Mwandishi:
Dkt. Mangwella S, MD
Mhariri:
Dkt. Salome A, MD
Imeboreshwa:
4 Februari 2026, 03:33:12

Rubella: Dalili, Vipimo, Uchunguzi na Matibabu
Rubella, unaojulikana pia kama German measles (Surua ya Ujerumani), ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na kirusi cha Rubella. Ugonjwa huu huambukizwa kwa urahisi kupitia matone ya hewa yanayotoka kwa mtu aliyeambukizwa anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza.
Ingawa Rubella mara nyingi huwa ugonjwa mwepesi kwa watoto na watu wazima, ni hatari sana kwa wajawazito, hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito, kwani inaweza kusababisha Rubella ya kuzaliwa kwa mtoto.
Kirusi cha Rubella
Kirusi cha Rubella ni cha familia ya Matonaviridae
Hushambulia mfumo wa upumuaji kisha kuenea mwilini kupitia damu
Binadamu ndiye mwenyeji pekee wa kirusi hiki
Rubella huambukizwa vipi?
Rubella huambukizwa kwa:
Kuvuta hewa yenye matone ya mate au makamasi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa
Kugusogeleana au kugusana na mtu mwenye Rubella
Mama mjamzito kumwambukiza mtoto aliyeko tumboni
Mtu anaweza kuambukiza Rubella hata kabla dalili hazijaanza, jambo linaloongeza kasi ya maambukizi.
Dalili za Ugonjwa wa Rubella
Dalili za Rubella hutofautiana kulingana na umri na hali ya kinga ya mgonjwa. Kwa baadhi ya watu, dalili huwa nyepesi au hazionekani kabisa.
Dalili za awali za Rubella
Homa ya wastani (chini ya nyuzijoto 38.5°C)
Mafua na pua kutoa makamasi
Macho kuwa mekundu (Homa ya konjaktiva)
Koo kuuma
Uchovu na mwili kulegea
Maumivu ya kichwa
Dalili kuu za Rubella (upele)
Baada ya siku 1–5 za dalili za awali, upele huanza kuonekana:
Upele mwekundu unaoanzia usoni kwa watu weupe na watu wa asili ya afrika huweka kuwa wa rangi ya Hudhurungi, zambarau, Waridi iliyokolea au Kijivu cha majivu
Kusambaa hadi shingoni, kifuani, mgongoni, mikononi na miguuni
Upele hudumu kwa siku 3–5
Hauambatani sana na muwasho mkali
Dalili nyingine muhimu za Rubella
Kuvimba tezi za limfu (hasa nyuma ya masikio na shingoni)
Maumivu ya viungo (huonekana zaidi kwa wanawake watu wazima)
Maumivu ya misuli
Rubella kwa wajawazito (Hatari kubwa)
Rubella kwa mama mjamzito inaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtoto:
Hatari kwa mtoto aliyeko tumboni
Kuharibika kwa mimba
Mtoto kuzaliwa akiwa amekufa
Mtoto kuzaliwa na Kasoro za kuzaliwa (kasoro za kiuumbaji)
Rubella ya Kuzaliwa
Hii hutokea mtoto anapoambukizwa Rubella akiwa tumboni.
Dalili za Rubella ya kuzaliwa kwa mtoto
Upofu au matatizo ya macho
Uziwi
Kasoro za moyo
Kichwa kuwa kidogo (maikrosefali)
Ukuaji duni
Ulemavu wa akili
Ini na wengu kuvimba
Wakati gani wa kumwona daktari haraka?
Unapaswa kutafuta huduma ya afya mara moja ikiwa:
Unashuku Rubella ukiwa mjamzito
Umepata upele na homa
Umegusana na mtu mwenye Rubella
Mtoto ana dalili zifuatazo
Homa na upele unaosambaa haraka
Kuvimba tezi limfu za shingo au nyuma ya masikio
Dalili za machoni au masikioni
Upo kwenye makundi maalumu
Wajawazito
Watoto wachanga
Watu wenye kinga dhaifu (Virusi vya UKIMWI, saratani, n.k.)
