni kawaida ikiwa si nyingi sana.
3. Kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi ni tatizo?
Kutokwa na damu nyingi ni tatizo endapo pedi hujaa haraka au hedhi hudumu zaidi ya siku 7.
4. Damu ya hedhi yenye utelezi inaashiria nini?
Damu yenye utelezi mara nyingi ni mchanganyiko wa damu na ute wa kizazi na huwa kawaida.
5. Kutokwa na damu kidogo kabla ya hedhi ni kawaida?
Kutokwa na damu kidogo kabla ya hedhi kunaweza kuwa kawaida, lakini kikizidi au kuambatana na maumivu, ni vema kumwona daktari.
6. Kutokwa na damu ya kahawia wakati wa hedhi maana yake nini?
Damu ya kahawia ni damu ya zamani inayotoka taratibu; mara nyingi hutokea mwanzoni au mwishoni mwa hedhi.
7. Damu ya hedhi kunuka ni kawaida?
Damu ya hedhi kunuka sana si kawaida na inaweza kuashiria maambukizi.
8. Sindano ya kuzuia damu ya hedhi hufanya kazi vipi?
Sindano ya kuzuia hedhi hubadilisha homoni na inaweza kupunguza au kusimamisha hedhi kwa muda.
9. Hedhi ya kawaida hudumu siku ngapi?
Hedhi ya kawaida hudumu siku 3–7.
10. Ni lini hedhi nyingi huwa hatari?
Hedhi huwa hatari endapo inasababisha upungufu wa damu, kizunguzungu, au kuhitaji kubadilisha pedi mara kwa mara sana.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
29 Januari 2026, 11:06:24
Rejea za mada hii
Hurskainen R, et al. Psychosocial and other characteristics of women complaining of menorrhagia. BJOG. 2001;108:281–288.
Greenberg M. The meaning of menorrhagia. J Psychosom Res. 1983;27:209–215.
Grant C, et al. Management of menorrhagia in primary care. J Epidemiol Community Health. 2000;54:709–713.
Warner PE, et al. Menorrhagia I: measured blood loss. Am J Obstet Gynecol. 2004;190:1216–1223.
Kadir RA, et al. Frequency of inherited bleeding disorders in women with menorrhagia. Lancet. 1998;351:485–489.
James AH, et al. Heavy menstrual bleeding: work-up and management. Int J Womens Health. 2018;10:287–295.
