top of page

Mwandishi:

Dkt. Benjamin L, MD,

Mhariri:

Dkt. James NL, MD

Imeboreshwa:

27 Septemba 2026, 13:42:56

Mimi ni mwanamke nina changamoto sijajua tatizo nini nikiwa nakojoa haja ndogo sehemu ya haja kubwa hua Kuna majimaji yanatoka au wakati mwingine nikiwa nimetulia tu kuna muda unasikia kama majimaji hivi shida itakua nini?

Majimaji yanayotoka kwenye njia ya haja kubwa (anus) wakati wa kukojoa au hata bila kujisaidia si dalili ya kawaida ikiwa yanajirudia. Chanzo kinaweza kuwa tofauti, na rangi, harufu na kama kuna maumivu husaidia kutofautisha.


Sababu zinazowezekana ni:


  • Ute wa puru: Puru inaweza kutoa ute kidogo, lakini ikiwa unatoka mara kwa mara au kwa kiasi kikubwa, unahitaji kuchunguzwa.
  • Uvimbekinga kwenye puru (proktaitisi): inaweza kusababisha ute au majimaji kutoka kwenye anus, maumivu, kuwasha, hisia ya kutaka kujisaidia mara kwa mara au damu. Inaweza kutokana na maambukizi, ikiwemo baadhi ya magonjwa ya zinaa.
  • Bawasiri au michubuko kwenye eneo la njia ya haka kubwa: inaweza kuambatana na ute, kuwasha au damu.
  • Maambukizi ya utumbo: yanaweza kusababisha ute, kuharisha, maumivu ya tumbo au haja kubwa kubadilika.
  • Fistula ya njia ya haja kubwa: inaweza kusababisha majimaji au usaha unaotoka mara kwa mara kupitia tundu karibu na njia ya haja kubwa, hasa kama kuna uvimbe, maumivu au harufu mbaya.
  • Tatizo la njia ya mkojo au uke: wakati mwingine majimaji yanayodhaniwa kutoka njia ya haja kubwa yanaweza kuwa yanatoka kwenye uke au njia ya mkojo. Hivyo ni muhimu kutambua mahali hasa yanapotoka.

Kwa kuwa majimaji yanaonekana wakati wa kukojoa, ni muhimu pia kuhakikisha kama kweli yanatoka kwenye njia ya haja kubwa, au yanatoka ukeni na kuonekana kana kwamba yanatoka nyuma.


Ikiwa majimaji yana damu, usaha, harufu mbaya, au kuna maumivu ya njia ya haja kubwa/tumbo, homa, kuharisha sana, uvimbe karibu na anus au maumivu wakati wa kujisaidia, ni vizuri kwenda hospitali kwa uchunguzi.


Daktari anaweza kuchunguza eneo la njia ya haka kubwa na uke na kufanya vipimo vya mkojo, kinyesi au maambukizi ya zinaa kulingana na dalili.


Usitumie antibiotiki au dawa za kuingiza kwenye anus bila kujua chanzo, kwa sababu matibabu hutegemea sababu iliyogunduliwa.


Pata zawadi kwa kutoa maoni yako kuboresha mfumo huu, Bofya 👉Shiriki.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

25 Agosti 2026, 21:59:24

​

bottom of page