Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
ULY CLINIC
20 Agosti 2026, 16:31:11
Purslane (Mboga ya purslane)
Purslane, inayojulikana kisayansi kama Portulaca oleracea, ni mmea unaoweza kutumika kama mboga na unaopatikana katika maeneo mbalimbali duniani. Majani na mashina yake machanga yanaweza kuliwa na hutumiwa katika vyakula vya jamii mbalimbali.

Purslane ina virutubisho na misombo ya mimea kama mafuta ya omega-3 ya mimea aina ya alpha-linolenic acid (ALA), vitamini, madini, nyuzilishe, carotenoids na polyphenols. Kwa sababu ya mchanganyiko huu, mmea umefanyiwa tafiti nyingi kuhusu uwezo wake wa kusaidia afya ya umetaboli, hasa sukari ya damu, mafuta kwenye damu na baadhi ya viashiria vya uchochezikinga.
Ushahidi wa tafiti za binadamu unaonyesha kuwa purslane inaweza kuwa na manufaa katika baadhi ya vipengele vya afya, hasa kupunguza sukari ya mfungo kwenye damu, traiglaiseraidi, kolestro ya jumla, viashiria vya uchochezi kinga (CRP), huku baadhi ya tafiti zikionyesha pia kuwa huongeza kolestro nzito(HDL) inayofahamika kuwa ni nzuri na kupungua kwa shinikizo la damu la juu. Hata hivyo, ukubwa wa athari hutofautiana kati ya tafiti na ushahidi wa muda mrefu bado ni mdogo.
Purslane ina virutubisho gani?
Purslane ina mchanganyiko wa virutubisho unaoifanya iwe mboga yenye thamani katika lishe. Ina vitamini na madini mbalimbali pamoja na nyuzilishe na kampaundi ya mimea yenye shughuli za kuondoa sumu ya oksijeni huru kwenye damu.
Moja ya sifa zinazotajwa zaidi kuhusu purslane ni kuwa na alpha-linolenic acid (ALA), ambayo ni mafuta ta omega-3 inayopatikana katika mimea. ALA ni muhimu katika lishe, ingawa mwili hubadilisha sehemu yake kuwa EPA na DHA kwa kiwango kidogo.
Purslane pia ina carotenoids na polyphenols. Kampaundi hizi zimehusishwa na uwezo wa kuuondoa sumu ya oksijeni huru kwenye damu na imekuwa mojawapo ya sababu zinazofanya mmea huu uchunguzwe katika tafiti za afya ya umetaboli na uchochezikinga.
Faida za purslane kulingana na tafiti
1. Inaweza kusaidia kupunguza sukari ya damu
Hii ni mojawapo ya faida za purslane ambazo zimechunguzwa zaidi kwa binadamu. Meta-analysis ya tafiti za randomized controlled trials iliyoangalia watu wenye kisukari cha aina ya 2 ilionyesha kuwa matumizi ya purslane yalihusishwa na kupungua kwa sukari ya mfungo kwneye damu ya kufunga (FBG). Meta-analysis ya 2023 pia ilipata kupungua kwa sukari ya mfungo kwenye damu, lakini haikuonyesha mabadiliko muhimu katika HbA1c, insulini au HOMA-IR.
Utafiti mwingine wa meta-analysis uliounganisha tafiti 16 na washiriki 1,122 ulionyesha pia kupungua kwa sukari ya mfungo kwenye damu pamoja na baadhi ya viashiria vya msongo wa oksijeni huru kwenye damu. Hata hivyo, HbA1c haikupungua kwa kiwango cha maana kitakwimu.
Kwa hiyo, ushahidi wa sasa unaonyesha uwezekano wa purslane kusaidia udhibiti wa sukari ya damu, lakini athari hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa sawa na matibabu ya kisukari. Mtu mwenye kisukari anapaswa kuendelea na matibabu na ufuatiliaji aliopewa na mtaalamu wa afya.
2. Inaweza kusaidia kupunguza traiglaiseraidi
Tafiti za binadamu zimeonyesha ushahidi unaoelekea kuwa mzuri zaidi kuhusu traiglaiseraidi. Meta-analysis ya tafiti 13 za randomized controlled trials ilionyesha kuwa matumizi ya purslane yalihusishwa na kupungua kwa traiglaiseraidi kwa wastani wa takribani 16.72 mg/dL ikilinganishwa na makundi ya udhibiti.
