top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Tabia ya kukufanya upate usingizi kwa wakati

Kulala kwa wakati hujengwa na tabia za kila siku: kulala na kuamka saa zile zile, chumba cha giza, kimya na kisicho na joto kali, kuweka simu mbali na kitanda, kuepuka mlo mkubwa, kahawa, chai kali na pombe saa 3 kabla ya kulala, na kufanya mazoezi au kazi mchana. Ukiwa kitandani bila usingizi zaidi ya dakika 20, amka ufanye jambo tulivu kisha urudi – kitanda kiwe cha usingizi tu. Tabia hizi ni sehemu ya tiba ya mazungumzo ya kukosa usingizi (CBT-I).

Kushusha homa kwa vichanga na watu wazima

Homa ni joto la mwili 38°C au zaidi – ishara ya kinga kupambana na maambukizi. Tanzania, kila homa inahitaji kipimo cha malaria. Mtoto chini ya miezi 3 mwenye 38°C au zaidi – hospitali mara moja, hata kama anaonekana mzima. Kwa watoto wakubwa na watu wazima: pumzika, kunywa maji mengi (endelea kunyonyesha), vaa nguo nyepesi, na tumia paracetamol au ibuprofen kwa dozi ya umri/uzito kama homa inaleta usumbufu – lengo ni faraja, si kushusha namba. Ibuprofen kwa watoto miezi 3+ wanaokunywa vizuri tu; usimpe mtoto aspirin. Usimwogeshe mtoto maji baridi au kumfunika sana; kufuta kwa maji ya uvuguvugu kunaweza kuongeza faraja. Homa zaidi ya siku 2 kwa mtoto au 3 kwa mtu mzima, au dalili za hatari – kituoni. Makala hii haitoi dozi; fuata maelekezo ya mfamasia au kwenye kifungashio.

Njia za dawa kuingia mwilini

Dawa huingia mwilini kwa njia mbalimbali, na kila njia ina sababu yake. Mdomo – kumeza, chini ya ulimi au kusukutua – ndiyo rahisi na ya kawaida, lakini chakula, asidi ya tumbo na ini huweza kupunguza kiasi kinachofika damuni. Sindano (chini ya ngozi, ndani ya ngozi, kwenye msuli, kwenye mshipa) hufanya kazi haraka na kwa uhakika, lakini zinahitaji mtaalamu, usafi na huleta maumivu. Matone (macho, pua, masikio) na krimu za ngozi hutibu sehemu husika moja kwa moja. Njia ya haja kubwa (suppository) husaidia anayetapika, mtoto au asiyeweza kumeza. Ukeni – kwa maambukizi ya uke na baadhi ya dawa za homoni. Kuvuta (inhaler, nebulizer) – dawa za pumu hufika mapafuni moja kwa moja kwa dozi ndogo. Vibandiko vya ngozi hutoa dawa taratibu kwa saa au siku. Usibadilishe njia bila ushauri: kidonge cha ukeni si cha kumeza, matone ya sikio si ya jicho, na dawa za kuvuta lazima zitumike kwa mbinu sahihi.

Kutolewa ovari mwanzoni mwa ujauzito

Miezi ya mwanzo ya ujauzito, homoni ya progesterone inayoshikilia mimba hutengenezwa na korpasi luteamu kwenye ovari. Kati ya wiki 7 na 10 kondo la nyuma huchukua kazi hiyo. Ovari zote mbili (au ovari yenye korpasi luteamu) zikiondolewa kabla ya hapo, mimba huweza kuharibika – hivyo madaktari humpa mama progesterone hadi wiki 10 hadi 12. Baada ya hapo mimba huendelea bila ovari.

Magonjwa yanaoathiri uke, humwathiri kichanga

Baadhi ya maambukizi ya uke na shingo ya kizazi ujauzitoni yanaweza kumdhuru mtoto: bakteria vaginosis na trikomona huongeza hatari ya kuzaa njiti na chupa kupasuka mapema; kisonono na klamidia huweza kumwambukiza mtoto wakati wa kuzaliwa (macho kutoa usaha, nimonia); malengelenge (herpes) ya mara ya kwanza karibu na kujifungua ni hatari sana kwa kichanga; na bakteria wa GBS husababisha maambukizi ya damu kwa kichanga. Kupima na kutibu mapema ujauzitoni humkinga mtoto.

Maziwa ya ng'ombe kwa mtoto chini ya miezi 12

Maziwa ya mama ndiyo bora hadi miaka 2 au zaidi. Mtoto chini ya miezi 6 asipewe maziwa ya ng'ombe kabisa – kama hanyonyi, apewe formula ya watoto. Kwa mtoto wa miezi 6 hadi 11 asiyenyonya, mwongozo wa WHO (2023) unaruhusu maziwa ya wanyama yaliyochemshwa (yenye mafuta kamili) au formula, pamoja na vyakula vyenye madini chuma. Maziwa ya ng'ombe mengi kupita kiasi huleta upungufu wa damu.

bottom of page