top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Je, mtu akinywa pombe anatakiwa akae muda gani kabla ya kuchanjwa?

Hakuna muda rasmi wa lazima wa kuacha pombe kabla ya chanjo, na kunywa kidogo hakuzuii mtu kuchanjwa. Hata hivyo pombe nyingi hupunguza uwezo wa mwili kutengeneza kinga na hufanya maudhi ya chanjo yajisikie zaidi. Kwa hiyo epuka pombe nyingi angalau saa 24 kabla ya kuchanjwa na siku 2 hadi 3 baada ya kuchanjwa. Usiende kuchanjwa ukiwa umelewa.

Je, ngozi kuwasha ni dalili ya VVU?

Ngozi kuwasha si dalili maalumu ya VVU – watu wengi wanaowashwa hawana VVU. Kwa mwenye VVU, muwasho ni wa kawaida zaidi: vipele vya muwasho vya VVU (PPE), fangasi, upele, ngozi kavu, seborrhoeic dermatitis, au mzio wa dawa. Njia pekee ya kujua kama una VVU ni kupima. Maelezo kamili yako kwenye makala ya mwili kuwashwa na UKIMWI.

Maumivu ya kitovu yanayodumu kwa muda mrefu: Sababu, Uchunguzi na Tiba

Maumivu ya kitovu ya muda mrefu, hasa yanayozidi ukila, ukikohoa au ukibonyeza, pamoja na kitovu kuvimba, mara nyingi ni ngiri ya kitovu – utumbo au mafuta kupenya kwenye udhaifu wa ukuta wa tumbo. Visababishi vingine ni maambukizi au kifuko cha maji/uchafu kwenye kitovu, utumbo (vidonda vya tumbo, appendix mwanzoni), na kwa mwanamke, endometriosis ya kitovu – kinundu kinachouma, kuvimba au kutoa damu wakati wa hedhi. Ngiri inayouma ghafla, kuwa ngumu, kubadilika rangi au pamoja na kutapika ni dharura.

Gesi tumboni, Gastraitisi na Yuriki asidi: Hatua za Kitabibu na Tiba Lishe

Swali: mgonjwa ana gesi, tumbo kuunguruma, kifua kuwaka, koo kukauka, maumivu ya viungo, hisia ya chakula kukwama kooni na choo kigumu, licha ya pantoprazole; ameambiwa ana gastraitisi na yuriki asidi. Majibu: dalili hizi mara nyingi hutokana na kucheua tindikali (GERD), gastraitisi, H. pylori, dawa za maumivu (NSAIDs), kuvimbiwa na mtindo wa maisha. Hatua za kitabibu: kumeza PPI dakika 30–60 kabla ya chakula kwa muda unaoshauriwa, kupima H. pylori, kuepuka NSAIDs, na kutibu kuvimbiwa. Hisia ya chakula kukwama (dysphagia) au kupungua uzito ni dalili za hatari zinazohitaji endoskopi. Kwa yuriki asidi: kiwango cha juu bila gauti hakihitaji dawa; maumivu ya viungo yanahitaji uchunguzi (gauti au visababishi vingine). Tiba lishe: milo midogo, kula polepole, kutolala saa 3 baada ya kula, kupunguza mafuta, pilipili, pombe, soda na vyakula vya sukari; kwa gauti punguza nyama za ndani, dagaa/vyakula vya bahari kwa wingi, bia na vinywaji vya sukari (fructose); kula mboga, matunda, nafaka zisizokobolewa na maji ya kutosha.

Kipimo kusoma mimba ipo siku chache baada ya kutoa mimba

Siku chache baada ya mimba kutoka, kipimo cha mkojo karibu kila mara bado huwa chanya, kwa sababu homoni ya hCG hushuka taratibu kwa wiki 2 hadi 4 (hadi 6). Kwa hiyo kipimo cha siku 4 hakisaidii kujua kama mimba imetoka. "Kinyama" kilichotoka huweza kuwa mfuko wa mimba au mabonge ya damu tu. Matiti kuuma huweza kuendelea wiki 1. Kuthibitisha: kipimo cha mkojo wiki 3–4 baada ya tukio, au hCG ya damu mara mbili, au ultrasound. Damu kidogo sana, dalili za ujauzito kuendelea au maumivu ya upande mmoja ni sababu ya kwenda kituo cha afya mapema.

Kukosa hedhi baada ya sindano ya uzazi wa mpango: Visababishi na Matibabu

Kukosa hedhi baada ya kutumia sindano ya uzazi wa mpango ni jambo la kawaida na si ugonjwa. Homoni ya projestini iliyomo kwenye sindano ya Depo hufanya utando wa ndani wa mfuko wa uzazi kuwa mwembamba, hivyo hakuna damu ya kutoka. Baada ya mwaka mmoja wa matumizi, karibu nusu ya wanawake hawapati hedhi kabisa. Damu haikusanyiki tumboni, na hali hii haimaanishi kizazi kimeharibika.

bottom of page