top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

Imeboreshwa:

10 Februari 2026, 08:37:53

PEP: Matumizi, Madhara na Tahadhari kwa Mtumiaji

PEP: Matumizi, Madhara na Tahadhari kwa Mtumiaji

Swali la msingi

“Daktari, nilifanya ngono bila kinga jana usiku na sijui hali ya mwenzi wangu. Nimechelewa kuanza dawa, je PEP inaweza kunisaidia na nifanye nini nikianza kuitumia?”


Majibu

PEP ni kifupi cha Post-Exposure Prophylaxis, yaani kinga baada ya mtu kukutana na hatari ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU). Dawa hizi hutolewa kwa dharura ili kuzuia virusi visiweze kuingia na kujijenga mwilini. Ni njia ya dharura inayotumika baada ya tukio la hatari, na tofauti na PrEP (Pre-Exposure Prophylaxis) inayotumika kabla ya tukio kama kinga ya muda mrefu.


PEP inafanyaje kazi?

PEP ni mchanganyiko wa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs). Dawa hizi hufanya kazi kwa kuzuia virusi visizaliane mwanzoni mwa maambukizi, kabla havijashikamana na seli za mwili.

  • Ikiwa itaanza mapema (ndani ya masaa 72), PEP hupunguza uwezekano wa kuambukizwa kwa kiwango kikubwa.

  • Ikiwa itachelewa kuanza baada ya masaa 72, virusi vinaweza kuwa tayari vimeingia kwenye seli za mwili, hivyo dawa hazitakuwa na ufanisi wa kuzuia maambukizi.


Ni nani anaweza kupewa PEP?

PEP inapendekezwa kwa mtu yeyote aliye katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU, ikiwemo:

  • Mtu aliyefanya ngono bila kinga na mwenye hali ya VVU isiyojulikana au anajulikana kuwa na VVU.

  • Wale waliopata jeraha la sindano kazini (mfano kwa wahudumu wa afya).

  • Mtu aliyelawitiwa au kulazimishwa kufanya tendo la ngono bila kinga.

  • Kushirikiana vifaa vyenye damu kama sindano.


Jinsi ya kutumia PEP

  1. Anza mapema iwezekanavyo – ndani ya saa 2 hadi 72 baada ya tukio.

  2. Dawa huchukuliwa kwa siku 28 mfululizo bila kuruka dozi.

  3. Usimamishe bila ushauri wa daktari, hata kama unajisikia vizuri.

  4. Ni lazima ichukuliwe sambamba na ushauri nasaha na kufuata ratiba za vipimo vya VVU.


Madhara

Wagonjwa wanaotumia PEP wanaweza kupata madhara madogo ya muda mfupi kama:

  • Kichefuchefu na kutapika.

  • Kizunguzungu.

  • Uchovu.

  • Kuharisha.

Madhara haya mara nyingi huisha baada ya siku chache. Ni muhimu kumjulisha daktari kama madhara ni makubwa. Kusoma kuhusu madhara zaidi ingia kwenye makala ya maudhi ya PEP.


Madhara ya muda mrefu yameandikwa kwenye makala ya madhara ya kutumia PEP


Vipimo na Ufuatiliaji

Mtu anayepokea PEP anatakiwa kufanyiwa vipimo vya VVU:

  • Kabla ya kuanza PEP (baseline test).

  • Baada ya wiki 4.

  • Baada ya wiki 12 (au miezi 3) kuhakikisha hali.

Wakati wa ufuatiliaji, daktari pia hutathmini iwapo kuendelea na PrEP baada ya PEP ni muhimu, hasa kwa mtu aliye katika hatari endelevu ya kuambukizwa.


Tofauti kuu za PEP na PrEP

  • PEP: Inatolewa baada ya tukio la hatari, kwa siku 28 tu.

  • PrEP: Inatolewa kabla ya tukio la hatari, na ni ya muda mrefu kwa mtu aliye kwenye hatari ya mara kwa mara.


Tahadhari muhimu kwa mtumiaji

  • Anza mapema: Usichelewe zaidi ya masaa 72 baada ya tukio la hatari.

  • Usiache dawa bila ushauri: Kukatisha dawa kabla ya siku 28 hupunguza ufanisi.

  • Endelea kutumia kondomu: PEP haibadilishi kinga nyingine wakati wa matumizi.

  • Shirikiana na daktari: Mweleze historia yako ya kiafya, dawa nyingine unazotumia, au kama una ujauzito/unyevu (unyonyeshaji).

  • Fikiria kuhusu PrEP: Ikiwa unaendelea kuwa kwenye hatari ya mara kwa mara, daktari anaweza kupendekeza kuanza PrEP baada ya PEP.


Hitimisho

PEP ni ulinzi wa dharura wenye ufanisi mkubwa iwapo itatumika mapema na kwa usahihi. Hata hivyo, haina nafasi ya kuzuia maambukizi ikiwa imecheleweshwa zaidi ya saa 72. Ili kupata manufaa kamili ya PEP, zingatia: kuanza mapema, kufuata ratiba ya dawa, kutumia kinga nyingine kama kondomu, na kufanya vipimo vya mara kwa mara.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara

1. Je, PEP inaweza kuzuia VVU kwa asilimia 100?

Hapana. PEP hupunguza hatari kwa kiasi kikubwa, lakini haijahakikishwa kuzuia maambukizi kwa asilimia 100.

2. Nini kitatokea nikichelewa kuanza PEP baada ya saa 72?

PEP haitakuwa na ufanisi tena. Ni muhimu kuanza ndani ya muda wa dharura (masaa 72).

3. Je, ninaweza kushiriki ngono bila kondomu nikiwa kwenye PEP?

Hapana. PEP haitoi kinga ya haraka kabisa. Endelea kutumia kondomu wakati wote.

