top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

17 Machi 2025, 16:15:27

Ni yapi madhara ya Misoprostol?

Ni nini madhara ya kutumia misoprostol kwa mwanamke?


Misoprostol ni dawa inayotumika kutoa mimba, kutibu vidonda vya tumbo, na kuzuia au kutibu kutokwa na damu baada ya kujifungua. Kama ilivyo kwa dawa nyingine, Misoprostol inaweza kusababisha madhara mbalimbali yanayoweza kuwa ya kawaida au makali.


Katika makala hii neno madhara humaanisha maudhi ya dawa, na maudhi makali humaanisha madhara makubwa ya kutumia dawa na vile vile madhara ya kawaida humaanisha maudhi madogo ya dawa.


Maudhi ya kawaida

Maudhi ya kawaida hutokea kwa watu wengi na hupotea baada ya muda. Maudhi hayo ya kutumia misoprostol pamoja na yafuatayo;

  • Maumivu ya tumbo – Hili ni jambo la kawaida kwani dawa husababisha mji wa mimba kusinyaa (contractions).

  • Kutokwa na damu nyingi – Hasa wakati wa kutoa mimba, lakini inapaswa kupungua baada ya siku chache.

  • Kichefuchefu na kutapika – Hasa ndani ya masaa machache baada ya kutumia dawa.

  • Kuharisha – Misoprostol inaweza kusababisha kuhara kwa muda mfupi.

  • Maumivu ya kichwa na kizunguzungu – Haya hutokea mara kwa mara lakini hupotea yenyewe.


Maudhi Makali

Maudhi haya makali yanakuhitaji utafute msaada wa daktari haraka ambayo ni;

  • Kutokwa na damu nyingi kupita kiasi – Ikiwa unabadili pedi zaidi ya 2 kwa saa moja mfululizo kwa masaa kadhaa, unapaswa kupata msaada wa haraka.

  • Homa au baridi kali – Inaweza kuwa ishara ya maambukizi ikiwa joto linazidi 38°C (100.4°F) kwa zaidi ya saa 24.

  • Maumivu makali ya tumbo yasiyopungua – Ikiwa maumivu hayawezi kupunguzwa na dawa za maumivu kama Ibuprofen, unapaswa kuona daktari.

  • Harufu mbaya kutoka ukeni – Inaweza kuwa dalili ya maambukizi ya uterasi (endometritis).

  • Dalili za mzio mkali – Kama vile uvimbe wa uso, midomo, au ugumu wa kupumua.


Madhara ya nadra

  • Baadhi ya wanawake wanaweza kupata mzunguko wa hedhi usio wa kawaida kwa muda baada ya kutumia Misoprostol.

  • Kwa wachache, inaweza kusababisha mimba isitoke kabisa, na hivyo kuhitaji matibabu zaidi kama upasuaji wa kusafisha mji wa mimba.

  • Ikiwa itatumiwa katika ujauzito na haitosababisha mimba kutoka, inaweza kusababisha kasoro kwa mtoto aliyezaliwa.


Nini cha kufanya ikiwa unapata madhara ya misoprostol?


  • Madhara madogo kama kichefuchefu na kuhara yanaweza kudhibitiwa kwa kunywa maji mengi na kula vyakula laini.

  • Ili kupunguza hatari ya kuharisha, tumia Misoprostol pamoja na chakula na kabla ya kulala.

  • Misoprostol inaweza kusababisha matatizo ya hedhi, hivyo mjulishe mtoa huduma wa afya ikiwa unapata matone ya damu, maumivu makali ya hedhi, au hedhi nzito na yenye maumivu.


Hitimisho

Misoprostol husababisha maumivu ya tumbo, kutokwa na damu, kichefuchefu, na kuhara, lakini pia inaweza kusababisha madhara makali kama kutokwa na damu nyingi au maambukizi. Ikiwa unapata dalili za hatari kama kutokwa na damu nyingi, maumivu makali, au homa, tafuta matibabu ya haraka kwa kuwasilaina na daktari wako.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeboreshwa,

17 Machi 2025, 16:15:27

Rejea za mada hii

  1. NCBI. Misoprostol. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK539873/. Imechukuliwa 15.03.2025

  2. NCBI. Misoprostol. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK583257/. Imechukuliwa 15.03.2025

  3. NCBI. Misoprostol for Cervical Ripening and Induction of Labour: A Review of Clinical Effectiveness, Cost-Effectiveness and Guidelines. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK538944/. Imechukuliwa 15.03.2025

  4. ULY CLINIC. Misoprostol. https://www.ulyclinic.com/dawa/misoprostol-.  Imechukuliwa 15.03.2025

bottom of page