top of page

Mwandishi:

Mhariri:

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD, Dkt. Salome A, M.D

19 Januari 2026, 13:35:44

Image-empty-state.png

Dalili za uchungu wiki ya 40

Imeboreshwa:

Wiki ya 40 ya ujauzito ni hatua muhimu sana kwani ni kilele cha safari ya ujauzito. Katika wiki hii, ukuaji wa mtoto huwa umekamilika kikamilifu, na mtoto ana uwezo wa kuishi nje ya tumbo la uzazi bila matatizo makubwa. Uzito wa mtoto hukadiriwa kuwa kati ya kilo 3.4 hadi 4.5, huku urefu wake ukiwa wastani wa sentimita 50–52 (inchi ~20). Mzunguko wa kichwa chake kwa kawaida huwa sawa au karibu sawa na mzingo wa tumbo, ishara ya ukuaji uliosawazika.


Kwa mama, wiki ya 40 huambatana na mabadiliko makubwa ya mwili na hisia, mengi yakiwa ni ishara za maandalizi ya uchungu wa kujifungua. Uchungu wa kweli unaweza kuanza wakati wowote ndani ya masaa 24–72, ingawa kwa baadhi ya wanawake unaweza kuchelewa kidogo bila kuwa tatizo.


Mabadiliko ya Mwili wa Mama Wiki ya 40

Katika kipindi hiki:

  • Kupumua kwa shida kunaweza kupungua kwa sababu mtoto hushuka kuelekea nyonga

  • Kimo cha mimba huonekana kimepungua kidogo

  • Kubana kwa misuli ya miguu huweza kuongezeka

  • Uchovu, wasiwasi na msisimko wa kihisia huongezeka

Haya yote ni sehemu ya maandalizi ya mwili kwa tukio la kujifungua.


Dalili za uchungu wiki ya 40

Miongoni mwa dalili za uchungu katika wiki ya 40 ni kama zifuatazo;


Kujongea kwa misuli ya tumbo la chini

Kwenye wiki hii ya 40 mjamzito anaweza kupata dalili ya kubana kwa tumbo la uzazi kwa kiasi inayopotea na isiyo na maumivu makali na kutokea bila mpangilio wa kueleweka. Kubana huku huwa ishara ya majaribio ya tumbo la uzazi kujiandaa na uchungu wa kweli.


Kukosa usingizi

Mabadiliko ya homoni, maumivu ya mgongo, mawazo mengi, shauku kubwa ya kujifungua na harakati za mtoto husababisha kukosa usingizi au kuamka mara kwa mara usiku.


Kuwashwa tumbo

Ngozi ya tumbo hutanuka zaidi mtoto anaposhuka, hali inayoweza kusababisha kuwashwa, kuvuta au hisia za kukaza kwa tumbo la chini.


Kuharisha

Homoni za uchungu (hasa prostaglandini) huongeza harakati za kujongea kwa misuli na kushuka kwa mtoto kwenye nyonga, hivyo kuharisha kunaweza kuwa ishara ya mwili kujiandaa kwa uchungu.


Kuzibuka kwa kifuniko cha shingo ya kizazi

Kutokwa na makamasi mengi ukeni yanayoweza kuwa ya rangi ya maji, pinki, au kuwa na michirizi ya damu. Dalili hii ni kiashiria cha kutoka kwa kifuniko cha shingo ya kizazi ambacho huzuia vimelea kutoka ukeni kuingia kwenye kizazi. 


Makamasi yanaweza kutoka kwa dakika chache, masaa au siku kadhaa kabla ya uchungu kuanza. Dalili hii huwa haigunduliwi na wanawake wengi.


Maumivu ya mgongo

Maumivu mara nyingi huwa ya mgongo wa chini yaani katika maeneo ya kiuno, ambayo huwa endelevu na huwa makali ya kutovumilika kwenye hatua za mwisho za uchungu. Maumivu haya yanahusishwa kusababishwa na mgandamizo kwenye via na mishipa ya fahamu ya mfuko wa matumbo(peritoniamu) kutokana na unaoletwa na kukua kwa kizazi.


Hisia za kujisaidia

Ni ishara ya mgandamizo kwenye matumbo na kibofu cha mkojo hivyo kupelekea hisia za kutaka kujisaidia. Hi pia humaanisha mtoto anajongea uelekeo wa kutoka nje ya kizazi kwa jina jingine mtoto kushuka. Mara nyingi hizia hizi huletwa na mgandamizo wa kichwa cha mtoto kwenye maeneo tajwa.


Kupasuka kwa chupa ya uzazi

Kati ya wanawake 10, mjamzito mmoja hupata dalili hii ambayo hutokea sana nyumbani wakati umelala. Baadhi ya nyakati chupa ya uzazi hupasuka kwenye uchungu na wakati mwingine hupasuliwa kwneye hatua ya pili ya uchungu.


