Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
ULY CLINIC
Imeboreshwa:
27 Novemba 2026, 07:24:13

Lishe kamili kwa mtoto wa miezi 11 kwa ukuaji wa kawaida
Mtoto wa miezi 11 anahitaji milo 3 hadi 4 kwa siku na vitafunwa 1 hadi 2, kila mlo ukiwa nusu hadi robo tatu ya kikombe cha mililita 250, huku akiendelea kunyonya. Chakula kiwe cha familia kilichokatwa vipande vidogo laini, chenye protini, wanga, mafuta, vitamini na madini, na kila siku kiwe na chakula cha asili ya wanyama, mikunde, mboga za majani na matunda.
Mtoto wa miezi 11 anahitaji lishe yenye mchanganyiko wa vyakula vya protini, wanga, mafuta, vitamini na madini, sambamba na kunyonyeshwa maziwa ya mama. Lishe hii humsaidia kukua kwa afya, kuimarisha ubongo na kuzuia magonjwa.
Huu ni mwezi wa mpito kuelekea chakula cha familia. Makala hii inaeleza malengo ya lishe, ratiba ya mlo wa wiki kwa vyakula vinavyopatikana Tanzania, maelekezo ya kuandaa chakula, kujilisha, usafi na dalili za hatari.
Kwa ufupi
Jambo | Mtoto wa miezi 11 |
Kunyonya | Endelea mara 3 hadi 5 au zaidi kwa siku; usiachishe ghafla |
Milo mikuu | Mara 3 hadi 4 kwa siku |
Vitafunwa | Mara 1 hadi 2 kwa siku |
Kiasi kwa mlo | Nusu hadi robo tatu ya kikombe cha mililita 250 |
Muundo | Chakula cha familia kilichokatwa vipande vidogo laini |
Kunywa | Maji safi kwa kikombe; epuka soda na juisi za viwandani |
Lengo la lishe kwa mtoto wa miezi 11
Kuendeleza ukuaji wa mwili na viungo.
Kuimarisha uwezo wa akili na kujifunza.
Kuongeza kinga ya mwili dhidi ya maambukizi.
Kuepusha tatizo la utapiamlo na uzito mdogo.
Kumwandaa kula chakula cha familia akiwa na mwaka mmoja.
Ratiba kamili ya mlo wa wiki: mtoto wa miezi 11
Siku | Asubuhi (7–8am) | Saa 10 Jioni (10am) | Mchana (1–2pm) | Saa 4 Jioni (4pm) | Usiku (7–8pm) |
Jumatatu | Uji wa lishe + kijiko cha mafuta ya alizeti | Parachichi lililopondwa | Wali laini + samaki + mchicha | Papai lililopondwa | Ugali laini + maharage + mboga |
Jumanne | Uji wa ulezi + siagi ya karanga | Ndizi mbivu iliyopondwa | Wali laini + kuku/mchuzi wa nyama + mboga | Viazi vitamu vilivyopondwa | Uji mzito wa lishe + maziwa ya ng’ombe |
Jumatano | Uji wa mahindi + nazi | Papai au embe | Ndizi za kupika + dengu + mchicha | Parachichi au tunda lolote laini | Ugali laini + yai + mboga |
Alhamisi | Uji wa mtama + karanga | Parachichi au papai | Wali laini + dagaa waliopondwa + matembele | Uji mwepesi | Viazi mviringo + mboga za majani |
Ijumaa | Uji wa mchanganyiko wa nafaka + siagi ya karanga | Ndizi mbivu iliyopondwa | Ugali laini + maharage + kisamvu | Papai au embe | Wali laini + samaki |
Jumamosi | Uji wa lishe + kijiko cha mafuta ya nazi | Parachichi | Wali laini + yai + mboga za majani | Uji mwepesi | Ndizi ya kupika + maharage laini |
Jumapili | Uji wa mahindi + siagi ya karanga | Papai au parachichi | Wali laini + dagaa waliopondwa + mchicha | Ndizi mbivu au viazi vilivyopondwa | Ugali laini + mboga ya majani + maziwa ya ng’ombe kidogo |
Ratiba hii ni mfano. Badilisha vyakula kulingana na msimu na kinachopatikana nyumbani, ukihakikisha kila siku kuna nafaka au mizizi, mikunde, mboga ya majani, tunda, na chakula cha asili ya wanyama. Nyonyesha kati ya milo na kabla ya kulala.
