Mwandishi:
Mhhariri
Imeboreshwa:
Dkt. Salome A, MD
Dkt. Benjamin L, MD
29 Oktoba 2026, 21:46:40
Kiharusi (stroke)
Maelezo ya jumla
Kiharusi, au stroke, ni hali ya ghafla ambapo sehemu ya ubongo inakosa damu yenye oksijeni na seli zake kuanza kufa ndani ya dakika chache. Kuna aina kuu mbili:
Kiharusi cha kuziba mshipa (ischaemic stroke) – mshipa wa damu wa ubongo huzibwa na damu iliyoganda au mafuta yaliyojikusanya. Ni takribani 8 kati ya 10 ya viharusi duniani.
Kiharusi cha kuvuja damu (haemorrhagic stroke) – mshipa wa damu hupasuka na damu kuvuja ndani au kuzunguka ubongo, mara nyingi kwa sababu ya shinikizo la juu la damu lisilodhibitiwa. Ni cha kawaida zaidi Afrika kuliko nchi za Magharibi.
Dalili zinazokuja na kupotea zenyewe ndani ya muda mfupi huitwa kiharusi cha mpito (TIA) – ni onyo kwamba kiharusi kikubwa kinaweza kufuata.
Kiharusi ni dharura. Matibabu ya mapema yanaweza kuokoa sehemu kubwa ya ubongo na kupunguza ulemavu.

Takwimu za ugonjwa
Kiharusi ni chanzo cha pili cha vifo duniani na chanzo kikuu cha ulemavu kwa watu wazima. Kila mwaka takribani watu milioni 12 hupata kiharusi na karibu milioni 7 hufariki, wengi wao wakiwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Tafiti za Tanzania (mf. Hai na Dar es Salaam) zimeonyesha viwango vya kiharusi vilivyo sawa au juu kuliko nchi tajiri, na kwa umri mdogo zaidi – wagonjwa wengi wakiwa chini ya miaka 60. Sababu kuu ni shinikizo la juu la damu ambalo halijagunduliwa au halitibiwi ipasavyo.
Visababishi na vihatarishi
Vihatarishi vinavyoweza kudhibitiwa
Shinikizo la juu la damu – kihatarishi kikubwa kuliko vyote.
Kisukari.
Lehemu (cholesterol) nyingi kwenye damu.
Uvutaji sigara.
Unywaji pombe kupita kiasi.
Unene uliokithiri na kutofanya mazoezi.
Mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio (atrial fibrillation) na magonjwa mengine ya moyo.
Ugonjwa wa seli mundu.
VVU, hasa visipotibiwa.
Lishe yenye chumvi nyingi.
Vihatarishi visivyodhibitika
Umri mkubwa.
Historia ya kiharusi au TIA.
Historia ya kiharusi kwenye familia.
Jinsi ugonjwa unavyotokea
Ubongo hutumia takribani asilimia 20 ya oksijeni ya mwili lakini hauwezi kuhifadhi akiba. Mshipa ukiziba, seli zilizo katikati ya eneo hilo hufa ndani ya dakika chache. Seli zinazozunguka eneo hilo (penumbra) hupata damu kidogo kutoka mishipa jirani na zinaweza kuokolewa kwa saa chache kama mtiririko wa damu utarejeshwa haraka – ndiyo maana muda ni muhimu sana.
Katika kiharusi cha kuvuja damu, damu iliyovuja hukandamiza ubongo na kuongeza shinikizo ndani ya fuvu. Kila sehemu ya ubongo huongoza kazi fulani, hivyo dalili hutegemea eneo lililoathirika: upande wa kushoto wa ubongo huongoza upande wa kulia wa mwili na, kwa watu wengi, uwezo wa kuongea.
Dalili na viashiria
Dalili huja ghafla. Njia rahisi ya kukumbuka ni U-M-S-M:
U – Uso: upande mmoja wa uso kulegea au kupinda; mdomo kuegemea upande mmoja anapotabasamu.
M – Mkono (na mguu): udhaifu au ganzi upande mmoja; kushindwa kuinua mikono yote miwili sawasawa.
