top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Uchafu ukeni siku chachebaada ya Kutoa Mimba kwa Dawa: Mwongozo kwa wanawake

Baada ya mimba kutoka kwa dawa, damu na uchafu wa kahawia au mwekundu hafifu usio na harufu kali, unaopungua taratibu kwa wiki 2 hadi 4, ni kawaida – kizazi kinajisafisha. Uchafu wa njano au kijani, mzito kama usaha, wenye harufu mbaya, au unaoambatana na homa, maumivu makali ya tumbo au kutetemeka huashiria maambukizi au mabaki ya mimba na unahitaji hospitali. Tiba hutegemea chanzo: antibayotiki kwa maambukizi, na kuondoa mabaki kwa njia salama. Huduma ya baada ya mimba kutoka (PAC) ni halali na inapatikana.

Je maziwa ya ngombe husababisha upungufu wa damu kwa watoto?

Yanaweza, yakitolewa mapema au kwa wingi. Maziwa ya ng'ombe yana madini chuma kidogo yanayofyonzwa vibaya, kalsiamu na casein yake hupunguza ufyonzaji wa madini chuma kutoka vyakula vingine, kwa vichanga yanaweza kusababisha damu kidogo kuvuja kwenye utumbo, na yakinywewa mengi humshibisha mtoto asile vyakula vyenye madini chuma. WHO (2023) inasema mtoto chini ya miezi 6 asipewe maziwa ya ng'ombe; miezi 6 hadi 11 asiyenyonya anaweza kupewa maziwa kamili yaliyochemshwa/pasteurized pamoja na vyakula vyenye madini chuma; baada ya mwaka 1 yasizidi vikombe 2 kwa siku.

Levonorgestrel hutibu nini?

Levonorgestrel ni homoni ya projestini inayotumika hasa kuzuia mimba: kwenye vidonge vya dharura (P2/Postinor), vidonge vya projestini pekee, vidonge vya vichocheo viwili, kipandikizi (Jadelle) na kitanzi cha homoni (LNG-IUD). Kitanzi cha levonorgestrel pia hutibu hedhi yenye damu nyingi, hupunguza maumivu ya hedhi na endometriosis, na hulinda ukuta wa kizazi kwa wanaotumia estrojeni wakati wa komahedhi. Haitibu maambukizi wala magonjwa ya zinaa.

Ute wa maziwa mgando bila harufu wala muwasho ukeni: Je kuna tatizo?

Ute mweupe mzito bila harufu, muwasho wala maumivu mara nyingi ni wa kawaida – hubadilika katika mzunguko wa hedhi (mzito baada ya uovuleshaji na kabla ya hedhi), ujauzitoni, ukitumia vidonge vya majira au kitanzi cha homoni. Ute mzito kama maziwa mgando ukiambatana na muwasho, wekundu au kuchoma kukojoa mara nyingi ni fangasi. Bila dalili hizo, uchunguzi si lazima; lakini ute ukibadilika rangi kuwa njano-kijani au kijivu, ukiwa na harufu, au ukiambatana na maumivu ya tumbo au damu baada ya tendo – kachunguzwe.

Pozi la mwanamke kufika kileleni kirahisi

Wanawake wengi hawafiki kileleni kwa uume kuingia ukeni peke yake: tafiti kubwa zinaonyesha ni karibu wanawake 18 kati ya 100 tu wanaofika kileleni hivyo, na wengi wanahitaji kisimi kuguswa au kusuguliwa moja kwa moja. Kwa hiyo mapozi yanayosaidia zaidi ni yale yanayompa mwanamke udhibiti wa kasi, kina na pembe, au yanayoruhusu kisimi kusuguliwa – kwa mwili wa mwenza, kwa mkono wake au kwa mkono wa mwenza.

Je, mtoto mchanga anaweza kupewa maziwa ya ng’ombe?

Mtoto chini ya miezi 6 hapaswi kupewa maziwa ya ng'ombe ya kawaida: yana protini na chumvi nyingi zinazochosha figo zake, hayana madini chuma ya kutosha na huweza kusababisha damu kidogo kupotea tumboni. Chakula bora ni maziwa ya mama; asipopata, mbadala ni maziwa ya mama mwingine aliyepimwa VVU, maziwa ya benki ya maziwa, au maziwa maalumu ya watoto (formula). Maziwa ya ng'ombe yaliyorekebishwa hutumika kwa dharura tu na kwa muda mfupi, kwa maelekezo ya mtoa huduma. Kuanzia miezi 6, mtoto asiyenyonya anaweza kupewa maziwa ya wanyama yaliyochemshwa pamoja na vyakula vingine.

bottom of page