Baadhi ya nyakahu huwa ni vigumu kutofautisha kati ya mkojo na maji ya chupa ya uzazi. Hata hivyo kupasuka kwa chupa ya uzazi huambatana na maji mengi yanayochuruzika kwenye mapaja kama mtu amesimama na huwa meupe, hayana harufu na hutoka mengi kwa ghafla au kuendelea kumwagika taratibu.


Kama ukipata dalili hii hakikisha kuwa si mkojo kwa kunusa, na kama ikionekana si mkojo unapaswa kuzingatia utoshiriki ngono au kutumia pedi ya kuchomeka ukeni au kufanya chochote kinachoweza kuingiza bakteria ukeni. Wakati huu onana na mtoa huduma ya afya. 


Maji yakiwa na rangi tofauti na maji au harufu huweza kuashiria, maambukizi, au kuchanganyika  na choo cha mtoto.


Mabadiliko ya urefu na upana wa shingo ya kizazi

Shingo ya kizazi huwa fupi na nyembamba. Hii ni ishara kwamba sehemu ya chini ya kizazi inajiandaa kwa ajili ya kutoa mtoto kwa kuwa shingo kuwa nyembamba hufanya iweze kutanuka kirahisi Zaidi. Dalili hii hupimwa na mtaalamu wa afya kwa kutia vidole viwili ukeni ili kuifikia shingo ya kizazi.


Ongezeko kipenyo cha shingo ya kizazi

Kuongezeka kwa kipenyo cha shingo ya kizazi ni dalili inayoashiria kufunguka kwa njia ya uzazi ili kichwa cha mtoto. Kizio cha kipimo hiki ni sentimita na kipenyo cha mwisho cha kutanuka ni sentimita 10. Dalili hii huwezi kuifahamu mwenyewe, mtaalamu wa afya hupima shingo ya kizazi kupitia uke kutumia vidole viwili kila baada ya masaa 2 hadi 4 ikitegemea hatua ya uchungu uliyonayo. Hatua za awali za uchungu huweza kuchukua muda kabla ya kwenda kuwa uchungu wa kujifungua


Je, ni salama kujifungua wiki ya 40

Ndiyo. Wiki ya 40 ni wakati salama na wa kawaida kabisa wa kujifungua. Mtoto huwa amekomaa kikamilifu, na endapo uchungu utaanza, mama huruhusiwa kujifungua kawaida au kwa msaada wa kitaalamu kulingana na hali.


Ikiwa uchungu haujaanza:

  • Daktari anaweza kufanya kipimo cha ultrasound

  • Kupima kiwango cha maji ya uzazi

  • Kufuatilia mapigo ya moyo ya mtoto


Wakati gani wa kwenda hospitali haraka (Wiki ya 40 ya ujauzito)?

Jedwali lifuatalo linaeleza kwa muhtasari dalili hatarishi zinazomhusu mwanamke aliye katika wiki ya 40 ya ujauzito, na wakati sahihi wa kwenda hospitali haraka. Linalenga kuwasaidia wajawazito na walezi wao kutambua ishara za hatari mapema ili kuchukua hatua stahiki kwa wakati, kulinda afya ya mama na mtoto.

Dalili / Hali

Maelezo kwa ufupi

Kupasuka kwa chupa ya uzazi

Maji yanatoka ghafla au kuchuruzika mfululizo hata bila uchungu; nenda hospitali mara moja.

Maji ya uzazi yenye rangi/harufu

Maji ya kijani, njano, kahawia au yenye harufu mbaya huashiria hatari (maambukizi au mekoniamu(Kinyesi cha mtoto).

Kutokwa damu nyingi ukeni

Damu nyingi kama ya hedhi au zaidi si ya kawaida; inaweza kuashiria tatizo kubwa.

Uchungu mkali unaokuja mara kwa mara

Maumivu kila dakika 5 au chini ya hapo kwa zaidi ya saa 1 (hasa uchungu wa kwanza).

Mtoto kupunguza au kutocheza

Harakati za kucheza zikipungua sana au kutokuwepo ni ishara ya hatari.

Maumivu makali ya kichwa/kizunguzungu/kuona giza

Huashiria presha ya juu ya ujauzito inayoelekea kifafa cha mimba (presha tangulizi ya kifafa cha mimba).

Homa au dalili za maambukizi

Homa, kutetemeka au maumivu makali ya tumbo bila mpangilio wa uchungu.

Hisia kali ya kusukuma/kutaka kujisaidia

Huashiria mtoto yuko karibu kutoka.

Uvimbe mkubwa wa ghafla

Uso, mikono au miguu kuvimba ghafla, hasa na maumivu ya kichwa/kutoona vizuri.

Wasiwasi usio wa kawaida

Ukihisi “kuna kitu si sawa”, ni bora kwenda hospitali mapema.

Kumbuka

Ni heri kufika hospitali mapema na kubainika uko salama kuliko kuchelewa na kuhatarisha afya ya mama na mtoto. Endelea kuwa na mawasiliano ya karibu na mtoa huduma wako wa afya unapokaribia kujifungua.