S – Sauti: kushindwa kuongea, kuongea kwa kukwama au maneno yasiyoeleweka, kushindwa kuelewa.
M – Muda: ukiona dalili hizi, piga simu au mpeleke hospitali mara moja, na kumbuka saa dalili zilipoanza.
Dalili nyingine
Kupoteza uwezo wa kuona jicho moja au nusu ya kuona.
Kizunguzungu kikali, kuyumba au kushindwa kutembea.
Maumivu makali ya ghafla ya kichwa – "maumivu makubwa kuliko yote maishani" (hasa kiharusi cha kuvuja damu).
Kutapika, kusinzia au kupoteza fahamu.
Kushindwa kumeza.
Vipimo
CT scan ya kichwa – kipimo cha kwanza na cha haraka; hutofautisha kiharusi cha kuziba na cha kuvuja damu. Hii ni muhimu kwa sababu matibabu yao ni tofauti.
MRI – huonyesha zaidi, pale inapopatikana.
Sukari ya damu – kupima mara moja, kwa sababu sukari kushuka huiga kiharusi.
Shinikizo la damu, kipimo kamili cha damu, figo, lehemu na vipimo vya kuganda kwa damu.
ECG na Echo ya moyo – kutafuta mapigo yasiyo na mpangilio na chanzo cha damu iliyoganda.
Ultrasound ya mishipa ya shingo (carotid Doppler).
Kipimo cha VVU, na kwa vijana, vipimo vya seli mundu na tabia ya damu kuganda.
Matibabu
Matibabu hufanyika hospitalini, kwa mujibu wa mwongozo wa Tanzania (STG 2026):
Kiharusi cha kuziba mshipa
Dawa ya kuyeyusha damu iliyoganda (thrombolysis) – kwa wagonjwa wanaostahili waliofika ndani ya saa 4.5 tangu dalili kuanza, katika hospitali zenye uwezo huu.
Kuondoa damu iliyoganda kwa kifaa maalum (thrombectomy) – katika vituo vichache vya kibingwa.
Aspirini – huanzishwa baada ya CT kuthibitisha hakuna damu iliyovuja.
Kudhibiti sukari, homa na oksijeni; shinikizo la damu hushushwa taratibu tu kwa ushauri wa daktari.
Kiharusi cha kuvuja damu
Kushusha shinikizo la juu la damu kwa uangalifu.
Kurekebisha matatizo ya kuganda kwa damu.
Upasuaji wa kuondoa damu au kupunguza shinikizo kwa baadhi ya wagonjwa.
Huduma kwa wote
Kuchunguza uwezo wa kumeza kabla ya kula au kunywa – kuzuia nimonia ya kuvuta.
Kugeuzwa kitandani kila saa 2 kuzuia vidonda.
Mazoezi ya viungo (fiziotherapia), mazoezi ya kuongea na ya kazi za kila siku – kuanza mapema.
Kuzuia kiharusi kingine: dawa za shinikizo la damu, dawa za lehemu (statins), aspirini au dawa nyingine za kuzuia damu kuganda kulingana na chanzo, na kudhibiti kisukari.
Matatizo yanayoweza kutokea
Kupooza upande mmoja wa mwili.
Kushindwa kuongea au kuelewa (aphasia).
Shida ya kumeza na nimonia ya kuvuta.
Damu kuganda kwenye miguu.
Vidonda vya kulalia.
Degedege.
Sonona, kubadilika tabia na kusahau.
Kushindwa kujizuia mkojo.
Kiharusi kingine.
Kifo.
Kinga
Pima shinikizo la damu angalau mara moja kwa mwaka; ukiwa na shinikizo la juu, tumia dawa kila siku hata ukijisikia mzima.
Punguza chumvi – chini ya kijiko kidogo kimoja kwa siku.
Acha sigara na punguza pombe.
Fanya mazoezi angalau dakika 30 siku nyingi za wiki.
Kula matunda, mboga, nafaka zisizokobolewa; punguza mafuta mengi na sukari.
Dhibiti kisukari na lehemu.
Tibu mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio.
Ukipata dalili za kiharusi cha mpito, nenda hospitali siku hiyo hiyo.
