Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dkt Benjamin L, MD
Dkt. Peter A, MD
1 Novemba 2026, 18:09:02

Maumivu ya tumbo chini ya kitovu
Maumivu ya tumbo chini ya kitovu ni maumivu katika sehemu ya chini ya tumbo, katikati, upande wa kulia au wa kushoto. Chanzo kinaweza kuwa utumbo, kama choo kigumu, gesi, kidole tumbo au utumbo nyeti; njia ya mkojo, kama UTI au mawe; au, kwa wanawake, via vya uzazi, kama hedhi, PID, mimba nje ya kizazi au sisti kwenye ovari. Kwa wanaume, maumivu ya korodani yanaweza pia kuhisiwa hapa.
Aina ya maumivu, mahali yalipo, yalivyoanza, muda yanayodumu na dalili zinazoambatana husaidia kujua chanzo. Maumivu makali ya ghafla, homa, kutapika kusikoisha, tumbo kuvimba au kuwa gumu, damu, kuzimia, au maumivu pamoja na hedhi kuchelewa yanahitaji uchunguzi wa haraka.
Eneo hili ni sehemu ya chini ya tumbo kati ya kitovu na mfupa wa kinena, pamoja na pande za kulia na kushoto. Hapa kuna utumbo mdogo na mpana, kidole tumbo upande wa kulia, kibofu cha mkojo, mirija ya mkojo na, kwa mwanamke, kizazi, mirija ya uzazi na ovari.
Baadhi ya visababishi ni vya kawaida na hupungua vyenyewe, lakini vingine vinahitaji uchunguzi wa haraka kwa sababu vinaweza kuleta madhara makubwa matibabu yakichelewa. Maumivu yanaweza kuwa ya kuchoma, kukata, kubana, kuchomachoma, kuja kwa vipindi au kuwa ya kudumu, na kila aina hutoa dokezo kuhusu chanzo.
Kwa maumivu ya juu ya kitovu soma Maumivu ya tumbo la juu ya kitovu.
Aina na jinsi inavyojitokeza
Mahali maumivu yalipo linaweza kusaidia kuelekeza uchunguzi, lakini haliwezi kuthibitisha ugonjwa peke yake.
Chini kulia: inaweza kuhusishwa na appendicitis, matatizo ya utumbo, njia ya mkojo au baadhi ya matatizo ya viungo vya uzazi.
Chini kushoto: inaweza kuhusishwa na diverticulitis, matatizo ya utumbo, kufunga choo, njia ya mkojo au viungo vya uzazi.
Katikati chini ya kitovu: inaweza kuhusishwa na kibofu cha mkojo, utumbo, kufunga choo au matatizo ya viungo vya fupanyonga.
Kwa sababu magonjwa mbalimbali yanaweza kusababisha maumivu katika eneo moja, uchunguzi wa daktari ni muhimu hasa maumivu yanapokuwa makali au yanaendelea.
Aina ya maumivu
Maumivu ya kunyonga yanayokuja kwa mawimbi: mara nyingi utumbo au mrija wa mkojo.
Maumivu ya kila mwezi: hedhi, ovulesheni au endometriosisi.
Maumivu ya ghafla makali sana: kidole tumbo, sisti iliyojisokota au kupasuka, mimba nje ya kizazi, korodani kujisokota.
Maumivu ya muda mrefu yanayojirudia: utumbo nyeti, PID sugu, endometriosisi, faibroidi.
Visababishi
1. Kufunga choo
Kufunga choo(kufunga kwa haja kubwa) kunaweza kusababisha maumivu au kubana sehemu ya chini ya tumbo, hasa ikiwa kinyesi kimekaa kwa muda mrefu kwenye utumbo mpana. Mtu anaweza pia kupata tumbo kujaa, gesi na kujisikia haja kubwa lakini akashindwa kujisaidia vizuri.
2. Ujazo wa gesi tumboni
Gesi nyingi katika utumbo zinaweza kusababisha maumivu ya kubana ambayo huja na kuondoka na wakati mwingine huhama kutoka sehemu moja ya tumbo kwenda nyingine. Mara nyingi maumivu hupungua baada ya kutoa gesi au kupata haja kubwa.
3. Maambukizi ya njia ya mkojo
Maambukizi ya kibofu yanaweza kusababisha maumivu chini ya kitovu, hasa katikati ya tumbo. Mara nyingi huambatana na kuungua wakati wa kukojoa, kukojoa mara kwa mara, kuhisi haja ya kukojoa haraka au mkojo kuwa na harufu isiyo ya kawaida.