Vipimo vya Ugonjwa wa Rubella
Historia ya mgonjwa na dalili
Upele wa ghafla
Homa nyepesi
Kusogeleana na mtu aliye na Rubella
Hali ya chanjo
Vipimo vya maabara (damu)
Rubella IgM – Huonyesha maambukizi ya karibuni
Rubella IgG – Huonyesha kinga ya awali au chanjo
PCR – Hutumika kuthibitisha kirusi (hasa kwa watoto wachanga)
Vigezo vya kuthibitisha Rubella
Rubella hutambuliwa iwapo:
Kipimo cha IgM ni chanya
Kuna dalili za kitabibu zinazoendana na Rubella
Historia ya kutopata chanjo ipo
Ushahidi wa maambukizi kwa mtoto aliyezaliwa (Rubella ya kuzaliwa)
Matibabu ya Rubella
Hakuna dawa maalum ya kuua kirusi cha Rubella. Matibabu hulenga kupunguza dalili:
Paracetamol kwa homa na maumivu
Kupumzika vya kutosha
Kunywa maji mengi
Kutenga mgonjwa ili kuzuia maambukizi
Aspirin haishauriwi kwa watoto kwa sababu ya hatari ya Sindromu ya Reye
Jinsi ya kujikinga na Rubella
Chanjo (kinga bora zaidi)
Chanjo ya MR au MMR (Measles, Mumps, Rubella)
Hutolewa utotoni na dozi ya nyongeza
Wanawake wanashauriwa kupima kinga kabla ya mimba
Njia nyingine za kujikinga
Epuka kugusana na wagonjwa
Funika mdomo unapokohoa au kupiga chafya
Kunawa mikono mara kwa mara
Ripoti visa vya Rubella kwa kituo cha afya
Maswali yanayoulizwa Mara kwa Mara na majibu yake
1. Rubella ni ugonjwa hatari?
Kwa watoto na watu wazima wengi, Rubella ni ugonjwa mwepesi unaopona wenyewe bila madhara makubwa.
Hata hivyo, kwa mwanamke mjamzito, Rubella ni hatari sana, hasa katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito(kipindi cha kwanza cha ujauzito), kwa sababu inaweza kusababisha kuharibika kwa mimba, mtoto kufia tumboni, au kasoro za kudumu za kuzaliwa(kasoro za kiuumbaji).
2. Rubella na surua ni ugonjwa mmoja?
Hapana. Rubella na Surua ni magonjwa mawili tofauti kabisa. Ingawa yote husababisha upele, Rubella husababishwa na kirusi cha Rubella, wakati Surua husababishwa na kirusi cha Measles. Surua huwa kali zaidi, huku Rubella ikiwa hatari zaidi kwa wajawazito.
3. Je, mtu anaweza kupata Rubella zaidi ya mara moja?
Kwa kawaida hapana.Mtu akishapata Rubella au akichanjwa, mwili hutengeneza kinga ya kudumu ya maisha(antibodi), hivyo uwezekano wa kupata Rubella tena ni mdogo sana.
Rubella huambukiza kwa muda gani?
Mtu aliye na Rubella huambukiza wengine:
Kuanzia siku 7 kabla ya upele kuonekana
Hadi siku 7 baada ya upele kuisha
Hii maana yake ni kwamba mtu anaweza kuambukiza hata kabla hajajua ana Rubella.
Mwanamke mjamzito akipata Rubella afanye nini?
Mwanamke mjamzito akihisi au kuthibitika kuwa na Rubella anapaswa:
Kumwona daktari haraka sana
Kufanyiwa vipimo vya damu (Rubella IgM na IgG)
Kupata ushauri wa kitaalamu wa uzazi ili kutathmini hatari kwa mtoto aliyeko tumboni
Hatua za mapema husaidia kufanya maamuzi sahihi ya kitabibu.
Chanjo ya Rubella ni salama?
Ndiyo. Chanjo ya Rubella (MR au MMR)Â ni salama, imefanyiwa tafiti nyingi, na ina ufanisi mkubwa sana. Chanjo hii imepunguza kwa kiasi kikubwa visa vya Rubella na Rubella ya kuzaliwa (CRS)Â duniani, na ni njia bora zaidi ya kujikinga.
Mtoto aliyezaliwa na ulemavu kutokana na rubella anaweza kupona?
Kwa bahati mbaya, madhara mengi ya kuzaliwa nayo ni ya kudumu, kama uziwi, upofu au matatizo ya moyo. Hata hivyo, utambuzi wa mapema na ufuatiliaji wa kitabibu husaidia mtoto kupata huduma maalum, kuboresha ukuaji, na kuongeza ubora wa maisha.
Rubella ipo Tanzania?
Ndiyo. Rubella bado ipo Tanzania, lakini visa vimepungua sana kutokana na mpango wa chanjo ya taifa.Hata hivyo, Rubella bado hutokea zaidi kwa watu wasiopata chanjo, ndiyo maana chanjo na ufuatiliaji wa afya ya jamii ni muhimu sana.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
4 Februari 2026, 03:33:12
Rejea za mada hii
World Health Organization. Rubella vaccines: WHO position paper. Wkly Epidemiol Rec. 2020.
CDC. Rubella (German Measles). Centers for Disease Control and Prevention.
Plotkin SA, et al. Vaccines. 7th ed. Elsevier; 2018.
Reef SE, et al. Global burden of congenital rubella syndrome. Bull World Health Organ. 2009.
Best JM. Rubella. Semin Fetal Neonatal Med. 2007.