Meta-analysis nyingine iliyochapishwa mwaka 2024 ilipata kupungua kwa triglycerides kwa takribani 21.30 mg/dL katika wagonjwa wenye kisukari cha aina ya 2.
Hii inaifanya purslane kuwa chakula cha kuvutia katika lishe inayolenga afya ya kimetaboli. Hata hivyo, kiasi cha purslane kilichotumika katika tafiti na namna ilivyotolewa kilitofautiana, hivyo matokeo haya hayawezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa kula kiasi chochote cha purslane kutapunguza traiglaiseraidi kwa kiwango fulani.
3. Inaweza kusaidia kupunguza kolestro ya jumla
Ushahidi wa meta-analysis unaonyesha pia uwezekano wa purslane kupunguza kolestro ya jumla. Katika meta-analysis ya tafiti 13, matumizi ya purslane yalihusishwa na kupungua kwa cholesterol ya jumla kwa wastani wa karibu 9.97 mg/dL.
Meta-analysis ya 2024 kwa watu wenye kisukari cha aina ya 2 ilionyesha athari kubwa zaidi, ikiwa na kupungua kwa cholesterol ya jumla kwa wastani wa 17.75 mg/dL.
Matokeo haya yanaonyesha uwezekano wa purslane kuchangia kuboresha baadhi ya vipengele vya mafuta kwenye damu. Hata hivyo, kolestro inapaswa kutathminiwa kwa ujumla pamoja na kolestro nyepesi(LDL), kolestro nzito (HDL), traiglaiseraidi, uzito, shinikizo la damu na hatari nyingine za ugonjwa wa moyo.
4. Inaweza kuongeza Kolestro nzito kwneye damu (HDL)
Baadhi ya tafiti pia zimeonyesha ongezeko la kolestro nzito kwenye damu(HDL), ambayo mara nyingi huitwa “kolestro nzuri”.
Tafiti ya Meta-analysis ya 2023 ilionyesha ongezeko la kolestro nzito kwa wastani wa takribani 4.09 mg/dL, huku meta-analysis ya 2024 kwa watu wenye kisukari cha aina ya 2 ikionyesha ongezeko la takribani 6.17 mg/dL.
Hata hivyo, matokeo haya hayamaanishi kwamba purslane inaweza kutumika peke yake kurekebisha cholesterol. Kolestro nzito ni sehemu moja tu ya tathmini ya afya ya moyo, na kupunguza kolestro nyepesi (LDL)L na traiglaiseraidi pamoja na kudhibiti shinikizo la damu huwa muhimu zaidi katika kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo.
5. Inaweza kupunguza baadhi ya viashiria vya uchochezi
Purslane pia imechunguzwa kuhusu athari zake kwenye uchochezi (inflammation). Meta-analysis ya tafiti za binadamu ilionyesha kuwa matumizi ya purslane yalipunguza kiwango cha viashiria vya uchochezi kinga (C-reactive protein (CRP)) kwa wastani wa takribani 1.22 mg/L.
Meta-analysis ya 2024 kwa wagonjwa wenye kisukari cha aina ya 2 pia ilipata kupungua kwa CRP, kwa wastani wa takribani 1.44 mg/L.
CRP ni kiashiria cha uchochezi kinga mwilini, lakini kupungua kwake hakumaanishi moja kwa moja kwamba purslane inatibu ugonjwa unaosababisha uchochezi. Kwa hiyo, faida hii inapaswa kueleweka kama mabadiliko ya kiashiria cha uchochezi, si tiba ya ugonjwa maalumu.
6. Inaweza kupunguza Msongo wa oksijeni huru kwenye damu
Purslane ina misombo ya mimea yenye shughuli za antioxidant, na tafiti za binadamu zimechunguza kama matumizi yake yanaweza kubadilisha viashiria vya msongo wa oksijeni huru kwenye damu
Meta-analysis ya tafiti 16 za randomized clinical trials ilionyesha kuwa matumizi ya purslane yalipunguza kampaundi za malondialdehyde (MDA) na kuongeza kiwango cha jumla cha viondoa oksijeni huru kwenye damu (TAC). Haya ni mabadiliko yanayoashiria kupungua kwa baadhi ya viashiria vya oxidative stress na kuongezeka kwa uwezo wa antioxidant wa mwili.
Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya kuboresha ishara za msongo wa oksijeni huru kwenye damu kwenye vipimo vya damu na kuthibitisha kwamba mmea huo unapunguza hatari ya ugonjwa fulani. Ushahidi wa mwisho kuhusu matokeo ya muda mrefu ya kiafya bado unahitaji tafiti zaidi.
7. Inaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu
Ushahidi kuhusu shinikizo la damu umeanza kuwa wa kuvutia. Meta-analysis iliyochapishwa hivi karibuni na iliyojumuisha tafiti tano za randomized controlled trials ilionyesha kuwa purslane ilihusishwa na kupungua kwa shinikizo la sistoli kwa wastani wa takribani 3.06 mmHg. Hata hivyo, haikuonyesha kupungua kwa maana katika shinikizo la dayastoli kwa ujumla.
Utafiti mmoja wa randomized placebo-controlled kwa watu wenye kisukari cha aina ya 2 pia uliona kupungua kwa shinikizo la sistoli katika kundi lililotumia dondoo za purslane baada ya wiki 12.
Hata hivyo, tofauti kubwa kati ya tafiti ilisababisha kutokuwa na uhakika katika baadhi ya matokeo. Kwa hiyo, purslane inaweza kuwa sehemu ya lishe yenye afya kwa moyo, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya dawa za shinikizo la damu kwa mtu aliyeandikiwa matibabu.
8. Inaweza kusaidia baadhi ya magonjwa ya sindromu ya kimetaboli
Sindromu ya kimetaboli inahusisha mkusanyiko wa matatizo kama sukari ya juu, mafuta yasiyo ya kawaida kwenye damu, shinikizo la damu na unene wa tumbo. Kwa sababu purslane imeonyesha athari katika baadhi ya magonjwa haya, imechunguzwa kama sehemu inayoweza kusaidia udhibiti wa hali hii.
Mapitio ya tafiti kuhusu purslane na sindromu ya umetaboli yaliripoti uwezekano wa kuboresha sukari ya damu na baadhi ya vipengele vya mafuta kwenye damu. Waandishi walipendekeza kwamba athari za uondoaji wa sumu ya oksijeni huru kwenye damu, upunguzaji wa uchochezikinga na umetaboli zinaweza kuchangia matokeo hayo, lakini walisisitiza pia umuhimu wa tafiti zaidi za kitabibu.
Kwa hiyo, faida inayowezekana hapa ni kuboresha baadhi ya magonjwa ya sindromu ya umetaboli, si kusema kwamba purslane yenyewe inatibu sindromu hiyo.
Purslane na afya ya moyo
Purslane ina ALA, potassium na misombo mbalimbali ya mimea, na tafiti zake zimeonyesha mabadiliko katika baadhi ya vihatarishi vya ugonjwa wa moyo kama traiglaiseraidi, kolestro, HDL na shinikizo la damu la sistoli.
Hata hivyo, tafiti nyingi zimeangalia vipimo vya damu au shinikizo la damu badala ya matokeo makubwa kama mshtuko wa moyo, kiharusi au vifo vya moyo. Kwa hiyo, ushahidi uliopo haupaswi kutafsiriwa kwamba purslane imethibitishwa kuzuia matukio hayo.
Faida yake kubwa zaidi inaweza kuwa kama sehemu ya mlo wenye mboga nyingi, nyuzinyuzi, mafuta yenye afya na vyakula visivyochakatwa sana.
Purslane na kisukari
Ushahidi wa sasa unaonyesha kuwa purslane inaweza kusaidia kupunguza kiwango cha sukari ya mfungo kwenye damu, lakini athari kwenye HbA1c, insulin na upinzani wa insulini haijaonekana kwa uthabiti.
Hii ni tofauti muhimu kwa mtu mwenye kisukari. Kupungua kwa sukari ya damu ya kufunga katika tafiti hakumaanishi kwamba ugonjwa wa kisukari umepona au kwamba mtu anaweza kuacha dawa.
Kwa mtu mwenye kisukari, purslane inaweza kuonekana kama sehemu ya lishe, lakini mabadiliko yoyote makubwa katika matumizi yake hasa kama anatumiwa kwa kiasi kikubwa au kama dondoo yake yanapaswa kuzingatiwa pamoja na dawa na ufuatiliaji wa sukari.