4. Mawe kwenye njia ya mkojo
Jiwe linaposafiri kwenye ureta linaweza kusababisha maumivu makali yanayokuja kwa mawimbi na yanaweza kuanzia ubavuni au mgongoni na kuelekea chini ya tumbo au kinena. Mkojo unaweza pia kuwa na damu.
5. Uvimbe au maambukizi ya kidole tumbo
Appendicitis mara nyingi huanza kama maumivu karibu na kitovu na baadaye yanaweza kuhamia upande wa chini kulia wa tumbo. Maumivu yanaweza kuongezeka wakati wa kutembea, kukohoa au kufanya harakati, na yanaweza kuambatana na kichefuchefu, kutapika au homa.
6. Sindromu ya matumbo korofi (IBS)
IBS inaweza kusababisha maumivu ya tumbo yanayorudia pamoja na mabadiliko ya namna ya kupata haja kubwa, kama kuharisha, kufunga choo au kubadilishana hali hizo. Kujaa gesi na tumbo kujaa pia ni kawaida. Hata hivyo, dalili mpya au zinazoambatana na kupungua uzito, damu kwenye kinyesi au kuharisha usiku zinahitaji uchunguzi zaidi.
7. Ugonjwa wa uchochezi wa utumbo
Magonjwa kama Crohn na kolaitisi ya vidonda yanaweza kusababisha maumivu ya tumbo yanayorudia, kuharisha na wakati mwingine damu kwenye kinyesi. Mtu anaweza pia kupungua uzito au kupata uchovu kutokana na ugonjwa wa muda mrefu.
8. Uvimbe kinga kwenye pochi za utumbo mpana (Divatikulaitisi)
Divatikulaitisi hutokea vifuko vidogo vilivyopo kwenye ukuta wa utumbo mpana vinapovimba au kuambukizwa. Mara nyingi husababisha maumivu upande wa chini kushoto wa tumbo, pamoja na homa na mabadiliko ya haja kubwa.
9. Matatizo ya viungo vya uzazi
Kwa mtu mwenye viungo vya uzazi vya kike, maumivu ya chini ya tumbo yanaweza kutokana na sababu kama sisti ya ovari, kujinyongorota kwa ovari, endometriosisi au maambukizi ya viungo vya uzazi (PID). Baadhi ya hali hizi huhitaji uchunguzi wa haraka, hasa maumivu yanapoanza ghafla na kuwa makali.
Kwa mtu mwenye viungo vya uzazi vya kiume, maumivu ya chini ya tumbo yanaweza wakati mwingine kuhusishwa na tatizo la mfumo wa uzazi au mkojo, na maumivu kutoka kwenye korodani yanaweza pia kuhisiwa katika sehemu ya chini ya tumbo.
Visababishi vingine kwa wanawake
Maumivu ya hedhi na maumivu ya ovulesheni katikati ya mzunguko.
Mimba nje ya kizazi: dharura.
Mimba kuharibika.
Sisti kwenye ovari, hasa ikipasuka au kujisokota.
Faibroidi na endometriosisi.
Visababishi vingine kwa wanaume
Korodani kujisokota: maumivu yanaweza kuhisiwa tumbo la chini; ni dharura.
Tezi dume kuvimba kwa maambukizi.
Kibofu kujaa kwa kushindwa kukojoa, mara nyingi kwa wazee wenye tezi dume kubwa.
Ngiri ya kinena, hasa ikikwama.
Dalili zinazoambatana
Kuungua ukikojoa, kukojoa mara kwa mara: UTI.
Damu kwenye mkojo na maumivu kwenda kinena: mawe.
Homa na uchafu ukeni wenye harufu: PID.
Hedhi kuchelewa, damu kidogo ukeni, kizunguzungu: mimba nje ya kizazi.
Kuharisha, mara nyingine na damu: maambukizi au vidonda vya utumbo.
Choo kigumu, tumbo kujaa: choo kigumu au utumbo nyeti.
Kutapika, kushindwa kujisaidia na kutoa gesi: utumbo kuziba.
Homa, kukosa hamu ya kula, maumivu kuzidi ukitembea au kukohoa: kidole tumbo.