4. Je, ninaweza kunywa pombe nikiwa natumia PEP?

Kunywa pombe hakufanyi PEP kushindwa, lakini kunaweza kuongeza madhara kama kichefuchefu na uchovu. Inashauriwa kupunguza au kuepuka.

5. Je, PEP inafaa kwa wanawake wajawazito au wanaonyonyesha?

Ndiyo. Kuna dawa salama zinazoweza kutolewa chini ya ushauri wa daktari.

6. Je, nikiishia dozi au nikisahau siku moja, nifanye nini?

Kunywa dozi mara tu unapokumbuka. Usichukue dozi mara mbili kwa wakati mmoja.

7. Je, PEP inaweza kusababisha utasa au kuathiri uzazi?

Hapana. PEP haina madhara ya kudumu kwa uwezo wa kupata watoto.

8. Je, nikiwa nimetumia PEP mara moja, naweza kuitumia tena baadaye nikikumbana na tukio jingine?

Ndiyo, PEP inaweza kutolewa tena, lakini inapendekezwa kuzungumza na daktari kuhusu kuanza PrEP iwapo uko kwenye hatari mara kwa mara.

9. Je, kuna madhara makubwa ya PEP?

Madhara makubwa ni nadra. Mara nyingi ni dalili ndogo kama kichefuchefu, kuharisha au uchovu. Soma madhara katika makala ya ULY CLINIC ya madhara ya PEP

10. Baada ya kumaliza PEP, nifanye nini?

Fanya vipimo vya VVU kulingana na ratiba (wiki 4 na wiki 12). Daktari anaweza kupendekeza kuanza PrEP ikiwa hatari bado ipo.

11. Wiki mbili zimepita nikiwa natumia PrEP nikidhani ni PEP, kisha nimeanza PEP sasa. Je, PEP bado inaweza kufanya kazi au niache kutumia?

PEP ni dawa ya dharura inayozuia maambukizi ya VVU ikiwa itaanza ndani ya masaa 72 (siku 3) baada ya tukio la hatari. Ukichelewa zaidi ya hapo, PEP inapoteza ufanisi wake kwa sababu virusi vinaweza kuanza kuingia na kujijenga mwilini.

Kwa hali yako:

  • Kwa kuwa ulianza dawa sahihi (PEP) baada ya wiki mbili, tayari umepitisha muda wa dharura, hivyo PEP haitafanya kazi kwa ufanisi wa kuzuia maambukizi.

  • PrEP uliyokuwa unatumia awali haiwezi kufanya kazi ya dharura kama PEP, kwa sababu inahitaji kutumika kwa muda kabla ya tukio ili kulinda mwili.

  • Hivyo basi, kuendelea na PEP sasa hakutakupa kinga kamili.


Cha kufanya sasa:

  • Endelea na ushauri wa daktari aliyeanza kukuangalia.

  • Pima VVU kulingana na ratiba ya kitabibu (kwa mfano: mara moja sasa, kisha baada ya wiki 4, na tena baada ya wiki 12).

  • Kama bado uko kwenye hatari ya kupata maambukizi, unaweza kuendelea na PrEP kwa usahihi baada ya kumaliza tathmini na vipimo.

Kwa kifupi, PEP sasa haitaweza kufanya kazi kama kinga, lakini daktari wako atakushauri kuhusu vipimo na iwapo ni sahihi kuendelea na PrEP ili ujilinde dhidi ya maambukizi yajayo.

12. Je, nikisahau kunywa dozi ya PEP nifanye nini?

Ukisahau dozi, kunywa mara tu unapoikumbuka ikiwa haijapita zaidi ya saa 24.


Usinywe dozi mbili kwa wakati mmoja.


Ukikosa dozi mara nyingi, ufanisi wa PEP hupungua, kwa hiyo hakikisha unafuatilia saa zako au weka alama ya kukumbusha kwenye simu.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

7 Septemba 2025, 03:39:12

Rejea za mada hii

  1. World Health Organization. Consolidated guidelines on HIV prevention, testing, treatment, service delivery and monitoring: recommendations for a public health approach. Geneva: WHO; 2021.

  2. Centers for Disease Control and Prevention. Updated guidelines for antiretroviral postexposure prophylaxis after sexual, injection drug use, or other nonoccupational exposure to HIV — United States, 2016. MMWR Recomm Rep. 2016;65(17):1–20.

  3. Kuhar DT, Henderson DK, Struble KA, Heneine W, Thomas V, Cheever LW, et al. Updated US Public Health Service guidelines for the management of occupational exposures to HIV and recommendations for postexposure prophylaxis. Infect Control Hosp Epidemiol. 2013;34(9):875–92.

  4. Ford N, Shubber Z, Calmy A, Irvine C, Rapparini C, Ajose O, et al. Safety, efficacy, and adherence of post-exposure prophylaxis for HIV infection in children and adolescents: a systematic review. AIDS. 2014;28(18):2741–52.

  5. Cardo DM, Culver DH, Ciesielski CA, Srivastava PU, Marcus R, Abiteboul D, et al. A case–control study of HIV seroconversion in health care workers after percutaneous exposure. N Engl J Med. 1997;337(21):1485–90.

  6. Mayer KH, Oldenburg CE, Novak DS, Elsesser SA, Krakower DS, Mimiaga MJ. Early adopters: correlates of HIV chemoprophylaxis use in recent online samples of US men who have sex with men. AIDS Behav. 2016;20(7):1489–98.

  7. Jain S, Mayer KH. Practical guidance for nonoccupational postexposure prophylaxis to prevent HIV infection: an editorial review. AIDS. 2014;28(10):1545–54.

bottom of page