Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dkt. Sospeter M, MD
Dkt. Lugonda B, MD
2 Novemba 2026, 07:19:52
Kufunga uzazi kwa mwanamke (kufunga mirija ya uzazi)
Kufunga uzazi kwa mwanamke (kufunga mirija ya uzazi, kufunga kizazi, tubal ligation) ni upasuaji mdogo wa kufunga, kukata au kuondoa mirija miwili ya uzazi (mirija ya falopia), ili yai lisiweze kukutana na mbegu za kiume. Ni njia ya kudumu ya uzazi wa mpango kwa mwanamke aliye na uhakika kwamba hataki watoto tena. Inazuia mimba kwa zaidi ya 99%, haibadilishi homoni, na hedhi inaendelea kama kawaida.
Kwa sababu ni ya kudumu, uamuzi huu unahitaji ushauri kamili na ridhaa yako ya hiari (Mwongozo wa Taifa, STG 2026). Kufungua mirija baadaye ni upasuaji mkubwa, wa gharama, na mafanikio yake si ya uhakika. Kama huna uhakika, njia za muda mrefu kama kitanzi cha kopa au njiti zina nguvu karibu sawa na zinaweza kuachwa wakati wowote.
Kufunga uzazi kwa mwanamke ni nini?
Mirija ya uzazi ni mirija miwili myembamba inayounganisha ovari na mfuko wa kizazi. Kila mwezi yai husafiri kupitia mmoja wa mirija hii, na kwa kawaida ndimo yai hukutana na mbegu za kiume. Kufunga uzazi kunaziba njia hii pande zote mbili.
Kufunga na kukata (tubal ligation): sehemu ya kila mrija hufungwa kwa uzi na kukatwa; njia inayotumika zaidi Tanzania.
Kubana mirija kwa vibanio maalumu au pete (kwa laparoskopi).
Kuunguza mirija kwa umeme (kwa laparoskopi).
Kuondoa mirija yote (salpingectomy): inaongezeka duniani kwa sababu, mbali na kuzuia mimba, hupunguza hatari ya saratani ya ovari.
Kwa mwanaume, njia inayolingana ni vasektomi; soma Kufunga uzazi kwa mwanaume.
Inafanyaje kazi?
Mirija ikishafungwa au kukatwa, yai haliwezi kusafiri kukutana na mbegu, na mbegu haziwezi kufikia yai. Urutubishaji hautokei, hivyo mimba haitungi. Ovari zinaendelea kufanya kazi na kutoa homoni na mayai kama kawaida; yai linalotolewa huyeyuka na kufyonzwa na mwili bila madhara.
Ufanisi wake
Muda tangu upasuaji | Wanaopata mimba kati ya 100 |
Mwaka wa kwanza | Takribani 0.5 (chini ya 1) |
Ndani ya miaka 10 | Takribani 2 |
Kinga huanza mara moja baada ya upasuaji (tofauti na vasektomi, inayohitaji miezi 3).
Kufunga uzazi si kinga ya asilimia 100: mara chache mirija hujiunga yenyewe au upasuaji haukuziba kabisa.
Wanawake waliofunga uzazi wakiwa na umri mdogo wana hatari kubwa kidogo zaidi ya mimba kutokea.
Mimba ikitokea baada ya kufunga uzazi, kuna uwezekano mkubwa (hadi 1 kati ya 3) kuwa ni mimba nje ya kizazi, ambayo ni hatari. Kwa hiyo mwanamke aliyefunga uzazi akikosa hedhi au kupata maumivu makali ya tumbo upande mmoja, aende hospitali haraka.
Nani anaweza kufunga uzazi?
Mwanamke yeyote anaweza kufunga uzazi kama ameamua kwa hiari yake, baada ya kupata maelezo kamili, kwamba hataki watoto tena. Hakuna kiwango cha chini cha idadi ya watoto au umri kinachohitajika kisheria. WHO inasema hakuna hali ya kiafya inayomzuia kabisa mwanamke kufunga uzazi; baadhi ya hali zinahitaji tu kuahirisha, tahadhari au kufanyiwa hospitali kubwa:
Kuahirisha: mimba, maambukizi ya via vya uzazi au ya kidonda kwa sasa, damu ukeni isiyojulikana chanzo, upungufu mkali wa damu, homa au ugonjwa mkali kwa sasa, au siku 7 hadi wiki 6 baada ya kujifungua.