Lini umwone daktari
Mara moja (dharura): uso kupinda, mkono au mguu kulegea, kushindwa kuongea, kupoteza kuona, kuyumba ghafla, au maumivu makali ya ghafla ya kichwa – hata kama dalili zimepotea.
Usimpe mgonjwa chakula, maji wala dawa kwa mdomo kabla ya kuchunguzwa – anaweza kupaliwa.
Baada ya kiharusi: kuhudhuria kliniki ya kufuatilia, mazoezi na dawa za kuzuia kiharusi kingine.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Kijana anaweza kupata kiharusi?
Anaweza. Ingawa ni kawaida zaidi kwa wazee, vijana hupata kiharusi kwa sababu ya shinikizo la juu la damu, seli mundu, VVU, magonjwa ya moyo, dawa za kulevya au tabia ya damu kuganda.
2. Kiharusi kinaweza kutokea bila kupoteza fahamu?
Kinaweza, na mara nyingi hutokea hivyo. Wagonjwa wengi wako macho lakini wana udhaifu upande mmoja au shida ya kuongea.
3. Nimpe mgonjwa aspirini nikiona dalili za kiharusi?
Usimpe kabla ya CT scan. Kama ni kiharusi cha kuvuja damu, aspirini inaweza kuzidisha damu kuvuja. Mpeleke hospitali haraka.
4. Mgonjwa wa kiharusi atapona kabisa?
Inategemea ukubwa na eneo la kiharusi na kasi ya matibabu. Wengi hupata nafuu kubwa ndani ya miezi 3–6 ya kwanza kwa mazoezi, na nafuu huweza kuendelea hadi mwaka mmoja au zaidi.
5. Mazoezi ya viungo yanaanza lini?
Mapema iwezekanavyo, mara mgonjwa anapotengemaa – mara nyingi ndani ya siku chache. Mazoezi ya mapema hupunguza ulemavu.
6. Kwa nini shinikizo la damu halishushwi haraka mara baada ya kiharusi?
Katika kiharusi cha kuziba mshipa, shinikizo la juu kidogo husaidia damu kufika kwenye sehemu ya ubongo inayookolewa. Daktari hulishusha taratibu kwa kiwango maalum.
7. Dawa za kuzuia kiharusi kingine zinatumika kwa muda gani?
Kwa kawaida maisha yote. Kuacha dawa za shinikizo la damu, lehemu au za kuzuia damu kuganda huongeza hatari ya kiharusi kingine.
8. Kiharusi kinarithiwa?
Si moja kwa moja, lakini vihatarishi kama shinikizo la juu la damu na kisukari hurithiwa. Historia ya familia ni sababu ya kupima mara kwa mara.
9. Mgonjwa wa kiharusi anaweza kula nini?
Mwanzoni, apimwe uwezo wa kumeza. Baadaye ale chakula chenye chumvi kidogo, mboga, matunda, protini za kutosha na mafuta kidogo. Wenye shida ya kumeza hupewa vyakula laini.
10. Kiharusi na kupooza uso (Bell's palsy) vinatofautianaje?
Bell's palsy huathiri uso tu, ikiwemo paji la uso, bila udhaifu wa mkono au mguu. Kiharusi mara nyingi huacha paji la uso likifanya kazi na huambatana na dalili nyingine. Kama kuna shaka yoyote, ichukulie kama kiharusi na nenda hospitali.
Imeandikwa:
29 Oktoba 2026, 18:08:45
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba, au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii
Rejea za mada hii:
Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026. Sections: Initial management of acute ischemic stroke; Prevention of atherosclerotic ischaemic heart disease and stroke.
World Stroke Organization. Global stroke fact sheet 2025. Geneva: WSO; 2025.
Walker RW, Rolfe M, Kelly PJ, et al. Mortality and recovery after stroke in the Gambia and Tanzania. Stroke. 2003;34(7):1604–1609.
Powers WJ, Rabinstein AA, Ackerson T, et al. Guidelines for the early management of patients with acute ischemic stroke: 2019 update. Stroke. 2019;50(12):e344–e418.