Purslane na afya ya ini
Baadhi ya tafiti za kliniki zimeonyesha mabadiliko katika vipimo vya ini baada ya matumizi ya purslane. Kwa mfano, utafiti mdogo wa watu wenye kisukari cha aina ya 2 uliripoti kupungua kwa ALT, AST na GGT katika kundi lililotumia mbegu za purslane.
Hata hivyo, huu ulikuwa utafiti mdogo na hauwezi kutosha kuthibitisha kwamba purslane inatibu ugonjwa wa ini. Kwa sasa, ni sahihi kusema kwamba kuna ushahidi wa awali wa athari kwenye baadhi ya vipimo vya ini, lakini tafiti kubwa zaidi zinahitajika.
Jinsi ya kutumia purslane kama chakula
Purslane inaweza kutumiwa kama mboga katika kachumbali, supu au vyakula vilivyopikwa. Majani na mashina machanga yanaweza kuliwa kulingana na aina ya maandalizi yanayotumika.
Mmea unapaswa kuoshwa vizuri kwa maji salama kabla ya kuliwa. Pia epuka mimea iliyokusanywa karibu na barabara, maeneo yenye uchafu, mifereji ya maji machafu au maeneo ambayo yanaweza kuwa yametibiwa kwa dawa za kilimo.
Jambo muhimu zaidi ni kuutambua mmea kwa usahihi. Mimea ya porini inayofanana kwa mwonekano inaweza kuwa na tofauti kubwa katika usalama wake.
Madhara na tahadhari
Purslane kwa ujumla imetumika kama chakula na imechunguzwa katika tafiti za binadamu, lakini matumizi ya kiasi kikubwa au dondoo yake yanahitaji tahadhari zaidi kuliko matumizi yake kama mboga. Katika tafiti za kliniki, madhara makubwa hayajaonekana kwa kiwango kikubwa, ingawa baadhi ya tafiti zimeripoti madhara madogo kama kuvimbiwa.
Purslane pia ina oxalate, hivyo watu wenye historia ya mawe kwenye figo yanayohusiana na calcium oxalate wanapaswa kuwa waangalifu kuhusu kiasi wanachotumia.
Pia ina potassium. Mtu mwenye ugonjwa wa figo unaopunguza uwezo wa figo kutoa potassium au anayeshauriwa kupunguza potassium anapaswa kupata ushauri wa mtaalamu kabla ya kutumia kiasi kikubwa cha purslane.
Nani anapaswa kuwa mwangalifu?
Tahadhari zaidi inafaa kwa:
Watu wenye ugonjwa wa figo.
Watu wenye historia ya mawe ya figo yanayohusiana na oxalate.
Watu wanaoshauriwa kupunguza potassium.
Watu wanaotumia dawa zinazoathiri kiwango cha potassium.
Wajawazito au wanaonyonyesha wanaotaka kutumia purslane kama dawa au extract badala ya kiasi cha kawaida cha chakula.
Mtu asiye na uhakika kuhusu utambulisho wa mmea alioupata.
Hitimisho
Purslane (Portulaca oleracea) ni mboga yenye virutubisho na misombo ya mimea yenye manufaa, na ushahidi wa tafiti za binadamu unaonyesha kuwa matumizi yake yanaweza kusaidia kupunguza sukari ya damu ya kufunga, triglycerides, cholesterol ya jumla na CRP, huku baadhi ya tafiti zikionyesha ongezeko la HDL, kupungua kwa msongo wa sumu ya oksijeni huru kwenye damu na kupungua kwa shinikizo la damu la sistoli.
Kwa hiyo, purslane inaweza kuwa sehemu nzuri ya lishe yenye afya, hasa kwa mtu anayehitaji kuongeza mboga na virutubisho mbalimbali kwenye mlo. Hata hivyo, ukubwa wa faida hutofautiana kati ya tafiti, na ushahidi wa matokeo ya muda mrefu kama kuzuia mshtuko wa moyo, kiharusi au kutibu kisukari bado haujathibitishwa; hivyo matumizi yake yanafaa kuonekana kama sehemu ya lishe na si mbadala wa matibabu yaliyothibitishwa.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara kuhusu purslane na majibu yake
1. Je, purslane inaweza kuliwa kila siku?
Purslane inaweza kutumiwa kama mboga katika mlo, lakini hakuna sababu ya kutegemea mmea huu pekee kila siku ili kupata virutubisho. Lishe bora inapaswa kuwa na aina mbalimbali za mboga, matunda, nafaka, protini na mafuta yenye afya. Kutofautisha aina za vyakula husaidia kupata virutubisho mbalimbali ambavyo mmea mmoja hauwezi kutoa kwa kiwango kinachotosheleza.