Dalili za hatari
Si kila maumivu ya tumbo ni dharura, lakini maumivu makali sana, yanayoanza ghafla au yanayoongezeka haraka yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito. Baadhi ya hali zinazoweza kusababisha maumivu makali ni:
Kuziba kwa utumbo, hasa ikiwa kuna tumbo kuvimba, kutapika na kushindwa kutoa kinyesi au gesi
Kutoboka kwa utumbo au kiungo kingine cha ndani ya tumbo
Ischemia ya utumbo, ambapo sehemu ya utumbo hupata damu kidogo au hukosa damu
Uvimbe kinga kwenye kidole tumbo(Homa ya kidole tumbo)
Diverticulitis kali
Kuvimba kwa Kongosho (michomokinga ya kongosho)
Kujinyongorota kwa ovari
Maambukizi makali ndani ya tumbo na peritonaitisi
Kupasuka kwa aneurysm ya aota ya tumbo, hasa kwa mtu mwenye hatari zake
Tatizo la moyo ambalo linaweza kujionesha kama maumivu ya tumbo badala ya maumivu ya kifua.
Nenda hospitali au kituo cha huduma za dharura ikiwa maumivu:
Yameanza ghafla na ni makali sana
Yanaendelea kuongezeka au hayapungui
Yanaambatana na homa kali
Yanaambatana na kutapika kusikokoma
Yanaambatana na damu kwenye kinyesi au mkojo
Tumbo limevimba sana au kuwa gumu
Maumivu yanaongezeka unapogusa au kusogeza tumbo
Unapata kizunguzungu, kuzimia, udhaifu mkubwa au dalili za kushuka kwa shinikizo la damu
Huwezi kutoa kinyesi au gesi pamoja na tumbo kujaa na kuvimba
Una maumivu makali yanayoambatana na kutokwa damu ukeni ikiwa una viungo vya uzazi vya kike
Kwa maumivu ya muda mrefu, kupungua uzito bila sababu, damu kwenye kinyesi, homa inayorudia, maumivu yanayokuamsha usingizini au kutapika mara kwa mara pia ni sababu za kufanyiwa uchunguzi badala ya kuendelea kujitibu nyumbani.
Kwa mwanaume: maumivu ya ghafla ya korodani pamoja na tumbo la chini.
Maumivu ukiwa na mimba, au hedhi imechelewa.
Vipimo
Hakuna kipimo kimoja kinachofaa kwa kila mtu mwenye maumivu ya tumbo. Daktari huanza kwa kuuliza historia ya maumivu na kufanya uchunguzi wa mwili, kisha huamua vipimo kulingana na dalili.
Vipimo vinaweza kujumuisha:
Kipimo cha mkojo kutafuta UTI au damu inayoweza kuhusishwa na mawe.
Picha kamili ya damu (CBC) kutafuta dalili za maambukizi au upungufu wa damu.
Vipimo vingine vya damu kulingana na kinachoshukiwa.
Ultrasound, hasa katika kutathmini njia ya mkojo au viungo vya fupanyonga.
CT scan katika baadhi ya maumivu makali ya chini ya tumbo, hasa inaposhukiwa appendicitis, diverticulitis, kuziba kwa utumbo au tatizo jingine la ndani ya tumbo.
Kwa mwanamke aliye katika umri wa kupata ujauzito, kipimo cha ujauzito ni sehemu muhimu ya uchunguzi wa maumivu makali ya tumbo, hata kama anatumia njia ya uzazi wa mpango, kwa sababu matokeo yake yanaweza kubadilisha kabisa aina ya vipimo na matibabu yanayohitajika.
Uchunguzi wa nyonga na kipimo cha uchafu ukeni: PID na magonjwa ya zinaa.
Kipimo cha kinyesi: maambukizi, minyoo, damu iliyojificha.
Kolonoskopi: kwa damu kwenye kinyesi, mabadiliko ya choo ya muda mrefu au mtu wa miaka 45 au zaidi.
Matibabu na huduma ya nyumbani
Matibabu hutegemea chanzo (STG 2026)
UTI na PID: antibiotiki kwa mujibu wa mwongozo; kwa PID mwenzi pia anatibiwa.
Kidole tumbo, mimba nje ya kizazi, sisti iliyojisokota, utumbo kuziba: upasuaji au matibabu ya hospitali.
Mawe madogo ya mrija wa mkojo: maji ya kutosha na dawa za maumivu; mengi hutoka yenyewe.
Choo kigumu na utumbo nyeti: nyuzilishe, maji, mazoezi, na dawa za kulainisha choo kwa muda mfupi.
Maumivu ya hedhi: dawa za maumivu, kitambaa cha maji ya uvuguvugu, na kutibu chanzo kama kipo.
