top of page

Miguu na Kisukari

​

Imeandikwa na daktari wa ulyclinic

​

1.Namna kisukari kinavyoathiri miguu

​

Watu wenye kisukari si rahisi kuhisi majeraha endapo yatatokea kwenye miguu kwa sababu ya kupungua kwa hisia, hivyo huwa hatarini kupata majeraha makubwa.

Kisukari huweza kusaabisha uharibufu katika mishipa ya fahamu kwa lugha nyingine uhalibifu huu hufahamika kama diabetic peripheral neuropathy, pia husababisha kupungua kwa mzunguko wa damu kwenye miguu na vikanyagio na hufahamika kwa pamoja magonjwa ya mishipa ya fahamu na mishipa ya damu kwenye miguu. Matokeo ya uharibifu huu ni kukosa hisia kwenye maeneo ya miguu dhidi ya majeraha kama malenge au kukatwa au kuchomwa na kitu. Kisukari pia hufanya majeraha haya kutopona haraka. Endapo maambukizi yatatokea kwenye majeraha haya na yasipotibiwa huweza kuleta madhara makubwa sana.

​

2. Namna ya kutunza miguu

Tiba kinga ni muhimu siku zote katika matibabu. Matunzo mazuri ya kila siku ya miguu huweza kukusaidia kuwa na miguu yenye afya njema

  1. Unda kikapu chako chenye vifaa kwa ajii ya utunzaji wa miguu yako, kinatakiwa kiwe na vitu vifuatavyo. Kikatio cha kucha, mafuta ya losheni na kioo kidogo cha kushika mkononi(Ukiwa na vitu vyako hivi basi fuata mambo yafuatayo kila siku

  2. Osha miguu yako kwenye maji ya uvuguvugu (yasiwe ya moto), kwa kutumia sabuni isiyo kali, usiloweke miguu yako kwani huweza kusababisha miguu kukauka.

  3. Kausha miguu yako kwa uangalifu, usisahau kukausha katikati ya vidole.

  4. Tizama na chunguza miguu yako sehemu zote, kati ya kidole kimoja na kingine,ili kuhakikisha hakuna michaniko au jeraha au kucha ndefu, malenge n.k tumia kioo cha mkononi ili kuona kwenye kikanyagio au mwombe mtu mwingine akuangalie sehemu hizo kama unatatizo.

  5. Osha vidonda au mikwaruzo kwa kutumia sababuni na maji, kisha funika kwa kitambaa kikavu na maalumu kwa ajiri ya ngozi.

  6. Kata kucha zako vema, kwa kutumia kikata kucha, ni vema usitumie wembe kwani huweza kukata kucha vibaya pamoja na ngozi na kukusababishia kidonda.  Usikate kucha kuwa fupi sana.

  7. Paka mafuta ya losheni nzuri kwenye miguu na kikanyagio. Futa losheni ya ziada ambayo haijafyonzwa, usipake losheni kati ya kidole na kidole kwa sababu majimaji ya losheni yakizidi huweza kusababisha kutokea kwa maambukizi.

  8. Vaa soksi safi na zinazokutosha vema kila siku, ikiwezekana vaa soksi nyeupe ili hata kama ukitobolewa au kukatwa na kitu soksi hiyo itavia damu, hivyo utajua mapema kuna shida imetokea.

​

Ushauri wa msingi

​

Mambo ya kufanya

​

Vaa viatu vinavyokupasa kuvaa, vinatakiwa vikutoshe vema, vyenye kisigino kifupi au visivyo na kisigino (ili kuzuia kuanguka) na visiwe vya kubana au kukufinya. Nunua viatu hivi kwenye maduka yenye wataalamu wa viatu au wasiliana na daktari wako wa kisukari ili akupe ushauri na mahali pa kupata viatu maalumu.

  • Nunua viatu wakati wa mchana- kwa sababu miguu yako huvimba kiasi wakati huo na utapata namba nzuri ya kiatu ambacho hakitakubana wakati miguu ikivimba kiasi.

  • Vaa soksi wakati wa usiku kama unahisi baridi miguuni

  • Nyanyua juu miguu yako unapokuwa umekaa kwenye kiti kwa mda mrefu

  • Chezesha vidole vyako na chezesha magoti na miguu huku na huko kwa dakika kadhaa mara nyingi mchana ili kusaidia mzunguko wa damu kwenye miguu na vikanyagio.

  • Fanya mazoezi kwa kuzingatia ratiba ili kuimarisha mzunguko wa damu.

  • Kagua miguu yako kila siku haswa angalia joto la ngozi kwa kushika mguu, na utofauti kati ya mguu mmoja na mwingine.

​

Marufuku

​

  • Kutumia madawa ya kujinunulia mwenyewe kwenye famasi ili kutibu maoteo ya vinyama kwenye miguu(wasiliana na daktari wako)

  • Kuvaa vitu vya kubana kwenye miguu, kama soksi za kubana sana au viatu vyenye kisigino kirefu

  • Kutembea miguu wazi(bila kuvaa viatu) hata kama ni ndani ya nyumba. Nunua viatu vya kutumia ndani tu na viwe na sifa ile kama ilivyotajwa kwenye mambo ya kufanya.

  • Kunawa na maji ya moto kwenye miguu au kuweka kitu cha moto kwenye miguu

  • Kuvuta sigara, kuvuta sigara hupunguza mzunguko wa damu na uwezo wa mwili kuponesha vidonda na huongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya kukatwa viungo vya mwili(kama miguu)

 

Wasiliana na daktari wako siku zote kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatu yoyote

​

Pata ushauri na tiba kutoka kwa daktari wa ULY clinic kwa kubonyeza hapa au piga namba za simu chini ya tovuti hii.

​

Imeboreshwa 12.03.2020

​

Rejea​

Utangulizi
Kutunza miguu
ushauri
Marufuku
bottom of page