Hitimisho

Wiki ya 40 ya ujauzito ni kipindi nyeti lakini cha kawaida kabisa katika safari ya uzazi. Mwili wa mama huwa umejiandaa kikamilifu kwa ajili ya uchungu, huku mtoto akiwa amekomaa na tayari kuzaliwa. Dalili kama kubana kwa tumbo, maumivu ya mgongo, kutoka kwa makamasi ya shingo ya kizazi, kuharisha na kupasuka kwa chupa ya uzazi ni ishara muhimu zinazoonyesha kuwa muda wa kujifungua unakaribia au umefika.


Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa si wanawake wote hupata dalili hizi kwa mpangilio au kwa wakati mmoja. Ufuatiliaji wa karibu wa mtaalamu wa afya, kutulia kisaikolojia, na kuepuka matumizi ya dawa au njia za kuamsha uchungu bila ushauri wa kitaalamu ni hatua muhimu za kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.


Endapo kuna dalili zisizo za kawaida kama damu nyingi, harufu mbaya ya maji ya uzazi au maumivu makali yasiyoelezeka, ni lazima kufika kituo cha afya haraka.


Kwa ujumla, kuwa na uelewa sahihi wa dalili za uchungu wiki ya 40 humsaidia mama kuwa tayari kimwili na kiakili, na huchangia kujifungua salama na kwa amani.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je, kuchelewa kupata uchungu baada ya wiki ya 40 ni hatari?

Si lazima. Baadhi ya mimba huanza uchungu wiki ya 41 bila tatizo, mradi mtoto na mama wanafuatiliwa kitaalamu.

2. Nifanye nini nikiwa na dalili za uchungu lakini haziongezeki?

Endelea kufuatilia dalili, kunywa maji ya kutosha na wasiliana na mtoa huduma ya afya kama dalili zitadumu au kuongezeka.

3. Je, Uchungu wa uongo ni uchungu wa kweli katika wiki hizi 40?

Hapana. Ni uchungu wa maandalizi, hauongezeki kwa nguvu wala mpangilio kama uchungu wa kweli.

4. Maji ya uzazi yakipasuka bila uchungu nifanye nini?

Nenda hospitali mara moja hata kama huna maumivu.

5. Je, ngono inaweza kuchochea uchungu wiki ya 40?

Ndiyo, kwa baadhi ya wanawake shahawa husaidia kulainisha shingo ya kizazi, lakini si lazima kwa wote.

6. Je, kunywa chai au dawa za asili ni salama kuamsha uchungu?

Hapana bila ushauri wa mtaalamu. Baadhi ya dawa za asili zinaweza kuwa hatari.

7. Nitajuaje tofauti ya mkojo na maji ya uzazi?

Maji ya uzazi hayadhibitiwi, hayana harufu na huendelea kutoka hata baada ya kujikamua.

8. Je, kila maumivu ya mgongo ni ishara ya uchungu?

Hapana, lakini maumivu ya mgongo yanayoambatana na kubana kwa tumbo mara kwa mara huashiria uchungu.

9. Je, nifike hospitali lini hospitali endapo nina uchungu katika wiki ya 40?

Ukiona kubana kwa tumbo kila dakika 5–10, maji ya uzazi yamepasuka, au damu nyingi ukeni.

10. Je, uchungu unaweza kuanza ghafla bila dalili nyingi?

Ndiyo, kwa baadhi ya wanawake uchungu huanza ghafla na kuwa mkali haraka.


ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

21 Julai 2023, 14:47:09

Rejea za dawa

  1. Pregnancy week by week. Week 40. https://www.thebump.com/pregnancy-week-by-week/40-weeks-pregnant. Imechukuliwa 20.07.2023

  2. World Health Organization. WHO recommendations on intrapartum care for a positive childbirth experience. Geneva: World Health Organization; 2018.

  3. World Health Organization. Pregnancy, childbirth, postpartum and newborn care: A guide for essential practice. 3rd ed. Geneva: WHO; 2015.

  4. Cunningham FG, Leveno KJ, Bloom SL, Spong CY, Dashe JS, Hoffman BL, et al. Williams Obstetrics. 26th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2022.

  5. American College of Obstetricians and Gynecologists. Warning signs during pregnancy and labor. ACOG Patient Education; 2023.

  6. Royal College of Obstetricians and Gynaecologists. When to seek medical help during pregnancy and labour. London: RCOG; 2021.

  7. Ministry of Health Tanzania. Focused Antenatal Care Guidelines. Dar es Salaam: MoH; 2018.

  8. National Institute for Health and Care Excellence. Intrapartum care for healthy women and babies (NICE Guideline CG190). London: NICE; 2023 update.

  9. March of Dimes. Signs of labor and when to go to the hospital. March of Dimes Foundation; 2022.

  10. UNICEF. Maternal health: Danger signs during pregnancy, labour and after birth. New York: UNICEF; 2021.

  11. Katz VL, Lentz GM, Lobo RA, Gershenson DM. Comprehensive Gynecology. 8th ed. Philadelphia: Elsevier; 2021.

bottom of page