top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Utofauti wa HIV-1 na HIV-2

Kuna aina mbili za VVU. VVU-1 kimeenea duniani kote, ikiwemo Tanzania, na husababisha UKIMWI kwa kasi zaidi. VVU-2 hupatikana zaidi Afrika Magharibi, huambukiza kwa kiwango kidogo zaidi na huharibu kinga taratibu zaidi. Tofauti muhimu ya matibabu: VVU-2 hakitibiki kwa efavirenz wala nevirapine, lakini hutibika kwa dawa zenye dolutegravir.

Dalili zinazoambatana na kuota meno

Utafiti uliofuatilia watoto kila siku (Macknin 2000) ulionyesha kuota meno huambatana na dalili ndogo kwa siku chache: kujing'ata, udenda, kukuna fizi, kunyonya vidole, kutotulia, kukosa usingizi, kukuna masikio, kukosa hamu ya kula, harara usoni na joto kupanda kidogo. Kuota meno HAKULETI homa kali (zaidi ya 38.5°C), kuharisha, kutapika wala kikohozi – hizo ni dalili za ugonjwa unaohitaji uchunguzi.

Kunyonyesha ipasavyo husinyaza kizazi haraka

Mtoto anaponyonya, mwili wa mama hutoa homoni ya oxytocin inayotoa maziwa na kusinyaza kizazi. Kwa hiyo kunyonyesha mara kwa mara husaidia kizazi kurudi kwenye ukubwa wake (kwa kawaida ndani ya wiki 6) na hupunguza damu baada ya kujifungua. Maumivu ya tumbo kama ya hedhi wakati wa kunyonyesha siku za mwanzo ni ishara ya kizazi kusinyaa.

Matumizi ya vidonge vya majira

Vidonge vya majira ni vya aina mbili: vidonge vya mchanganyiko vyenye estrojeni na projestini, na vidonge vya homoni moja vyenye projestini pekee, ambavyo hufaa kwa mama anayenyonyesha au mwanamke asiyeweza kutumia estrojeni. Huzuia mimba kwa kuzuia ovari kutoa yai na kufanya ute wa shingo ya kizazi kuwa mzito ili mbegu zisipite. Vikitumika kwa usahihi kila siku, chini ya mwanamke 1 kati ya 100 hupata mimba kwa mwaka.

Mfungo katika Afya

Mfungo – kuacha kula kwa saa fulani, kwa sababu za imani (k.m. Ramadhani, Kwaresma) au za afya (mfungo wa vipindi/intermittent fasting, k.m. kula ndani ya saa 8 kwa siku) – unaweza kuwa salama na wenye faida kwa watu wengi wenye afya. Ushahidi: mfungo wa vipindi husaidia kupunguza uzito, na tafiti zinaonyesha matokeo yanafanana na kupunguza kalori kwa njia ya kawaida (Rynders 2019); huweza kuboresha kidogo sukari, insulini na presha kwa baadhi; mwili hutumia mafuta zaidi kama nishati wakati wa mfungo. Madai kwamba mfungo "huondoa sumu mwilini" hayana ushahidi – ini na figo ndio huondoa taka mwilini. Faida hupotea kama wakati wa kula mtu anakula vyakula vya mafuta na sukari nyingi kupita kiasi. Fanya mfungo wa kiafya: kunywa maji ya kutosha wakati unaoruhusiwa, futari/daku yenye protini, nafaka nzima, mboga na matunda, epuka kula kupita kiasi, punguza sukari na vyakula vya kukaanga, na lala vya kutosha. Tahadhari – ushauri wa daktari kabla: wenye kisukari (hasa wanaotumia insulini au sulfonylurea – hatari ya sukari kushuka; mwongozo wa IDF-DAR), wajawazito na wanaonyonyesha, watoto, wenye magonjwa ya figo, moyo, vidonda vya tumbo, historia ya matatizo ya kula, na wenye uzito mdogo.

Mahudhurio mabovu ya kliniki

Kutohudhuria kliniki ya mama mjamzito ipasavyo huhatarisha afya ya mama na mtoto aliye tumboni, kwa sababu matatizo kama presha ya ujauzito, upungufu wa damu, VVU, kaswende, malaria na mtoto kukaa vibaya hugunduliwa mapema kliniki. Anza kliniki mapema – kabla ya wiki 12 – na hudhuria kila unapopangiwa; WHO inashauri angalau mahudhurio 8 kabla ya kujifungua.

bottom of page