top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Kikokotoo cha BMI na Ushauri wa Mlo wa wiki

BMI (uwiano wa uzito kwa urefu) hukokotolewa kwa kugawa uzito (kilo) kwa urefu (mita) mara mbili. Kwa watu wazima (WHO): chini ya 18.5 – uzito mdogo; 18.5 hadi 24.9 – kawaida; 25 hadi 29.9 – uzito uliozidi; 30 au zaidi – unene uliopitiliza. Kikokotoo hiki hukupa kundi lako na mpango wa mlo wa wiki unaoendana nalo. BMI haitofautishi misuli na mafuta, haitumiki ujauzitoni, na kwa watoto hutumika BMI-kwa-umri; pima pia mzingo wa kiuno.

Fangasi sugu kichwani na kwenye kucha: Sababu, Uchunguzi na Matibabu

Fangasi kichwani (tinea capitis) na kwenye kucha (onychomycosis) huhitaji tiba ya kumeza ya muda mrefu, na kushindwa kupona mara nyingi hutokana na: kutumia dawa kwa muda mfupi au dozi isiyo sahihi, dawa isiyolingana na aina ya fangasi (k.m. Microsporum kichwani hujibu zaidi griseofulvin, Trichophyton hujibu terbinafine), kuambukizwa tena kutoka kwa chanuo, kofia, viatu au wanafamilia, kisukari au kinga dhaifu, au si fangasi kabisa (psoriasis, eczema, kucha kuumia). Pia kuna aina mpya za fangasi wa ngozi (T. indotineae) zinazoshindwa na terbinafine. Hatua muhimu ni uchunguzi: kipimo cha KOH kwa hadubini na culture ya ngozi/nywele/kucha kabla ya kubadili dawa. Fluconazole haipendekezwi kama dawa kuu kwa haya. Kucha hukua polepole: hata dawa ikifanya kazi, kucha mpya safi huchukua miezi 6 (vidole vya mkono) hadi 12–18 (vidole vya mguu). Mafuta ya mti wa chai na tiba nyingine za nyumbani – tafiti ndogo zimeonyesha faida kidogo; tafiti kubwa zinahitajika, na hazitibu fangasi kichwani. Dozi na muda huamuliwa na daktari wa ngozi.

Manii huishi kwa muda gani kwenye kizazi?

Mbegu za kiume (manii) zinaweza kuishi ndani ya ute wa shingo ya kizazi hadi siku 5, hasa siku za uovuleshaji ambapo ute ni mwepesi na rafiki. Kwa wastani huishi siku 2 hadi 3. Tafiti chache zimeona mbegu hadi siku 7 au zaidi kwenye shingo ya kizazi, lakini hazijathibitisha kuwa bado zinaweza kurutubisha yai. Nje ya mwili, kwenye ngozi au nguo, hufa ndani ya dakika chache zikikauka. Ndiyo maana siku za kushika mimba ni 6 – siku 5 kabla ya uovuleshaji na siku yenyewe.

Kuchubuka sehemu za siri za mwanamke: Sababu, Dalili, Uchunguzi na Tiba

Kuchubuka kwa ngozi ya nje ya uke (vulva) huambatana na kuwasha, kuungua, maumivu, nyufa ndogo au madoa mekundu/meupe. Visababishi vikuu: msuguano (nguo za kubana, jasho, mazoezi, ngono bila kilainishi au maandalizi), fangasi (sababu ya kawaida sana – wekundu, nyufa, uchafu mweupe mzito), mzio au muwasho wa sabuni, manukato, pedi zenye manukato, dawa za kuosha uke, kondomu za mpira, vilainishi au spermicide, ukavu wa uke (kunyonyesha, komahedhi, Depo), kunyoa, herpes (malengelenge madogo yanayouma), ukurutu/psoriasis, na lichen sclerosus (ngozi nyeupe nyembamba inayong'aa, kuwasha sana – inahitaji daktari wa ngozi kwa sababu huongeza kidogo hatari ya saratani isipotibiwa). Uchunguzi: kuangalia, sampuli ya fangasi/herpes, vipimo vya zinaa na sukari, na wakati mwingine sampuli ya ngozi (biopsy). Tiba hutegemea chanzo: kuacha vichochezi, kuosha kwa maji safi tu, mafuta ya kulinda ngozi (petroleum jelly), kilainishi cha maji wakati wa ngono, na dawa (za fangasi, herpes, au steroid kwa lichen sclerosus/ukurutu) kwa ushauri wa mtaalamu.

Vidonda na maumivu kwenye uume mara baada ya ngono

Vidonda au maumivu kwenye uume baada ya ngono husababishwa na mambo mawili makuu: jeraha na maambukizi. Jeraha: msuguano mkali au ukavu huchubua ngozi au kupasua kamba ya chini ya kichwa cha uume (frenulum) – huuma, hutoa damu kidogo na hupona ndani ya siku chache. Maambukizi: herpes (malengelenge madogo yanayouma, hujirudia mahali palepale), kaswende (kidonda kimoja kigumu KISICHOUMA – hupotea chenyewe lakini ugonjwa unaendelea), chancroid (kidonda laini kinachouma na mitoki kuvimba), na fangasi wa kichwa cha uume (balanitis – wekundu, kuwasha, nyufa, hasa kwa wasiotahiriwa na wenye kisukari). Pia mzio wa kondomu ya mpira au vilainishi, na mzio wa dawa (fixed drug eruption). Vidonda vya sehemu za siri huongeza hatari ya kuambukizwa VVU. Uchunguzi: uchunguzi wa daktari, kipimo cha kaswende, VVU, sampuli ya herpes, sukari. Usipake dawa kali au spiriti.

Kikokotoo cha Siku Salama na Hatari kwa Ujauzito

Kikokotoo hiki kinatumia tarehe ya kwanza ya hedhi ya mwisho na urefu wa mzunguko (siku 21 hadi 45) kuonyesha siku zenye uwezekano mkubwa (nyekundu), wa kati (njano) na mdogo (bluu) wa kupata mimba. Kinasaidia kupanga mimba. Kwa kuepuka mimba, siku 'salama' si salama kabisa – njia ya kalenda hushindwa mara nyingi, hasa kama mzunguko haubadiliki kwa usawa.

bottom of page