top of page

Mwandishi:

Mhariri:

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

19 Juni 2021, 07:58:58

Kutapika nyongo
shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.

Kutapika nyongo

Nyongo ni majimaji yanayozalishwa na ini kisha kuhifadhiwa kwenye kibofu cha nyongo kinapatikana chini kidogo ya ini. Maji ya nyongo huwa na rangi yake ya kijani inayoelekea njano kwa kuwa huwa na chumvi, bilirubini, kolestro, madini yenye chaji na maji. Mtu alapo chakula nyongo hutolewa kuingia tumboni ili kusaidia umeng’enyaji wa vyakula vya mafuta.


Kama unatapika majimaji ya kijani yanayoelekea kuwa njano ni dhahiri inaweza kuwa ni nyongo.

Kuna visababishi kadhaa vya kutapika nyongo, vinaweza kuwa visababishi vya kawaida au vile vya kuhitaji matibabu ya dharura.


Matibabu ya kutapika nyongo hulenga haswa kisababishi, tiba huhusisha mabadiliko ya kimaisha, kutumia dawa au upasuaji.


Visababishi


Visababishi vya kutapika nyongo vinaweza kuwa


  • Kutapika wakati tumbo halina kitu

  • Kunywa pombe nyingi

  • Kula sumu ya chakula

  • Homa ya asubuhi

  • Kuziba kwa utumbo

  • Ugonjwa wa kucheua nyongo


Vipimo


Wakati mwingine vipimo vinaweza visihitajike endapo kisabaishi kinafahamika. Utakapofika hospitali kwa tatizo la kutapika nyongo, miongoni mwa vipimo vifuatavyo vianaweza shauriwa vifanyike kulingana na dalili ulizonazo ili kusaidia tambua au thibitisha kisababishi;


  • Ultrasound ya tumbo

  • CT scan ya tumbo

  • Enema ya bariamu au hewa

  • X- ray ya tumbo

  • Vipimo vingine kama kiasi cha madini mwilini n.k


Matibabu


Matibabu ya kutapika nyongo hutegemea kisababishi cha tatizo


Endapo kisababishi ni kunywa pombe nyingi au kula sumu ya chakula utatakiwa kupelekwa hospitali ili ukaongezewe maji na madini kupitia mishipa ya damu.


Endapo una ugonjwa wa kucheua nyongo, utapewa matibabu ya dawa ili kusaidia usicheue nyongo. Endapo matibabu ya dawa hayatafanya kazi, basi utashauriwa na kufanyiwa tiba ya upasuaji. Maelezo zaidi ya ‘kucheua nyongo’ na tiba yake yameelezewa kwenye sehemu nyingine katika tovuti hii ya uly clinic.


Endapo kisababishi ni kuziba kwa utumbo kutokana na sababu yoyote,kama henia, kujinyonga kwa utumbo, saratani ya matumbo, daivetikulaitiz n.k utapatiwa matibabu ya dawa au upasuaji kulingana na kisababishi. Makala ya kujinyonga kwa utumbo na matibabu yake vimeelezewa zaidi sehemu nyingine ya tovuti hii ya ulyclinic.


Kinga


Utapunguza hatari ya kutapika nyongo kwa kufanya mabadiliko yafuatayo;


  • Acha kuvuta tumbaku au sigara ili kujiondoa kwenye hatari ya saratani ya utumbo mpana

  • Kula mlo kamili wenye matunda na mboga za majani kwa wingi ili kujikinga na hatari ya saratani ya tumbo na magonjwa ya kuziba kwa utumbo

  • Tumia njia njema ya kunyanyua vitu vizito ili kujiking ana hatari ya kupata henia

  • Usichanganye pombe na usinywe zaidi ya kiwango kinacho shauriwa kiafya


Wakati gani uonane na daktari haraka?


Endapo unatapika nyongo na kupata dalili zifuatazo unapaswa kuonana na daktari haraka;


  • Homa

  • Kupumua kwa shida

  • Kupungua uzito

  • Kutopata haja kubwa kusiko kawaida

  • Kutapika kusikoisha

  • Kutojamba

  • Kuvimba kwa tumbo

  • Matapishi ya rangi nyekundu au rangi ya unga wa kahawa(nyeusi)

  • Maumivu makali ya tumbo

  • Maumivu ya kifua


Wapi unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu kutapika nyongo?

Pata taarifa zaidi kuhusu kutapika kwa kubofya hapa


Majina mbadala ya kutapika nyongo

Baadhi ya watu hutumia majina yafuatayo kumaanisha kutapika nyongo ni;


  • Kucheua nyongo

  • Kutapika matapishi ya kijani

  • Kutapika matapishi ya njano

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeboreshwa, 

8 Oktoba 2021, 04:53:06

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

​

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada

1. Bowel obstruction. health.harvard.edu/diseases-and-conditions/bowel-obstruction. Imechukuliwa 19.06.2021

2. Mayo Clinic Staff. Bile reflux. mayoclinic.org/diseases-conditions/bile-reflux/basics/definition/con-20025548. Imechukuliwa 19.06.2021

3. Mayo Clinic Staff. Intestinal obstruction: symptoms and causes.
mayoclinic.org/diseases-conditions/intestinal-obstruction/symptoms-causes/dxc-20168463. Imechukuliwa 19.06.2021

4. Nausea and vomiting in adults. nhs.uk/conditions/vomiting-adults/Pages/Introduction.aspx. Imechukuliwa 19.06.2021

5. Small bowel obstruction. ddc.musc.edu/public/diseases/small-intestine/small-bowel-obstruction.html. Imechukuliwa 19.06.2021

6. Treating colorectal cancer. cancer.org/cancer/colon-rectal-cancer/treating.html. Imechukuliwa 19.06.2021

bottom of page