Maelekezo muhimu ya kuandaa chakula
Uji wa lishe: changanya unga wa nafaka kama mahindi, mtama, ulezi au mchele, na ongeza mafuta ya alizeti, ufuta au nazi kwa nishati zaidi.
Mafuta bora: ongeza kijiko kimoja kidogo cha mafuta bora kwenye milo.
Mboga za majani: safisha na pika hadi ziive; zikate vipande vidogo au zipondwe.
Samaki na dagaa: ondoa kwa makini mifupa midogo.
Mayai: chemsha hadi yai liive vizuri; nusu hadi yai zima kwa siku linafaa.
Nyama: kuku au nyama isiyo na mafuta mengi ipikwe vizuri, isagwe au ikatwe vipande vidogo, na ilishwe kwa kiasi kidogo.
Matunda: toa matunda laini au yaliyopondwa kama papai, parachichi, embe na ndizi mbivu.
Vyakula muhimu kwa umri wa miezi 11
Aina ya Lishe | Vyanzo vya Asili Vinavyopatikana Tanzania |
Wanga (Nishati) | Wali, ugali wa dona, viazi mviringo, viazi vitamu, ndizi za kupika |
Protini | Samaki wadogo/dagaa, kuku, nyama, mayai, maharage, dengu, njegere |
Mafuta bora | Mafuta ya alizeti, ufuta, nazi, siagi ya karanga, parachichi |
Matunda | Papai, embe, parachichi, papai, ndizi mbivu |
Mboga za majani | Mchicha, kisamvu, matembele, majani ya maboga |
Maziwa | Maziwa ya mama, maziwa ya ng’ombe yaliyochemshwa kidogo |
Vyakula vya asili ya wanyama, kama dagaa, maini, nyama na mayai, vina madini chuma na zinki ambavyo mtoto wa umri huu anahitaji sana. Matunda yenye vitamini C husaidia mwili kufyonza madini chuma kutoka kwenye maharage na mboga za majani.
Kujilisha: kijiko na kikombe
Mtoto wa miezi 11 hupenda kufanya mambo mwenyewe. Mpe kijiko chake ajaribu kujilisha huku wewe ukimsaidia kwa kijiko kingine, na mpe vipande laini vya kushika. Atamwaga chakula mwanzoni, na hilo ni sehemu ya kujifunza.
Mfundishe kunywa kwa kikombe kidogo wazi. Kama anatumia chupa ya kunyonyea, anza kupunguza taratibu; chupa ni vigumu kusafisha na huongeza hatari ya kuharisha na kuoza kwa meno.
Vidokezo kwa wazazi
Mlo upondwe au kukatwa kulingana na uwezo wa mtoto kutafuna.
Mtoto aketi wima anapopewa chakula.
Tumia vyombo safi na mikono safi.
Usimlishe mtoto kwa haraka; mpe muda wa kula.
Epuka chumvi, sukari na vyakula vya viwandani.
Endelea kunyonyesha maziwa ya mama mara 3 hadi 5 au zaidi kwa siku.
Mpe chakula chenye rangi na ladha tofauti ili kuhamasisha kula.
Kula naye pamoja na familia; mtoto hujifunza kwa kuiga.
Je, niachishe kunyonyesha mtoto akikaribia mwaka mmoja?
Hakuna sababu ya kuachisha kunyonyesha mtoto akifikisha mwaka mmoja. Inashauriwa kuendelea kunyonyesha pamoja na chakula cha nyongeza hadi miaka 2 au zaidi. Maziwa ya mama yanaendelea kumpa protini bora, mafuta, vitamini na kinga. Kama mama anaamua kuachisha, afanye taratibu kwa wiki kadhaa, na mtoto apate maziwa mengine na mlo mmoja wa ziada.
Mtoto akiwa mgonjwa
Mtoto mgonjwa aendelee kunyonya mara nyingi zaidi na apewe chakula laini anachokipenda kidogo kidogo. Baada ya kupona mpe mlo mmoja wa ziada kila siku kwa wiki mbili. Mtoto anayeharisha apewe ORS na zinki kituoni na aendelee kula. Soma kuharisha kwa mtoto.
Vyakula vya kuepuka
Asali kabla ya mwaka 1.
Chumvi nyingi, sukari na viungo vikali.
Soda, juisi za viwandani, chai na kahawa.
