Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
ULY CLINIC
31 Oktoba 2026, 15:23:37

Kikokotoo cha Siku Salama na Hatari kwa Ujauzito
Jibu kwa ufupi
Jibu kwa ufupi: Kikokotoo kinakuonyesha siku zako za rutuba kwa urahisi. Ni kizuri kwa wanaotafuta mimba. Kama unataka kuepuka mimba, kitumie pamoja na kondomu au njia nyingine ya kisasa – siku za "uwezekano mdogo" bado zina hatari.
Maelezo
Jinsi ya kutumia
Weka tarehe ya kwanza ya hedhi yako ya mwisho.
Weka urefu wa mzunguko wako – siku kutoka mwanzo wa hedhi moja hadi mwanzo wa inayofuata (21 hadi 45).
Bonyeza "Hesabu Siku Salama na Hatari".
Soma matokeo: Mkubwa (nyekundu) – dirisha la rutuba; Wa kati (njano) – siku zinazokaribia; Mdogo (bluu) – uwezekano mdogo.
Kinavyohesabu
Uovuleshaji hutokea karibu siku 14 kabla ya hedhi inayofuata – soma Kukokotoa siku ya uovuleshaji.
Dirisha la rutuba ni siku 6: siku 5 kabla ya uovuleshaji na siku ya uovuleshaji, kwa sababu mbegu za kiume huishi hadi siku 5.
Mipaka ya kikokotoo
Uovuleshaji unaweza kuwahi au kuchelewa kwa msongo, ugonjwa, safari au kunyonyesha.
Njia ya kalenda pekee hushindwa kwa takriban wanawake 12 hadi 24 kati ya 100 kwa mwaka kwa matumizi ya kawaida.
Inafaa zaidi kwa mizunguko ya siku 26 hadi 32 isiyobadilika.
Haifai baada ya kujifungua, wakati wa kunyonyesha, baada ya P2 au ukiacha njia za homoni hivi karibuni.
Haikukingi magonjwa ya zinaa.
Nini cha kufanya
Unatafuta mimba: shiriki tendo kila siku 1 hadi 2 katika siku nyekundu na njano.
Unaepuka mimba: tumia kondomu au njia ya kisasa; kama unatumia kalenda, epuka tendo bila kinga siku zote za nyekundu na njano.
Andika tarehe za hedhi kwa miezi 6 kujua kama mzunguko wako unabadilika.
Ukifanya tendo bila kinga siku ya hatari – P2 ndani ya siku 3 hadi 5; soma Madhara ya kutumia P2 mara kwa mara.
Kikokotoo hakichagui jinsia ya mtoto – soma Kikokotoo cha jinsia.
Dalili za hatari
Hedhi imechelewa na maumivu makali upande mmoja wa tumbo, au kizunguzungu – mimba nje ya kizazi; hospitali mara moja.
Lini umwone daktari
Mzunguko ni mfupi kuliko siku 21, mrefu kuliko 45, au unatofautiana kwa zaidi ya siku 7 kila mwezi.
Mmetafuta mimba mwaka 1 bila mafanikio – soma Ugumba.
Hedhi imechelewa – soma Hedhi kuchelewa.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Siku za bluu ni salama kabisa?
Hapana. Uwezekano ni mdogo lakini si sifuri, hasa kama mzunguko wako hubadilika.
2. Mzunguko wangu ni siku 35, kikokotoo kitanifaa?
Ndiyo, weka 35. Uovuleshaji utakuwa karibu siku ya 21.
3. Mzunguko wangu haueleweki, nitumie kikokotoo?
Hakitakuwa sahihi. Tumia njia nyingine ya uzazi wa mpango na mwone mtoa huduma.
4. Nimefanya tendo siku nyekundu, nifanyeje kama sitaki mimba?
Tumia P2 haraka iwezekanavyo, ndani ya siku 3 hadi 5.
5. Nataka mimba, nishiriki tendo siku gani?
Kila siku 1 hadi 2 katika siku nyekundu na njano.
6. Nanyonyesha, naweza kutumia kikokotoo?
Si sahihi wakati wa kunyonyesha kwa sababu uovuleshaji haujulikani. Ongea na mtoa huduma.
7. Kikokotoo kinakinga magonjwa ya zinaa?
Hapana. Tumia kondomu.
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 19:07:17
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
Rejea za mada hii:
World Health Organization. Family Planning: A Global Handbook for Providers. 2022 update – Fertility awareness methods.
Wilcox AJ, Weinberg CR, Baird DD. Timing of sexual intercourse in relation to ovulation. N Engl J Med. 1995;333(23):1517–21.
Fritz MA, Speroff L. Clinical Gynecologic Endocrinology and Infertility. 9th ed. Philadelphia: Lippincott Williams & Wilkins; 2019.

