top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

ULY CLINIC

24 Agosti 2026, 03:43:15

Homa: Maana, Dalili, Vipimo na Matibabu

Homa; Maana, dalili, visababishi vipimo na kinga

 

Homa kitabibu humaanisha kuongezeka kwa joto la mwili zaidi ya lile la kawaida (nyuzi joto  za sentigredi 37), mara nyingi husababishwa na ugonjwa unaoendelea mwilini. Mtu akipata  homa inamaanisha mwili umetambua kuna kitu kisicho cha kawaida kinaendelea. Katika tiba homa pia hujulikana kwa jina la hyperthermia, pyrexia na kupanda kwa joto la mwili.

​

Kwa watu wazima, homa inaweza  kusababisha mtu kujihisi vibaya, hata hivyo huna haja ya kuogopa endapo homa si kali au si zaidi ya nyuzi joto za sentigredi 39.4. Homa kwa watoto hata ikiongezeka kwa kiasi kidogo, mara nyingi huweza kumaanisha kuna tatizo la hatari ndani ya mwili wa mtoto.


Homa huweza kupotea ndani ya siu chache, matumizi ya dawa pia yanaweza kutuliza homa. Dawa za kutuliza homa haziwezi kuondoa chanzo cha homa, hivyo ni vema kuwasiliana na daktari ili kujua tatizo ni nini hata baada ya homa kutulia baada ya kunywa dawa za kutuliza homa.

 

Je unashauriwa kutumia dawa za kutuliza homa kabla ya kuwasiliana na daktari?

Dawa za kutuliza homa au zile za kutuliza maumivu mara nyingi hazishauriwi kutumika, hii ni kwa sababu hufisha ishara mbalimbali ambazo daktari angeziona ili kutambua kirahisi ni nini kinachosababisha homa hiyo. Hata hivyo unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa afya mara moja kwa ushauri ili akuambie kama kuaa umuhimu wa kutumia dawa au la kabla ya kumwona.

 

Dalili za homa

 Dalili za homa hutegemea kisababishi, pamoja na hivyo huweza kuja pamoja na;

  • ​Kutokwa na jasho

  • Kutetemeka mwili

  • Maumivu ya kichwa

  • Maumivu ya misuli

  • Kukosa hamu ya kula

  • Mtoto kulialiabila kubembelezeka

  • Kuishiwa maji mwilini

  • Uchovu wa mwili

  • Kupata degedege kwa watoto kati ya miezi 6 na miaka mitano

 

Namna gani ya kutambua kuwa una homa

Homa inaweza kutambuliwa kwa kutumia kipimajoto,  vipimajoto vipo vya aina nyingi ambavyo ni;

  • Vipima joto vya kwapani

  • Vipima joto vya kinywa

  • Vipima joto vya paji la uso

  • Vipimajoto vya njia ya haja kubwa

  • Vipima joto vya masikio

​

Kumbuka;

Unawezakuhisi kuwa unahoma na hali huna homa, ni vema kujua joto lako la mwili kwa kutumia kipima joto, nunua kipima joto ukae nacho nyumbani kwani ni muhimu sana na utamsaidia daktari  kufanya maamuzi ya kitiba endapo umempigia simu wakatiumepima joto lao au mtoto wako.

 

Kipimajoto gani ni kizuri?

Kama unataka kununua kipimajoto chako, ni vema kupata kipima joto cha njia ya haja kubwa au kile cha kuweka kinywani. Vipima joto hivi ni vizuri na vinaleta majibu sahihi zaidi kwa kuwa husoma joto la ndnai ya mwili.

 

Joto la kawaida ni nyuzi joto za sentigredi ngapi?

Joto la kawaida la mwili ni nyuzi za sentigredi 37, hata hivyo joto linaweza kutofautiana kwa pointi kadhaa mfano nyuzi joto 36.1hadi nyuzi joto 37.2 huchukuliwa kama joto la kawaida.

 

Ni wakati gani umwone daktari?