Karanga nzima, zabibu nzima, pipi ngumu na vipande vigumu vya mviringo.
Maziwa ya ng'ombe kama kinywaji kikuu badala ya maziwa ya mama kabla ya mwaka 1.
Dalili za hatari
Mpeleke mtoto kituo cha afya kama:
Uzito hauongezeki kwa miezi miwili au unashuka.
Anakataa kula na kunyonya kabisa.
Anaharisha zaidi ya siku 3, au kinyesi kina damu.
Anatapika kila kitu.
Viganja ni vyeupe, amelegea au ana usingizi mwingi.
Ana kupumua kwa shida au uvimbe wa uso baada ya kula.
Soma pia lishe ya mtoto, lishe bora kwa mtoto wa miezi 10, lishe kamili kwa mtoto wa miezi 12 na ukuaji wa mtoto wa mwezi 10 hadi 11.
Mlo wa kuongeza uzito: mtoto wa miezi 11
Kwanza: pima kama uzito ni mdogo kweli
Kabla ya kubadilisha lishe, mpeleke mtoto kliniki apimwe uzito, urefu na mzunguko wa mkono, na uzito wake ulinganishwe na chati ya ukuaji kwenye kadi ya kliniki. Watoto wengi wanaoonekana wembamba wanakua vizuri kwenye mstari wao. Mtoto ambaye uzito wake umesimama, umeshuka, au yuko chini kabisa ya chati, anahitaji uchunguzi wa magonjwa kama malaria, minyoo, kuharisha, kifua kikuu au VVU, pamoja na ushauri wa lishe. Soma dalili za utapiamlo.
Jinsi ya kuongeza nishati kwenye chakula
Mtoto ana tumbo dogo, hivyo kila kijiko kinapaswa kuwa na nishati nyingi. Njia rahisi ni hizi:
Ongeza kijiko cha mafuta ya alizeti au ya ufuta kwenye uji au chakula.
Ongeza siagi ya karanga au karanga zilizosagwa kwenye uji.
Pika uji kwa tui la nazi au maziwa badala ya maji pekee.
Pika uji mzito, si mwepesi kama maji.
Ponda parachichi kwenye chakula.
Tumia unga wa mchanganyiko wa nafaka na jamii ya mikunde.
Jedwali la mbadala wa viambato
Kundi la chakula | Chakula | Mbadala unaopatikana Tanzania |
Protini | Mayai | Dagaa waliopondwa, samaki wadogo, maini, maharage |
Mafuta bora | Mafuta ya alizeti | Tui la nazi, mafuta ya ufuta, siagi ya karanga |
Wanga | Ugali laini | Wali laini, viazi, ndizi za kupika |
Matunda | Parachichi | Papai, embe, ndizi mbivu |
Mboga za majani | Mchicha | Matembele, kisamvu, majani ya maboga |
Maziwa | Maziwa ya mama | Maziwa ya ng'ombe kidogo yaliyochemshwa ndani ya uji au chakula |
Uji wa lishe | Mahindi, karanga na ulezi | Mtama, mchele au nafaka nyingine mchanganyiko |
Mtoto anapokataa kula
Mlishe kwa subira, ukiongea naye na kumtia moyo, bila kumlazimisha.
Mpe vyakula tofauti na rangi tofauti.
Mlishe akiwa na njaa, si mara baada ya kunyonya sana.
Punguza vitu vya kumvuruga kama televisheni.
Akiugua, endelea kumpa chakula kidogo kidogo mara nyingi, na baada ya kupona mpe mlo mmoja wa ziada kila siku kwa wiki 2.
Majina mengine ya mada hii
Watu hutafuta mada hii kwa majina haya pia:
Chakula cha mtoto wa miezi 11
Mlo kamili kwa mtoto wa miezi 11
Ratiba ya chakula ya mtoto wa miezi kumi na moja
Mtoto wa miezi 11 ale nini
Hitimisho
Kwa mtoto wa miezi 11, lishe bora ni msingi wa afya na ukuaji wa akili na mwili. Vyakula vyote vinavyotolewa kwa mtoto vinapaswa kuandaliwa kwa usafi na kwa kuzingatia uwezo wa mtoto kutafuna.
Kila familia inaweza kutumia vyakula rahisi vya kienyeji vyenye thamani kubwa ya lishe ili kumpa mtoto lishe bora bila gharama kubwa. Endelea kunyonyesha, na kama kuna wasiwasi wowote kuhusu afya au chakula cha mtoto, wasiliana na mtaalamu wa afya.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Mtoto wa miezi 11 anapaswa kula mara ngapi?