Hospitali yenye vifaa zaidi: kisukari kisichodhibitiwa, shinikizo kubwa la damu, ugonjwa wa moyo, unene mkubwa, historia ya upasuaji mwingi wa tumbo, au VVU yenye magonjwa nyemelezi.
Kufunga uzazi kunafaa hasa kwa mwanamke ambaye mimba nyingine itakuwa hatari kubwa kwa maisha yake, mradi amefanya uamuzi mwenyewe.
Kabla ya kuamua: maswali ya kujiuliza
Wanawake wengi hufurahia uamuzi wao, lakini baadhi hujuta baadaye. Kujuta ni kwa kawaida zaidi kwa:
Mwanamke mwenye umri chini ya miaka 30 (hatari ya kujuta ni mara 2 zaidi).
Aliyefanya uamuzi wakati wa msongo, kama mara baada ya kujifungua au kupoteza mimba, bila kuwa ameupanga kabla.
Aliye na watoto wachache au hana mtoto.
Aliyeshinikizwa na mume, familia au mtu mwingine.
Ndoa au uhusiano usio imara; kuachika au kupata mwenzi mpya anayetaka watoto ni sababu kubwa ya kujuta.
Kifo cha mtoto baadaye.
Jiulize: Kama nikiachika au mwenzi wangu akifariki, ningetaka mtoto na mwenzi mpya? Kama mtoto wangu akifariki, ningetaka mwingine? Kama jibu ni "labda", njia ya muda mrefu ni bora kwako kwa sasa. Uamuzi ni wako; mume au mtu mwingine hawezi kukulazimisha, wala kukuzuia.
Njia mbadala za muda mrefu
Kama huna uhakika kamili, njia hizi zina nguvu karibu sawa na kufunga uzazi, na unaweza kuziacha wakati wowote:
[Kitanzi cha kopa (IUCD)](/uzazi-wa-mpango/kitanzi-chenye-madini-ya-shaba): bila homoni, zaidi ya 99%, hadi miaka 10-12, kinaweza kutolewa wakati wowote.
Kitanzi cha homoni: zaidi ya 99%, miaka 5-8, hedhi nyepesi sana.
[Njiti](/uzazi-wa-mpango/njiti-ya-uzazi-wa-mpango): zaidi ya 99%, miaka 3-5.
Vasektomi kwa mume: kama wanandoa wote wawili wameamua, vasektomi ni rahisi zaidi, salama zaidi na nafuu kuliko kufunga uzazi kwa mwanamke.
Wakati gani upasuaji unaweza kufanyika?
Wakati | Maelezo |
Ndani ya siku 7 baada ya kujifungua (vizuri zaidi ndani ya saa 48) | Mfuko wa kizazi bado uko juu, hivyo mirija inafikiwa kwa urahisi kwa mchano mdogo karibu na kitovu |
Wakati wa upasuaji wa kujifungua (C-section) | Hushauriwa kwa wanaoutaka, kwa sababu huepusha upasuaji mwingine; uamuzi ufanywe kabla ya siku ya upasuaji, si wakati wa uchungu |
Kuanzia wiki 6 baada ya kujifungua | Wakati wowote baadaye |
Wakati wowote usipokuwa mjamzito | Mara nyingi ndani ya siku 7 tangu hedhi ianze, au ukiwa unatumia njia nyingine kwa usahihi |
Baada ya mimba kuharibika au kutolewa | Ndani ya siku 7, kama hakuna maambukizi |
Wakati wa upasuaji mwingine wa tumbo | Inawezekana kama uamuzi ulikwisha kufanywa kabla |
Huwezi kufunga uzazi ukiwa mjamzito. Kama una mimba na unataka kufunga uzazi, utasubiri mpaka wakati wa kujifungua.
Aina za upasuaji
Minilaparotomi: mchano mdogo (sentimita 2-5) chini ya tumbo karibu na mstari wa nywele za sehemu za siri, au chini ya kitovu baada ya kujifungua. Daktari huvuta kila mrija nje, huufunga na kuukata. Hufanyika mara nyingi kwa ganzi ya eneo pamoja na dawa ya kutuliza, bila nusukaputi. Hii ndiyo njia inayotumika zaidi Tanzania.