Baadhi ya wakati, homa husababishwa na sababu ambazo hupaswi kuwa na hofu kama vile;

  • Mazoezi makali

  • Kuingia hedhi au kuingia siku za kuchavushwa kwa yai(ovulesheni)

  • Mabadiliko ya hali ya hewa(asubuhi joto la mwili huwa chini kidogo na machana huwa juu kidogo kutokana na kupigwa na mwangawa jua)

 

Unapaswa kutafuta msaada wa haraka endapo mtoto  ana hali zifuatazo;

  • Kichanga kupata homa isiyo na sababu au watoto chini ya mwaka mmoja na joto la mwili ni zaidi ya nyuzi joto za sentigredi 37.9 na kuendelea. Licha ya kuwa na dalili zingine kama zilivyoorodheshwa hapo juu

  • Mtoto amepata chanjo hivi karibuni

  • Ana maambukizi au tatizo kubwa la kiafya linalofahamika mfano kuwa na kinga za mwili za chini au matumizi ya dawa za kushusha kinga za mwili

  • Kwa mtoto mdogo zaidi ya mwaka mmoja endapo amekuwa mchovu, mkali, hali ya kutapika kunakojirdia  maumivu ya kichwa, tumbo, kuharisha au dalili zingine

  • Endapo mtoto zaidi ya mwaka mmoja aliachwa ndani ya gari lenye joto.

  • Endapo homa kwa mtoto iimedumu zaidi ya siku tatu bila kupotea

  • Endapo mtoto wa zaidi ya mwaka mmoja anashindwa kukuangalia macho kwa macho na ana homa

  • Mtoto kutoacha kulia licha ya kubembelezwa

  • Maumivu ya kifua

  • Kupumua kwa shida

  • Kushindwa kutembea/kusimama

 

Kwa watu wazima mwone daktari endapo joto limepanda zaidi ya nyuzi 39.4 digrii za sentigredi pamoja na;

  

Ni nini husababisha homa?

Homa hutokea endapo sehemu ya mwili inayoitwa hypothalamus ikiamuru kiwango cha joto ndani ya mwili kupanda kutoka cha kawaida (nyuzi joto 37 za sentigredi) kwenda cha juu. Kiwango kikipanda  mwili huitikia kwa kuhisi baridi kali, kutetemeka na kujongea kwa misuli ili joto hilo lifikie pale ambapo tezi ya hypothalamus imeamuru lifikiwe. Hii hutokea makusudi ili kupambana na maambukizi yaliyoingia ndani ya mwili.​

Mara nyingi  visababishi vya homa vinaweza kujulikana, hata hivyo kuna wakati huwa havifahamiki kabisa.


Visababishi vya homa vinvyojulikana huwa pamoja na;

  • Maambukizi mbalimbali kama ya bakteria kwenye ogani na mifumo mbalimbali mwilini(mapafu, ini, figo, mfumo wa mkojo n.k, maambukizi ya vimelea vya malaria n.k)

  • Maambukizi ya virusi

  • Kukaa kwenye joto kali

  • Kiharusi

  • Matumizi ya dawa ya kulevya kama kokeini na amphetamine

  • Magonjwa Fulani ya mwili kama homa ya rheumatoidi athraitizi, lupasi, inflamatori baweli

  • Vimbe za saratani

  • Madhaifu ya homoni mwilini kama hyperthyroidism

  • Matumizi ya dawa aina zingine kama zile za kushusha shinikizo la damu au kifafa

  • Kutumia baadhi ya chanjo kama vile chanjo ya dondakoo, tetenasi na pneumococcal

  • Sababu zisizojulikana

 

Madhara ya homa

Kwa watoto kuanzia miezi sita na miaka mi 5, wanaweza kupata degedege kutokana na homa, mbali na degedege hupoteza fahamu na kutetemeka sehemu zote za mwili kama mtu mwenye pepo pia hutokea.

​

Ni vema kuwasiliana na daktari haraka kupata uchunguzi maana degedege la mara kwa mara huweza kupelekea kupata mtindio wa ubongo na kifafa siku za mbeleni.

 

Endapo mtoto atapata degedege fanya mambo yafuatayo;

​

  • Mlaze mtoto kifudifudi kwenye sakafu

  • Ondoa vitu vyenye ncha kali kwenye mazingira ya karibu na mtoto

  • Legeza nguo zilizobana

  • Mshike mtoto ili kuzuia kujiumiza kwa kugonga vitu vilivyokaribu naye au sakafu

  • Usiweke kitu chochote kwenye kinywa cha mtoto

  • Ondoa chochote kilichopo kwenye kinywa cha mtoto baada ya degedege kutulia(usiweke kidole wakati degedege linaendelea kuepukwa kung’atwa

  • Mpeleke mtoto hospitali mapema u piga namba za simu kw huduma ya kwanza ukiwa nyumbani

 

Je unaweza kujikinga kupata homa?

