top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Viashiria vya Uhai

Ni ishara za msingi zinazoonyesha hali ya mwili na utendaji wa mifumo muhimu ya mwili, na hivyo kutoa taarifa kuhusu uhai na hali ya jumla ya mtu. Viashiria hivi hujumuisha joto la mwili, mapigo ya moyo, kasi ya kupumua na shinikizo la damu. Katika huduma za kisasa, kiwango cha oksijeni kwenye damu (SpO₂) pia hupimwa mara nyingi, hasa kwa wagonjwa wenye hali au dalili zinazohusisha mfumo wa upumuaji.

Kukosa hamu ya kula

Ni dalili inayoweza kusababishwa na maambukizi, matatizo ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula, msongo wa mawazo, dawa au magonjwa mbalimbali ya mwili. Matibabu hutegemea chanzo na yanaweza kujumuisha kutibu ugonjwa unaosababisha tatizo, kuboresha lishe, kutumia dawa za kuongeza hamu ya kula pale inapoelekezwa na daktari, pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu ikiwa hali inaendelea.

Mambo ya kuzingatia unapokuwa kwenye dozi ya PEP

Tumia dawa kila siku kwa siku 28, hudhuria miadi na vipimo vyote vilivyopangwa, na tumia kondomu au epuka matukio mapya ya hatari hadi daktari atakapokushauri vinginevyo. Usiache dawa mwenyewe, usikose dozi mara kwa mara, wala usipuuze dalili hatarishi au miadi ya ufuatiliaji, kwani hatua hizi huongeza uwezekano wa PEP kufanya kazi ipasavyo.

Hisia za kucheza kwa tumbo kwa mwanaume au mwanamke asiye mjamzito

Mara nyingi husababishwa na harakati za kawaida za utumbo, gesi, misuli ya tumbo kujikaza yenyewe au mabadiliko ya mfumo wa fahamu, na si lazima iwe ishara ya ujauzito au ugonjwa mkubwa. Hata hivyo, ikiwa hali hii inaendelea kwa muda mrefu au inaambatana na maumivu makali, kupungua uzito, kutapika, damu kwenye choo au dalili nyingine zisizo za kawaida, uchunguzi wa kitabibu unahitajika ili kubaini chanzo halisi.

Maumivu ya nyonga

Hutokana na madhaifu kwenye mfupa wa nyonga, maungio yake, misuli, kano, mishipa au neva zinazouzunguka nyonga. Visababishi ni kama majeraha, uchakavu wa maungio, magonjwa ya uchochezi kinga, osteoporosisi, matatizo ya neva na kwa nadra, maambukizi au saratani ya mfupa. Kwa kuwa maumivu haya yanaweza kufanana na yale yanayotokana na via vilivyopo ndani ya nyonga, uchunguzi wa kitabibu ni muhimu ili kubaini chanzo halisi na kupata matibabu ya mapema yanayosaidia kupunguza maumivu, kurejesha uwezo wa kutembea na kuzuia ulemavu wa kudumu.

Kilainishi gani kinatumika ili mwanamke asichubuke ukeni?

Kuna aina mbalimbali za vilainishi kama vile vyenye maji, silikoni na mafuta, kila aina ina matumizi na tahadhari zake. Kuchagua aina sahihi ya kilainishi na kukitumia kwa usahihi huongeza faraja, hupunguza msuguano na husaidia kuepuka madhara kama muwasho au kuathiri kondomu. Hata hivyo, maumivu au ukavu wa uke unaoendelea unapaswa kuchunguzwa ili kubaini chanzo chake.

bottom of page