Pia kiasi kinacholiwa ni muhimu. Kula kama sehemu ya mlo wa kawaida ni tofauti na kutumia kiasi kikubwa kama dawa au juisi iliyokolea. Matumizi ya kiasi kikubwa yanaweza kuongeza ulaji wa baadhi ya misombo kama oxalates na potassium.
Kwa mtu mwenye ugonjwa wa figo, historia ya mawe ya figo au anayeshauriwa kupunguza potassium, matumizi ya mara kwa mara yanapaswa kujadiliwa na mtaalamu wa afya. Hivyo, usalama wa purslane haupaswi kutathminiwa kwa mmea pekee bali pia hali ya afya ya mtu.
2. Purslane inaweza kusaidia kushusha sukari kwenye damu?
Kuna tafiti zinazochunguza uwezekano wa purslane kuwa na athari kwenye udhibiti wa sukari, lakini ushahidi uliopo haujatosha kuifanya iwe tiba ya kisukari. Matokeo ya utafiti yanaweza kutofautiana kulingana na sehemu ya mmea iliyotumika, kiasi, namna ilivyotayarishwa na aina ya utafiti.
Mtu mwenye kisukari anapaswa kuendelea kufuatilia sukari na kutumia dawa au tiba nyingine alizoelekezwa. Kubadilisha dawa na purslane bila usimamizi kunaweza kufanya sukari ipande na kuongeza hatari ya matatizo ya kisukari.
Ikiwa mtu anataka kuongeza purslane kwenye mlo akiwa na kisukari, ni bora kuitumia kama mboga ndani ya mpango wa lishe unaofaa. Hii ni tofauti kabisa na kutumia dondoo, juisi iliyokolea au virutubisho vya purslane kwa madai ya kutibu kisukari.
3. Purslane inaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu?
Purslane ina baadhi ya virutubisho vinavyohusishwa na afya ya moyo na mishipa, na tafiti zimechunguza athari zake zinazowezekana kwenye shinikizo la damu. Hata hivyo, ushahidi huo haujatosha kusema kwamba purslane inaweza kutumika kama tiba ya shinikizo la damu.
Shinikizo la damu mara nyingi halitoi dalili, hivyo mtu hawezi kujua kama limepungua kwa kutegemea jinsi anavyojisikia. Kipimo cha shinikizo la damu ndicho kinachotakiwa kutumika kufuatilia hali hii.
Mtu anayetumia dawa za shinikizo la damu hapaswi kuacha dawa kwa sababu ameanza kula purslane. Ikiwa anataka kuitumia mara kwa mara au kwa kiasi kikubwa kama kirutubisho, ni vizuri kumjulisha mtoa huduma, hasa ikiwa anatumia dawa zinazoweza kuathiri shinikizo la damu au potassium.
4. Kwa nini purslane inatajwa kuwa chanzo cha omega-3?
Purslane ina alpha-linolenic acid (ALA), ambayo ni omega-3 inayotokana na mimea. ALA ni sehemu muhimu ya lishe na mwili unaweza kuibadilisha kwa kiasi fulani kuwa aina nyingine za omega-3, hasa EPA na DHA.
Hata hivyo, kiasi cha ALA kinachobadilishwa kuwa EPA na DHA huwa si kikubwa. Kwa hiyo, si sahihi kusema kwamba purslane ina maana sawa kabisa na kula samaki wenye mafuta kwa ajili ya kupata EPA na DHA.
Mtu anayepata omega-3 kutoka kwenye vyakula vya mimea anaweza kutumia purslane pamoja na vyanzo vingine vya ALA kama mbegu za kitani, chia na jozi. Kwa mtu anayehitaji EPA au DHA kwa sababu maalumu za kiafya, mtoa huduma anaweza kushauri vyanzo vinavyofaa zaidi.
5. Je, purslane inaweza kusaidia kupunguza uzito?
Purslane inaweza kuwa sehemu ya mlo wa mtu anayelenga uzito unaofaa kwa sababu ni mboga yenye maji mengi na inaweza kuongeza kiasi cha chakula chenye virutubisho bila kutegemea vyakula vyenye nishati nyingi.