Inaweza kuwa ngumu kujikinga kupata homa, hata hivyo kuna vitu unavyoweza kufanya ili kujikinga kama vile;

  • Kupunguza hatari ya kupata maambukizi kwa kunawa mikono yako kabla ya kula baada ya kwenda chooni, baada ya kutoka kwenye mkusanyiko wa watuw engi, baada ya kutoka kwa mtu anayeumwa, baada ya kuhudumia mifugo na baada ya kusafiri kwenye usafiri wa watu wengi

  • Beba kitakasa mikono endapo huwezi kupata maji ya kunawa haswa unapokuwa unasafiri kwenye usafiri wa watu wengi, kwenda hospitali kusalimu wagonjwa au kukutana na mtu anayeumwa au kuhudumia mtu anayeumwa

  • Zuia kugusa maeneo ya uso wako na kinywani maana huweza kupitisha maambukizi na kuingia mwilini mwako

  • Funika kinywa unapopiga chafya, au geukia upande mwingine unapokuwa unapiga chafya, kisha nawa mikono ili usishike maeneo na kuwaambukiza wengine

  • Usitumie vyombo vya watoto  kama vile vikombe vya maji na beseni za kuogea

 

Matibabu ya homa ukiwa nyumbani ni yapi?

Matibabu nyumbani huwa pamoja na;

  • Kupunguza idadi ya nguo mwilini

  • Kukanda mwili kwa kutumia kitambaa cha baridi

  • Kunywa majiya kutosha mara kwa mara hii huweza kuzuia pia kupoteza maji mwilini kutokana na homa

  • Kupata muda wa kupumzika ili kuupa mwili nguvu ya kupambana na maradhiyaliyoingia mwilini. Hata hivyo hakikisha unafanya shughuli ndogondogo na kula mlo kamili

  • Kutumia dawa za kununua duka la dawa bariki kama parasetamo, aspirini(zuia dawa hii kutumika kwa watoto chini ya miaka mitatu kuzuia kupata tatizo la kufisha la sindromu ya Reye’s) 


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara kuhusu homa na majibu yake

1. Je homa inaweza kuwa dalili ya ugonjwa hatari hata kama mtu anaonekana bado ana nguvu?

Ndiyo, homa inaweza kuwa ishara ya ugonjwa mdogo unaopita wenyewe au inaweza kuwa dalili ya tatizo kubwa linalohitaji matibabu ya haraka. Wakati mwingine mtu anaweza kuwa na homa lakini bado anaendelea na shughuli zake za kawaida, hali ambayo inaweza kumfanya apuuze tatizo. Hata hivyo, baadhi ya maambukizi au magonjwa ya ndani yanaweza kuanza taratibu kabla ya dalili nyingine kali kujitokeza.


Mfano, maambukizi kama malaria, nimonia, maambukizi ya njia ya mkojo, sumu ya bakteria kwenye damu (sepsisi), au baadhi ya magonjwa ya mfumo wa kinga yanaweza kuanza na homa pekee au dalili chache. Ukali wa ugonjwa haupimwi kwa kiwango cha homa pekee, bali pia hutegemea hali ya mgonjwa kwa ujumla, umri, magonjwa mengine aliyonayo na muda ambao homa imeendelea.


Ni muhimu kutazama mabadiliko mengine yanayoambatana na homa kama vile kupungua kwa uwezo wa kufanya shughuli, kushindwa kula au kunywa, kuchanganyikiwa, kupumua kwa shida, au hali ya kudhoofika ghafla. Katika mazingira haya, kutafuta ushauri wa mtaalamu wa afya ni muhimu hata kama homa haionekani kuwa kali sana.