Huduma ya nyumbani
Kunywa maji ya kutosha, glasi 8 au zaidi kwa siku.
Weka kitambaa cha maji ya uvuguvugu chini ya tumbo kwa maumivu ya hedhi au ya kunyonga.
Kula chakula chenye nyuzilishe kama maharage, mboga, matunda na nafaka zisizokobolewa.
Usisubiri nyumbani maumivu yanayozidi kila saa, wala kujitibu kwa dawa za minyoo au antibiotiki bila kipimo.
Kinga
Kunywa maji ya kutosha na usibane mkojo kwa muda mrefu.
Ngono salama na kondomu ili kuzuia PID na magonjwa ya zinaa.
Lishe yenye nyuzilishe na mazoezi ili kuzuia choo kigumu.
Usafi wa chakula na maji.
Hudhuria kliniki mapema ukipata mimba.
Lini umwone daktari
Maumivu yanayodumu zaidi ya siku 1 hadi 2, au yanayojirudia kila mwezi kwa ukali.
Uchafu ukeni usio wa kawaida au maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Mabadiliko ya choo yanayodumu zaidi ya wiki 3.
Maumivu pamoja na kupungua uzito, damu kwenye kinyesi, homa inayorudia au maumivu yanayokuamsha usingizini.
Maumivu kwa mjamzito.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Maumivu chini ya kitovu yanaweza kuwa kwa sababu ya gesi tu?
Gesi inaweza kusababisha maumivu ya kubana au kuchomachoma chini ya tumbo, hasa ikiwa yanaambatana na tumbo kujaa na kujisikia gesi. Mara nyingi maumivu hubadilika-badilika na yanaweza kupungua baada ya kutoa gesi au kupata haja kubwa. Hata hivyo, si salama kuhitimisha kuwa kila maumivu ni gesi. Maumivu makali, mapya au yanayoendelea yanapaswa kuchunguzwa kwa sababu appendicitis, kuziba kwa utumbo na matatizo mengine yanaweza kuanza kwa maumivu yanayofanana na ya gesi.
2. Kwa nini tumbo la chini linauma baada ya kufanya tendo la ndoa?
Maumivu baada ya tendo la ndoa yanaweza kutokana na msuguano, kukaza kwa misuli ya fupanyonga au shinikizo kwenye viungo vya ndani. Kwa baadhi ya watu, maumivu yanaweza pia kuhusishwa na matatizo kama endometriosisi, PID au uvimbe/sisti kwenye ovari. Ikiwa maumivu yanarudia kila baada ya tendo la ndoa, ni makali, yanaambatana na uchafu usio wa kawaida ukeni, homa au damu baada ya tendo la ndoa, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.
3. Maumivu chini ya kitovu yanaweza kusababishwa na kibofu hata kama sioni damu kwenye mkojo?
UTI inaweza kusababisha maumivu chini ya kitovu bila damu kuonekana kwa macho. Dalili nyingine muhimu ni kuungua wakati wa kukojoa, kukojoa mara nyingi au kuhisi haja ya kukojoa mara kwa mara. Mawe kwenye njia ya mkojo yanaweza pia kusababisha maumivu makali na damu kwenye mkojo, lakini si kila mtu ataona damu kwa macho. Kipimo cha mkojo kinaweza kusaidia katika kutafuta dalili za maambukizi au damu.
4. Kwa nini maumivu chini ya kitovu yanaweza kwenda mpaka mgongoni?
Baadhi ya viungo vya tumbo na njia ya mkojo vina uhusiano wa mishipa unaoweza kufanya maumivu yahisikike sehemu nyingine. Kwa mfano, mawe kwenye njia ya mkojo yanaweza kuleta maumivu yanayosafiri kutoka ubavuni au mgongoni kuelekea chini ya tumbo na kinena. Maumivu ya tumbo yanayosambaa mgongoni, hasa yakifuatana na kutapika au hali mbaya kwa ujumla, yanaweza pia kuhitaji uchunguzi wa haraka kwa sababu baadhi ya magonjwa makubwa ya tumbo yanaweza kufanya hivyo.
5. Je, maumivu chini ya kitovu yanaweza kuwa kutokana na minyoo?
Baadhi ya maambukizi ya vimelea vya utumbo yanaweza kusababisha maumivu ya tumbo, kuharisha au mabadiliko mengine ya mfumo wa chakula. Hata hivyo, maumivu chini ya kitovu pekee hayawezi kuthibitisha kwamba mtu ana minyoo. Ikiwa kuna dalili zinazoashiria maambukizi ya vimelea, daktari anaweza kuamua kama kipimo cha kinyesi au uchunguzi mwingine unahitajika. Ni bora kutambua chanzo kabla ya kutumia dawa za minyoo mara kwa mara.
