Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Sospeter B, MD
21 Juni 2025, 15:08:38

Kutoshika mimba kwa muda mrefu: Visababishi na hatua za kuchukua ni zipi?
Swali na maelezo ya msingi
"Habari daktari. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28. Nimewahi kushika mimba mara mbili – ya kwanza ilitoka katika miezi ya sita hadi nane, na ya pili niliitoa kwa kutumia dawa za asili. Tangu hapo, nimekuwa nikijaribu kupata mimba bila mafanikio kwa muda mrefu. Tayari nimeshatumia dawa za kukomaza mayai niliyoandikiwa hospitalini, lakini bado sijafanikiwa. Mzunguko wangu wa hedhi huwa hauna mpangilio – unabadilika badilika. Pia, nimeshawahi kuugua magonjwa ya zinaa hapo nyuma. Mume wangu ana watoto, kwa hiyo sidhani kama ana matatizo ya uzazi. Naomba msaada: nifanye nini ili niweze kushika mimba?"
Majibu
Ugumba wa pili ni nini?
Ugumba wa pili ni hali ambapo mwanamke aliyeahi kupata ujauzito awali hushindwa kushika tena mimba baada ya miezi 12 au zaidi ya kujaribu (au miezi 6 kwa wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35). Ni hali ya kawaida inayowaathiri wanawake wengi walio na historia ya mimba zilizopita.
Visababishi vya kutopata mimba
Sababu zinazowezekana kwa kisa kama hiki ni
1. Uovuleshaji usio wa kawaida
Hali ambapo yai halitolewi kwa mpangilio sahihi kutoka kwenye ovari. Mzunguko wa hedhi unaobadilika-badilika ni ishara ya tatizo hili.
Visababishi vya uovuleshaji usio wa kawaida unaweza kuwa:
Sindromu ya vifukomaji vingi kwenye ovari (PCOS)
Msongo wa mawazo
Uzito kupita kiasi au upungufu wa uzito
Mabadiliko ya homoni (TSH, Prolactin)
Vipimo vya utambuzi:
FSH, LH, Prolactin, TSH, AMH
Ultrasound ya ovari
2. Mirija ya uzazi iliyojiziba
Magonjwa ya zinaa kama klamidia au PID yanaweza kusababisha mirija ya uzazi kupata makovu na kuziba. Hii huzuia yai kusafiri kwenda kurutubishwa.
Kipimo muhimu cha utambuzi
Hysterosalpingogram (HSG) – kuangalia kama hali ya mirija ya uzazi kama imeziba au la na kama ipo kawaida au la.
3. Mabadiliko kwenye mji wa mimba
Historia ya mimba kutoka au utoaji wa mimba unaweza kusababisha makovu ndani ya kizazi (Sindromu ya Asherman) au mabadiliko mengine yanayozuia ujauzito kutungwa.
Vipimo vya utambuzi
Ultrasound ya uke
Hysteroscopi
4. Manii za mwanaume kukosa ubora
Ingawa mume ana watoto, bado anaweza kuwa na matatizo kwa sasa. Umri, dawa, au mtindo wa maisha huweza kushusha ubora wa mbegu na hivyo ni lazima mwanaume pia kuchunguzwa afya yake.
Kipimo muhimu kufanyika ni kile cha kuangalia ubora wa mbegu zake.
Vipimo muhimu vya awali
Vipimo vifuatavyo ni muhimu kufanyika katika hatua za awali za kufahamu kisababishi;
Kipimo | Lengo |
HSG | Kuchunguza hali ya mirija ya uzazi |
FSH, LH, Prolactin | Kuchunguza homoni za uovuleshaji |
AMH | Kuangalia akiba ya mayai |
Ultrasound | Kuchunguza ovari na kizazi |
Uchunguzi wa mbegu za mwanaume | Kuchunguza ubora wa mbegu za mume |
Visababishi vingine vya ugumba
Si lazima kwa kisa hiki lakini ni muhimu kufahamu
1. Endometriosis
Tishu za kizazi kukua nje ya mji wa mimba, huleta maumivu na ugumba.
2. Tatizo la kinga ya mwili
Mwili kutengeneza kingamwili dhidi ya mbegu au yai.
3. Makovu kwenye kiazi
Kwa mfano, Asherman’s syndrome baada ya D&C au utoaji wa mimba usio salama.
4. Umri mkubwa wa uzazi
Mimba hupungua kwa kasi baada ya miaka 35.
5. Dawa au tiba za mionzi
Dawa za saratani, mionzi au baadhi ya dawa maalum huathiri uzazi.
6. Msongo wa mawazo
Stress huathiri homoni za ovulation na kupunguza nafasi ya kushika mimba.
7. Ugumba usioelezeka
Wote wawili wanaonekana kawaida lakini mimba haitungi – hali hii huwatokea hata asilimia 15 ya wanandoa.
Hatua unazoweza kuchukua
Onana na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake/mtaalamu wa uzazi
Fanya vipimo vya msingi haraka iwezekanavyo (wewe na mume wako)
Fuatilia ovulation nyumbani au kwa daktari
Dhibiti uzito na msongo wa mawazo
Epuka dawa za mitishamba bila ushauri wa kitabibu
Kunywa folic acid kila siku
Hitimisho
Kutopata mimba baada ya muda mrefu wa kujaribu siyo mwisho wa matumaini. Sababu nyingi zinaweza kutibika, hasa zikigundulika mapema. Muhimu zaidi ni:
Kufanya uchunguzi wa kitaalamu,
Kuepuka kubahatisha dawa au ushauri wa mitaani,
Kuelimika kuhusu mwili wako.
Matibabu yapo. Muda ndio silaha muhimu zaidi.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeboreshwa,
21 Juni 2025, 15:08:38
Rejea za mada hii
Practice Committee of the American Society for Reproductive Medicine. Diagnostic evaluation of the infertile female: a committee opinion. Fertil Steril. 2015;103(6):e44–e50.
World Health Organization. Sexually transmitted infections (STIs). WHO; 2023. Available from: https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/sexually-transmitted-infections-(stis)
Fritz MA, Speroff L. Clinical Gynecologic Endocrinology and Infertility. 8th ed. Philadelphia: Lippincott Williams & Wilkins; 2011.
American College of Obstetricians and Gynecologists. Evaluation and treatment of recurrent pregnancy loss. ACOG Practice Bulletin No. 200. Obstet Gynecol. 2018;132(1):e1–e17.
Zegers-Hochschild F, Adamson GD, Dyer S, et al. The International Glossary on Infertility and Fertility Care, 2017. Hum Reprod. 2017;32(9):1786–1801.
Johnson NP, Hummelshoj L. Consensus on current management of endometriosis. Hum Reprod. 2013;28(6):1552–68.
Check JH. Ovulation disorders and treatment options. Clin Exp Obstet Gynecol. 2013;40(4):482–5.
UpToDate. Evaluation of the infertile couple. [Internet]. 2024. Available from: https://www.uptodate.com
American Society for Reproductive Medicine. Testing and interpreting measures of ovarian reserve: a committee opinion. Fertil Steril. 2015;103(3):e9–e17.
The Practice Committee of the American Society for Reproductive Medicine. Unexplained infertility: a committee opinion. Fertil Steril. 2023;120(4):649–655.