Hata hivyo, hakuna ushahidi wa kutosha kusema kwamba purslane yenyewe "huchoma mafuta" au husababisha kupungua uzito bila mabadiliko mengine ya lishe na shughuli za mwili. Kupungua uzito kwa afya hutegemea uwiano wa nishati unaotumika na unaopatikana kutoka kwenye chakula kwa muda.
Kwa hiyo, mtu anaweza kuitumia kama sehemu ya mboga kwenye mlo wenye afya, lakini si kama dawa ya kupunguza uzito. Matokeo mazuri zaidi hutokana na mpango mzima unaohusisha chakula bora, shughuli za mwili, usingizi wa kutosha na tabia endelevu.
6. Je, purslane inaweza kutumika kutibu mawe ya figo?
Purslane haipaswi kuchukuliwa kama tiba ya mawe ya figo. Kinyume chake, ina kmpaundi oxalate, ambazo ni muhimu kuzingatiwa kwa watu wanaopata aina fulani ya mawe ya figo, hasa mawe ya calcium oxalate.
Aina za mawe ya figo hutofautiana na sababu zake pia hutofautiana. Kwa hiyo, ushauri wa lishe kwa mtu mwenye mawe ya figo unapaswa kuzingatia aina ya jiwe, matokeo ya vipimo na hali ya figo.
Mtu mwenye historia ya mawe ya figo anapaswa kupata ushauri wa kitabibu au wa lishe kabla ya kutumia purslane kwa kiasi kikubwa. Kunywa maji ya kutosha kulingana na ushauri wa mtaalamu na kutibu chanzo cha mawe ni muhimu zaidi kuliko kutegemea mmea huu.
7. Je, purslane ni salama kwa mtu mwenye ugonjwa wa figo?
Usalama wake hutegemea kiwango cha ugonjwa wa figo na ushauri wa lishe aliopewa mgonjwa. Purslane ina potassium, na baadhi ya wagonjwa wenye ugonjwa wa figo wanaweza kushindwa kuondoa potassium kwa ufanisi.
Potassium nyingi kwenye damu inaweza kuwa hatari kwa sababu inaweza kuathiri mfumo wa umeme wa moyo. Hivyo, mtu mwenye ugonjwa wa figo hapaswi kudhani kwamba kwa sababu purslane ni mboga basi anaweza kula kiasi chochote bila kuzingatia hali yake.
Ikiwa una ugonjwa wa figo, kiasi kinachofaa cha purslane kinapaswa kuamuliwa kulingana na utendaji wa figo, kiwango cha potassium kwenye damu na mpango wako wa lishe. Hii ni muhimu zaidi ikiwa unatumia dawa zinazoweza kuongeza potassium.
8. Je, purslane inaweza kuliwa ikiwa ni mmea uliotoka porini?
Purslane inayoota porini inaweza kuliwa ikiwa imetambuliwa kwa uhakika na imeoteshwa katika mazingira salama. Hatari kubwa ya mimea ya porini si mmea pekee, bali uwezekano wa kuchanganya na mmea mwingine wenye sumu au kutumia mmea uliogusana na kemikali hatari.
Mimea inayoota karibu na barabara, maeneo yenye taka, mifereji ya maji machafu au mashamba yaliyotibiwa kwa dawa za kilimo inaweza kuwa na uchafu au kemikali ambazo haziwezi kuondolewa kwa kuosha kawaida.
Kwa hiyo, ikiwa huwezi kutambua purslane kwa uhakika, usile mmea huo. Ni salama zaidi kupata kutoka kwa chanzo kinachoaminika au kutumia mmea uliotambuliwa na mtu mwenye ujuzi wa mimea inayoliwa.
9. Je, purslane inaweza kutumika wakati wa ujauzito?
Kutumia purslane kama sehemu ndogo ya chakula ni tofauti na kutumia kiasi kikubwa kama dawa, dondoo au juisi iliyokolea. Ushahidi wa kutosha wa usalama wa matumizi ya kiasi kikubwa wakati wa ujauzito haupo.
Wakati wa ujauzito, bidhaa za mimea zinapaswa kutumiwa kwa tahadhari kwa sababu "asili" haimaanishi moja kwa moja kuwa ni salama kwa mama na mtoto. Baadhi ya misombo ya mimea inaweza kuwa na athari ambazo hazijafanyiwa utafiti wa kutosha kwa wajawazito.
