Mwandishi:
Dkt. Benjamin L, MD,
Mhariri:
Dkt. James NL, MD
Imeboreshwa:
27 Septemba 2026, 13:41:50
Nina changamoto sijajua tatizo nini nikiwa nakojoa haja ndogo sehemu ya haja kubwa hua Kuna majimaji yanatoka au wakati mwingine nikiwa nimetulia tu kuna muda unasikia kama majimaji hivi shida itakua nini? Mimi ni mwanaume
Majimaji yanayotoka kwenye njia ya haja kubwa si jambo la kawaida ikiwa yanajirudia, lakini chanzo kinaweza kuwa tofauti na si lazima yawe ugonjwa wa zinaa.
Kwa mwanaume, sababu zinazowezekana ni:
- Ute wa kwenye puru (rektamu): wakati mwingine puru inaweza kutoa ute kidogo, hasa wakati wa haja kubwa au kujikaza.
- Uvimbekinga kwenye puru (proktaitisi): inaweza kusababisha ute au usaha kutoka kwenye njia ya haka kubwa, pamoja na hisia ya kutaka kujisaidia mara kwa mara, maumivu, kuwasha au damu. Maambukizi ya gono, chlamydia, herpes na kaswende yanaweza kusababisha hali hii, hasa ikiwa kulikuwa na ngono ya njia ya haja kubwa.
- Uvimbe kinga wa tezi dume(prostataitisi): kwa baadhi ya wanaume, ute wa tezi dume unaweza kuonekana kupitia njia ya haja kubwa, na unaweza kuambatana na maumivu kati ya korodani na anus, matatizo ya kukojoa au maumivu wakati wa kumwaga.
- Magonjwa ya utumbo au puru, kama bawasiri, maambukizi ya utumbo, au magonjwa ya uchochezi ya utumbo, pia yanaweza kusababisha ute.
Kwa maelezo kwamba majimaji hutoka wakati wa kukojoa au hata ukiwa umekaa bila kujisaidia, ni vizuri kuchunguzwa badala ya kudhani ni ute wa kawaida. Daktari anaweza kuangalia njia ya haja kubwa/puru na, kulingana na dalili, kufanya vipimo vya mkojo, magonjwa ya zinaa na wakati mwingine kuchukua ute kwenye puru kwa vipimo.
Ikiwa kuna damu kwenye majimaji, usaha, maumivu ya njia ya haka kubwa, maumivu wakati wa kujisaidia, homa, maumivu ya chini ya tumbo, au maumivu/uvimbe wa korodani, ni muhimu kwenda hospitali mapema.
Na kama kulikuwa na ngono bila kinga, hasa ngono ya njia ya haja kubwa, ni muhimu kumwambia daktari kwa sababu inaweza kubadilisha aina ya vipimo vinavyohitajika.
Pata zawadi kwa kutoa maoni yako kuboresha mfumo huu, Bofya 👉Shiriki.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
26 Agosti 2026, 10:26:24