2. Kwa nini baadhi ya watu hupata homa mara kwa mara kuliko wengine?

Kupata homa mara kwa mara kunaweza kusababishwa na sababu mbalimbali zinazohusiana na mazingira, mfumo wa kinga, au hali ya afya ya mtu. Baadhi ya watu hukutana mara nyingi na vimelea vya magonjwa kutokana na kazi zao, mazingira wanayoishi, au kuwa karibu na watu wengi, hivyo kuongeza uwezekano wa kupata maambukizi.


Mfumo wa kinga unapokuwa dhaifu unaweza kufanya mwili ushindwe kupambana vizuri na vimelea vinavyoingia mwilini. Hali hii inaweza kutokea kwa watu wenye magonjwa fulani, wanaotumia dawa zinazopunguza kinga ya mwili, au wenye upungufu wa virutubisho muhimu vinavyosaidia mfumo wa kinga kufanya kazi vizuri.


Hata hivyo, homa inayojirudia haipaswi kupuuzwa kwa sababu wakati mwingine inaweza kuashiria tatizo linalohitaji uchunguzi zaidi. Daktari anaweza kuhitaji kujua mara ambazo homa hutokea, muda wake, dalili zinazoambatana nayo na vipimo mbalimbali ili kutafuta chanzo halisi badala ya kutibu homa pekee.

3. Je mtoto anayepata homa mara kwa mara anaweza kuathirika ukuaji wake?

Kwa watoto wadogo, homa ni jambo linalotokea mara nyingi kwa sababu mfumo wao wa kinga bado unajifunza kutambua na kupambana na aina mbalimbali za maambukizi. Watoto wanaweza kupata homa mara kadhaa kwa mwaka hasa wanapoanza kukutana na watoto wengine shuleni, kwenye vituo vya kulelea watoto au katika mazingira yenye msongamano wa watu.


Homa yenyewe mara nyingi haisababishi madhara ya kudumu kwa ukuaji wa mtoto ikiwa chanzo chake kinatambuliwa na kutibiwa vizuri. Tatizo linaweza kutokea pale mtoto anapokuwa na maambukizi yanayojirudia bila kutibiwa, anakosa lishe ya kutosha, au anapoteza maji na nguvu mara kwa mara kutokana na ugonjwa.


Mzazi anapaswa kuangalia zaidi hali ya mtoto kati ya vipindi vya homa. Mtoto anayerejea kuwa mchangamfu, anakula vizuri na anakua kawaida mara nyingi hana tatizo kubwa. Lakini mtoto anayepungua uzito, kuchelewa kukua, kuchoka muda wote au kupata maambukizi mengi yasiyo ya kawaida anahitaji uchunguzi wa kitaalamu.

4. Je homa inaweza kutokea bila kuwa na maambukizi yoyote?

Ndiyo, homa inaweza kutokea hata bila kuwepo kwa maambukizi. Ingawa maambukizi ndiyo sababu inayojulikana zaidi, mwili unaweza kuongeza joto kutokana na hali nyingine zinazochochea mfumo wa kinga au kubadilisha namna mwili unavyodhibiti joto.


Baadhi ya magonjwa ya kinga ya mwili, baadhi ya saratani, au matatizo ya mfumo wa homoni yanaweza kusababisha mtu kupata homa bila kuwepo kwa bakteria au virusi. Pia baadhi ya dawa zinaweza kusababisha mwili kuitikia kwa kuongeza joto kama sehemu ya athari zake.


Kwa sababu hiyo, mtu mwenye homa ya muda mrefu bila sababu inayoeleweka anapaswa kufanyiwa uchunguzi badala ya kutumia dawa za kushusha homa kila mara. Uchunguzi wa kina husaidia kutambua chanzo na kutoa matibabu yanayolenga tatizo halisi.

5. Kwa nini homa huambatana na baridi na kutetemeka wakati mwili una joto?

Wakati mwili unapoanzisha homa, ubongo hubadilisha kiwango cha joto ambacho mwili unatakiwa kufikia. Ingawa mwili unaweza kuwa na joto kuliko kawaida, ubongo unaweza kuufanya mtu ajisikie kama ana baridi kwa sababu bado haujafikia kiwango kipya cha joto kilichowekwa.


Ndiyo maana mtu mwenye homa anaweza kutetemeka, kutafuta blanketi au kujisikia baridi sana licha ya kuwa mwili wake una joto. Kutetemeka ni njia ya mwili kuzalisha joto zaidi kupitia mikazo midogo ya misuli ili kufikia kiwango kipya cha joto.