Kwa hiyo, mjamzito anayataka kutumia purslane kama dawa au kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida ya chakula anapaswa kuzungumza na mtoa huduma wa afya kabla ya kufanya hivyo. Hii inasaidia kutofautisha matumizi ya kawaida ya chakula na matumizi ya kitabibu ambayo yanaweza kuwa na hatari zisizojulikana.
10. Je, purslane inaweza kuchukua nafasi ya dawa za hospitalini?
Purslane inaweza kuwa chakula chenye virutubisho, lakini haiwezi kuchukuliwa moja kwa moja kuwa mbadala wa dawa zilizoandikwa kwa ajili ya kutibu magonjwa. Ukweli kwamba mmea una antioxidants, omega-3 au madini fulani hauonyeshi kwamba una uwezo wa kutibu ugonjwa kwa kiwango kinachohitajika kitabibu.
Kwa mfano, mtu mwenye kisukari, shinikizo la damu, ugonjwa wa figo au cholesterol nyingi anahitaji mpango wa matibabu unaotegemea uchunguzi wa hali yake. Kuacha dawa na kutumia mmea pekee kunaweza kusababisha ugonjwa kutodhibitiwa.
Purslane inaweza kuwa sehemu ya lishe yenye afya kwa mtu anayefaa kuitumia, lakini matumizi yake yanapaswa kuonekana kama sehemu ya lishe, si mbadala wa matibabu yaliyothibitishwa. Mtu anayefikiria kutumia dondoo au virutubisho vya purslane pamoja na dawa anapaswa kumjulisha mtoa huduma wa afya ili kuangalia uwezekano wa mwingiliano au madhara.
Imeandikwa;
20 Agosti 2026, 16:20:13
Bofya hapa kusoma zaidi kuhusu namna ya kuandaa vyakula mbalimbali vinavyoweza kukukinga dhidi ya magonjwa ya shinikizo la damu la juu na Kisukari, pia kuupa mwili wako uwezo wa kudhibiti magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu(presha).
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Rejea za mada hii
Guo D, Birjandi R, Moghimi Esfandabadi F, Haedi A, Fujiang C. The effects of purslane (Portulaca oleracea) on C-reactive protein, lipid profile, and glycemic control in patients with type 2 diabetes mellitus: a GRADE-assessed systematic review and meta-analysis of randomized controlled trials. Prostaglandins Other Lipid Mediat. 2024;175:106917. doi:10.1016/j.prostaglandins.2024.106917.
Zargari M, et al. The effects of purslane consumption on lipid profile and C-reactive protein: a systematic review and dose-response meta-analysis. 2023.
Uddin MK, Juraimi AS, Hossain MS, Nahar MAU, Ali ME, Rahman MM. Purslane weed (Portulaca oleracea): a prospective plant source of nutrition, omega-3 fatty acid, and antioxidant attributes. ScientificWorldJournal. 2014;2014:951019. doi:10.1155/2014/951019.
Ghorani V, Saadat S, Khazdair MR, Gholamnezhad Z, El-Seedi H, Boskabady MH. Phytochemical characteristics and anti-inflammatory, immunoregulatory, and antioxidant effects of Portulaca oleracea L.: a comprehensive review. Evid Based Complement Alternat Med. 2023;2023:2075444. doi:10.1155/2023/2075444.
Zhou YX, Xin HL, Rahman K, Wang SJ, Peng C, Zhang H. Portulaca oleracea L.: a review of phytochemistry and pharmacological effects. Biomed Res Int. 2015;2015:925631. doi:10.1155/2015/925631.
Iranshahy M, Javadi B, Iranshahi M, Jahanbakhsh SP, Mahyari S, Hassani FV, et al. A review of traditional uses, phytochemistry and pharmacology of Portulaca oleracea L. J Ethnopharmacol. 2017;205:158-72. doi:10.1016/j.jep.2017.05.004.
Alam MA, Juraimi AS, Rafii MY, Hamid AA, Aslani F, Hasan MM, et al. Evaluation of antioxidant properties and nutritional composition of purslane (Portulaca oleracea) from arid regions. 2025.
Ghorbani A, et al. A review on bioactive phytochemicals and ethnopharmacological potential of purslane (Portulaca oleracea L.). Heliyon. 2021;7:e08669. doi:10.1016/j.heliyon.2021.e08669.