Anapaswa kula milo mikuu 3 hadi 4 na vitafunwa 1 hadi 2 kwa siku, huku akiendelea kunyonya. Kila mlo uwe nusu hadi robo tatu ya kikombe cha mililita 250, kulingana na hamu yake na jinsi anavyokua.
2. Mtoto wa miezi 11 anaweza kula chakula cha familia?
Mtoto wa miezi 11 anaweza kula chakula cha familia kilichokatwa vipande vidogo laini, ukitoa sehemu yake kabla ya kuongeza chumvi na viungo vikali. Hii humzoesha chakula cha familia na humfundisha kwa kuiga watu wanaokula pamoja naye.
3. Je, niachishe kunyonyesha mtoto wa miezi 11?
Hakuna haja ya kuachisha. Inashauriwa kuendelea kunyonyesha pamoja na chakula hadi miaka 2 au zaidi, kwa sababu maziwa ya mama yanaendelea kutoa protini, vitamini na kinga. Mama akiamua kuachisha, afanye taratibu na mtoto apate maziwa mengine na mlo wa ziada.
4. Mtoto wa miezi 11 anaweza kunywa maziwa ya ng'ombe?
Maziwa ya ng'ombe yaliyochemshwa yanaweza kutumika kwa kiasi kidogo kwenye uji au chakula. Kama kinywaji kikuu ni bora kusubiri hadi mwaka 1, kwa sababu yana madini chuma kidogo. Baada ya mwaka 1 maziwa ya ng'ombe yaliyochemshwa yanaweza kuwa kinywaji cha kila siku.
5. Mtoto wa miezi 11 anaweza kula nyama ya kuku?
Kuku aliyepikwa vizuri, aliyesagwa au kukatwa vipande vidogo bila mifupa, ni chakula kizuri cha protini kwa mtoto wa miezi 11. Ondoa ngozi yenye mafuta mengi na mifupa midogo. Maini ya kuku ni chanzo bora zaidi cha madini chuma.
6. Ninawezaje kumfundisha mtoto wa miezi 11 kujilisha?
Mpe kijiko chake huku ukimsaidia kwa kijiko kingine, mpe vipande laini vya kushika, na mkalishe pamoja na familia wakati wa kula. Ruhusu amwage chakula, kwa sababu ni sehemu ya kujifunza. Kaa naye muda wote anapokula kwa sababu ya hatari ya kukabwa.
7. Mtoto wa miezi 11 bado anatumia chupa; nifanye nini?
Anza kumfundisha kunywa kwa kikombe kidogo wazi na punguza chupa taratibu. Chupa ni vigumu kusafisha, huongeza hatari ya kuharisha, na kunyonya chupa usiku huchangia kuoza kwa meno. Usimlaze na chupa mdomoni.
8. Mtoto wa miezi 11 anachagua chakula; nifanyeje?
Kuchagua chakula ni kawaida katika umri huu. Endelea kumpa vyakula tofauti kidogo kidogo bila kumlazimisha, changanya chakula kipya na anachokipenda, na kula naye pamoja. Ladha mpya inaweza kuhitaji kujaribiwa mara nyingi kabla hajaipenda.
9. Ni vyakula gani vyenye madini chuma kwa mtoto wa miezi 11?
Maini, nyama, dagaa, samaki na mayai vina madini chuma yanayofyonzwa vizuri. Maharage, dengu na mboga za majani za kijani nazo zina madini chuma, hasa zikiliwa pamoja na tunda lenye vitamini C kama papai au chungwa. Epuka chai wakati wa kula.
10. Mtoto wa miezi 11 anahitaji maji kiasi gani?
Hakuna kiasi maalum; mpe maji safi yaliyochemshwa kwa kikombe wakati wa milo na anapoonekana na kiu, hasa wakati wa joto. Maji yasichukue nafasi ya kunyonya wala chakula. Mkojo mweupe au wa njano hafifu unaonyesha anapata maji ya kutosha.
11. Mtoto wa miezi 11 akiwa mgonjwa ale vipi?
Aendelee kunyonya mara nyingi zaidi na apewe chakula laini anachokipenda kidogo kidogo mara nyingi. Baada ya kupona apewe mlo mmoja wa ziada kila siku kwa wiki mbili. Kama hanywi kabisa, anatapika kila kitu au amelegea, mpeleke kituo cha afya haraka.