Baada ya homa kushuka au mwili kuanza kurudi katika hali yake ya kawaida, mtu anaweza kuanza kutokwa jasho kwa sababu mwili unajaribu kupunguza joto lililozidi. Mabadiliko haya ni sehemu ya namna mwili unavyodhibiti joto wakati wa ugonjwa.

6. Je kunywa maji mengi kunaweza kusaidia mtu mwenye homa kupona haraka?

Kunywa maji ya kutosha ni sehemu muhimu ya kujihudumia wakati wa homa kwa sababu mwili unaweza kupoteza maji zaidi kuliko kawaida. Hali hii inaweza kusababishwa na kutokwa jasho, kupumua kwa haraka, kutokula au kunywa vizuri, au kuwepo kwa ugonjwa unaosababisha kupoteza maji.


Maji husaidia mwili kufanya kazi zake muhimu kama kusafirisha virutubisho, kudhibiti joto la mwili na kusaidia viungo kama figo kufanya kazi vizuri. Mtu mwenye upungufu wa maji anaweza kuongeza dalili kama uchovu, kizunguzungu, mdomo kukauka na udhaifu wa mwili.


Hata hivyo, kunywa maji pekee hakutibu chanzo cha homa kama kuna maambukizi au ugonjwa mwingine unaohitaji tiba maalumu. Ni njia ya kusaidia mwili wakati chanzo cha tatizo kinatafutwa au kinatibiwa.

7. Je ni salama kuoga wakati mtu ana homa?

Kwa watu wengi, kuoga wakati wa homa ni salama na kunaweza kusaidia mtu kujisikia vizuri zaidi, hasa kama anahisi mwili una jasho au kutokuwa na raha. Kuoga kwa maji ya kawaida au yenye uvuguvugu kunaweza kusaidia usafi wa mwili bila kuusumbua mwili.


Hata hivyo, kutumia maji ya baridi sana wakati wa homa si jambo linaloshauriwa kwa sababu linaweza kusababisha mwili kuanza kutetemeka. Kutetemeka kunaweza kuongeza uzalishaji wa joto ndani ya mwili na kumfanya mtu ajisikie vibaya zaidi.


Lengo la kuoga si kuondoa ugonjwa au kushusha homa moja kwa moja, bali ni kusaidia faraja ya mgonjwa. Mtu mwenye homa anapaswa pia kuzingatia kupumzika, kula kadiri anavyoweza na kutafuta msaada wa afya ikiwa kuna dalili zinazoonyesha tatizo kubwa.

8. Je homa ya muda mrefu inaweza kuashiria saratani?

Katika baadhi ya hali, homa ya muda mrefu inaweza kuonekana kwa watu wenye aina fulani za saratani, lakini hii si sababu ya kawaida ya homa kwa watu wengi. Mara nyingi homa husababishwa na maambukizi ya kawaida kuliko saratani.


Homa inayohusishwa na saratani mara nyingi huambatana na dalili nyingine kama kupungua uzito bila sababu, uchovu wa muda mrefu, kutokwa jasho jingi hasa usiku, au mabadiliko mengine yasiyo ya kawaida mwilini. Dalili hizi zinahitaji uchunguzi wa kitaalamu badala ya kufanya hitimisho haraka.


Mtu mwenye homa inayodumu kwa muda mrefu bila sababu inayojulikana anapaswa kumuona mtaalamu wa afya kwa tathmini. Uchunguzi wa mapema husaidia kugundua sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha hali hiyo na kuanza matibabu yanayofaa.

9. Je homa inaweza kuzuia mtu kufanya mazoezi au kazi?

Mtu mwenye homa anashauriwa kupunguza shughuli nzito za mwili kwa sababu mwili huwa unatumia nguvu nyingi kupambana na chanzo cha homa. Kufanya mazoezi makali wakati wa homa kunaweza kuongeza uchovu na kuchelewesha mwili kurudi katika hali yake ya kawaida.


Wakati mwili unapambana na ugonjwa, mahitaji yake ya nishati huongezeka. Kupumzika husaidia mwili kuelekeza nguvu zaidi katika mfumo wa kinga badala ya kutumia nguvu nyingi kwenye shughuli za kimwili.