Laparoskopi: matundu 1-2 madogo kwenye tumbo; kifaa chenye kamera huingizwa ili kuona mirija, kisha mirija hubanwa, huunguzwa au hukatwa. Mara nyingi hufanyika kwa nusukaputi; kupona ni haraka zaidi, lakini inahitaji vifaa na wataalamu maalumu.
Wakati wa upasuaji wa kujifungua: mirija hufungwa na kukatwa au huondolewa kupitia mchano ule ule.
Upasuaji huchukua takribani dakika 15 hadi 30. Kila njia ina faida na hasara; daktari atakushauri inayofaa kwako.
Maandalizi na vipimo kabla ya upasuaji
Ushauri kamili: njia mbadala, ufanisi, hatari, na kwamba ni ya kudumu. Utasaini fomu ya ridhaa ya hiari baada ya kuelewa.
Historia ya afya na uchunguzi wa mwili, ikiwemo uchunguzi wa nyonga.
Kipimo cha ujauzito kwa mkojo.
Kipimo cha wingi wa damu (Hb) na, kama inahitajika, vipimo vingine vya damu au picha ya mawimbi ya sauti (ultrasound).
Kutokula kwa saa 6 kabla, kama utapewa nusukaputi au dawa nyingi za kutuliza.
Oga, vaa nguo safi zenye nafasi, na panga mtu wa kukurudisha nyumbani.
Baada ya upasuaji: utegemee nini?
Mara nyingi unaruhusiwa kurudi nyumbani siku hiyo hiyo au siku inayofuata, isipokuwa kama upasuaji ulifanyika baada ya kujifungua au unahitaji uangalizi zaidi.
Maumivu ya tumbo na ya kidonda kwa siku chache; utapewa dawa za maumivu.
Uchovu, kizunguzungu, tumbo kujaa gesi.
Maumivu ya bega kwa siku 1-2 baada ya laparoskopi, kutokana na gesi iliyotumika.
Wanawake wengi hurudi kwenye kazi nyepesi baada ya siku 2-3, na kazi za kawaida baada ya wiki 1.
Mshono huondolewa (kama hauyeyuki) baada ya siku 7; utapangiwa kurudi kliniki ndani ya wiki 1-2.
Tunza kidonda kikavu na safi, kama ulivyoelekezwa. Soma Kutunza kidonda cha upasuaji nyumbani.
Ruksa na mwiko baada ya upasuaji
Epuka kubeba mizigo mizito kwa angalau wiki 1 (wiki 6 kama upasuaji ulifanyika pamoja na kujifungua kwa upasuaji).
Epuka tendo la ndoa kwa angalau wiki 1, au mpaka maumivu yaishe.
Usiloweke kidonda kwenye maji (kuogelea, kukaa ndani ya beseni) mpaka kipone; kuoga kwa kumwagia ni sawa baada ya saa 24-48.
Unaweza kutembea na kufanya kazi nyepesi; kutembea husaidia kupona.
Kufunga uzazi hakukulindi dhidi ya magonjwa ya zinaa; tumia kondomu kama kuna hatari.
Faida za kufunga uzazi
Kinga ya kudumu na yenye nguvu kubwa; huhitaji tena kukumbuka kidonge, sindano au safari za kliniki.
Haina homoni: hakuna maudhi ya homoni, na hedhi yako inabaki kama ilivyo kwa asili.
Hakuathiri tendo la ndoa; wanawake wengi hufurahia tendo zaidi kwa sababu hawana hofu ya mimba.
Hupunguza hatari ya saratani ya ovari (zaidi kama mirija yote imeondolewa).
Hupunguza hatari ya maambukizi makali ya via vya uzazi (PID) kwa baadhi.
Hufanyika mara moja tu; kwa muda mrefu ni nafuu kuliko njia za kila mara, na mara nyingi hutolewa bure katika hospitali za serikali.
Hatari na madhara
Kufunga uzazi ni salama kwa wanawake wengi kikifanywa na mtaalamu aliyefundishwa. Madhara makubwa ni nadra (chini ya 1 kati ya 100). Yanaweza kuwa:
Maambukizi ya kidonda au ndani ya tumbo.
Kuvuja damu au damu kuvilia chini ya ngozi au ndani ya tumbo.
Kufumuka kwa kidonda.
Kujeruhiwa kwa utumbo, kibofu cha mkojo au mishipa mikubwa ya damu (nadra sana, zaidi kwa laparoskopi).
