Vidokezo vya Afya

Kunyonyesha ipasavyo husinyaza kizazi haraka
Kizazi hurejea kwenye umbo lake la asili mara baada ya kujifungua kwa mama anayeyonyesha kama inavyotakiwa, hii ni kwa sababu, unyonyeshaji huchochea uzalishaji kwa wingi wa homoni oxytocin inayofanya kazi ya kuchochea utoaji wa maziwa na kusinyaza kizazi kirejee kwenye umbo lake la asili.

Kunyonyesha ni njia mojawapo ya uzazi wa mpango
Mzunguko wa hedhi huchelewa rejea kwa mama endapo anayenyonyesha kama inavyotakiwa katika miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua, hii hupelekea kutopata mimba katika kipindi hiki na hivyo huwa njia mojawapo ya uzazi wa mpango. Kumbuka uzalishaji wa mayai kipindi hiki huweza endelea kwa baadhi ya wanawake na hivyo kuwa hatarini kupata ujauzito.

Kuongezewa damu
Ni tendo la kitiba la kuongeza ujazo wa damu iliyotolewa kwa mtu mwenye afya kwenda kwa muhitaji kupitia mishipa ya damu. Sababu zinazopelekea kuongezewa damu mara nyingi hutokana na ajali, upasuaji na magonjwa yanayomaliza damu. Kuna njia zingine za kuongeza damu, hata hivyo si rahisi kutumika kama mbadala wa kuongezewa damu.

Kupasuka chupa ya uzazi kabla ya wakati
Kupasuka kwa chupa ya uzazi kabla ya kutimiza wiki 37 kamili za ujauzito hujulikana kama 'kupasuka kwa chupa ya uzazi kabla ya wakati'. Tatizo hili hutokea kwa ujauzito 3 kati ya 100, kuwahi pata matibabu sahihi hukinga madhara ya kujifungua mtoto njiti, maambukizi ndani ya mfuko wa uzazi na magonjwa kwa mtoto.