6. Kwa nini maumivu ya chini ya tumbo yanatokea kabla au wakati wa hedhi?
Mabadiliko yanayohusiana na hedhi yanaweza kusababisha misuli ya kizazi kukaza na kuleta maumivu chini ya tumbo. Kwa baadhi ya wanawake, maumivu huwa ya kawaida na huanza muda mfupi kabla au mwanzoni mwa hedhi. Hata hivyo, maumivu yanayokuwa makali sana, mapya, yanazidi kadiri miezi inavyopita au yanaathiri sana shughuli za kila siku yanaweza kuhitaji uchunguzi wa sababu nyingine kama endometriosis au tatizo la ovari.
7. Je, maumivu chini ya kitovu yanaweza kuwa ya misuli?
Misuli ya ukuta wa tumbo inaweza kuumia baada ya kubeba vitu vizito, kufanya mazoezi makali, kukohoa sana au kupata jeraha. Maumivu ya aina hii mara nyingi huongezeka unapokaza misuli au kufanya harakati fulani. Hata hivyo, maumivu yanayoongezeka unapokaza misuli hayaondoi kabisa uwezekano wa tatizo la ndani ya tumbo. Ikiwa maumivu ni mapya na makali au yanaambatana na dalili nyingine, uchunguzi bado unaweza kuhitajika.
8. Maumivu chini ya kitovu yanayoanza usiku yanaashiria ugonjwa gani?
Muda ambao maumivu hutokea unaweza kutoa dokezo, lakini maumivu ya usiku pekee hayawezi kutambua ugonjwa fulani. Gesi, matatizo ya utumbo, mawe kwenye njia ya mkojo na hali nyingine zinaweza kufanya maumivu yaonekane zaidi wakati wa usiku. Kama maumivu yanakuamsha mara kwa mara kutoka usingizini, yanaongezeka au yanaambatana na kupungua uzito, homa, damu kwenye kinyesi au kutapika, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi.
9. Je, ni salama kutumia dawa ya maumivu kabla sijajua chanzo?
Si kila dawa ya maumivu inafaa kwa kila mtu, kwa sababu uchaguzi wa dawa hutegemea umri, magonjwa mengine, dawa anazotumia na sababu inayoshukiwa. Kwa maumivu makali, jambo muhimu zaidi ni kutafuta chanzo badala ya kuficha dalili na kuendelea na matibabu ya nyumbani. Hospitalini, dawa za kutuliza maumivu zinaweza kutolewa wakati uchunguzi unaendelea; tafiti zimeonyesha hazifichi dalili kiasi cha kuzuia daktari kugundua chanzo. Nyumbani, epuka kunywa dawa nyingi za maumivu na kusubiri maumivu makali yanayoongezeka.
10. Nina maumivu chini ya kitovu lakini vipimo vya awali viko kawaida; bado nahitaji kuendelea na uchunguzi?
Inaweza kuwa hivyo. Baadhi ya magonjwa hayawezi kuthibitishwa au kuondolewa kwa kipimo kimoja. Daktari huunganisha historia ya dalili, uchunguzi wa mwili na vipimo vya damu, mkojo au picha kulingana na hali. Ikiwa maumivu yanaendelea, yanarudia mara kwa mara au yanaongezeka licha ya vipimo vya awali kuwa kawaida, ni muhimu kurudi kwa daktari kwa tathmini upya. Matokeo ya kawaida ya kipimo kimoja hayamaanishi kila chanzo cha maumivu kimeondolewa.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
30 Oktoba 2026, 12:50:14
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada hii:
Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026.
Cartwright SL, Knudson MP. Evaluation of acute abdominal pain in adults. Am Fam Physician. 2008;77(7):971–8.
American College of Radiology. ACR Appropriateness Criteria: right lower quadrant pain; left lower quadrant pain; acute pelvic pain in the reproductive age group. Reston: ACR; 2023.
Manterola C, Vial M, Moraga J, Astudillo P. Analgesia in patients with acute abdominal pain. Cochrane Database Syst Rev. 2011;(1):CD005660.
World Health Organization. Sexually transmitted and other reproductive tract infections: a guide to essential practice. Geneva: WHO; 2005.