Madhara ya dawa za ganzi au nusukaputi.
Makovu ndani ya tumbo, na mara chache maumivu ya tumbo ya muda mrefu.
Mimba (nadra), na kama ikitokea, uwezekano mkubwa wa kuwa nje ya kizazi.
Mambo yanayoongeza hatari ya madhara
Historia ya upasuaji mwingine wa tumbo au maambukizi ya nyonga (makovu ndani ya tumbo).
Unene mkubwa (obeziti).
Kisukari, hasa kisichodhibitiwa.
Upungufu mkubwa wa damu.
Uvutaji sigara na magonjwa ya moyo au mapafu (hasa kwa nusukaputi).
Kufunga uzazi hakubadilishi nini
Imani | Ukweli |
Kufunga uzazi huleta ukomo wa hedhi mapema. | Ovari zinaendelea kufanya kazi; ukomo wa hedhi huja wakati wake wa kawaida. |
Hedhi itakoma au damu itajikusanya tumboni. | Hedhi inaendelea kama kawaida. Yai linalotolewa hufyonzwa na mwili. |
Kufunga uzazi hupunguza hamu ya tendo la ndoa. | Homoni haziathiriwi; hamu na raha ya tendo hubaki kama ilivyo. |
Mwanamke atanenepa au kudhoofika. | Hakuna ushahidi; uwezo wa kufanya kazi nzito unarudi baada ya kupona. |
Kufunga uzazi kunasababisha saratani. | Kunapunguza hatari ya saratani ya ovari, na hakuongezi saratani nyingine. |
Mwanamke anahitaji ruhusa ya mume. | Mwanamke mtu mzima anaamua mwenyewe; ni vizuri kujadili na mume, lakini sheria na miongozo ya afya inahitaji ridhaa yake mwenyewe. |
Kama ukibadilisha mawazo baadaye
Kufungua mirija ya uzazi (tubal reversal) ni upasuaji mkubwa wa tumbo unaohitaji madaktari bingwa, ni wa gharama kubwa, na haupatikani katika hospitali nyingi Tanzania. Mafanikio hutegemea umri wako, aina ya upasuaji uliofanyika (kukatwa kwa kiasi kidogo ni rahisi kurejesha; kuunguzwa au kuondolewa kabisa ni vigumu au haiwezekani), na urefu wa mirija uliobaki. Hata ikifanikiwa, hatari ya mimba nje ya kizazi huongezeka.
Njia nyingine ni upandikizaji wa mimba kwenye maabara (IVF), ambayo pia ni ghali. Soma zaidi: Kufungua uzazi kwa mwanamke.
Lini uwasiliane na daktari haraka
Homa ya nyuzi joto 38 au zaidi.
Kuzimia, kizunguzungu kikali, au kupoteza fahamu.
Maumivu makali ya tumbo yanayoongezeka, hasa baada ya saa 12 tangu upasuaji.
Damu inayotoka kwenye kidonda, au bendeji kulowa damu.
Usaha, uchafu unaonuka, wekundu au uvimbe unaoongezeka kwenye kidonda.
Kutapika kusikoisha au tumbo kuvimba sana.
Wakati wowote baadaye: hedhi kukosa au dalili za ujauzito, hasa pamoja na maumivu ya tumbo upande mmoja (mimba nje ya kizazi).
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Uzazi wa mpango wa kudumu ni nini?
Uzazi wa mpango wa kudumu ni upasuaji unaozuia mimba kwa maisha yote. Kwa mwanamke, mirija ya uzazi hufungwa, hukatwa au huondolewa ili yai lisikutane na mbegu. Kwa mwanaume, mirija inayobeba mbegu (vas deferens) hukatwa na kufungwa; upasuaji huu huitwa vasektomi. Njia hizi zinafaa kwa watu waliokamilisha kabisa mpango wao wa kupata watoto, baada ya ushauri kamili na ridhaa ya hiari.
2. Kufunga mirija ya uzazi ni salama?
Kufunga mirija ya uzazi ni salama sana kikifanywa na mtaalamu aliyefundishwa katika mazingira sahihi. Madhara makubwa kama maambukizi, kuvuja damu au kujeruhiwa kwa viungo vya ndani hutokea kwa chini ya mwanamke 1 kati ya 100. Maumivu madogo na uchovu ni ya muda mfupi. Hatari huongezeka kidogo kwa wenye unene mkubwa, kisukari, au historia ya upasuaji mwingi wa tumbo.
