Magonjwa na saratani mbalimbali
Sehemu hii utasoma kuhusu hali na magonjwa mbalimbali

Fangasi kwenye damu
Ni maambukizi makubwa ya fangasi kwenye damu yanayoweza kusambaa hadi kwenye ogani muhimu na kusababisha sepsisi. Dalili zinaweza kujumuisha homa, kutetemeka, udhaifu mkubwa, mapigo ya moyo kwenda haraka, kupumua kwa kasi, kuchanganyikiwa au shinikizo la damu kushuka; hivyo kutambua mapema, kuthibitisha kwa vipimo vya damu na kuanza matibabu maalumu ya kuua fangasi ni muhimu.

Kuvunjika kwa mfupa: Watoto wadogo
Fupakola, mifupa ya mkono wa mbele, fupapaja na mifupa ya mguu ni miongoni mwa mifupa inayoweza kuvunjika mara nyingi kutokana na kuanguka, kucheza au ajali. Ikiwa kuna shaka ya kuvunjika, mtoto anapaswa kupelekwa hospitali kwa uchunguzi hata kama dalili si kali, na anahitaji huduma ya haraka zaidi ikiwa kuna mwonekano wa kupinda, kidonda kinachoonyesha mfupa, maumivu makali, uvimbe unaoongezeka, ganzi, vidole kuwa vya bluu au baridi, kutokwa damu nyingi au kushindwa kabisa kutumia kiungo.

Uvimbe maji kwenye Ovari (Sisti)
Ni uvimbe unaoweza kuwa na majimaji au tishu na huwa si saratani. Sisti ndogo, rahisi, yenye majimaji pekee, isiyo na dalili na yenye muonekano wa kawaida kwenye ultrasound mara nyingi hufuatiliwa tu na huweza kutoweka yenyewe. Sisti kubwa, inayoendelea kukua au kuwepo, yenye muonekano changamano/sehemu ngumu, inayosababisha dalili kubwa au yenye viashiria vya saratani inaweza kuhitaji uchunguzi zaidi na wakati mwingine upasuaji kulingana na tathmini ya daktari.

Folikulaitisi: Uvimbekinga wa vinyeleo
Ni kuvimba kwa vinyweleo ambako kunaweza kusababisha vipele vidogo, kuwasha, maumivu au usaha, na huweza kuchochewa na bakteria, fangasi, jasho, msuguano au kunyoa. Kutambua chanzo ni muhimu kwa matibabu sahihi, hasa ikiwa vipele vinajirudia, vinaacha makovu au haviponi baada ya hatua za kawaida za kutunza ngozi.