12. Nitajuaje kama mtoto wa miezi 11 anakula vya kutosha?
Mstari wa uzito kwenye kadi unapanda, ana nguvu, anacheza, anasimama au kutembea akishikilia, na anakojoa mara kadhaa kwa siku. Viganja vyeupe, uzito usioongezeka kwa miezi miwili au kuchelewa kwa hatua za maendeleo ni sababu ya kumwona mtaalamu.
13. Nimpe yai zima au nusu?
Mtoto wa miezi 11 anaweza kula yai zima lililopikwa vizuri hadi kiini kikawe kigumu, likiwa limepondwa au kukatwa vipande vidogo. Yai ni chanzo kizuri cha protini na mafuta. Kama anakataa, anza na nusu na uongeze.
14. Vitu gani huongeza uzito haraka bila madhara?
Mafuta ya kupikia, siagi ya karanga, tui la nazi, parachichi, maziwa ndani ya uji, mayai, samaki na dagaa huongeza nishati na protini. Viongeze kwenye milo ya kawaida badala ya kumpa sukari, soda au biskuti.
15. Mtoto wangu anakula vizuri lakini uzito haupandi. Kwa nini?
Huenda ana ugonjwa unaozuia uzito kupanda, kama minyoo, malaria ya mara kwa mara, kuharisha, maambukizi ya mkojo, kifua kikuu au VVU, au milo haina nishati ya kutosha. Mpeleke kliniki kwa uchunguzi na ushauri wa lishe.
16. Nimpe asali kwenye uji?
Usimpe asali kabla ya miezi 12. Asali huweza kuwa na vijidudu vinavyotoa sumu inayomdhuru mtoto mdogo. Baada ya mwaka mmoja, asali kidogo inaruhusiwa, lakini sukari iwe kidogo.
Maelezo haya ni ya kielimu tu, ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.
Ikiwa unataka ushauri zaidi kutoka ULY CLINIC, wasilisha swali lako kwa kubofya mawasiliano yetu
Imeandikwa,
3 Julai 2025, 12:29:38
Rejea za mada hii:
World Health Organization (WHO). Guideline: Updates on HIV and infant feeding. Geneva: WHO; 2016.
Black RE, Allen LH, Bhutta ZA, Caulfield LE, de Onis M, Ezzati M, et al. Maternal and child undernutrition: global and regional exposures and health consequences. Lancet. 2008;371(9608):243–260.
Ministry of Health, Community Development, Gender, Elderly and Children (Tanzania Mainland). National Nutrition Survey Report. Dar es Salaam: MoHCDGEC; 2020.
Dewey KG, Adu-Afarwuah S. Systematic review of the efficacy and effectiveness of complementary feeding interventions in developing countries. Matern Child Nutr. 2008;4 Suppl 1:24–85.
United Nations Children’s Fund (UNICEF). Infant and Young Child Feeding Programming Guide. New York: UNICEF; 2011.
Tanzania Food and Nutrition Centre (TFNC). Infant and Young Child Feeding Counselling Package. Dar es Salaam: TFNC; 2015.
Pan American Health Organization (PAHO). Guiding Principles for Complementary Feeding of the Breastfed Child. Washington, DC: PAHO; 2003.
Michaelsen KF, Hoppe C, Roos N, Kaestel P, Stougaard M, Lauritzen L, et al. Choice of foods and ingredients for moderately malnourished children 6 months to 5 years of age. Food Nutr Bull. 2009;30(3 Suppl):S343–404.
United States Agency for International Development (USAID). Essential Nutrition Actions and Essential Hygiene Actions Framework. Washington, DC: USAID; 2021.
WHO Multicentre Growth Reference Study Group. WHO Child Growth Standards: Length/height-for-age, weight-for-age, weight-for-length, weight-for-height and body mass index-for-age. Geneva: WHO; 2006.
Arimond M, Ruel MT. Dietary diversity is associated with child nutritional status: evidence from 11 demographic and health surveys. J Nutr. 2004;134(10):2579–85.
World Bank Group. Ending Child Malnutrition: A Position Paper on Nutrition. Washington, DC: World Bank; 2013.
World Health Organization. WHO guideline for complementary feeding of infants and young children 6-23 months of age. Geneva: World Health Organization; 2023.
Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026.