3. Tofauti ya kufunga uzazi kwa mwanamke na kwa mwanaume ni ipi?
Kwa mwanamke, upasuaji hufanyika tumboni kupitia mchano mdogo (minilaparotomi) au matundu madogo (laparoskopi), na kinga huanza mara moja. Kwa mwanaume, vasektomi hufanyika kwenye korodani kwa ganzi ya eneo, huchukua dakika 10-30, hana mchano tumboni, na hupona haraka, lakini kinga huanza baada ya takribani miezi 3. Vasektomi ni salama zaidi, rahisi zaidi na nafuu zaidi kati ya hizi mbili.
4. Kufunga uzazi kunaathiri hamu ya tendo la ndoa?
Kufunga uzazi hakuathiri hamu ya tendo la ndoa, uwezo wa kufika kileleni, wala ukavu wa uke, kwa sababu ovari zinaendelea kutoa homoni kama kawaida. Kwa mwanaume, vasektomi haiathiri nguvu za kiume wala kiasi cha shahawa kwa kiasi kinachoonekana. Wenzi wengi husema tendo huwa la kufurahisha zaidi kwa sababu hawana tena hofu ya mimba.
5. Ufanisi wa kufunga uzazi ni kiasi gani?
Kufunga uzazi kuna ufanisi wa zaidi ya 99%: takribani mwanamke 1 kati ya 200 hupata mimba katika mwaka wa kwanza, na takribani 2 kati ya 100 ndani ya miaka 10. Si kinga ya asilimia 100, kwa sababu mara chache mirija hujiunga. Mimba ikitokea, mara nyingi huwa nje ya kizazi, hivyo dalili za mimba au maumivu makali ya tumbo yanahitaji kwenda hospitali haraka.
6. Naweza kubadilisha mawazo baadaye nikataka kupata mtoto?
Kufunga uzazi hakukusudiwi kubadilishwa. Upasuaji wa kufungua mirija upo, lakini ni mkubwa, ghali, haupatikani katika hospitali nyingi, na mafanikio yake si ya uhakika, hasa kama mirija iliunguzwa au kuondolewa. IVF ni njia nyingine, pia ghali. Kwa hiyo fikiria kwa kina, jadili na mtoa huduma, na kama una shaka yoyote, chagua njia ya muda mrefu kama kitanzi cha kopa au njiti.
7. Kufunga uzazi kunalinda dhidi ya magonjwa ya zinaa?
Kufunga uzazi hakukulindi dhidi ya VVU, kisonono, kaswende, klamidia wala magonjwa mengine ya zinaa; huzuia mimba tu. Kama kuna hatari ya maambukizi, endelea kutumia kondomu kila tendo, hata baada ya kufunga uzazi. Kupima VVU na magonjwa ya zinaa pamoja na mwenzi ni sehemu nzuri ya huduma.
8. Ni nani anayefaa zaidi kufunga uzazi?
Kufunga uzazi kunafaa zaidi kwa mwanamke aliyekamilisha mpango wake wa kupata watoto na ana uhakika hataki tena, mwanamke ambaye mimba nyingine itakuwa hatari kwa maisha yake, na wanandoa waliokubaliana baada ya majadiliano ya kina. Kunafaa pia kwa wanaotaka njia ya kudumu isiyohitaji kukumbuka chochote. Uamuzi lazima uwe wa hiari, bila kushinikizwa.
9. Kuna madhara ya muda mrefu ya kufunga uzazi?
Kwa wanawake wengi, hakuna madhara ya muda mrefu. Tafiti kubwa hazijaonyesha kufunga uzazi kuleta ukomo wa hedhi mapema, hedhi nzito, kuongezeka uzito, wala saratani; badala yake hupunguza saratani ya ovari. Wachache hupata maumivu ya tumbo ya muda mrefu kwa sababu ya makovu ya ndani. Madhara makubwa zaidi ya muda mrefu ni kujuta kwa wale waliobadilisha mawazo.
10. Ni lazima kuwa na watoto kabla ya kufunga uzazi?
Kisheria na kitaalamu, si lazima mwanamke awe na watoto, au idadi fulani ya watoto, ili kufunga uzazi. Hata hivyo, wanawake wasio na watoto au wenye umri chini ya miaka 30 wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujuta baadaye. Kwa hiyo mtoa huduma atakuuliza maswali zaidi na kukueleza njia mbadala za muda mrefu, ili uamuzi wako uwe wa uhakika.