Baada ya homa kuisha, mtu anapaswa kurudi kwenye shughuli taratibu kulingana na jinsi anavyojisikia.


Kurudi haraka kwenye kazi nzito wakati bado mwili haujapata nguvu kunaweza kusababisha uchovu mkubwa au kurefusha kipindi cha kupona.

10. Kwa nini baadhi ya watu hupata homa usiku zaidi kuliko mchana?

Mwili wa binadamu una mabadiliko ya kawaida ya joto yanayofuata saa ya mwili (rithimu ya sikadiani). Kwa kawaida joto la mwili huwa na mabadiliko madogo ndani ya siku, na kwa baadhi ya watu linaweza kuwa juu zaidi nyakati za jioni au usiku.


Wakati mtu ana ugonjwa unaosababisha homa, mabadiliko haya ya kawaida yanaweza kufanya ongezeko la joto lionekane zaidi wakati wa usiku. Pia, wakati wa usiku mtu huwa ametulia zaidi hivyo anaweza kugundua dalili kama kutetemeka, maumivu ya mwili au jasho kwa urahisi zaidi.


Homa inayoongezeka usiku pekee haimaanishi moja kwa moja kuwa kuna ugonjwa fulani maalumu. Kinachosaidia zaidi ni kuangalia muda wa homa, dalili nyingine zinazoambatana nayo na hali ya jumla ya mgonjwa ili kujua kama kuna haja ya uchunguzi zaidi.


Imeandikwa:

12 Julai 2026, 06:53:42

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

​

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

Rejea za mada hii:

  1. Fever. Healthline. https://www.healthline.com/health/fever. Imechukuliwa 28.06.2020

  2. Goldman L, et al., eds. Approach to fever or suspected infection in the normal host. In: Goldman-Cecil Medicine. 25th ed. Philadelphia, Pa.: Saunders Elsevier; 2016. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 28.06.2020

  3. Fever. Merck Manual Professional Version. https://www.merckmanuals.com/professional/infectious-diseases/biology-of-infectious-disease/fever. Imechukuliwa 28.06.2020

  4. Fever in infants and children. Merck Manual Professional Version. https://www.merckmanuals.com/professional/pediatrics/symptoms-in-infants-and-children/fever-in-infants-and-children. Imechukuliwa 28.06.2020

  5. Temperature regulation and the pathogenesis of fever. In: Mandell, Douglas, and Bennett's Principles and Practice of Infectious Diseases. 9th ed. Elsevier; 2020. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 28.06.2020

  6. Fever. In: Nelson Textbook of Pediatrics. 20th ed. Philadelphia, Pa.: Elsevier; 2016. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 28.06.2020

  7. Ward MA. Fever in infants and children: Pathophysiology and management. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 28.06.2020

  8. Rosen's Emergency Medicine: Concepts and Clinical Practice. 8th ed. Philadelphia, Pa.: Saunders Elsevier; 2014. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 28.06.2020

  9. Fever. Emergencies A-Z. American College of Emergency Physicians. http://www.emergencycareforyou.org/Emergency-101/Emergencies-A-Z/Fever. Imechukuliwa 28.06.2020

  10. Fever in the adult patient. In: Rosen's Emergency Medicine: Concepts and Clinical Practice. 8th ed. Philadelphia, Pa.: Saunders Elsevier; 2014. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 28.06.2020

  11. Approach to the adult with fever of unknown origin. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 28.06.2020

  12. Febrile seizures fact sheet. National Institute of Neurological Disorders and Stroke. https://www.ninds.nih.gov/Disorders/Patient-Caregiver-Education/Fact-Sheets/Febrile-Seizures-Fact-Sheet. Imechukuliwa 28.06.2020

  13. When and how to wash your hands. Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/handwashing/when-how-handwashing.html. Imechukuliwa 28.06.2020

  14. How to protect yourself & others. Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/coronavirus/2019-ncov/prevent-getting-sick/prevention.html. Imechukuliwa 28.06.2020

  15. WebMD. Fever. https://www.webmd.com/first-aid/fevers-causes-symptoms-treatments#2. Imechukuliwa 28.06.2020

bottom of page