11. Naweza kwenda nyumbani siku hiyo hiyo baada ya kufunga uzazi?
Wanawake wengi waliofunga uzazi kwa minilaparotomi au laparoskopi, bila kujifungua siku hiyo, huruhusiwa kurudi nyumbani siku hiyo hiyo au kesho yake, baada ya kupumzika saa kadhaa na kukaguliwa. Kama upasuaji ulifanyika baada ya kujifungua au pamoja na upasuaji wa kujifungua, utakaa wodini muda ule ule wa kawaida. Panga mtu wa kukusindikiza nyumbani.
12. Kufunga uzazi kunauma?
Wakati wa upasuaji hutasikia maumivu makali kwa sababu ya ganzi ya eneo na dawa ya kutuliza, au nusukaputi. Unaweza kuhisi kuvutwa au shinikizo tumboni wakati mirija inavutwa. Baada ya upasuaji, maumivu ya tumbo na ya kidonda kwa siku 2-3 ni ya kawaida na hupungua kwa dawa za maumivu. Maumivu yanayoongezeka badala ya kupungua yanahitaji kuonana na daktari.
13. Kufunga uzazi kunafanyika bure Tanzania?
Katika hospitali nyingi za serikali na vituo vya mashirika ya uzazi wa mpango Tanzania, huduma ya kufunga uzazi hutolewa bure au kwa gharama ndogo, kama sehemu ya huduma za uzazi wa mpango. Hospitali binafsi hutoza gharama tofauti. Uliza kituo chako cha karibu, au mkunga wakati wa kliniki ya wajawazito kama unataka kufunga uzazi baada ya kujifungua.
14. Ninaweza kufunga uzazi wakati wa upasuaji wa kujifungua?
Kufunga uzazi wakati wa upasuaji wa kujifungua (C-section) kunawezekana na huepusha upasuaji mwingine baadaye. Hata hivyo, uamuzi huu unapaswa kufanywa mapema, wakati wa kliniki ya wajawazito, na kusaini ridhaa kabla, si wakati wa uchungu au maumivu, ili uwe wa hiari na wa uhakika. Kama mtoto ana matatizo makubwa wakati wa kuzaliwa, daktari anaweza kushauri kuahirisha.
Imeandikwa:
7 Aprili 2026, 13:02:54
ULY clinic inakushauri siku zote ufuate ushauri wa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia mawasiliano yetu.
Rejea za mada hii:
World Health Organization Department of Sexual and Reproductive Health and Research (WHO/SRH), Johns Hopkins Bloomberg School of Public Health Center for Communication Programs (CCP). Family Planning: A Global Handbook for Providers. 2022 update. Baltimore and Geneva: CCP and WHO; 2022.
World Health Organization. Medical eligibility criteria for contraceptive use. 5th ed. Geneva: WHO; 2015.
American College of Obstetricians and Gynecologists. ACOG Practice Bulletin No. 208: Benefits and risks of sterilization. Obstet Gynecol. 2019;133(3):e194-e207.
Peterson HB, Xia Z, Hughes JM, Wilcox LS, Tylor LR, Trussell J. The risk of pregnancy after tubal sterilization: findings from the U.S. Collaborative Review of Sterilization. Am J Obstet Gynecol. 1996;174(4):1161-70.
Hillis SD, Marchbanks PA, Tylor LR, Peterson HB. Poststerilization regret: findings from the United States Collaborative Review of Sterilization. Obstet Gynecol. 1999;93(6):889-95.
Marino S, Canela CD, Nama N. Tubal sterilization. In: StatPearls. Treasure Island (FL): StatPearls Publishing; 2024.
Danis RB, Della Badia CR, Richard SD. Postpartum permanent sterilization: could bilateral salpingectomy replace bilateral tubal ligation? J Minim Invasive Gynecol. 2016;23(6):928-32.
Castellano T, Zerden M, Marsh L, Boggess K. Risks and benefits of salpingectomy at the time of sterilization. Obstet Gynecol Surv. 2017;72(11):663-8.
Hatcher RA, Nelson AL, Trussell J, et al. Contraceptive Technology. 21st ed. New York: Ayer Company Publishers; 2018.
Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026.
